Home Latest News UTURUKI: Jaribio la mapinduzi kumpa nguvu Erdogan

UTURUKI: Jaribio la mapinduzi kumpa nguvu Erdogan

946
0
SHARE
Reccep Tayyip Erdogan

NA HILAL K SUED,

Nchi ya Uturuki ina historia kubwa. Kwa zaidi ya miaka 600 kuanzia karne ya 12 ilikuwa kitovu cha Dola ya Ottoman iliyotawala maeneo mengi ya Mashariki ya Kati, Afrika ya Kaskazini na Ulaya pia na ilikuja kusambaratika mapema karne iliyopita tu — mwaka 1922.

Iliweza kuwa kitovu cha dola hiyo kubwa kutokana na mahali ilipo katika ramani ya dunia – yaani kati ya mabara ya Asia na Ulaya, hivyo kuwa kiunganisho cha biashara na staarabu mbili za mabara hayo mawili yenye historia kubwa.

Ni nchi ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa ikisikika sana – hasa baada ya ujio madarakani kwa kiongozi wa sasa, Reccep Tayyip Erdogan aliyeingia madarakani kwa kura kama Waziri Mkuu mwaka 2003. Chama chake, AKP kilishinda uchaguzi pamoja na kwamba kilikuwa na mlengo wa Kiisilamu. Katiba ya nchi hiyo inakataza vyama vyenye mafungamano ya kidini.

Baada ya vipindi vyake viwili vya miaka 10 Erdogan alisukuma Bungeni mabadiliko ya katiba na kuanzisha nafasi ya urais wa mamlaka kamili (Executive President) na katika uchaguzi wa 2014 chama chake kilishinda na yeye kuwa Rais wa 12 wa nchi hiyo.

Huko nyuma – mwaka 1923 – yaani baada ya kusambaratika rasmi kwa Dola ya Ottoman na kuanzishwa rasmi kwa nchi ya Uturuki kama inavyojulikana sasa, marais walikuwepo lakini hawakuwa na mamlaka kamili – shughuli zote za kiserikali zilifanywa na Waziri Mkuu.

Kwa ujumla Erdogan amekuwa akipambana na upinzani mkubwa – hususan siku hizi za karibuni na hasa hasa namna hali ya kisiasa Mashariki ya Kati ilivyobadilika kutokana mapigano nchini Syria na Iraq – nchi ambazo inapakana nazo.

Tukiachilia mbali wale wapiganaji wa Kikurdi wanaopigania kujitenga na kutaka nchi yao – Kurdistan – kuna hawa wa ‘Dola ya Kiislamu’ ISIS (au ISIL) ambao kuanzia miaka mitatu iliyopita walitwaa maeneo mengi ya Iraq na Syria ingawa sasa wapiganaji hao wanaanza kurudishwa nyuma. Hivyo vurugu hizo za kijeshi mara nyingine zimekuwa zikuvuka mipaka na kuingia Uturuki.

Aidha wapinzani wa Erdogan wamekuwa wakishirikiana na wapiganaji wa ISIS kufanya mashambulizi nchini Uturuki katika miji kadha ikiwemo mji mkuu wa Ankara hali kadhalika Istanbul na kuleta wasiwasi mkubwa kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kukosa ulinzi. Kwa mfano mashambulizi ya kigaidi katika uwanja wa ndege wa Istanbul tarere 28 Juni yalisababisha vifo vya watu 45, na wengi kujeruhiwa.

Hali kadhalika kuanzia mwaka 2013 kumekuwepo nchini humo misuguano ya ndani kwa ndani ya kijamii na ya kisiasa ambapo maandamano makubwa yalikuwa yakifanyika kupinga ufisadi, ukandamizaji na hali ngumu ya maisha, achilia mbali ile ya kukosekana kwa hali ya usalama kama nilivyotaja. Maandamano dhidi ya ufisadi yaliwang’oa mawaziri watatu wa Erdogan.

Hata hivyo si wananchi wengi wa Uturuki waliweza kufikiria nchi kukumbwa na jaribio la mapinduzi ya kijeshi kama hili hivi karibuni. Hii ni kwa sababu mahusiano kati ya serikali na majenerali wa jeshi la nchi hiyo yalianza kuimarika chini ya Erdogan baada ya mikiki mikiki ya uingiliaji wa jeshi katika masuala ya siasa kama ilivyokuwa wakifanya – kwa kisingizio cha kuilinda Katiba ya Uturuki inayosisitiza utawala ki-secular.

Aidha Erdogan aliwaachia huru majenerali kadha wa jeshi waliokuwa wamehukumiwa vifungo gerezani. Lakini wiki iliyopita kumetokea uvumi nchini uliokuwa ukienea kwa kasi katika mitandao ya kijamii kwamba jaribia hili la mapindizi lilikuwa limepangwa tu na Erdogan mwenyewe kwa lengo la kutaka kujijiengea umaarufu. Utawala wake umesema utawasaka wote waliohusika kueneza habari hizo alizoziita za ‘uwongo’.

Mara ya mwisho mapinduzi ya kijeshi kutokea nchini Uturuki yalikuwa mwaka 1980 pale Mkuu wa Majeshi, Ahmet Kenan Evren alipoupindua utawala wa kiraia wa Rais Suleyman Demirel na Waziri wake mkuu Bulent Ecevit. Mapinduzi hayo ya kijeshi yalikuwa ya tatu tangu taifa hilo lilipoanzishwa mwaka 1923 – mengine yalitokea 1960 na 1971.

Evren alitawala kijeshi hadi 1983 kuliporejeshwa utawala wa kidemokrasia ambapo aligombea urais na kushinda kwa asilimia 90. Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kufanyika mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo na kupitishwa kwa kura ya maoni, kura ambayo kukubalika kwake kulikumbwa na utata mkubwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema jaribio la mapinduzi la hivi karibuni litaleta mtikisiko mkubwa wa aina yake nchini Uturuki. Iwapo Erdogan atarejesha hali ya utulivu, basi ataibuka kuwa na nguvu zaidi na ari zaidi ya kupambana na wapinzani wake wa kisiasa, na hasa kutokana na ile hatua yake aliyochukua ya kubadilisha katiba kwa lengo la kuwepo kwa Urais wa mamlaka kamili (executive president).

Tangu aingie madarakani Erdogan amejijengea umahiri mkubwa wa kupambana na wapinzani wake mbali mbali, ndani na nje ya nchi. Hata hivyo kwanza kabisa itabidi alisafishe jeshi ambalo ndiyo lilijaribu kumng’oa madarakani.

Historia inaonyesha kwamba wananchi wanaona utawala wa kijeshi siyo mbadala mzuri wa utawala kama ilivyokuwa hapo zamani na kwamba waliohusika ni maafisa wachache tu wa jeshi hilo. Lakini ‘wachache’ hawa waliweza kuratibu na kuhamasisha askari wengi na silaha nzito nzito hususan katika miji ya Ankara na Istanbul. Kule Ankara ndege za kijeshi za waasi zilishambulia majengo ya Bunge la nchi hiyo na majengo mengine.

Hasira zake nyingine zitaelekezwa kwa kikundi cha Kiisilamu kinachoongozwa na Fethullah Gulen, ambaye hapo awali alikuwa swahiba wa Erdogan na ambaye alimsaidia sana kuingia madarakani lakini wakaja kufarakana mwaka 2013. Sasa hivi Gulen yuko uhamishoni nchni Marekani. Serikali ya Erdogan inasema mkono wa Gulen unaonekana sana katika jaribio hili la mapinduzi ingawa yeye anakanusha kata kata kuhusika.

Mapema mwaka huu serikali ya Uturuki ilikitangaza kikundi cha Gulen kuwa cha kigaidi na tayari kiongozi wake mmoja na swahiba wake mkuu Halis Hanci amekamatwa. Alikuwa amerudi Uturuki kutoka nje siku mbili tu kabla ya jaribio la mapinduzi. Aliyekamatwa pia ni mwipwa wake – Muhammet said Gulen pamoja na mamia ya wafuasi wengine.

Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim aliitaka serikali ya Obama kumrejesha mara moja nyumbani Gulen na kuongeza kwamba “nchi yoyote iliyo nyuma ya mtu huyu kamwe si rafiki wa Uturuki.”

Wachunguzi wa mambo wanaona kauli hii inaashiria kuzuka kwa hali kubwa ya sintofahamu baina Uturuki na Marekani – nchi mbili ambazo zimo katika Umoja wa Kujihami wa Nchi za Ulaya na Marekani – NATO.

Makala hii imetayarishwa kwa msaada wa vianzo mbali mbali vya Intaneti.