Home Latest News UVUVI HARAMU: Uhaba wa samaki wakubwa waanza kuinyemelea Tanzania

UVUVI HARAMU: Uhaba wa samaki wakubwa waanza kuinyemelea Tanzania

1875
0
SHARE
Wananchi wakishuhudia makokoro yakiteketezwa

NA OSCAR ASSENGA, MKINGA

TANZANIA ni mojawapo ya nchi ambazo zinafaidika na biashara ya uvuvi. Hata hivyo biashara hiyo imeendelea kukumbwa na kadhia mbalimbali ikiwamo uvuvi haramu ambao kwa namna moja au nyingine, umetajwa kuanza kusababisha uhaba wa samaki wakubwa kama vile Jodari.

Uvuvi haramu hutekelezwa kwa kutumia nyavu ndogo na mafataki au baruti. Aina hii ya uvuvi imetajwa kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kwa asilimia kubwa madhara ya kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha samaki wakubwa kutoweka na kwenda ukanda mwengine wa bahari.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa uvuvi huo haramu, ambao umesababisha kukosekana kwa chakula cha samaki wakubwa. Jambo hili linasababisha samaki hao kuhamia maeneo mengine ambako wanaweza kupata chakula cha uhakika na kusipokuwa na usumbufu.
Jodari ambao hupatikana kwenye nchi za Kenya, Somalia, Yemeni, Madagascar na Msumbiji ambao wakati mwengine wanaingia ukanda wa bahari hiyo kwa ajili ya kutafuta chakula na kufanya makazi yao huenda wakashindwa kuwepo kutokana na uvuvi huo haramu.

Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Idara ya Uvuvi Kitengo cha Udhibiti Mazao ya Uvuvi na Masoko Kanda ya Kaskazini –Tanga, Juvinaries Nyandoto, anasema uvuvi haramu umekuwa ni tatizo kubwa kwa ukanda wa Bahari ya Hindi kwa asilimia kubwa, kwani baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia nyavu ndogo ambazo husababisha kuvuliwa samaki wadogo ambao ndio chakula cha samaki wakubwa.

Uvuvi haramu ambao umekuwa ukifanyika kupitia nyavu ambazo hazistahili kuvulia samaki, umechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya samaki wakubwa ambao wanapatikana kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi kutoweka.

Nyandoto ambaye pia ni Mratibu wa mradi wa Swiofish katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga anasema, suala la uvuvi haramu hasa katika maeneo mengi limekuwa likishika kasi siku hadi siku kutokana na baadhi ya wavuvi kushindwa kufuata sheria zilizopo ikiwemo kutotumia nyavu ndogo ambazo hazipaswi kutumika.

“Ukiangalia pamoja na juhudi kubwa ambazo tumekuwa tukizifanya kupitia mikutano mbalimbali ya wananchi lakini bado jamii imekuwa ikiendelea na uvuvi haramu hivyo nasi tumejipanga kuhakikisha tunapambana na hali hiyo ili kuweza kuitokomeza “ anasema.

Aidha, pia anataja aina nyengine ya nyavu ambao hutumiwa na wavuvi haramu katika ukanda huo zinazosababisha kuharibu mazalia ya samaki kubwa ni nyavu za viringishi ambao ni hatari sana kwa uvuaji wake kwani zinapokuwa zikiviringishwa kwenye maji hasa madogo zinachangia uharibifu mkubwa.

Anasema nyavu za ‘ringineti’ ambazo zimekuwa zikitumiwa na wavuvi haramu, nazo zimekuwa ni tatizo kubwa kwa ustawi wa ukuaji wa samaki wadogo lakini pia kukosekana kwa chakula cha samaki wakubwa. Hali hii inasababisha kuanza kuadimika kwa samaki katika kwenye ukanda huo.

Pamoja na kuwepo kwa uvuvi huo haramu, Idara hiyo imeanza mkakati kabambe wa kuhakikisha wanaukomesha kwa kutoa elimu kwa jamii na kuunda kamati ndogo za utunzaji wa mazingira na rasilimali za Bahari (BMU) ambazo zitakuwa chachu ya mapambano dhidi ya masuala hayo.

Nyandoto anasema vikundi hivyo vitasaidia kupambana na uvuvi haramu uliopo kwenye maeneo mbalimbali na kusababisha uharibifu wa rasilimali za bahari na hivyo kuchangia upungufu wa samaki.

Anasema pamoja na kuwepo kwa kamati hizo lakini lazima jamii itambue kuwa, kuendelea na uvuvi huo haramu kila wakati kwenye ukanda huo, utasababisha kupungua kwa wingi wa samaki ambao wanapatikana lakini pia, kuwafukuza wengine ambao wana maeneo ya mazalia.

“Ukiangalia vita kubwa ni uvuvi haramu hasa wa mabomu kwani utakuta mtu yupo doria lakini hana dhana nzuri ya kukabiliana na vitendo tuone namna ya kuweza kuzipatia ufumbuzi ili kulinda rasilimali za bahari,” anasema.

Aidha, anasema jamii ya wakazi wa wilaya hiyo wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa kupambana na shughuli za uvuvi haramu kwa madhara yake ni makubwa ikiwemo kusababisha uhaba wa samaki.

Sambamba na hilo, anasema kuwa wapo kwenye mkakati kabambe wa kuhakikisha wanakabiliana na wimbi la uvuvi haramu kwa vitendo. Wanataka kufanya hivi ili kusaidia ongezeko la samaki ambao wanaweza kuongeza ukuzaji wa pato la Taifa.

Anasema katika suala hilo serikali haina budi kuhakikisha inaweka msukumo mkubwa kuzibiti jambo hilo, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda ambao kwa asilimia kubwa unaweza kutumika rasilimali za bahari kwenye baadhi ya viwanda hivyo.

Lakini pia anasisistiza kuwa, vita dhidi ya uvuvi haramu kwa kutumia mabomu unasababisha pia samaki wengi kukimbia kwenye maeneo mengine ya ukanda wa bahari jambo ambalo linapelekea ukosefu wa samaki.

“Katika kuhakikisha suala hili linapata mafanikio makubwa lazima kuongeza nguvu ya ziada kwa wananchi kuelimishwa madhara yanayotokana na uvuvi haramu kwa lengo la kupambana kwa vitendo na jambo hilo,” anasema.

Naye Afisa Uvuvi Mwandamizi Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Upendo Hamida, anasema maeneo ya ukanda wa Bahari ya Hindi yana mchango mkubwa kwenye nchi ikiwemo upatikanaji wa chakula kwa wakazi hao pamoja na kuongeza ajira ambazo huwasaidia kuongeza kipato chao. Lakini hali ilivyo sasa haya yote yanakabiliwa na tishio.

“Uvuvi haramu ni tishio kubwa. Na zaidi kwa uvuvi wa mabomu kwa sababu madhara yake ni makubwa sana. Unachangia mazalia ya samaki kuharibika na kupelekea wengi wao kukimbiza makazi yao,” anasema.

Aidha, anasema kutokana na kuwepo kwa hali hiyo jamii ya watanzania hasa wanaishi pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi, wanapaswa kubadilika na kupinga kwa vitendo suala la uvuvi haramu, ili kutunza rasilimali za bahari kwa ajili ya faida ya Taifa na vizazi vijavyo.