Home Latest News UTAWALA WA SHERIA UNA TAFSIRI MOJA

UTAWALA WA SHERIA UNA TAFSIRI MOJA

878
0
SHARE

NA HILAL K SUED,

WIKI iliyopita vyombo vinavyosimamia sheria na utoaji haki nchini vilikuwa gumzo kubwa kutokana na yaliyojiri kwenye sherehe za Siku ya Sheria zilizofikia kileleni jijini Dar es Salaam siku ya Alhamisi ambapo Rais Dk. John Magufuli, alikuwa mgeni wa heshima.

Tukiachilia mbali tukio la yule mama aliyeingilia mkutano akiwa na bango lililokuwa na ujumbe ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa unahusiana na kile kilichozungumzwa, medani nzima ya sheria na vyombo vya utoaji haki navyo viliwekwa ‘kizimbani.’

Alianza Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye siku nne kabla katika uzinduzi wa sherehe hizo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwa kuzitaka Mahakama kutoa haki kwa wakati bila kuingiliwa na chombo chochote au mtu yeyote ili kuifanya iweze kuaminiwa na wananchi.

Aliongeza kwa kusema ili Mahakama itende haki kwa wakati, lazima ishirikiane na wadau wote ili kuleta ufanisi. Alisema huo ndio msingi wa amani na utulivu na ndio msingi wa maendeleo.

Huo pekee ulikuwa ni ujumbe mzito na bila shaka umekuja wakati malalamiko mengi kutoka kwa jamii yanainyooeshea vidole tasnia hiyo muhimu katika kulinda amani. Sikumbuki mara nyingine ya mwisho baada ya kustaafu urais, mwanasiasa huyu mkongwe alijionyesha katika ubora wake kikauli.

Na siku ya Alhamisi naye Rais Magufuli alionekana kupigilia msumari suala hilo na hakuongea kiujumla, bali kwa kuyataja maeneo husika yenye mapungufu, ingawa kuna mengine aliyosema yameibua mjadala wa kipekee katika tasnia hiyo ya kusimamia na utoaji haki. Nitalielezea hili hapo mbele.

Kwa hali yoyote ile haya yote ni tofauti kabisa na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo viongozi wa juu katika utawala hupenda kulizunguka hili neno ‘haki’ au kupishana nalo kimakusudi kama vile halipo katika msamiati. Badala yake hupenda kutumia neno ‘amani’ kusisitiza uwepo wa amani na hata kuhimiza sala na maombi katika nyumba za ibada kuliombea taifa amani.

Hivi kweli hawa wanafahamu kwamba hapa duniani hakuna kitu azizi, kitu cha thamani kubwa kama haki? Na tunapozungumzia mataifa mbalimbali na mifumo yao ya tawala, haki huwa ni chimbuko ambalo mema mengine yote huzaliwa na makubwa miongoni mwake ni amani na utulivu.

Na kwa binadamu ambao wana hulka ya udhaifu, vitu hivi huwa ni adimu kuvipata, pembejeo zake huwa ni kazi kubwa kuziingiza kwa sababu haki daima hukinzana na urafiki, udugu na uswahiba na siku zote haki inatakiwa itekelezwe pasipo na macho.

Ni vigumu kuielezea ‘haki’ ni nini, isipokuwa tu katika kuonyesha matokeo yake kwa jamii au kwa mtu au kikundi cha watu fulani. Hii ni pamoja na hali ya kuridhika na kuwepo maelewano au kutokana na ‘amri’ ya kiimani (divine command) au sheria za asili (natural law). Vile vile ni kutokana na suala zima la viwango vya kimaadili (ethical standards) vinavyokuwepo.

Hata hivyo, msisitizo wa kuwepo kwa haki uko katika maeneo mawili; kuitoa kwa hiari (distribution) au kuitoa kama malipo na/au kisasi kwa mabaya mtu aliyotenda.

Eneo hili la pili linahusisha utoaji wa adhabu kwa lengo la kutoa tahadhari kwa wengine au kuwaridhisha wengine ambao waliathirika au wanaofuata sheria. Lakini yote mawili haya pamoja na kuwepo au kutokuwepo kwa uhuru wa mahakama huliweka suala zima la ‘haki’ kutizamwa kwa karibu sana na jamii.

Winston Churchill, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa Vita ya Pili ya Dunia (1939-1945), vita ambayo ilisababisha umwagaji mkubwa wa damu duniani kwa wapiganaji na raia pia aliwahi kunena hivi: “Historia hapa duniani inatukumbusha jambo moja kuu, kwamba wakati mataifa yana nguvu kubwa za kijeshi huwa hayazingatii haki na kwamba wakati yakitaka kuzingatia haki, hujikuta hayana nguvu.”

Na hii ndiyo siku zote imekuwa changamoto (au njiapanda) kubwa kwa binadamu na ni kielelezo tosha cha hali iliyopo sasa hivi, hali ya kutoweka kwa dunia inayosimamia haki.

Kitu kingine watawala wasichopenda ni utawala wa sheria kwa sababu hapo ndipo hasa misingi ya haki hupatikana. Kuna maana gani ya kuwepo kwa Katiba na sheria mbalimbali wakati kwa tafsiri au imani za watawala wanaopaswa kuzifuata ni wananchi tu na si wao? Kwa watawala kutofuata utawala wa sheria ni uminywaji wa haki na kunaweza pia kupoteza amani ya nchi.

Nitatoa mfano. Katika hotuba yake Alhamisi iliyopita Rais Magufuli alitaja kitu kimoja ambacho kimezua gumzo kubwa katika medani ya sheria nchini na inahusu wanasheria binafsi. Miongoni mwa lawama alizozielekeza kwa jamii hii zinahusu wale wanasheria wanaowatetea watuhumiwa wanaokamatwa ‘red handed’ wakati wakifanya uhalifu wao nao wakamatwe na wawekwe ndani.

Misingi ya katiba na sheria haisemi hivyo, mtu yeyote ana haki ya kujitetea (au kutetewa) mbele ya mahakama. Hivyo kwa mantiki hii mtu akimpiga mtu risasi akafa mbele ya mashahidi (red-handed), Serikali huona umuhimu wa kumpatia mtu huyo mwanasheria wa kumtetea kwenye kesi iwapo mwenyewe atashindwa kugharamia. Basi kwanini wauaji wa namna hii wasihukumiwe moja kwa moja bila kesi?

Hata hivyo, mojawapo ya tuhuma alizotoa Rais Magufuli kwa wanasheria wa Serikali ni kushindwa kwao kesi mara kwa mara. Ingawa hakuenda kwa undani sana katika hili lakini ni vyema nikasema hapa kwamba hiyo inatokana na upelelezi na utayarishaji wa kesi. Aidha, kuna suala la kubambikiziwa kesi na au kesi zinazosukumwa kisiasa tu.

Miaka mitatu iliyopita makada kadha wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa nyakati tofauti walifunguliwa mashtaka ya ugaidi yakiwemo ya kula njama kudhuru/kuua na kumwagia mtu mwingine tindikali.

Kesi hizo zilishindwa mahakamani kwa sababu zilionekana kusukumwa kisiasa zaidi na watayarisha mashtaka hawakuisoma vizuri sheria ya ugaidi.

Na kuhusu mapungufu ya utoaji haki kwa upande wa mahakama kama alivyotaja Magufuli Alhamisi iliyopita, linanikumbusha mtikisiko wa kashfa ya Escrow zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Ile orodha iliyotajwa sana ya waliopokea fedha za ufisadi huo walikuwemo majaji wawili wa Mahakama Kuu ambao bado hatujasikia waliundiwa Tume ya Kijaji kuwachunguza. Huenda bado wako kazini na wanaendelea kusikiliza kesi.

Na hata kwa wale ‘wapokeaji’ wengine walishughulikiwa kwa namna tofauti tofauti. Kuna baadhi waliishia kuitwa na kuhojiwa na kamati za Bunge, wengine waliitwa mbele ya Tume ya Maadili na wengine walifikishwa mahakamani. Haikueleweka vigezo gani vilitumika katika mgawanyo huu.