Home Habari kuu Usiri wa Magufuli, Shein watesa wengi urais Z’bar

Usiri wa Magufuli, Shein watesa wengi urais Z’bar

1487
0
SHARE

Mwandishi -Dodoma

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijipanga kwa uchaguzi wa urais wa Zanzibar, Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli na Makamu wake upande wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein wamekuwa na mazungumzo ya ana kwa ana hivyo kuongeza joto la siasa juu usiri ulioko bana yao kwamba ni nani hasa atakuwa mgombea wa chama hicho kumrithi Dk. Shein Oktoba maka huu.

Hali hiyo inatokana na uamuzi wa viongozi hao wa juu wa CCM kukutana kwa nyakati tofauti ambapo inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya mazungumzo yao ni nani atarithi viatu vya Dk. Shein na kuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane.

Licha ya hali hiyo viongozi hao wametajwa kuwa kwenye mikakati kadhaa ya kupata mgombea ambaye atakayeshindana na vyama vingine vya upinzani ili chama hicho kikibaki salama bila mpasuko wa makundi hivyo kujihakikishia umoja ambao ni silaha muhimu kwa ushindi katika uchaguzi huo.

Kwa mara kadhaa viongozi hao wa juu wamekuwa wakikutana na kujadili masuala kadhaa kuhusu hatima ya CCM na majaliwa yake kuelekea Uchaguzi Mkuu, Juni 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. John Magufuli alikutana na Rais Dk. Shein, katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu Chamwino, ilielezwa kuwa kilihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally, kuzungumzia masuala ya chama hicho.

Majadiliano hayo yalikuwa yakihusisha viongozi hao yaligusia masuala kadhaa ikiwamo kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalumu ambapo utateua mgombea urais unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

“Pia suala la uteuzi wa mgombea urais limebaki kuwa siri nzito kwa viongozi maana kwa sasa wapo ambao wamekuwa wakijihakikishia ni wao. Ingawa hata hivyo lolote linaweza kutokea.

“Tunaamini CCM kwa kuwa ni chama kiongozi nchini na Afrika kitakuja na mgombea bora ambaye atakuja kumaliza siasa za mivutano Zanzibar ikiwamo kuwaunganisha viongozi wote.

“…hata baada ya kikao cha viongozi hao pia ujue hadi kupata mgombea ni mchakato mrefu ndani ya CCM kwani baada ya wanachama kuchukua fomu … ni lazima kura zipite kwa Kamati Kuu Maalumu ya CCM Zanzibar ambayo huwa kama njia, lakini pia mapendekezo hayo yatakwenda Dodoma na kujadiliwa na Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu,” alisema mmoja wa viongozi wa waandamizi wa CCM upande wa Zanzibar.

Hata hivyo, viongozi hao wakuu wawili wa nchi (Rais Magufuli na Shein), walikutana tena jana Juni 10, jijini Dodoma ambapo safari hii wakiwa wawili pasi na kushirikisha viongozi wengine kama ilivyokuwa kwenye kikao cha awali.

Rais Magufuli na mwenzake Shein walikutana kabla ya kufanyika kwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM  kilichofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, ambako walijadili masuala kadhaa kabla ya kuingia kikaoni.

Inatarajiwa kwamba kikao hicho cha Kamati Kuu ndicho kitatoka na utaratibu wa namna ya kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali ikiwamo urais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Hadi sasa yamekuwa yakitajwa makundi kadhaa ya wana CCM ikiwamo wengine kuanza mchakato wa kuendesha kura za maoni kupitia mtandao, kama njia ya ushawishi ya kujua jina la mgombea gani linakubalika kabla ya uteuzi wa mwisho wa chama.

Yapo majina ambayo yamekuwa yakitajwa licha ya CCM kuzuia makada wake wenye nia kuwania kiti hicho kujiepusha na harakati zozote za kujipitishapitisha kwa wanachama kabla ya wakati kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.

Makada ambao wanatajwa huenda akapatikana mmoja wao atayemrithi Dk. Shein ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi,  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor na Waziri wa Maji wa Serikali ya Muungano, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.

Pamoja na hatua hiyo mapema hivi karibuni Profesa Mbarawa alikaririwa  akisema kuwa kwa sasa anafikiri suala la maji kwa wananchi na siyo urais wa Zanzibar.

Wengine wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Mwakilishi wa Jimbo la Donge, Dk. Khalid Salum Mohamed ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Usi Gavu, Mohamed Aboud Mohamed, Khamis Mussa Omar, Salama Aboud Talib, Haji Omari Kheri, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa pamoja na Mahmoud Thabit Kombo.

Kutokana na hali hiyo taarifa kutoka ndani ya CCM upande wa Zanzibar makundi ya wahafidhina yameanza kuibuka, huku ushawishi ukijengwa kwamba kwa kipindi hiki ni lazima apatikane mgombea kutoka upande wa Unguja badala ya Pemba.

Hilo linachangiwa na histori ya Visiwa vya Zanzibar hasa kwa CCM waliopo upande wa Unguja kuona wenzao wa Pemba kuwa si wana mapinduzi halisi. 

JPM NA SIFA

Rais Magufuli akizungumza na wenyeviti na viongozi wa CCM Januari 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, alikumbusha kuwa mwaka huu nchi inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu na kwamba Desemba mwaka jana wakati wa vikao vya chama jijini Mwanza walipata fursa ya kujadiliana na kuelekezana masuala kadhaa.

Pamoja na hali hiyo aliwahakikishia wana CCM kuwa anashirikiana vema na Rais Shein huku akimtaja kuwa ni mpole, msikivu na asiye na makuu.

“Ninataka kuhakikisha wana CCM tunashrikiana sana na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Shein ni mpole, msikivu hana makuu.

“Angezaliwa mwingine katika uchaguzi unaokuja anayefanana na Shein mambo yangekuwa safi sana,” alisema Rais Magufuli.

MAALIM SEIFA NA UCHAGUZI

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad, mapema wiki hii alijitokea mbele ya umma na kusema kuwa licha ya hujuma kadhaa zinazojitokeza kuelekea Uchaguzi Mkuu katu chama chake hakitasusia uchaguzi mwaka huu.

Alisema mwaka 2020 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Alisema duniani kote, kipindi cha uchaguzi mkuu ni cha kipekee cha kuamua kuijenga nchi au kuibomoa nchi. Uchaguzi unaoiacha nchi salama na tulivu ni lazima ufanyike kwenye mazingira ya haki, uhuru, na uwazi.

“Kinyume chake, chaguzi huzaa uhasama, chuki na machafuko katika Taifa. ACT Wazalendo tunapenda uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uwe wa kuijenga badala ya kuibomoa Tanzania. Tunahitaji kuwa na uchaguzi utakaowaacha Watanzania wakiwa na furaha na matumaini baada ya kutekeleza haki na wajibu wao wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi wanaowataka.

“Kwa bahati mbaya, ikiwa imesalia miezi miwili tu kuelekea kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, mazingira ya kisiasa nchini hayatoi taswira ya uchaguzi unaoweza kuiacha nchi yetu salama. Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likiwa halina umoja.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likikosa maelewano ambayo yangefanikisha uchaguzi kufanyika kwa amani. Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likiwa katika mazingira mabaya na mfumo mbovu wa uendeshaji chaguzi kuliko wakati mwengine wowote wa historia yetu,” alisema Maalim Seif.

Alisema kwa kutambua wajibu wao na kwa lengo la kusaidia kuepusha nchi yetu isifike huko, ACT Wazalendo inawasilisha hoja kwa wadau wa uchaguzi kuhusu vikwazo vilivyopo ambavyo vinakwamisha kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Maalim Seif ambaye atawania urais wa Zanzibar kwa mara ya sita tangu mwaka 1995, alisema mapendekezo yao kuhusu mambo ya lazima yanayopaswa kuwapo ili uchaguzi mkuu uweze kuwa huru na wa haki ni pamoja na Tume ya Uchaguzi kuwa huru.

Alidai kwamba Tume za Uchaguzi si Huru: “Kwa muundo wake, Tume zetu zote mbili, kwa maana ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), zinaonekana kuwa ni Tume za Rais badala ya kuwa Tume Huru za Uchaguzi.”

Alisema hujuma hizo zina lengo la kuhakikisha kuwa maelfu ya wananchi wa Zanzibar wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura ambapo hadi sasa ZEC wameshakamilisha kazi ya uandikishaji kwa upande wa Pemba takwimu zinaonyesha kuwa ZEC imeandikisha jumla ya wananchi 109,567.

“Ukilinganisha na wananchi walioandikishwa mwaka 2015 ambao ni 145,066 utagundua kuwa wananchi 35,499 kwa mikoa miwili ya Pemba pekee wameachwa nje ya Daftari la Wapiga Kura kwa makusudi ili kuwanyima haki yako ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Hali hii haiwezi kutoa taaswira ya kuwa tunaweza kuwa na uchagzi huru na wa haki,” alisisitiza.

Alitaja hujuma kwenye Ugawaji wa Majimbo Zanzibar kuwa ZEC imetangaza dhamira yake ya kutaka kupitia upya idadi na mipaka ya majimbo ya Uchaguzi Zanzibar, ambayo alisema ni jambo la kushangaza sana.

“ZEC hii imekata majimbo mwaka 2015 ambapo iliongeza majimbo kutoka 50 na kuwa na majimbo 54. Si jambo lililotarajiwa hata kidogo kuona kuwa ZEC watafikiria kukata majimbo baada ya miaka mitano tu tokea kukata majimbo hayo. Tunafahamu kuwa kinachoisukuma ZEC kukata majimbo ni shinikizo kutoka CCM inayozidi kufifia kila uchao kule Zanzibar na ambayo inahangaika kuona vipi inaweza kukwepa hasira za wananchi kupitia masanduku ya kura,” alisema.

Alisema pamoja na hali hiyo katu ACT Wazalendo, hatasusia uchaguzi ujao na badala yake watashiriki kwa njia yoyote ile.

Katika Uchaguzi wa mwaka 2015, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi jambo lilomfanya aliyekuwa mgombea urais wa CUF kwa wakati huo Maalim Seif kutangaza kususia uchaguzi huo yeye na wawakilishi pamoja na madiwani jambo ambalo lilikifanya chama hicho kukosa uwakilishi ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.