Home Tukumbushane Utozaji kodi- mradi mkubwa kwa serikali zote duniani

Utozaji kodi- mradi mkubwa kwa serikali zote duniani

2963
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Wiki iliyopita kuliibuka mtafaruku mkubwa nchini pale serikali ilipotangaza kampeni kabambe dhidi ya wamiliki wa visima vya maji wasiovilipia kodi ambavyo pia vilipaswa kuombewa vibali. Serikali ilisema suala hilo linatokana na sheria iliyopo kwa miaka mingi tu chini ya mamlaka ya Bonde la mito Wami na Rufiji kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji.

Watu walionekana kuuliza – hata visima vya maji vinatakiwa vilipiwe? Iko wapi ile kauli mbiu ya “Maji ni Uhai?” Hata hivyo sheria ni sheria tu na inawezekana wengi wetu hawakufahamu uwepo wa sheria hiyo na mamlaka husika pia ilikuwa kimya sana hadi juzi tu kuibuka ghafla.

Baadaye serikali, kupitia Katibu Mkuu Wizara ya Maji Kitila Mkumba alijitokeza na kufafanua kwamba ni visima vya urefu upi hasa na kwa matumizi gani ndiyo vinapaswa kulipiwa, lakini bado kuna watu waliendelea kulizungumzia suala hilo kupitia mitandaao ya jamii na sehemu nyingine.

Ikumbukwe kwamba zaidi ya muongo mmoja uliopita na kurudi nyuma jiji la Dar es Salaam na vitongoji wake lilikuwa na tatizo kubwa sana la uhaba maji chini ya iliyokuwa mamlaka ya maji wakati huo – NUWA – hadi ikapelekea kwa serikali kuibinafsisha NUWA kwa kampuni ya nje – City Water, ambayo nayo ilishindwa kurejesha huduma za maji za kuridhisha.

Watu wengi waliamua kuchimba visima katika maeneo yao – virefu na vifupi – kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani na kujengea nyumba. Pengine magorofa mengi mapya ya Kariakoo na sehemu nyingine yasijengwa bila ya visima vilivyochimbwa katika maeneo yake.

Na wakati huo huo wakazi wengi wa kawaida jijini hapa katika maeneo ambayo mabomba ya Dawasco yalikuwa yamekauka walipata maji kutokana na visima hivyo, huku baadhi ya wamiliki hao wakiwagawia bure majirani zao na wengine kuwalipisha. Kwa wamiliki wa visima waliokuwa wakiwauzia wengine maji kupitia miundo mbinu yao waliyoweka hadi kwa wateja wao Dawasco iliwabana kujiandikisha kwao na kuwalipisha ushuru.

Aidha tusisahau kwamba visima hivi vilileta ajira kwa vijana wasiokuwa na kazi kwa kusambaza maji kwa wakazi katika madumu kwa kutumia matololi. Sasa inawezekana baada ya Dawasco kurejesha huduma ya maji kwa wateja wengi ndiyo serikali imekuja na kampeni hii? Lakini wengi wanasema suala la msingi hapa ni kodi tu kwa serikali. Juzi juzi tu kulikuwapo habari kwamba hata mafundi wa simu na watengeneza radio wanatakiwa kukatia liseni shughuli zao na kulipia kodi.

Inasemekana hakuna kitu kisichotozwa kodi hapa duniani – labda hewa tunayopumua, ingawa sina hakika sana katika hili pia. Kutokana na hili, kodi zimetengeneza wahalifu wengi kuliko sheria yoyote ile serikali inayotunga.

Siku zote serikali huhakikisha hakuna shughuli yoyote ya binadamu katika dunia hii ambayo haiitozi kodi, kuiwekea liseni, kuisimamia na kuidhibiti. Hali kadhalika serikali huhakikisha raia wake wote waitumikie, ama kwa kuwamo katika orodha yake ya waajiriwa, au katika orodha yake ya walipa kodi wake.

Inasemekana kwamba wakati ukiwadia hatimaye kwa wanyonge kuutawala ulimwengu, wataukana kwa sababu kodi zitakuwa kubwa mno. Hii inadhihirishwa kutokana na kwamba utajiri umeanishwa kama kitu batili – na kimewekwa katika maandiko mawili muhimu – misahafu ya Mwenyezi Mungu na sheria za kodi.

Kodi ndiyo imekuwa suala ambalo serikali zote duniani zinalifukuzia tangu dunia ilipoumbwa, na ni suala ambalo ndilo hulisimamia vyema pengine kuliko masuala mengine yote katika nchi.

Ili kuonyesha inakwenda na wakati – katika enzi hizi za teknolojia, zimeanzishwa mashine maalum kwa wafanyabiashara – EFD – kuhakikisha inakusanya kodi iliyo sahihi bila kukwepa. Suala hili la EFD lilizua mgogoro mkubwa sana baina ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na wafanyabiashara.

Kuna baadhi ya watu wanasema kwamba kwa nini serikali yetu pia isitafute na kuweka mashine, mithili ya EFD – kwa ajili ya kuhakikisha inatumia vyema kodi inayokusanya?

Lakini kwa serikali yetu, naweza pia kuongezea kusema kwamba hata misamaha ya kodi inasimamiwa vyema, pamoja na kelele nyingi kutoka kwa watu mbali mbali wakiwemo Wabunge, kwani hadi sasa misamaha inaendelea kutolewa pamoja na ahadi za mara kwa mara za kuisitisha.

Lakini katika suala la serikali kusimamia vyema ulipaji kodi kuliko kusimamia vitu vingine serikali mara kwa mara imekuwa ikithibitisha hilo kwa wananchi wake kwa kutangaza kuongezeka kwa ukusanyaji kodi katika miaka ya hivi karibuni.

Ninadiriki kusema kwamba idadi kubwa ya wananchi hawashabikii sana hayo mafanikio yake katika ukusanyaji kodi. Kwa upande mmoja tunaweza kusema serikali inafanya hivyo kwa sauti mbili: Moja kama mkusanyaji mkubwa wa kodi na pili kama mfujaji mkubwa wa kodi hizo. Lakini hilo la pili ndilo linaonekana kero kubwa sana kwa wananchi.

Kwa wananchi wengi, serikali yaweza kutaja takwimu zote inazotaka kutaja, lakini hizo zitabakia hivyo hivyo – yaani takwimu tu, na hasa iwapo hazionekani kusaidia sana katika kuboresha maisha yao.

Benjamin Disraeli – mwanasiasa mashuhuri Mwingereza katika Karne ya 19 aliwahi kunena “Kuna aina tatu za udanganyifu: Udanganyifu, udanganyifu uliokithiri na takwimu.

Nukuu hii ya nusu kejeli inaelezea ‘nguvu’ ilioko nyuma ya tarakimu, na kwamba hata takwimu zilizo sahihi namna gani zaweza kutumika kuzipa nguvu zile hoja zisizo sahihi.

Kwa ujumla ni kwamba ukusanyaji kodi ni kitu kimoja, na kusimamia matumizi ya kodi hiyo ni suala jingine kabisa, na ni suala ambalo limekuwa likiiweka serikali hii miongoni mwa zile ambazo usimamizi wao ni mbovu.

Ubovu huu unathibitishwa bila ya chembe cha shaka na ripoti za kila mwaka za Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) ambazo zinatabainisha kwamba hali inazidi kuzorota mwaka hadi mwaka.

Na serikali kamwe haiwezi kusita kuanzisha kodi nyingine ikibidi, kama vile ilivyojaribu kuweka kodi ya kila mwezi kwa wamiliki wa simu za mkononi au kodi iliyomo katika manunuzi ya umeme wa LUKU kwa ajili ya kusaidia miradi ya kupeleka umeme vijijini.