Home Makala Kimataifa UTAFITI: TALIBAN HAIJASALIMU AMRI NA HAITASALIMU AMRI

UTAFITI: TALIBAN HAIJASALIMU AMRI NA HAITASALIMU AMRI

825
0
SHARE
Afghanistan's President Ashraf Ghani speaks during a news conference in Kabul, Afghanistan December 11, 2015. REUTERS/Omar Sobhani

KABUL, AFGHANISTAN

Utafiti mmoja uliendeshwa na Jason Lyall wa Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani uligundua kwamba wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan wana umoja wa nguvu sana katika kikundi chao.

Na matokeo ya hii ni kwamba maangamizi yoyote yafanywayo na vikosi vya nje hupunguza ufuasi, kasi na ari ya vikosi hivyo vya nje na kuongeza ufuasi. Kasi na ari wa Taliban.

Matokeo ya utafiti huu yamekuja miaka 16 baada ya Marekani kupeleka majeshi yake nchini Afghanistam kupambana na kile ilichokiita ugaidi wa kikundi cha Alqaeda cha osama bin Laden ambaye alichukua hifadhi nchini Afghanistan chini ya utawala wa Taliban wakati huo.

Tawala za Marekani tangu wa George W Bush zimekuwa zikibuni kila sababu za kuendelea na mapambano kule ingawa mara kadha zimekuwa zinaahidi kupunguza vikosi vyake. Kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2008 George W Bush alipunguza vikosi vyake lakini mwaka 2009 mrithi wake barack Obama alitangaza kuongeza vikosi. Vivyo hivyo kwa ujio wa Donald trump baada ya kuondoka kwa Obama.

Wiki moja tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kupeleka vikosi zaidi vya kijeshi nchini Afghanistan, tayari askari kutoka jimbo la Alaska walikuwa wanatayarishwa kwa kazi hiyo.

Brigedi ya tano ilioko jimboni humo itatoa askari 1,000 kati ya jumla ya askari 4,000 wanaopangwa kupelekwa Afghanistan katika azma ya Trump ya kuendeleza vita hiyo.

Hata wakati hayo yanafanyika, Marekani inaonekana haina mpango madhubuti ulio wazi na unaoeleweka kuhusu kitu gani inataka itimize huko, wakati huo huo maafisa wa Wizara yake ya Ulinzi (Pentagon) wakisema “hawako tayari kuendana na mpango wa Rais” kwa maelezo kwamba mpango mzima na ulio madhubuti bado unaandaliwa.

Na wakati huo huo msemaji mmoja wa wapiganaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid alijibu kauli ya Trump (ya kupeleka vikosi zaidi) kwa kusema kwamba ni vyema akavirudisha nyumbani vile vilivyopo nchini mwao kwani kikundi chao cha Taliban hakitashindwa vita hiyo.

Ingawa ni tamko la majigambo, lakini huo ndiyo ukweli. Mapema Machi mwaka huu Taliban walisambaza ripoti ikitaja ukubwa wa maeneo ya nchi wanayoyadhibiti. Kutokana na ripoti hiyo, wilaya 211 za kiutawala ama ziko mikononi mwao au bado zinapiganiwa vikali kuwania udhibiti.

Wachunguzi wa mambo wanasema takwimu hizi hazijatiwa chumvi sana kwani taarifa za vyombo vya habari na ile ya Mkaguzi Mkuu Maalum wa Kazi za Ujenzi Mpya wa nchi (Special Inspector General for Afghanistan Reconstruction -SIGAR) zinakadiria wilaya zilizo chini ya udhibiti wa Taliban na zile zinazopiganiwa vikali ni 171 – idadi ambayo haiko mbali sana na ile ya Taliban.

Kwa vyovyote vile, baada ya takriban miaka 16 ya uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan na gharama ya zaidi ya Dola 840 bilioni, kikundi cha Taliban hakijasalimu amri, na bado kiko ngangari.

Swali la kujiuliza ni kwa nini vita hii haina tena  msisimko miongoni mwa Wamarekani wengi na hata wanaoipanga na kuiratibu? Kuna baadhi wanakiri uwepo wa hali halisi kwamba ufumbuzi kupitia nguvu za jeshi siyo jibu sahihi na hauwezi kufanikiwa lakini bado wanaonekana wako tayari kushawishi upelekwaji askari zaidi, na wakati huo huo wakiwalaumu marais waliotangulia (hasa Obama), na kichwa ngumu cha majirani (hasa utawala wa Pakistan).

Lakini ukweli uko mbali sana kutokana haya yote yanayoendelea kuhusu nguvu za kijeshi za Marekani na hali halisi nchini Afghanistan.

Kwanza kabisa ni kwamba baada ya miaka 16 ya vita, askari wa Marekani sasa wanapata tabu sana kuziafiki sababu kubwa wanazoambiwa kuhusu uendelezaji wa vita hiyo. Osama bin Laden kisha kufa na “vita dhidi ya ugaidi” imegeuka kuwa ni janga, mateso na mauaji tu yasiyokuwa na mantiki au mwisho. Lakini kitu gani hasa kinafanya majeshi ya Marekani kuendelea kuwapo Afghanistan?

Sababu madhubuti kwa Marekani kuwapo Afghanistan haipo, lakini Taliban ipo. Askari wa Marekani waliambiwa kwamba wao “ni watu wema na wastaarabu” waliokuwa wanapelekwa kupigana Iraq na Afghanistan ili kusimika demokrasia, kujenga taasisi na kuanzisha tawala za kisheria.

Ukweli ni kwamba kwa Afghanistan ni tofauti kabisa. Tofauti iliyopo kati ya uongo uliosambazwa wakati wa kuipigia debe vita na vita yenyewe inayoendelea inazidi kuwa kubwa na imeanza kuwavunja moyo askari ambao wanatayarishwa kupelekwa Afghanistan.

Lakini pamoja na haya yote maafisa wa utawala wa Marekani na wale wa Afghanistan hawawezi kusema kwamba gharama ya karibu Dola trilioni moja ya vita hiyo haijaenda bure.Na Rais Trump, pamoja na kauli zake nyingi za kujenga Marekani mpya na kubwa hawezi kujibu swali hili rahisi: kama vita hiyo siyo ya kuijenga Afghanistan mpya, ni ya nini basi?

Mwaka mmoja uliopita, kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan Jenerali John Nicholson alisema kwamba malengo kuhusu vita hiyo yalikuwa yakienda vizuri.

Na Aprili mwaka huu, Anthony Box, mshauri mkuu wa masuala ya ulinzi aliyeazimwa na utawala wa Kabul alijigamba kwa kusema kwamba imani ya raia wa Afghanistan kwa serikali yao ilikuwa iko juu kabisa.

Ilikuwa ni kauli ya kushangaza sana, ikizingatiwa kwamba Umoja wa Mataifa umekuwa ukiripoti mashambulizi dhidi ya raia nchini Afghanistan yalifikia kilele mwaka 2016. Kauli kama hizi zinaonyesha kwamba kunapokosekana mafanikio ardhini, basi hayo yanaweza kupatikana kupitia vinywani.

Na Wamarekani ambao ajira na hadhi zao zinategemea mafanikio kutokana na vita hiyo hawapendi kukiri hali ya kushindwa. Na hivyo hivyo kwa Wafghanistani ambao hufaidika kwa kuwepo vita hiyo na misaada ya mamilioni ya Dola nchi hiyo inayopata, fedha ambazo pia huingia mifukoni mwa wachache ambao hata hawajawahi kushika silaha.

Watawala wa Afghanistan wanafahamu wazi kwamba ushindi wowote wanaojigamba nao siyo endelevu – kwani Wamarekani wakiacha tu kutoa fedha, basi utawala wao unaweza ukaanguka.

Na tofauti na askari wa Marekani, wapiganaji wa Taliban wanafahamu vyema jiografia ya nchi yao na jinsi ardhi ilivyo. Aidha Wamarekani hawana ujuzi wa lugha yao, utamaduni, na mara nyingi wanavurugika akili kujua sababu hasa ya wao kuwepo umbali wa makumi elfu ya kilomita nje ya mipaka ya nchi yao.