Home Afrika Mashariki UTEGEMEZI WA BAJETI EAC NI UDHAIFU KWA NCHI WANACHAMA

UTEGEMEZI WA BAJETI EAC NI UDHAIFU KWA NCHI WANACHAMA

1429
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU ARUSHA

TANZANIA na Kenya ndio wachangiaji wakubwa wa fedha zinazoiwezesha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) ijiendeshe katika majukumu yake ya kila siku zikifuatiwa na nchi zingine nne. Hata hivyo michango ya nchi hizo pekee haitoshi kuiendesha EAC.

Pamoja na kuwa wachangiaji lakini hata hiyo michango haitolewi kwa wakati hivyo kuwa kikwazo kiasi cha shughuli za kila siku za jumuiya kukwama au kufanyika kwa ufanisi mdogo.

Nchi zote sita, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zinachangia asilimia 40 pekee ya bajeti yote ya kuihudumia na kuendesha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Asilimia 60 inategemea ufadhili kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani na hasa nchi ya Ujerumani.

Ujerumani ndio mshirika namba moja wa EAC na huenda hili ni kwa sababu za kihistoria, na katika kuthibitisha hilo nchi hiyo ndio ilijenga bure hadi kuikamilisha majengo pacha ya makao makuu ya jumuiya hiyo Jijini Arusha.

Huku kuwa tegemezi ni kasoro na wakuu wa nchi wanachama na hasa Mwenyekiti wa sasa ambaye ni Rais wa Tanzania, Dk.  John Magufuli anayejulikana kwa kubana matumizi hakubaliani na utamaduni huu ndio maana alitoa maelekezo kwa sekretarieti kuangalia upya matumizi makubwa yasiyo na tija ya moja kwa moja kwa wananchi ili kupunguza gharama za uendeshaji wake.

Hata hivyo pamoja na utegemezi huo, EAC imeendelea kutekeleza miradi ya pamoja kati ya nchi wanachama kama sehemu ya utekelezaji wa mkataba ulioihuisha tena jumuiya hiyo iliyoanzishwa upya Novemba 30 mwaka 1999 baada ya ile ya awali kuvunjika mwaka 1977 miaka 10 baada ya kuanzishwa.

Miradi hiyo inahusisha miundombinu ya barabara, reli, madaraja, na  vituo vya ushuru wa pamoja (one stop border post). Miongoni mwa miradi mikubwa ni barabara ya Arusha – Namanga mpaka Athi River nchini Kenya, Kituo cha forodha cha Namanga, barabara ya Arusha Holili,Taveta hadi Voi na kituo cha ushuru cha pamoja cha Holili.

Wananchi wa Tanzania kama ilivyo kwa Wakenya, miradi hii ya barabara na vituo hivi vya forodha vinawanufaisha moja kwa moja kama matunda ya kuungana kwao na kuwa sehemu ya wananchi wa EAC.

Biashara na harakati zingine hasa usafiri na usafirishaji kutoka nchi moja kwenda nyingine umekuwa rahisi ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita. Urasimu umepungua kwa kiasi kikubwa, ukaguzi na upekuzi unafanyika kwa pamoja kati ya maofisa wa nchi zote jambo ambalo linaokoa muda mwingi uliokuwa ukipotea kwa ukaguzi na upekuzi.

Hali hii imechangia kuongezeka kwa biashara miongoni mwa nchi hizi, na ndio miongoni mwa faida zilizokusudiwa ambazo wananchi wangezipata.

Zipo changamoto ndogo na kubwa ambazo zimeendelea kuchelewesha kufikiwa kwa malengo hasa masuala ya siasa za ndani za nchi wanachama, hali ya uchumi, siasa, amani na usalama ndani ya baadhi ya nchi  ni kati ya changamoto zinazochelewesha kufikiwa kwa sarafu moja ya jumuiya, hati ya kusafiria, shirikisho la kisiasa na mambo mengine mengi yaliyoandikwa katika mkataba.

Kutokana na changamoto hizo EAC iliunda tume iliyokuja kutoa ripoti maarufu  ya Wako ambayo ilipendekeza kuundwa kwa Wizara maalumu kwa kila nchi ili kazi yake iwe ni kushughulikia masuala ya EAC. Kwa mujibu ripoti hiyo ilielezwa kuwa wananchi wengi bado hawaelewi faida ya uharakishwaji wa shirikisho la kisiasa.

Uelewa wa wananchi ni mdogo katika kujua dhana nzima ya EAC, wajibu na haki zinazopatikana, jukumu la kutoa elimu, kuhamasisha wananchi kuipenda EAC ndio ikawa kazi ya kwanza na muhimu kwa Wizara hizo, lakini ukosefu wa fedha au bajeti ndogo inayotengwa kuzihudumia imekuwa kikwazo cha kufanikisha jukumu hilo.