Home Makala USHUJAA WA OBAMA UPO NDANI YA VISA VYA WAZUNGU – 3

USHUJAA WA OBAMA UPO NDANI YA VISA VYA WAZUNGU – 3

589
0
SHARE

NA LUQMAN MALOTO


UTUKUFU WA OBAMA

BAADA ya wiki iliyopita kupitia visa hivyo kwa uchache, ndipo unaweza kupata majibu ni hatua kubwa kiasi gani kufikiwa na mtu mweusi baada ya Obama kupenya hatua ya uteuzi kwenye chama chake (Democrats) kisha kuwa Rais wa kwanza Mwafrika.

Usipojua visa vya Wazungu kwa Waafrika, unaweza kudhani Obama alifanikiwa kutwaa kiti cha Urais Marekani kwa bahati kisha unaweza ‘kuuchukilia poa’ Urais wake wa vipindi viwili mfululizo, yaani miaka nane.

Tena hapa nieleze kwa msisitizo kuwa Obama ndiye Rais wa kwanza Mmarekani mwenye asili ya Afrika. Kabla yake hakukuwa na mtu aliyewahi japo kusimamishwa na chama chake, katika vyama vikubwa Marekani vya Democrats na Republican kuwa mgombea Urais.

Msisitizo nimeuweka kwa sababu wapo watu humtaja mtu anayeitwa John Hanson kuwa Mwafrika wa kwanza kuwa Rais wa Marekani. Taarifa hiyo ni mkorogo mkubwa. Hakujawahi kuwa na kitu kama hicho.

Ukweli ni kuwa kuna akina John Hanson wawili, mmoja Mzungu, mwingine Mwafrika, hao ndiyo huchanganywa. Mzungu, alipata kuwa Rais wa Bunge la Marekani (Continental Congress) wakati wa mapinduzi, kuelekea kuundwa kwa Serikali mpya.

Ni kwamba baada ya Marekani kupata uhuru Julai 4, 1776, kila jimbo katika majimbo yake 13 ya awali, lilikuwa na mjumbe kwenye Continental Congress. Ni chombo hicho kilichofanikisha mazungumzo na mapendekezo ya kuundwa kwa Katiba kisha Serikali.

John Hanson (Mzungu) alikuwa Rais wa Continental Congress, hakuwa Rais wa Marekani. Mamlaka yake ni sawa tu na Spika wa Bunge, ingawa kwa wakati wake hakukuwa na Serikali. Rais wa Kwanza wa Marekani ni George Washington.

John Hanson (Mwafrika) ambaye huchanganywa na Mzungu, yeye alikuwa mtetezi wa haki za Wamarekani weusi. Na alipoona mambo ni magumu Marekani, aliwahamasisha Waafrika wenzake kutoroka Marekani na kusafiri mpaka Liberia.

Baada ya kufika Liberia, John Hanson, aligombea useneta kwenye Jimbo la Grand Bassa na kushinda. Hivyo, ukuu wa John Hanson (Mwafrika) ni kuwahamasisha Waafrika kuondoka Marekani na kuelekea Liberia kisha kuwa seneta Liberia.

Ufafanuzi huo, utoshe kujibu maneno kuwa Serikali ya Marekani imewahi kuwa na mtu mweusi mwenye nguvu miaka mingi kabla ya Obama, hiyo hapana. Obama amekuwa wa kipekee mno.

NDOTO YA KITAMBO

Obama siku alipotangazwa kuwa Rais mteule wa Marekani Novemba 2008, alisema ushindi wake ni kutimia kwa ndoto ya muda mrefu. Rais wa 43, George Bush, alipokuwa anaandaa mazingira ya kumkabidhi ofisi Obama, alisema ndoto ya muda mrefu ya Wamarekani ilikuwa imetimia.

Hakika ilikuwa ndoto ya muda mrefu na ilifuata baada ya harakati nyingi za watu Weusi. Wengi walifungwa kwa uonevu, wapo pia waliouawa. Huko nyuma, Mzungu hakutaka kusikia Mwafrika anapata mamlaka makubwa nchini Marekani.

Hiyo ilikuwa sababu miaka ya nyuma, kabla sheria hazijabadilishwa kipindi cha Rais wa 36, Lyndon Johnson, Mwafrika alikuwa haruhusiwi kupiga kura, achilia mbali kugombea ofisi yoyote ya umma iliyopatikana kwa njia ya kura.

Hata nadharia ya Wamarekani kutopiga kura ya kidemokrasia kuchagua Rais, badala yake watu 538 wa kura za majimbo, Electoral College, kuwa pekee wenye haki ya kuchagua Rais, inaelezwa iliwekwa ili kumdhibiti Mwafrika kuwa Rais wa Marekani.

Waafrika waliteseka mno Marekani. Ilikuwa mtu akitokeza kutaka kugombea Urais, Wazungu walimwinda wamuue. Kwao Mwafrika kugombea tu ilikuwa najisi, achilia mbali kushinda. Ni hapo unamwona Obama ni mkuu kiasi gani.

Kuanzia mwaka 2007, mara tu Obama alipotangaza nia ya kugombea tiketi ya Democrats ili ateuliwe kuwa mgombea Urais, Serikali ya Marekani iliboresha ulinzi dhidi yake, maana walishajua kuwa Wazungu wenye chuki, wasingechelewa kufanya yao.

Ukifuatilia visa vya wanaharakati 10 wa Wilmington Ten, waliofungwa kwa uonevu miaka 10 mpaka dunia ikaamka kupiga kelele ndiyo wakaachiwa miaka ya 1970, unaona jinsi maisha yalikuwa magumu kwa mtu Mweusi Marekani.

Wilmington Ten, waliongozwa na Mchungaji Benjamin Chavis ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Martin Luther King, Jr. nyakati za kuomba maafikiano kati ya watu wa rangi zote.

Ukitaka kuwajua Wazungu na visa vyao, zungumza na mzee James Richardson, ambaye watoto wake saba walipewa sumu wakafa, kisha kesi akasingiziwa yeye na akahukumiwa kifungo cha maisha jela.

Baada ya kusota jela miaka 21, ndipo ilikuja kubainika kuwa Richardson alionewa. Wakati wote kesi ikisikilizwa, utetezi wake ulipuuzwa na hakuna aliyeingia ndani yake kuona maumivu aliyokuwa nayo kwa kupoteza wanaye saba kwa mkupuo, wao wakahukumu tu.