Home Latest News Ustaarabu unahitajika kupunguza ajali

Ustaarabu unahitajika kupunguza ajali

1025
0
SHARE
Ajali iliyohusisha basi la mwendo kasi na gari ndogo
Ajali iliyohusisha basi la mwendo kasi na gari ndogo
Ajali iliyohusisha basi la mwendo kasi na gari ndogo

Na Leonard Mihafu,

MOJAWAPO kati ya mambo yanayogusa na kuunda habari katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni hili la awamu ya kwanza ya mradi wa Mabasi yaendayo haraka yanayofanya safari zake ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Changamoto zinazoukabili mradi huo zinatazamwa zaidi na kuibuliwa mijadala badala ya kuangaliwa utendaji kazi wake katika kutoa huduma kwa jamii.

Inadaiwa kuwa ndani ya siku 20 za mwanzo tangu mradi huo uanze ajali 32 zimetokea katika maeneo mbalimbali, huku ikielezwa kuwa kuna watu wamepoteza maisha.

Ipo mitizamo ambayo ndani yake iliyogawanyika katika makundi matatu.

Mosi, wapo wanaoamini kuwa mradi ni tatizo kwamba umeanzishwa mapema kabla ya  ya kuandaa miundombinu madhubuti.

Pili, baadhi wanaeleza kuwa watumiaji wa barabara za mabasi ya mwendo kasi (yaani wanaotumia barabara na hata kuhamia upande wa barabara za mwendo kasi) wamekuwa ni tatizo kwa utendaji wenye tija wa mabasi ya mwendo kasi.

Tatu, wapo baadhi ya watu waliofika mbali na kudai ya kwamba mradi huo haujaelimisha watu vya kutosha na hivyo husababisha ajali kutokana na wengi kutojua utaratibu, kanuni na utendaji wake.

Binafsi naunga mkono kundi la pili, kwamba ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa zaidi na watumiaji wa barabara, yaani waendesha boda boda, madereva wa magari na hata watembea kwa miguu ambao huingia barabara za mwendo kasi.

Ikumbukwe kuwa mabasi haya yametengewa barabara zake maalumu. Hii inanikumbusha juu ya utaratibu uliopo kwa treni, kwamba treni huwa hazigongi mtu wala gari bali zenyewe ndiyo hugongwa. Hii ina maana kuwa treni zina njia zake maalumu ikitokea ajali ya mtindo wa kugongana aliyeifuata barabara ndiyo anawajibika.

Utaratibu huu pia unaweza kutumika kuelezea suala hili ajali zinazotokea kwenye njia za mwendo kasi ni uvunjwaji wa sheria kama ilivyo kwa treni.

Pamoja na hayo yote tutazame kwa kina sakata la ajali za mabasi ya mwendo kasi linabeba picha gani?  Ajali hizi zinaonyesha mwendelezo wa hulka za kukosa ustaarabu mdogo wenye tija na manufaa, yaani kufuata sheria pasipo shuruti na uwepo wa uzembe wa hali ya juu. Hayo ni mambo mawili makubwa yanayobeba suala zima.

Ni ukweli usiopingika kuwa kuna sababu nyingi zinazosababisha zikiwemo uzembe, uvunjaji wa sheria za barabarani, ulevi, na ubovu wa vyombo vya moto vinavyoingia katika njia maalumu za mabasi ya mwendo kasi. Sababu hizi zote zinajikita katika watumiaji wa barabara kuanzia watembea kwa miguu hadi waendeshao vyombo vya moto. Lakini kwa ujumla wake naweza kusema ni kutotumia busara na uhaba wa ustaarabu.

Kwa muktadha huu, hili sakata linaonyesha tabia ya ajabu ilivyokithiri miongoni mwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu pia. Imekuwa  mazoea kwa baadhi ya watu kufuata sheria pale anapoonekana skari wa usalama barabarani. Hili ni tatizo kubwa ambalo limegharimu maisha na linaendelea kwa namna nyingine katika barabara za mabasi yaendayo kasi.

Busara inatufundisha kufuata sheria na kufanya lililo sahihi hata kama mtumia barabara uko peke yako. Kwa mantiki hiyo tunadhihirisha uhodari wa kupita dirishani hata ikiwa milango itakuwa wazi.

Ni kweli kuwa Dar es Salaam ni jiji lililo na idadi kubwa ya watu, ni jiji lililo na pilikapilika nyingi hali inayosababisha watu kuwa na mbinu mbalimbali za kuharakisha kufika katika maeneo yao ya biashara, vibaruani ama maofisini.

Pamoja na changamoto hiyo ni vema tuangalie Je, uharaka huo unaochangia kuvunja sheria una tija? je, haraka isiyo na mwisho mzuri inamnufaisha nani?

Yapo mambo ya msingi yanayofaa kuzingatiwa kubwa ni ustaarabu wa matumizi sahihi ya vyombo vya usafiri na barabara zake.

Ustaarabu ukizingatiwa hata sheria zitazingatiwa hayo yote yakizingatiwa upo uwezekano mkubwa wa kuepuka ajali za barabarani.

Ni vyema kufuata sheria pasipo uwepo ama uangalizi wa polisi wa usalama barabara. Busara yako ndiyo kupona yako, fuata sheria za barabarani ili zikulinde ili tuondokane na ajali hizi za mwendo kasi na nyinginezo.

Mwisho niseme kuhujumu mradi wa Mabasi ya mwendokasi ni kuliangamiza taifa na kulitia hasara ambayo itasababisha tushindwe kutoa huduma katika maeneo mengine. Raia mwema hutii sheria bila shuruti na hilo linawezekana katika utumiaji wa barabara sahihi.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili akibobea kwenye Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro. Anapatikana kwa baruapepe; leomartin911@gmail.com