Home Makala USHUJAA WA OBAMA UPO NDANI YA VISA VYA WAZUNGU – 2

USHUJAA WA OBAMA UPO NDANI YA VISA VYA WAZUNGU – 2

641
0
SHARE

MWANDISHI WETU


MWAKA 1951, mwanafunzi wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 16, Barbara Powell, alihamasisha wanafunzi wenzake Waafrika, kuikataa sheria ya Separate But Equal, ili wanafunzi wa rangi zote wawe na fursa ya kusoma pamoja bila kubaguana.

Kufuatia vuguvugu hilo la Barbara, mwanaharakati wa elimu sawa kwa wote, Oliver Brown, alifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu, dhidi ya Bodi ya Elimu ya Jiji la Topeka, Kansas, Marekani. Kesi hiyo inaitwa Brown v. Board of Education of Topeka, namba  347 U.S. 483, 1954.

Hukumu ilitoka kwa ushindi upande wa mlalamikaji, hivyo Mahakama Kuu, ikafuta sheria ya Separate But Equal, kwamba ilikuwa inakinzana na Katiba. Baada ya hapo, ikaamriwa kuwa watu wa rangi zote wachangie huduma za kijamii bila ubaguzi.

Mwaka 1956, mamlaka ya Jimbo la North Carolina, walianzisha mpango unaoitwa The Pearsall Plan ambao shabaha yake ni kuondoa utengano wa kibaguzi katika sekta ya elimu, hivyo kuruhusu Wazungu na Waafrika kusoma pamoja.

Kutokana na mkazo huo, mwaka 1957, binti mwenye umri wa miaka 15 wakati huo, alichaguliwa kujiunga masomo ya sekondari ya juu (high school). Binti huyo anaitwa Dorothy Counts, ila kwa sasa ni bibi mwenye umri wa miaka 75.

Dorothy ni Mmarekani mweusi. Alipangiwa kusoma Harry Harding High School ambayo ilikuwa na Wazungu watupu, kwa hiyo alikiona cha mtema kuni kwa Uafrika wake. Siku ya kwanza tu aliporipoti shule, yalitolewa maagizo aondolewe. Watoto wa Kizungu hawakutaka kusoma naye.

Zingatia Dorothy alikuwa na umri wa miaka 15 tu, akapigwa mawe, akazomewa na kufanyiwa kila aina ya ghasia. Mpigapicha Douglas Martin, alipiga picha tukio la Dorothy kupigwa na kunyanyaswa na Wazungu. Picha ya Douglas kuhusu Dorothy ilishinda tuzo ya Picha Bora ya Gazeti Duniani kwa mwaka 1957.

Kwa msukosuko huo, ilibidi familia nzima ya Dorothy ihame kutoka North Carolina mpaka Pennsylvania, baada ya manyanyaso kuzidi na hata vitisho vya kuuawa. Dorothy aliendelea na masomo Philadelphia kisha alitunukiwa shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Johnson C. Smith.

Mwaka 2008, Dorothy alitunukiwa diploma ya hesima na Harry Harding High School, mwaka 2010 shule hiyo ilimwomba Dorothy msamaha wa umma, vilevile kuanzia mwaka huo, maktaba ya Harry Harding High School, ilipewa jina la Dorothy Counts.

VEMA KUELEWA WAZUNGU

Mwaka 1962, James Meredith, alikuwa Mwafrika wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Mississippi. Hata hivyo, ilibidi Rais wa Marekani wakati huo, John Kennedy, aingilie kati na kumpa ulinzi Meredith.

Awali, Meredith aliomba kujiunga na chuo mara mbili akakataliwa. Baada ya hapo alikwenda mahakamani kuomba shauri lake la kuzuiwa kujiunga na chuo liangaliwe na Mahakama kwa kurejea hukumu ya Brown V. Board of Education of Topeka.

Mahakama iliamuru Meredith akubaliwe kujiunga na chuo lakini alikataliwa. kwa kutekeleza amri ya Mahakama, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Robert Kennedy aliagiza Meredith akubaliwe kujiunga na masomo lakini chuo kiligoma.

Gavana wa Mississippi, Ross Barnett, aliweka mkazo kuwa Meredith asijiunge na chuo hicho. Kesi ilirudi tena mahakamani, Barnett alikutwa na hatia ya kudharau Mahakama, akatozwa faini dola 10,000. Baada ya hapo Meredith alijiunga na chuo.

Kwa usalama wake, Serikali iliagiza vikosi vya polisi kuongozana na Meredith mpaka chuoni na kumsubiri amalize taratibu za kujiunga na chuo kisha wakaondoka naye.

Baada ya hapo, kwa mwaka mzima polisi walikuwa na kazi ya kumpeleka Meredith chuo na kuondoka naye ili kumlinda asishambuliwe na Wazungu ambao hawakutaka kabisa Mwafrika huyo asome chuoni hapo.

Mwaka 2002 kisha 2012, Chuo Kikuu cha Mississippi kilifanya maadhimisho ya miaka 40 kisha miaka 50 tangu mwanafunzi wa kwanza Mwafrika aliposoma chuoni hapo. Meredith ndiye mwanafunzi mwenyewe na mara hizo mbili alifika chuo na kuzungumza, kukumbusha nyakati za changamoto.

Juni 6, 1966, Meredith alishirikiana na mwanaharakati wa haki za binadamu, Martin Luther King Jr. kuandaa maandamano ya siku 19, waliyoyaita March Against Fear (Matembezi Dhidi ya Woga), ya umbali wa maili 220, kutoka Memphis, Tennessee mpaka Jackson, Mississippi.

Shabaha ya maandamano hayo, ilikuwa kukomesha ubaguzi wa rangi, eneo la Mississippi Delta. Maandamano hayo, yalikoma siku ya pili, baada ya kijana wa Kizungu, James Aubrey Norvell, kumpiga risasi na kumjeruhi Meredith.

VITUKO NI VINGI

Mwaka 1965, ikiwa ni baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Haki za Raia ya mwaka 1964 (Civil Rights Act of 1964) na Haki ya Kupiga Kura (Voting Rights Act of 1965), zilizopiga marufuku aina zote za ubaguzi wa kijinsia na rangi, Julian Bond aligombea ujumbe wa Seneti ya Georgia na kushinda.

Hata hivyo, wajumbe wenzake walikataa kukaa naye. Wajumbe 184 walipiga kura ya kumkataa, 12 ndiyo walimkubali. Kisingizio ni kuwa Bond alipinga Vita ya Vietnam. Hata hivyo, hoja ilielezwa ni Uafrika wa Bond.

Mtu kagombea kwenye wilaya yake ya uchaguzi, ameshinda kuwa mwakilishi, pamoja na hivyo, wajumbe wenzake kwa kumwona ni Mwafrika, walikataa kukaa naye. Mvutano ulikuwa mkubwa, Mahakama iliamua kisha Umoja wa Mataifa uliingilia kati.

Kesi ya Dred Scott dhidi ya Sandford, namba 60 U.S. 393, inathibitisha jinsi ambavyo Waafrika wamekuwa na vipindi vigumu Marekani. Mwaka 1857, Dred Scott na familia yake, walinyimwa uhuru na Mahakama Kuu, kwa maelezo kuwa Waafrika walikuwa bidhaa na siyo watu wenye kustahili uhuru.

Mahakama Kuu, chini ya Jaji Mkuu, Roger Taney, iliamua kumfanya Dred Scott na familia yake au Waafrika wengine kuwa watu huru, ingekuwa kuingilia haki za wamiliki wa watumwa.

Aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, James Buchanan, mwaka 1857, alichochea vita ya kiraia kupiganwa Marekani, baada ya agizo lake la Waafrika kudhibitiwa na ikibidi kuuawa ili watulie kwa wamiliki wao.

Mwaka 1861, Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, aliwakera Wazungu alipopitisha sheria ya kupiga marufuku biashara ya utumwa. Kuonesha kuwa Wazungu walichukizwa na Lincoln kwa uamuzi wake wa kiutu, mrithi wake, Andrew Johnson, alipitisha sheria ya kutowatambua Waafrika Marekani.