Home Habari kuu Utata magari ya waya Mlima Kilimanjaro

Utata magari ya waya Mlima Kilimanjaro

1176
0
SHARE

*Mhifadhi Mwandamizi aufananisha na ndoto

*Waziri Kigwangala asisitiza utakuwa rafiki wa mazingira

Na Mwandishi Wetu

MJADALA kuhusu mchakato unaoendelea wenye lengo la kuanzisha utalii wa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia magari maalumu yanayotumia umeme cable cars”, umezidi kupingwa.

Wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, ameendelea kusisitiza kuwa mradi huo ni muhimu kwa ukuaji wa utalii nchini, ni rafiki wa mazingira na utaongeza pato la Taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu siku chache zilizopita jijini Mwanza, Mhifadhi na mtaalamu wa masuala ya utalii kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA (jina tunalihifadhi), alisema mradi huo hauwezi kuwa na manufaa kwa Taifa kama inavyoelezwa.

Alisema kama mradi ambao mchakato wake bado upo katika hatua za awali utatekelezwa, utasababisha athari kubwa kwa mazingira ya eneo hilo, utaathiri ajira na mapato ya Serikali.

“Kama mradi huu utatekelezwa ni lazima utabadili sura ya asili ya eneo la Mlima Kilimanjaro, ambapo uasilia wa eneo hilo ni moja ya vivutio kwa watalii, kwani ni tofauti na milima mingine.

“Unapojenga miuondombinu ya cable cars, lazima uweke nguzo imara, sasa ili kuweka nguzo hizo ni lazima miti mingi ikatwe pamoja na mpangilio wa miamba kuvurugwa. Hili kwa vyovyote vile litaharibu uasilia mwa mlima, na tutakuwa na Mlima Kilimanjaro tofauti na tulio nao sasa.

“Jambo jingine muhimu la kufahamu na hili nazungumza kutokana na uzoefu nilioupata kutoka nchi ambazo zinatumia cable cars, mazingira ulipo Mlima Kilimanjaro, tusitarajie kupata fedha zinazotarajiwa.

“Milima maarufu duniani inayotumia mfumo huo ipo karibu na maeneo ya mijini, hivyo watumiaji wengi wa cable cars ni wakazi wa maeneo hayo ambao hutumia fursa hiyo kwa starehe zaidi kuliko malengo ya watalii ambao lengo lao kuu ni ku-experience nature” alisema.

Baadhi ya milima maarufu inayotumia cable cars ambayo ipo maeneo ya mijini ni Peak2Peak Gondola (Canada), Stanserhorn Cabrio (Uswizi), Table Mountain Aerial Cable way (Afrika Kusini), Bracci Funicular (Italia), Ba Na Hills Cable Car (Vietnam), Sugarloaf Mountain Gondola, Rio de Janerio (Brazil), Funicular de Sant Joan (Hispania) na Hartbeespoort Aerial Cable Way (Afrika Kusini).

Akizungumzia kuhusu hoja ya cable cars kutumika kuongeza mapato, alisema hilo haliwezekani, kwa sababu gharama kupanda magari huwa ni kati ya dola za Marekani 45 hadi 50 kwa mtu.

“Kama watapanda watalii mathalan 100, maana yake watalipa Dola za Marekani 4,500 au 5,000. Lakini watalii wanaopanda kwa utaratibu wa kawaida (hiking), mtalii mmoja hutumia hadi dola 2,000 mpaka anaposhuka.

“Naamini hata huyo mwekezaji atakapokuja na kutazama mazingira ya ulipo mlima, sidhani kama atakubali kuwekeza fedha nyingi, huku akiwa hajui ni kwa namna gani na lini zitarudi na ajae apate faida. Kwa hiyo hili suala naliona ni kama ndoto,” alisema.

Akizungumzia ajira, alisema kwa namna yoyote ile lazima soko la ajira litaathirika, kwa sababu mtalii anayepanda gari la umeme hahitaji wasaidizi kama ilivyozoeleza.

Kwa upande wake, Waziri Dk. Kigwangala ambaye juzi alizungumza na RAI kijijini Chato, mkoani Geita, alisisitiza kuwa mradi huo utakuwa wenye faida kubwa katika kukuza utalii na kuongeza mapato.

Alisema wazo la kuleta mradi huo, ni matokeo ya ubunifu mkubwa anaoufanya kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini, pamoja na kutoa fursa kwa makundi yote ya jamii kupata fursa ya kupanda Mlima Kilimanjaro.

Alisema siku zote amekuwa rafiki mkubwa wa mazingira, hata kufikia hatua ya kushauri baadhi ya mapori ya akiba yapandishwe hadhi na kuwa hifadhi za Taifa kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya uhifadhi wa maliasili.

“Mimi sifanyi siasa, bali nafanya kazi, hata suala la cable cars linatokana na maoni ya wananchi na wadau wengine. Wananchi wamekuwa wakitaka cable cars, kwa hiyo nimechukua mapendekezo yao na kuyafanyia kazi.

“Hata wenzetu wa mazingira wanataka kuingilia kati mradi wa cable cars Kilimanjaro. Lengo letu ni kukuza utalii, kuongeza mapato na kuboresha experience ya watalii wetu nchini.

“Tusipokuwa wabunifu tunaambiwa hatutumii vema utajiri wa vivutio vilivyopo nchini. Kama ni suala la nguzo mbona hata kwenye hifadhi zetu zipo nguzo za umeme? Sasa kwa nini kwa Kilimanjaro watu wanapinga?

“Mlolongo wa urasimu umeua biashara zetu na kukwamisha uwekezaji kwa muda mrefu sana hapa nchini. Hivi sasa tunajaribu kuondoa vikwazo ili kukuza uwekezaji na uchumi wetu.

“Nchi zinazokua kwa kasi zimeepuka sana njia hizo. Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake? Hizi haziharibu mazingira? Cable cars zinapita juu, zinaharibu mazingira gani?

Zaidi ya ekari 350,000 za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? ‘Watu wa mazingira’ wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano yakiwamo ya mkaa?

“Watalii watakaotumia cable cars na wale wa hiking ni tofauti. Hii ni product nyingine, itazalisha ajira nyingine zaidi bila kufuta ajira zilizopo sasa. Wanaopanda kwa cable cars kwa uzoefu wetu ni wazee, watoto na familia ambao hawana muda mrefu wa kupanda mlima,” alisema.

Alisema kwa sasa bado wanaendelea kufanya tathmini ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Environmetal Social Impact Assessment (ESIA), ambapo baada ya kukamilika, matokeo yatapelekwa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC).