Home Habari kuu Utafiti Haki Elimu wataja chanzo wanafunzi kufeli

Utafiti Haki Elimu wataja chanzo wanafunzi kufeli

424
0
SHARE

Andrew Msechu-Dar es Salaam

NAFASI hafifu ya wazazi na walezi katika kuhamasisha watoto kufanya vizuri katika masomo na mitihani yao ya mwisho imetajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kufeli kwa wanafunzi katika mikoa inayoongoza wka matokeo mabaya ya mitihani ya mwisho.

Akizungumza wakati wa kuswasilisha ripoti ya “Sababu Zinazochangia Mikoa Kufanya Vizuri au Kutofanya Vizuri Katika Matokeo ya Darasa la Saba Nchini” jana, Mkurugenzi Mtendajiw a Haki Elimu, Dk. John Kalage alisema hiyo ni sababu moja, lakini sababu zinatofautiana kati ya sehemu moja na nyingine.

Alisema kuna suala la baadhi ya wazazi kuweka thamani kudogo katika elimu hivyo kuwahamasisha watoto kufeli mitihani kwa makusudi ili wasipate alama za kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

“Kwa ujumla, watoto wanahamasishwa kufeli na kubaki nyumbani ili kusaidia kazi za nyumbani, kuolewa au kutafuta kazi kwa ili kusaidia familia. Suala hili linaibua  swali muhimu juu ya umuhimu wa elimu inayotolewa,” alisema Kalage.

Alisema sababu nyingine ni umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni na kutoka shuleni kwenda makao makuu ya wilaya, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya washiriki, hasa wanaotoka katika maeneo ya vijijini, walikuwa na mawazo kuwa, umbali mrefu kutoka katika maeneo wanayokaa wanafunzi na walimu  hadi shuleni vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kupata matokeo mabaya ya mtihani.

Alisema sababu ya tatu ni utofauti wa kimiundombinu na mazingira kutoka mkoa mmoja na mwingine, unaomaanisha tofauti za mikoa kwa maana ya upatikanaji wa rasilimali za kufundishia na kujifunzia.

“Ilifahamika kuwa, ukiachilia mbali matokeo ya darasa la saba, mikoa, wilaya na shule zina uhitaji sawa wa rasilimali za kufundishia na kujifunzia na miundombinu kama ilivyoainishwa katika ripoti kuu ya utafiti.

Alisema sababu nyingine ni changamoto zilizopo katika masuala ya kimenejimenti akitoa mfano kwa wastani,  Mkoa wa Geita, ambao ni moja kati ya mikoa inayofanya vizuri, una upungufu wa madarasa kwa asilimia 56 na madawati kwa asilimia 36, ambapo pia, kwa wastani.

Ilibainishwa kuwa Mkoa wa Singida ambao ni moja ya mikoa ambayo imekuwa haifanyi vizuri, una upungufu wa madarasa kwa asilimia 49 na upungufu wa madawati kwa asilimia 21 lakini Geita inaongoza kwa ufaulu ikilinganishwa na Singida.

Kalage alisema kukosekana kwa hamasa na mbinu za ziada katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ni sababu nyingine inayozorotesha kupata matokeo mazuri kwa maeneo yanayofanya vibaya katika mitihani hiyo.

Alisema mikoa ambayo imeonekana kuendelera kufanya vibaya kila wakati katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni pamoja na Singida, Dodoma, Mtwara, Mara, Tanga, Kigoma Tabora na Manyara na wkamba kama ilivyo kwa mikoa iliyofanya vizuri, ukichunguza kwa kina utagundua kuwa mikoa hiyo ina sifa ya changamoto walizozitaja.

Alisema japokuwa katika utafiti huo Haki Elimu ilitumia matokeoya darasa la saba ya mwaka 2016/17 kwa kuchagua mikoa michache iliyofanye vizuri pamoja na michache ambayo haikufanya vizuri, hiyo haimaanishi kuwa kunaweza kuwa na sababu tofauti katika mikoa ambayo hawakuifikia.

Alisema ni vyema matokeo hayo yachukuliwe kama sababu za jumla na iwe chachu kwa mikoa mingine kujitathmini na kutafuta sababu zinazopelekea ama ifanye vizuri, wastani au vibaya.

Alisema ni matumaini yake kuwa mamlaka zinazohusika, pamoja na wadau na watunga sera, mikoa, shule na wananchi watayatumia vyema matokeo ya utafiti huo kuboresha hali ya ujifunzaji na ufaulu katika ngazi ya elimu msingi.

“Lakini zaidi, ni matumaini yangu kuwa matokeo ya utafiti huu yatachochea mijadala zaidi kuhusiana na matokeo ya ujifunzaji kwa watoto wetu na namna bora ya kuboresha ufaulu ili kuinua elimu yetu.

“…hasa ikizingatiwa kwamba matokeo ya utafiti huu yanazinduliwa wiki chache tu baada ya matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne kutangazwa, ambayo pia yanaonesha mwendelezo huo huo wa baadhi ya mikoa kuendeela kufanya vizuri zaidi na baadhi kuendeela kuwa na matokeo yasiyoridhdisha,” alisema

Kalage alisema utafiti umegundua kuwa sababu tofauti za ufaulu ni kama juhudi za maeneo husika za kuongeza ufaulu kama hamasa kwa walimu, kuwaweka wanafunzi wa darasa la saba katika kambi za masomo kwaajili ya matayarisho ya mtihani wa darasa la saba na udanganyifu unaopelekea ufaulu katika mtihani wa darasa la saba.

“Hata hivyo, bado kuna maswali ya kujiuliza kuhusu kuhusisha ufaulu mzuri na udanganyifu kwani inaweza kuhamasisha wengine kufanya vitendo hivi ambavyo havikubaliki.

“Sababu hizi za tofauti ambazo zinaweza kuwa zimesababisha  muendelezo wa ufaulu mbovu katika matokeo ya darasa la saba ni pamoja na umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shule na makao makuu ya wilaya ambayo inawanyima wanafunzi manufaa kutoka wilayani ikiwemo pamoja na kufanyiwa uthibiti ubora,” alisisitiza.

Alisema ili kuboresha matokeo kuna umuhimu kwa mikoa yenye ufaulu mbovu kuiga mifano mizuri kutoka mikoa yenye ufaulu mzuri katika matokeo ya darasa la saba, ikiwemo kuwa na mkakati wa mkoa wa kuongeza ufaulu.

“Pia nni vyema kuhakikisha kuna juhudi za muendelezo kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali katika rasilimali ili kuimarisha miundombinu. Msisitizo uwekwe katika shule ambazo ziko mbali na makao makuu ya wilaya na wilaya ambazo ziko vijijini,” alisema.

Aliongeza kwua ni vyema jamii pia zisaidie kuonesha thamani ya elimu katika maeneo yao, ikimaanisha kuwa kuna umuhimu wa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu umuhimu wa kuwa na mfumo wa elimu wa aina moja kwa nchi nzima kama kama  elimu hii inasaidia jamii husika.

“Pamoja na vitu vingine, kuna umuhimu wa kuhamasisha wazazi kusaidia shule kwa michango ya fedha ili kuunganisha nguvu na fedha ikiwamo ruzuku zinazopelekwa kwaajili ya elimu bure zinazotolewa na serikali,” alisema.