Home Habari kuu Uthibiti ubora wa elimu Nyamagana ulivyoimarika

Uthibiti ubora wa elimu Nyamagana ulivyoimarika

1063
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

BAADHI ya wananchi bado hawafahamu umuhimu wa uthibiti ubora unaofanywa na Idara ya Uthibiti ubora wa shule za msingi hapa nchini.

Katika moja ya maboresho ya elimu nchini yanayoendelea kufanywa na Serikali, ni pamoja na kuunda idara ya Uthibiti ubora. Mthibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Nyamagana, Simforose Kinanga anazungumza na mwandishi NASHON KENNEDY kuhusu shughuli za Idara, utendaji, mafanikio na changamoto katika halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Swali: Unaweza kueleza ni majukumu yapi ya idara ya uthibiti ubora wa elimu hapa nchini?

Jibu: Katika kutekeleza majukumu yake kulingana na sheria Na.25 ya mwaka 1978 na rekebisho lake kipengere na. 10 ya 1995, Idara ya Uthibiti ubora ina majukumu mengi, lakini nitataja machache.

Moja ya jukumu la idara ni kuandaa mpango wa mwaka mzima unaoonesha majukumu ya kazi, zitakazofanyika na kupeleka wasimamizi wa elimu ngazi ya kata, wilaya na mkoa.

Majukumu mengine ya idara ni kukagua na kuzisimamia shule na asasi zote ili kuhakikisha kwamba sheria, kanuni, taratibu na nyaraka zote za elimu zinatekelezwa ipasavyo, kusimamia utekelezaji wa mtaala, kuthamanisha na kutathimini mwenendo mzima wa utoaji elimu katika ngazi ya awali hadi vyuo vya ualimu (monitoring, assessment and evaluation), kuongoza, kuelekeza na kusimamia uendeshaji wa shule ikiwa ni pamoja na mwenendo wa utawala, taaluma, afya, mazingira, nidhamu ya walimu na wanafunzi mtaala usio rasmi, michezo, utamaduni, dira na dhima ya shule, vyama vya masomo na mahusiano mazuri na jamii inayoizunguka shule.  

Majukumu mengine ni pamoja na kuhakikisha kuwa walimu wanafundisha kwa kuandaa vipindi vyote vya masomo walivyopangiwa, kufaragua zana za kufundishia na kujifunzia na kuwaelekeza wanafunzi kwa juhudi, maarifa na weledi, idara pia inawajibika kuwabaini walimu dhaifu ili kuwaelekeza kwa kuwezesha na kuseminisha ndani ya shule, kata na wilaya kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwabaini walimu mahiri na kuchukua majina yao na kuyaorodhesha katika benki ya viongozi watarajiwa wa idara ya elimu sanjari na kuwaandikia barua za pongezi pale wanapofanya kazi bora.

Kufanya ukaguzi kwa wingi zaidi katika shule 20 za mwisho katika mitihani ya darasa la IV na VII kitaifa ili kuweka mikakati rekebishi na endelevu itakayoweza kusaidia shule kujiondoa katika hali duni na kupanda kitaaluma na jukumu ni kufanya vikao na walimu, viongozi wa kata, kamati za shule na halmashauri ili kuhabarishana mambo mambo mazuri yaliyojitokeza katika asasi baada ya kukaguliwa ili kushirikiana kuyaboresha zaidi na yale ambayo ni duni kupanga mikakati ya kuyaondoa ama kuyaboresha.

Swali: Katika kipindi cha robo mwaka kilichopita, idara imeweza kutekeleza mambo gani ya msingi katika suala zima la uthibiti kwa halmashauri yako?

Jibu: Idara ililenga kufanya tathimini ya jumla ya shule za awali na msingi 17 na ufuatiliaji shule tatu katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, lakini kutokana na maelekezo yanayotolewa na wafadhili ya lipa kutokana na matokeo (EP4R), idara ilifanya tathimini ya jumla ya shule 33, 17 zikiwa za Serikali na 16 hazikuwa za Serikali na kufanya jumla ya shule 36 kufanyiwa tathimini katika kipindi hicho.

Swali: Baada ya tathimini hiyo hali ya utekelezaji ilikuwaje?

Jibu: Shule nyingi zimebainika kufanya vizuri kwenye maeneo ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la elimu ya awali na darasa la kwanza ambapo uandikishaji huo ulivuka lengo na walimu wengi wameishapata uelewa kuhusu mabadiliko ya mtaala wa elimu wa mwaka 2014.

Swali: Je, ni dosari gani mlizibaini katika kipindi hicho?

Jibu: Tulibaini shule kuwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa kwa uwiano wa 1:170-200, yaani darasa moja linaweza kuwa na idadi ya wanafunzi kati 170- 200.

Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa mtaala, hivyo kushusha taaluma ya wilaya na mkoa kwa ujumla.

Dosari nyingine tuligundua baadhi ya shule hazijabainishwa mipaka yake hali inayosababisha mwingiliano na jamii na hivyo kusababisha migogoro baina ya shule na jamii, shule kutokuwa na matundu ya choo ya kutosha mfano Shule ya Msingi Mabatini tumeikuta tundu moja la choo linatumiwa na wanafunzi 145, Shule ya Ibanda wanafunzi 123 kwa tundu moja la choo, hali inayosababisha usumbufu na utoro kwa wanafunzi.

Dosari nyingine tulizobaini ni shule kukosa ushirikiano wa kamati za shule na jamii mfano Shule ya Mwananchi na Nyamagana B hali inayosababisha ufaulu duni.

Baadhi ya shule pia tulizibaini kutokuwa na ofisi za walimu zikiwemo shule za Mabatini, Ibanda na Igogo B hali inayowafanya walimu kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na pia tulibaini shule za msingi za Iseni, Nyasubi, Sweya, Nyamagana na Igelegele kutokuandaa mpango wa jumla wa maendeleo ya shule na shule ya msingi Bujingwa ilikutwa kutokuwa na walimu wa kike.

Swali: Kama idara ya uthibiti ubora mna kitu gani cha mafanikio cha kujivunia?

Jibu: Idara katika kipindi cha Julai-Oktoba mwaka jana, iliweza kukagua shule kwa mfumo mpya wa shule kujitathimini yenyewe na kisha kukaguliwa na wathibiti ubora wa shule. Katika kipindi hicho, shule 38 zilifanyiwa tathimini ya jumla kwa kukaguliwa kwa siku tatu mfululizo kwa kila shule kupewa ushauri.

Kaguzi hizo zimefanyika kwa asilimia 200 kulingana na mpango kazi, kwani idara ilipanga kukagua shule 19 tu katika kipindi hicho. Jambo hili limewezekana kwa uwepo wa gari EDPF 1754 lililofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali (LANES).

Aidha Mpango wa EP4R, ulitoa fedha Sh 17,000,000 kwa ajili ya posho za watumishi na mafuta kwa mwezi Juni jambo ambalo lilisaidia na ushirikiano mzuri wa watumishi.

Aidha tangu mwaka 2016 hadi sasa idara imewezesha kusajili shule 16 mpya zisizo za serikali na inaendelea kuzisimamia ili ziweze kuimarika na kufuata sheria za elimu ili kufaulisha wanafunzi kwa kiwango cha kufikia utepewa kijani. Idara pia imeweza kusaidia usajili wa vituo 18 vya elimu masafa na ana kwa ana, visivyo kwa Serikali kwa kushirikiana na taasisi ya elimu ya watu wazima Mkoa (EWW).

Swali: Idara inakabiliana na changamoto gani?

Jibu: Idara imebaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya utoro kwa shule zilizokaguliwa kwa asilimia 35, tulibaini asilimia 60 ya walimu kutokuandaa vipindi vyao vyote vya masomo na pia walikuwa hawatumii zana za kufundishia na kujifunzia.

Baadhi ya walimu wakuu kutotimiza wajibu wao na baadhi ya wadau wa shule tarajiwa kwa shule zisizo za serikali, kuvunja sheria kwa kuwaweka wanafunzi kwenye shule ambazo hazijapata usajili kwa kisingizio cha masomo ya ziada na ‘day care’.

Swali: Mna mikakati gani ya kukabiliana na changamoto hizo?

Jibu: Mkakati uliopo ni kuhakikisha walimu wakuu kuwasimamia walimu wote, ili waweze kuandaa masomo yao kwa asilimia 100. Tumeelekeza walimu watakaoshindwa kutekeleza vema majukumu yao wapewe barua za onyo na waajiri wao.

Mkakati mwingine ni kwa kamati za shule na zile za maendeleo ya kata zikomeshe tabia za wizi wa vifaa vya shule kwa kuwapeleka wanaohisiwa wezi kwenye vyombo vya sheria kwa uchunguzi.

Aidha idara inatoa pongezi kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, kwa ushirikiano wanaoipatia idara na watendaji wengine kutoka idara ya elimu, viongozi wa kata, waratibu elimu kata, walimu wakuu, wadau wa elimu na wananchi.