Home Makala UTAPIAMLO VITA MPYA LINDI, MTWARA

UTAPIAMLO VITA MPYA LINDI, MTWARA

3879
0
SHARE

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

Mikoa ya Lindi na Mtwara ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la utapiamlo linalosababishwa na lishe duni. Watoto hudumaa  wakiwa chini ya umri wa miaka mitano, na hata ukuaji wao huwa wa taratibu na kusababisha madhara makubwa kiakili.

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa, bado hali sio ya kuridhisha juu ya tatizo hili la kukosa lishe bora.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limeweka Malengo ya Lishe 2025, ili kusaidia nchi zenye tatizo hilo, ikiwemo Tanzania, kupunguza kiwango cha tatizo la udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano  kwa asilimia 40 na  kupunguza kiwango cha tatizo la upungufu wa damu miongoni  mwa wanawake walio katika  umri wa uzazi kwa asilimia 50.

WHO linaendelea kupunguza kiwango cha  tatizo la watoto kuzaliwa  wakiwa na uzito pungufu  kwa asilimia 30, kuzuia kuongezeka kwa tatizo la uzito uliozidi  miongoni mwa watoto, kuongeza kiwango cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi  sita ya mwanzo, kwa angalau asilimia 50, kupunguza tatizo la ukondefu kwa watoto na kulidhibiti libakie chini ya asilimia 5.

Kwa mujibu wa WHO, katika kila kundi la watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano nchini, kuna watoto wawili waliodumaa, ingawa kati ya mwaka 1992 na 2014, kiwango cha udumavu nchini, kimepungua kwa asilimia 30. Idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 2.4 hadi milioni 2.7 katika kipindi hicho.

Mkurugenzi wa shirika la Aga Khan Foundation, Biko Evaristy anasema tatizo hilo limekuwa ni kubwa miongoni mwa jamii nyingi katika bara la Afrika, hali ambayo inalazimu mataifa kushirikiana, ili kulitatua kwa kupunguza, ama kumaliza tatizo kabisa.Anasema kuwa kuungana na jamii katika kupunguza tatizo hilo katika kipindi cha miaka 5, Aga Khan Foundation, liliweka kambi katika Wilaya mbili za mikoa ya Lindi na Mtwara na kutoa elimu na mafunzo ambayo yalionyesha matumaini yenye tija ndani ya jamii, kupitia mradi wa Kuboresha Huduma za Afya uliotekelezwa katika wilaya za Masasi, mkoani Mtwara na Kilwa, mkoani Lindi.

Anasema suala la utapiamlo huwa linaathiri hali ya afya na mazingira kutokana na watoto chini ya umri wa miaka 5, kuwa na lishe duni kunasababisha watoto kudumaa kiakili na kimwili, na kupata magonjwa ya mara kwa mara. Aidha, watoto huwa uwezo mdogo wa kufikiri.

“Udumavu sio mzuri unapokomaa katika jamii husababisha uwezo wa kufikiri kuwa mdogo, hivyo watu kuanza kurithishana na kuwa na mawazo sawa, ndio maana katika mradi huu udumavu tuliupa kipaumbele. Hivi sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto milioni 180 duniani walio chini ya miaka mitano, wamedumaa kiakili na kimwili kwa kusosa lishe bora.

“Lakini katika mradi huu pia tulijikita katika kutoa elimu ya lishe na unyonyeshaji watoto, na tuliweza kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika vituo vya kutolea huduma, lengo likiwa ni kuhakikisha utoaji wa huduma za afya, unakuwa wa kuridhisha,” alisema Biko

Mtoto anapokuwa na utapiamlo ni matokeo ya lishe duni mtoto mwenye utapiamlo anakuwa na nchi sita chini kuliko mtoto asiyedumama chini ya miaka mitano

Biko anasema mtoto aliyedumaa  hushindwa kurefuka na anakuwa katika hatari zaidi ya kufa kwa haraka huku urefu wake huwa sio sawa na mtoto anaepata lishe bora.

“Mtoto mwenye udumavu huwa na seli ndogo zisizohimili kulinda mwili kupokea magonjwa kulingana na uzito wenyewe wa tatizo ingawa jamii haijalipa kipaumbele hili tatizo, unachangia kupata magonjwa mbalimbali utotoni”

Kwa upande wake mhudumu wa afya ngazi ya jamii kata ya Chiungutwa Wilayani Masasi, Ziada Daniel anasema awali kabla hawajaingia katika mradi wa miaka mitano wa shirika lisilo la kiserikali la Aga khan foundation walikuwa wakipata taarifa nyingi za vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano ambavyo kwa kiasi kikubwa vilisababishwa na utapia mlo.

Anasema wazazi wengi mijini na vijijini wamekuwa wakidhani kuwa lishe bora ni mahindi, ulezi, mtama na karanga huku vyote vikichanganywa bila kuona kuwa baadhi yake ni vyakula vya kundi moja.

Anasema hii ilitokana na mazingira ya vijij vingi kushindwa kutunza watoto hasa katika suala la lishe ambalo lilikuwa halizingatiwi ambapo mtoto mchanga ndani ya siku 1000 tayari ameshapewa uji wa muhogo ama ugali ama chakula chochote bila kujali kuwa vya kula hivyo sio sahihi kwa mtoto mdogo.

“Miaka 7 iliyopita tulikuwa tukipima watoto kliniki wengi wanaingia kwenye kijivu ama nyekundu hali ambayo ilikuwa ni hatari hata uzito wao ulikuwa wamashaka lakini sasa tunajivunia kusema kuwa idadi ya watoto wenye uzito mdogo na udumavu katika wilaya yetu wamepungua hususani kata zilizofanikiwa kuingia katika mradi huu wa afya wa miaka mitano..

“Sisi huwa tunatoa elimu mtoto anapaswa kuwekewa karanga, mahindi, dagaa, viazi lishe ama boga na kuchanganya kwenye uji wakati mwingine unachukua maji ya mchicha ama matembele ndio unamnywesha mtoto wa miezi 6 hii inasaidia kulinda mwili na kumuondoa kwenye hatari ya kupata utapiamlo” anasema Daniel

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Afya Kituo cha Afya Chiwale, Issa Mwahave anasema kituo hicho ni moja kati ya vituo vinavyonufaika na mradi huo wa kuboresha maisha hali ambayo imeongeza idadi ya wanawake kufika kliniki kutokana na elimu waliyokuwa wakipatiwa.

Anasema suala la malezi kwa watoto lilikuwa gumu kwakuwa wazazi hawakuwa na muda wa kufatilia watoto wao hali ambayo iliongeza idadi ya watoto wenye utapiamlo kutokana na lishe duni wanayojitfutia bila usimamizi wa wazazi.

Mwahave anasema mafunzo hayo yamehamasisha jamii kuwapa watoto lishe bora, kutunza mazingira  bado changamoto ndogo ndogo hazikosekani ikiwemo ya kunawa mikopo wanapotoka kujisaidia bado inasumbua wanajamii.

“Lishe bora kwa mtoto inaendana na usafi wa mama na mazinginra waliyopo ndio changamoto kubwa inayowakabili watu vijiijni kwa sasa bado watu hawajajua umuhimu wa kunawa mikono pale wanapotoka kujisaidia kabla ya kuandaa chakula ama kabla ya kunyonyesha mtoto” alisema Mwahave

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngumbiagai anasema lishe inapaswa ipewe kipaumbele ili kujenga taifa lenye nguvu.

“Huwezi kuwa na maendeleo na huwezi kuwa na watu wnye nguvu na uwezo mzuri wa kufikiri kama afya zao zitakuwa na mgogoro na huwezi kutengeneza uchumi wa viwanda na watu goigoi lazima tusimamie lishe kwa watoto wakue vizuri wawe na akili zenye uwezo na ubunifu ili kujenga taifa lenye nguvu….

“Ambapo tunaanzia kuwaelimisha mama wajawazito ili kuanza kulea mtoto akiwa tumboni tusipowaeliemisha mama wajawazito wakapata elimu nzuri ya utunzaji tutegemee watoto mazezeta ili kupata watoto waliotimia lazima wapate elimu ili waweze kulea mimba vizuri” alisema Ngumbiagai

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Juma Satmah anasema halmashauri hiyo itajipanga ili elimu iweze kutolewa kwa watu wote ili iweze kusaidia mama kuanza kulea mtoto akiwa tumboni kwa kumpatia lishe bora.

“Unajua hili shirika limeenda mbali katika utekelezaji limeongeza nguvu kwenye malengo ya serikali hili jambo nasisi tutalipa uzito unaostahili hatutawaangusha tutaangalia namna ya kufanya ili kupunguza changamoto hii” anasema Satmah