Home Latest News Uvumbuzi wa niobium tusipojiandaa tutajuta

Uvumbuzi wa niobium tusipojiandaa tutajuta

996
0
SHARE
Mabomba yaliyotengenezwa kwa kutumia madini ya Niobium.

MOJA ya mambo ambayo tumekuwa na bahati nayo kama Taifa ni hazina kubwa ya madini pamoja na vivutio vya asili vya kimaumbile ambavyo ni lulu.

Tumebahatika kuwa na mlima mrefu kushinda yote katika Bara la Afrika, Kilimanjaro pamoja na mito na mabonde mengi ya kumfanya mtu aliyepo maelfu ya kilomita ughaibuni kuamua kujibana hadi atutembelee.

Wageni wanaokuja nchini wanakuja kushuhudia hayo maajabu ya maumbile kwa macho yao. Hawa tunawaita watalii wa kawaida.  Lakini kuna kundi lingine la watu ambao huja nchini kutokana na sababu hiyo hiyo ya kuona kile tulichotunukiwa na Mungu lakini kwa lengo si la kujifurahisha na kukata kiu yao ya kutaka kujua, la hasha. Hawa kinachowaleta ni masilahi ya kiuchumi. Wanafuata rasilimali zetu tulizopewa na Mungu.

Hili ni kundi la watu wanaokuja nchini kwa ajili ya kunufaika kiuchumi. Kinachowaleta ni masilahi hayo ndiyo yanayowaondoa pia nchini.

Ugunduzi wowote wa madini katika ardhi ya Tanzania ni mwaliko usio rasmi kwa wanaotaka faida ya kiuchumi kuja nchini. Na hili hivi sasa tayari limekuwa ni jambo la kawaida na Watanzania hawashangai kuona kila aina ya watu kutoka katika kila kona ya dunia. Ili mradi kila mmoja anakuja kutaka kufaidika.

Kwa mara nyingine tena nchi yetu imebahatika kuwa na madini adimu sana duniani kama ilivyobahatika kuwa na madini ya Tanzanite. Madini yenyewe yanaitwa niobium (inatamkwa nai-yo-biam). Hapana ubishi kwamba madini haya yanatafutwa sana duniani. Hivi sasa yanapatikana na kuchimbwa Brazil na Canada tu ingawa pia yanapatikana katika baadhi ya nchi za Afrika.

Uvumbuzi huu wa niobium ni wa kwanza duniani kote katika kipindi cha miaka 40.

Haya ni madini ambayo kila mtu anataka kuyanunua. Kwanini yanathaminishwa juu kiasi hicho hata kushinda madini yaliyozoeleka kwa karne kadhaa kama shaba? Nini kinayafanya madini hayo kuwa na thamani mara saba zaidi ya shaba tuliyoizoea?

Mwaka jana katika soko la dunia thamani ya madini ya niobium (inatamkwa nai-yo-biam) ilikuwa ni wastani wa dola za Marekani 40 kwa kilo moja. Linganisha na shaba ambayo thamani yake ilikuwa ni dola za Marekani 6 kwa kilo moja.

Madini haya ambayo jina lake limetokana na mungu wa kike wa Kigiriki aliyekuwa ishara ya mama mwombolezaji yanatumika kwa ajili ya kuzalisha chuma cha pua ngumu zaidi na nyepesi kwa ajili ya mabomba ya viwandani na kutengenezea vifaa vya kuundia ndege na huchimbwa sehemu tatu tu duniani kote.

Ni madini yenye umuhimu wa kipekee katika mapinduzi na maendeleo ya viwanda duniani na ndiyo sababu yalipothibitika kwamba yanapatikana nchini Tanzania vyombo vya habari vinavyoandika kuhusu uchumi na maendeleo ya madini kote duniani vilielekeza kalamu na kamera zao huku kwetu. Ni uvumbuzi mkubwa. Pamoja na kwamba kwa mara ya kwanza madini haya yalivumbuliwa mwaka 1801 na kupewa jina la columbium.

Niobium yanaangukia katika kundi la madini adimu ya ardhini pamoja na tantalum madini ambayo bila hayo mapinduzi katika sekta ya elektroniki pengine yasingeweza kufikia hapa yalipofika.

Brazil ndiyo inayoongoza duniani katika uzalishaji wa niobium kwa kutoa asilimia 85 ya mahitaji ikifuatiwa na Canada.

Marekani na Ulaya kwa zaidi ya miaka 30 sasa hazizalishi kabisa madini hayo pamoja na kwamba yanahitajika sana kwa ajili ya maendeleo ya viwanda hususan katika utengenezaji wa ndege na roketi. Na hata ikipatikana katika nchi hizo huwa ni kiwango cha chini sana cha ubora.

Kutokana na umuhimu wa madini hayo China, Japan na Korea ya Kusini zimelazimika kila moja kuilipa Brazil kiasi cha dola za Marekani bilioni 2 kwa ajili ya kujihakikishia upatikanaji wa niobium. Yote hiyo imefanyika kama njia ya kuzuia wateja wengine wakubwa kuingilia katika mtiririko wa upatikanaji wa madini hayo.

Moja ya sababu za nchi hizo kuitaka niobium kwa udi na uvumba ni kutokana na matetemeko ya ardhi ambayo yamekuwa yakiharibu miundo mbinu na kuua watu.

Niobium inahitajika kwa ajili ya kuzalisha chumba kigumu na chepesi kinachonyumbulika kirahisi ambacho ni muhimu katika ujenzi wa nyumba na miundombinu katika nchi hizo zilizo katika ukanda wa matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara.

China ndiyo inayoongoza duniani kwa matumizi ya niobium na nchi hiyo haizalishi madini hayo kwa kiwango chochote kile hivyo hutegemea kuiagiza kutoka nje.

Ni kutokana na unyeti wake ndiyo sababu mwaka 1974 likaundwa shirika lisilokuwa la kiserikali la kimataifa na kusajiliwa huko Ubelgiji kwa ajili ya kuratibu madini hayo. Shirika hilo liitwalo The Trade Association for the Global Tantalum and Nobium Industries limelenga katika kufuatilia na kudhiditi mlolongo wa upatikanaji wa madini hayo.

Asasi hiyo ambayo itakuwa na mkutano wake mkuu wa 57 huko Toulouse, Ufaransa Oktoba 16-19, 2016 inafuatilia uchimbaji, biashara, uyeyushaji, uzalishaji wa chuma, uzalishaji wa kapasita, na matumizi mengine kama ya kutengeneza vifaa vya tiba, utengenezaji wa vyombo vya anga kama ndege na maroketi.

Wakati tukijiandaa kuyachimba madini hayo ni vizuri asasi zetu zinazohusika na madini hususan wahandisi na wachumi wakajiandaa vyema katika kutetea masilahi ya Taifa letu.

Aidha, ni jambo jema kujiandaa kwa kutambua nafasi ya madini hayo katika soko la dunia na kuona ni kwa njia gani sisi tunaweza kufaidika na mradi wowote ule utokanao na madini hayo kuchimbwa.

Wataalamu wetu hawana budi kujizatiti na kuhakikisha kwamba wanakaa katika mstari unaotakiwa kutetea maslahi ya taifa letu.