Home Habari Utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi ya kata

Utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi ya kata

644
0
SHARE

NA ANNA HENGA

KUMEKUWEPO na ongezeko la migogoro ya ardhi mijini na vijijini, mingi ikisababishwa na tamaa, uzembe na rushwa kwa baadhi ya wafanyakazi katika idara mbalimbali zilizopewa dhamana ya kusimamia ardhi na pia kutokufahamu sheria za ardhi kwa watu wengi ambapo imepelekea kufanya mambo kinyume cha sheria.

Migogoro ya ardhi ni kile kitendo cha kutokuwepo maelewano kwa pande mbili au zaidi juu ya umiliki, mipaka, upangaji, mikopo, mauzo na aina nyingine ya ubishani ikihusisha sheria za ardhi.

Katika kutafuta njia ya utatuzi wa migogoro hii ndipo yalipoanzishwa Mabaraza ya Kata kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, No. 2 ya mwaka 2002 (The Land Dispute Courts Act) kupitia kifungu cha 10 cha sheria hiyo. 

Sheria hii pia inaeleza sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 ndizo zitakazotumika kwenye mabaraza, ikiwa ni pamoja na kuainisha uwezo na muundo wa baraza. 

Mabaraza ya ardhi ya kata yako katika kila wilaya na yana mamlaka ya kusuluhisha migogoro katika kata na wilaya husika kwa mujibu wa sheria ya mabaraza ya ardhi ya kata sura ya 206, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 (The Ward Tribunal Act, Cap 206 R.E 2002).

Pia mabaraza haya yanatambulika kisheria kwa mujibu wa sheria ya ardhi kifungu cha 167(1)(c) sura ya 113 iliyorejewa mwaka 2002 (Land Act, Cap 113 R.E 2002)

Idadi ya wajumbe

Kikao cha baraza kinapaswa kuwa na wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi nane na miongoni mwao watatu wawe wanawake.

Katika kusikiliza mashauri, mwenyekiti atateua wajumbe watatu miongoni mwao mmoja ni lazima awe mwanamke kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria namba 2 ya mwaka 2002.

MAMLAKA, UWEZO NA MAJUKUMU 

Jukumu la msingi la baraza ni kulinda amani na kuunganisha wadaiwa kwa njia ya usuluhishi na kuhakikisha usuluhishi wenye tija wa mgogoro unapatikana kwa kila pande kuondoka bila kinyongo, ugomvi au manung’uniko. Kwa mujibu wa kifungu cha nane cha Sheria ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata sura ya 206 ya mwaka 2002, zaidi ya mabaraza ya ardhi ya kata yana mamlaka kisheria kusikiliza mashauri ya ardhi pale ambapo usuluhishi umeshindikana na kutoa maamuzi juu ya umiliki wa ardhi kwa mujibu wa ushahidi na mashahidi watakaoletwa barazani kwa kuzingatia sheria.

Baraza lina uwezo wa kutembelea eneo la tukio lenye mgogoro ili kujiridhisha juu ya ukweli wa mgogoro ulioletwa barazani hapo. Ikumbukwe, baraza haliruhusiwi kuchukua ushahidi/nyaraka au kusikiliza mashahidi au kutoa maamuzi) wakati linapotembelea eneo la tukio. Kama kuna uhitaji wowote wa kujiridhisha na jambo fulani, baraza linaweza kumwita mtu huyo barazani kwa ufafanuzi au kuuliza ufafanuzi huo ila usichukuliwe kama ushahidi.

Kwa mujibu wa sheria, baraza lina uwezo wa kusikiliza shauri la mgogoro wa ardhi lisilozidi Sh milioni 3,000,000 kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria namba 2 ya mwaka 2002.

UENDESHWAJI WA MASHAURI KATIKA BARAZA 

Kwa mujibu wa sheria, baada ya kufunguliwa kwa shauri katika baraza, katibu wa baraza anapaswa kumtaarifu mwenyekiti wa baraza na kisha kuandaa wito maalumu kwa pande zote mbili kufika barazani kwa ajili ya kusomwa kwa malalamiko hayo.

Kutohudhuria au kupuuzia wito wa baraza kwa makusudi kama aliyepuuzia wito wa baraza ni mlalamikiwa, shauri litasikilizwa upande mmoja na kama aliyepuuzia wito huo ni mlalamikaji basi shauri litafutwa.

Mashauri yanapaswa kusikilizwa kwa uwazi, hii inamaanisha watu wote wanaruhusiwa kuingia na kusikiliza isipokuwa kama baraza likiona vinginevyo ili kuhakikisha haki inatendeka, linaweza kuzuia baadhi ya watu wasiingie kusikiliza shauri hilo.

MWENENDO WA SHAURI KATIKA BARAZA 

Kwa mujibu wa sheria, baraza halizuiwi na sheria zozote za upokeaji wa ushahidi kama zitumikavyo mahakama nyingine, pia lina uwezo wa kujitengenezea utaratibu wake wa namna ya kupokea ushahidi na kusikiliza mashahidi katika baraza. 

Isipokuwa, baraza haliwezi kujitengenezea utaratibu mbovu wa namna ya uendeshaji wa mashauri, bali wanapaswa kuzingatia utoaji haki na kuhakikisha utaratibu huo unapelekea haki kuonekana inatendeka bila upendeleo.

Kifungu cha 16 cha Sheria namba 2 ya mwaka 2002, baraza lina uwezo wa kuamuru kurudisha eneo la ardhi kwa mmiliki aliyeshinda, kuamuru mdaiwa kutekeleza masharti ya kimkataba, kutoa amri ya zuio la muda au la daima, kumuamuru mdaiwa kulipa kiasi anachodaiwa, kuamuru kulipwa kwa fidia, kuamuru aliyeshindwa kulipa gharama za aliyeshinda za kuendesha shauri zima na amri zingine ambazo kwa mujibu wa sheria wanaweza kuzitoa ili kuhakikisha haki inatendeka.

Endapo upande ulioshindwa hautekelezi amri, basi mtu huyo anaweza kupeleka maombi maalumu ya utekelezaji wa amri kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa mujibu wa kifungu cha 16 (3) cha Sheria na. 2 ya mwaka 2002. Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya litatekeleza hukumu hiyo kwa mujibu wa sheria.

RUFAA

Kifungu cha 20 cha Sheria namba 2 ya mwaka 2002, kimetoa haki ya rufaa endapo mtu au taasisi haijaridhika na uamuzi wa baraza fursa ya kukata rufaa ndani ya siku 45 tangu siku hukumu husika imetoka  kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

UWAKILISHI 

kifungu cha 18 (1) cha Sheria namba 2 ya mwaka 2002, mawakili hawaruhusiwi kumwakilisha mdaiwa yeyote katika baraza. Zaidi, kama anayeshtaki au kushtakiwa ni kampuni, basi mwakilishi yeyote wa kampuni hiyo(isipokuwa wakili) anaruhusiwa kuwakilisha.

Ikumbukwe ndugu wa karibu anaweza kumwakilisha mdaiwa yeyote mara baada ya mdaiwa huyo kuomba na baraza kuridhia. Sababu ni pamoja na kuwa mdaiwa ni mzee sana, anaumwa, kuwepo masomoni, kazi nje ya nchi.

UWAJIBISHAJI WA VIONGOZI WA BARAZA 

Malalamiko ya aina yoyote yanayohusiana na baraza, mlalamikaji anatakiwa kuyafikisha kwa mkurungezi wa jiji au hamlashauri kupitia kwa mwanasheria wa jiji au halmashauri ambaye ndio mamlaka ya nidhamu ya viongozi wa baraza.

CHANGAMOTO

Pamoja na sheria kuwa wazi kwa kiasi nilivyoeleza hapo juu, bado kumekuwa na changamoto nyingi katika uendeshwaji wa mabaraza ikiwemo kutekeleza majukumu nje ya mamlaka zao, kuendesha mashauri ya ardhi hata kama hawana mamlaka nayo, kutoa amri zisizo chini ya mamlaka yao na zisizotekelezeka, kupokea ushahidi na kusikiliza mashahidi wakati wa kutembelea eneo la tukio, kusikiliza mashauri pasipo kuwa na akidi inayofaa kisheria, kutotoa nakala ya hukumu na mwenendo wa shauri kwa wadaiwa kwa sababu zisizo za msingi, kutojali utawala wa sheria, kuhukumu kabla ya kusikiliza pande zote mbili.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).