Home Habari UTENGAJI KATA KUGAWA WANANCHI MULEBA

UTENGAJI KATA KUGAWA WANANCHI MULEBA

3150
0
SHARE

MACHO yameona kuna dalili za wananchi wa  kata za Kagoma na Kikuku waishio wilaya ya Muleba Mkoani Kagera kugawanyika kutokana na kile wanachokiita ukiukwaji wa taratibu a kuwatenganisha.

Malalamiko makubwa wanayoelekeza kwa Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, Chrisant Kamugisha ambaye pia ni Diwani wa Kata mpya ya Kikuku.

Kamugisha anadaiwa kukiuka utaratibu wa kushughulikia mchakato wa upatikanaji wa kata  mpya  ya Kikuku

Baadhi ya wajumbe wa serikali za vijiji kutoka katika kata ya Kagoma wamesema tayari wameshamwaandikia barua Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakitaka mchakato uanze upya.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsisha kata ya Kagoma Ziadi Ramadhani anasema mwenyekiti wa halmashauri hiyo hakufuata utaratibu kwa kuitisha mikutano ya vijiji katika kupatikana kata mpya ya Kikuku hivyo wananchi walio wengi wamegawanyika

“Mimi ni kiongozi, tulishangaa kusikia kuna mikutano inaendeshwa bila utaratibu. Kuna baadhi ya wananchi wangu waliletewa fomu wazijaze usiku ili kuonyesha kwamba kulikuwepo na mikutano iliyohalalisha kupatikana kwa kata hiyo mpya” anasema

Anasema kinachosikitisha huduma zote za kijamii na vyanzo vingi vya mapato vimeondolewa kutoka upande wa kata mama ya Kagoma na kupelekwa upande wa Kikuku ambako Kamugisha ndiye diwani wake.

“Inasikitisha kuona shule yetu ya sekondari, shule ya msingi, zahanati na baadhi ya mialo inayoongoza kwa kuongeza mapato katika maeneo yetu vimechukuliwa,”alisema

Salumoni Msasa anasema ni aibu kuona kwamba kata yao ya Kagoma imeondolewa vijiji vyake kutoka 8 na kubakia vitatu huku akisisitiza kwamba utaratibu wa namna hiyo hajawahi kuona.

“Sisi huku Kagoma tumebakia na vijiji vitatu. Tulikuwa tayari tumepima viwanja kwa ajili ya mji mdogo wa Kagoma, lakini vyote vimechukuliwa. Uliwahi kuona wapi hali hiyo?. Kata mpya ya Kikuku imepewa vijiji vitano vyote vina miundombinu na huduma za jamii,” alisema.

Kamugisha amekiri kuwepo malalamiko hayo lakini akasema mchakato huo unafanyiwa mapitio upya ingawa alisisitiza kwamba hakuhusika badala yake anaamini utaratibu ulifuatwa

“Utaratibu ulifuatwa, ingawa inaonekana watu wanataka kunidhalilisha. Ni kweli Kagoma imebakiwa na vijiji vitatu, lakini miundombinu mingine ipo.

“Ni ajabu na hatari tupu, badala ya kujadili maendeleo, sisi tunajadili malumbano na kejeli. Ngoja tuachie taasisi husika zifanye kazi zake na mimi nitakuwa tayari kwa chochote kitakachopatikana,” alisema.

Aliongeza anashangaa kuona watu wanasema vyanzo vya mapato vimechukuliwa huku wakijua wanachokisema si cha kweli kwani miundombinu ipo kata zote

“Wanasema wamejenga shule , hiyo shule ya sekondari imejengwa na serikali na hiyo shule ya msingi ni ya Kanisa la KKKT. Wanasema mialo, kule Kagoma wana mialo kama ilivyo Kikuku kwa hiyo ngoma droo” anasema

Mkuu wa wilaya ya Muleba Henry Ruyango alisema amekuwa akizisikia taarifa hizo ila hajapata malalamiko rasmi katika ofisi yake ingawa amesisitiza kuchukua hatua kama atapata rasmi malalamiko hayo.

“Nimezisikia sijapata rasmi malalamiko hayo ili nitashugulikia ingawa niliwahi kumwambia mwenyekiti wa halmashauri atafute namna ya kusikiliza wananchi wake kwa sababu yeye ndiye anayelalamikiwa na atafute suluhisho kwenye jambo hilo.”