Home Makala Uwazi kwenye mikataba ya madini bado ni changamoto

Uwazi kwenye mikataba ya madini bado ni changamoto

2711
0
SHARE

SIDI MGUMIA, ALIYEKUWA HANDENI

PAMOJA na kufanyika kwa marekebisho kadhaa kwenye sheria namba 14 ya Madini ya mwaka 2010, bado suala la kukosekana kwa uwazi kunaonekana kuwa ni changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo.

Marekebisho hayo yaliyozalisha sheria namba 7 ya mwaka 2017, yanatoa mamlaka ya kuundwa kwa Tume ya Madini.

Kifungu cha  21 cha sheria hiyo hiyo kimetoa mwongozo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda  Tume hiyo.

Mbali ya Sheria hiyo iliyoanza kutumika Julai 7, mwaka jana, kutoa mamlaka ya kuundwa kwa tume ya Madini, lakini imeongezewa vipengele kadhaa ikiwamo kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (Tanzania Mineral Audit Agency- TMAA).

Kuongezeka kwa malipo ya Mrabaha kutoka asilimia 4 kwa madini ya Metali kama vile dhahabu, shaba na  fedha hadi asilimia 6 na kuongezeka kwa malipo ya Mrabaha kutoka asilimia 5 kwa madini ya almasi na vito kama vile Tanzanite, Ruby na  Garnets hadi asilimia 6.

Aidha, kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha na Sheria ya Kodi, hivi sasa kila mtu au kampuni inayotaka kusafirisha madini nje yatakaguliwa na kuthaminishwa na atalipa ada ya ukaguzi ambayo ni asilimia moja ya thamani ya madini anayosafirisha.

Maboresho ya sheria hiyo yameifuta TMAA na watumishi wake kuwalekeza katika kukusanya maduhuli ya Serikali yanayotokana na madini ya Ujenzi na madini ya viwandani na pia kuhakiki vocha za malipo ya mrabaha, kukagua migodi ya wachimbaji wakubwa, wachimbaji wa kati na wachimbaji wadogo, kukagua miradi yote ya wazalishaji dhahabu kutokana na marudio kupitia teknolojia ya Vat leaching, kukagua maeneo ya viwanja vya ndege, bandari na mipakani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini na kupokea malipo ya tozo mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya Madini na kutoa huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo.

Pamoja na watumishi hao kupewa jukumu la ukaguzi wa migodi, bado wanaonekana kutotekeleza majukumu yao kwa weledi na uwazi, hali inayosababisha baadhi ya wawekezaji wasio waaminifu kutekeleza majukumu yao kinyume na taratibu.

Uwazi katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya madini ni muhimu ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa endelevu.

Miongoni mwa maeneo ambayo kwa kiasi fulani yameathiriwa na kukosekana kwa uwazi ni wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.

Wilaya ya Handeni ambayo kwa upande wa magharibi imepakana na wilaya ya Kilindi, mashariki imepakana na Pangani, Kaskazini wanaungana na Korogwe na Kusini wanapakana na mkoa wa Pwani, imebarikiwa kiasi kikubwa cha madini ya dhahabu.

Wilaya hii ambayo ni miongoni mwa wilaya kongwe za mkoa wa Tanga, inakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 7,366.41 huku sensa ya mwaka 2012 ikionesha kuwa na jumla ya wakazi 355,702.

Shughuli kuu zinazotajwa kuwaingizia kipato wakazi wengi wa wilaya hii ni kilimo na ufugaji, ambapo hadi kufikia mwaka 2014 ilikadiriwa kuwa pato la kila mkazi wa wilaya hiyo kwa mwaka ni Sh. 810,000.

Hatua ya kutegemea kilimo na ufugaji, inaifanya wilaya hiyo kuhangaika kujikwamua kiuchumi, huku ikiwa na rasilimali ya dhahabu ambayo ingeweza kusaidia kufanikisha kuwaondoa wananchi wa wilaya hiyo kwenye lindi la umasikini.

Handeni inayo maeneo kadhaa yenye dhahabu inayochimbwa na wachimbaji wadogo, huku eneo linalotajwa kuwa na kiasi kingi cha dhahabu la Magambazi, lililoko kata ya Kang’ata likimilikishwa kwa wachimbaji wakubwa.

Pamoja na kumilikishwa huko, ukweli ni kwamba mgodi huo hauna tija kwa wilaya hiyo, mkoa na hata mtu mmoja mmoja kutokana na kuwapo kwa mvurugano baina ya wanaoitwa wawekezaji.

Awali mgodi huo ulikuwa ukiendeshwa na wachimbaji wadogo, lakini kutokana na kiasi kikubwa cha madini yaliyopo kwenye milima ya Magambazi, serikali iliubinafsisha kwa kampuni ya CANACO.

Ubinafsishaji huo unadaiwa kufanyika kwa utaratibu stahiki, lakini kilichokuja kutokea ndicho kinacholeta uhalali wa mgodi huo kutokuwa na tija yoyote kwa wilaya ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Ukweli wa hilo unathibitishwa na wananchi na viongozi, katika mahojiano maalum yaliyofanywa na mwandishi wa makala haya, juu ya kukosekana kwa uwazi wa mikataba na usimamizi thabiti wa shughuli za migodi.

Hussein Said (30), mchimbaji mdogo, mkazi wa Handeni eneo la kwa Chogo anakiri wazi kuwa mgodi huo hauwanufaishi, zaidi umewasababishia umasikini kutokana na kufukuzwa kwa nguvu na kupoteza mali zao, huku wakiwa hawajashirikishwa kwenye hatua zote za kumpa eneo mwekezaji.

Anasema amefanya kazi kwenye mgodi wa Magambazi, alikuwa akijiingizia kipato, hata hivyo walikuja kutimuliwa na kuambiwa kuwa eneo anapewa mwekezaji na kwamba wao watafaidika kwa kupata ajira, lakini hadi sasa hakuna kilichotekelezwa.

“Hatuioni faida yoyote,  ile milima ya Magambazi ina mali nyingi, lakini wakubwa wameamua kuzikalia kwa maslahi yao, sasa mgodi hautunufaishi kabisa,”alisema.

Salim Mwinjuma (29) anasema alifanya kazi kwenye mgodi wa Magambazi kwa miaka 13 na kwa kipindi chote hicho walikaa kihalali wakiwa na leseni na hakukua na matatizo.

“Tuliokuwa pale ni wananchi wa hali ya chini, tuna miduara, tunachimba na tunalipa kodi, tumefanya hivyo kwa miaka mingi tangu mwaka 2004.

“Ilipofika mwaka 2009 ndio tukasikia kuwa kuna mwekezaji amekuja kwa hiyo ametaka kuwekeza katika eneo hilo, kweli CANACO alikuja kuonana na wanakijiji na baadhi ya wale wenzetu waliokuwa na kikundi cha watu 48 ambao ndio walikuwa waanzilishi wa eneo lile na ndio ambao walikuwa na leseni.

“Tumekaa baadae tukaambiwa kuwa baadhi ya wenzetu wamelaghaiwa na wameridhia kuliachia hilo eneo. Mkuu wa Wilaya wakati huo marehemu Muhingo Rweyemamu, alikuja akatuambia eneo lile limeshabinafsishwa.

“Pale tulikuwa kama watu 300 ambao tulikuwa tunajipatia kipato, akasema kwakua tulikuwa wengi tutafaidika na mwekezaji kwa kututafutia eneo jingine.

“Hata Mkuu wa mkoa wa wakati huo Chiku Galawa , nae alisema wazi kuwa kama tunataka kuhamishwa basi ni vema tutafutiwe leseni na sehemu iliyothibitishwa kuwa na dhahabu.”

Pamoja na mambo mengine Mwinjuma anasema hadi sasa ingawa Mkuu wa wilaya wa sasa, Godwin Gondwe amefika kuwasikiliza, lakini hakuna tija waliyoipata wale waliotimuliwa Magambazi, ambao sasa wengi wao wamezagaa mjini.

Khalidi Amir (41), aliyekuwa akichimba dhahabu Magambazi, alisema Serikali ilitoa amri ya kufukuzwa kwao, ambapo mabomu yalitumika kuwatimua.

“Mimi nilipoteza mali zangu zote vikiwemo duka na baa. Serikali haijachukua hatua yoyote ile. Tuko kwenye mgodi wa Kwedijava ambao hauna dhahabu nyingi kama ule wa Magambazi, mambo ni magumu sana.”

Akizungumzia kukosekana kwa uwazi kwenye mgodi wa Magambazi, Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni, William Makufwe, alisema Canaco Tanzania Limited ndiye mwekezaji aliyeingia mkataba na Serikali, jambo la kushangaza ni kwamba wamegawa kazi kwa kampuni nyingine ya Tanzania Gold Field (TGF) kwa sasa ndio wanapatikana kwenye mgodi huo.

“TGF ndio wako mgodini kwa sasa na wana mitambo yao pale na kuna ulinzi mkali, pia hawako tayari kuachia mgodi ingawa hawatambuliki kisheria,  sisi tunamjua Canaco kwasababu makubaliano yao waliyoandikiana hatuyajui, hakuna mahali walisajili makubaliano yao, sisi tumekuja kujua baadae kuwa waliingia wa makubaliano.

“Wameweka ulinzi mkali kwa sababu wanajilinda ili Canaco wasiingie kwenye mgodi. Kibaya zaidi Canaco anataka aingie kwenye mgodi ili aendelee kufanya kazi kwasababu kuna majukumu ambayo yanamlazimisha kuwa pale ili ayatekeleze, kwahiyo huo ndio utata uliopo.”

Makufwe alisema mvutano huo unaifanya Halmashauri kukosa mapato, kwani wanatakiwa wakusanye kodi ambayo haipatikani.

“Kama wilaya haipati fedha, hii haileti maana, sisi tunahitaji mwekezaji anayewekeza pale alipe hela ili tuendeshe Halmashauri, tujenge madarasa, tulime korosho, mihogo hiyo ndiyo kazi ninayoitaka mimi, sasa kama kuna watu walikubaliana kinyume na taratibu hilo, halituhusu.

“Hayo ninayokwambia mimi ndio ambayo yako sahihi kwa asilimia 100, sasa waliingiaje mkataba, mimi sijui.”

Alisema kilichopo ni kukosekana kwa usimamizi sahihi, lakini pia kosa ni la CANACO ambao walishindwa kuwa wawazi kwenye makubaliano ambayo waliingia na TGF.

“Sisi hatutaki kujua kuhusu ugomvi wao, tunachotaka sisi ni mgodi kufanya kazi na Halmashauri inapata mapato.

“Tunataka tupate ushuru wa huduma (service leavy), lakini pia watu wetu wapate ajira kwa ujumla.

“Naamini ufuatiliaji wa kina haukufanyika na tulikuja kujua kuwa aliyeko pale si CANACO ni TGF baada ya CANACO wenyewe kuja kulalamika na hiyo ni baada ya kuona kuwa ‘terms’ walizokubaliana hawajazitimiza.

“Kibaya zaidi hawa jamaa wanachenjua badala ya kuchimba, sasa ni kwanini wafanye hivyo  katika eneo ambalo linatakiwa kuchimbwa, mitambo iliyopo pale ni ya uchenjuaji na si uchimbaji. Na wanachofanya ni kuyafanyia kazi maudongo waliyoyaacha wachimbaji wadogo.

“Wanachokifanya ni kuendeleza uongo, hakuna uwekezaji uliofanyika. Sisi tulitarajia  kupata milioni 300 za ushuru wa huduma kwenye madini kwa 2017-2018, lakini tumeweza kukusanya milioni 14.4 ambayo ni sawa na asilimia tano tu.

“CANACO peke yake ilitakiwa itupatie asilimia 90 ya hiyo milioni 300, lakini hatujaipata, maana yake tumekosa zaidi ya Sh. milioni 290  na hii ni mfululizo wa mwaka 2015, 2016, 2017 na 2018.

Alisema kwenye machimbo ya Magambazi  kuna madini ya kutosha na kwamba panatakiwa mwekezaji mwenye uwezo wa kutosha, kitu ambacho kinakosekana.

Kwa uapnde wake ofisa madini wilaya ya Handeni Naiman Samana alisema mgodi huo uko kwenye leseni ML 525-2014 na unamilikiwa na kampuni Canaco Tanzania Limited.

Alisema wanachokijua wao makubaliano ya Canaco na TGF  hayakuwa rasmi, kwa maana serikali haikuhusishwa.

“Tunachokijua ni kwamba Tanzania Gold Field waliingia mkataba wa makubaliano na Canaco kwa ajili ya kuindeleza ile leseni, lakini kwa mara ya kwanza hawakuijulisha Serikali juu ya makubaliano yao, baadae Naibu Waziri wa Madini  (Dotto Biteko), alipokuja kuutembelea mgodi aliukuta mgogoro huo na kutaka apelekewe taarifa rasmi ili Serikali iweze kulifanyia kazi na kujua kama ni mkataba halali au la.

“Wamewasilisha taarifa zao na hapo palipofikia sasa, wasemaji wake ni wizara. Kimsingi, wamepewa (default notice) hati ya makosa ambayo kuna vingele wanatakiwa kuvibadilisha ambavyo vimeonekana kuwa na upungufu juu ya leseni na mkataba wao.

“Hapa sasa tunazungumzia vitu viwili leseni na mkataba, kwenye mkataba ndio waliambiwa wa wasilishe nyaraka zao Serikalini,  lakini kuhusiana na leseni kuna vitu ambavyo vinaonekana kukiukwa walipewa siku 45 kufanya marekebisho ya vitu hivyo ili waendane na sheria za umiliki wa leseni ambazo zimeanzia Agosti 15, mwaka huu.

Mmiliki anayetambulika na Serikali, Denis Dillip wa kampuni ya Canaco, kwa upande wake alisema kuwa wanashangazwa na TGF kufanya mambo kinyume na makubaliano ya mkataba.

“Kampuni hii ilipata leseni kwa taratibu za kuchimba kwenye mlima wa Magambazi,  si kwa taratibu hizo wanazofanya hawa jamaa kama ilivyo sasa, kunataratibu zinatakiwa zifuatwe juu ya mazingira, lakini hawa wanakwenda kinyume hatufahamu kwa nini wanaendelea kufanya hivyo.

“Labda TGF ameona dhahabu kidogo akaingia tamaa ya kutaka kuichimba,  alitakiwa asimame toka muda mrefu, lakini amekuwa akiendelea bila kufuata yale tuliyokubaliana,” alisema Denis.

Kwa upande wa TGF, mmoja wa wakurugenzi wake, ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini, alisema hawawezi kuzungumzia suala hilo kwakuwa lipo Mahakamani.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, amesema wao kama wawakilishi wa Rais hawawezi kuruhusu uwekezaji kama huo na lazima hatua zichukuliwe

“Tulitegemea kwa mwaka mzima Serikiali ingeweza kupata milioni 300 mpaka 700 kama Halmashauri peke yake, Serikali Kuu peke yake ipate zaidi ya bilioni moja, hiyo ni fedha ambayo inaingizwa kwenye bajeti ya serikali, lakini mwisho wa mwaka haionekani.

“Hawa wamepewa hiyo leseni kubwa ili waweze kuchimba, lakini hayo hayaendelei , kwahiyo sisi kama wawakilishi wa Rais hatuwezi kuruhusu hilo,” alisema Gondwe

Naibu Waziri Biteko alisema wazi kuwa amekuta hali isiyo ya kawaida katika mgodi wa Magambazi kwa mwekezaji aliyepewa kuendeleza mgodi huo kushindwa kufanya kazi.

Katika mazungumzo yake na wawekezaji wanaomiliki mgodi huo, alisema ni bora kufutwa kwa leseni za wamiliki hao kuliko kukaa nao kwani wanaisababishia Wilaya na serikali kuu hasara .

“Uzalishaji unaofanyika hapa ni wa ujanja ujanja, tunahitaji tuwe na wawekezaji ambao wanakuja, wanatambua kuwa mali hii ni ya Watanzania.”

Alimwagiza Afisa Madini kukagua hasara iliyopatikana  na fedha kiasi gani kimeshalipwa na wanapata nini na wanachokifanya kama kinatambulika rasmi na kama hakitambuliki basi waielekeze tume ya madini iwape default notice ili wasimamishe kazi zao,”alisema  Biteko

Kama hiyo haitoshi Agosti mwaka huu Biteko aliagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Handeni kuwakamata na kuzuia mali za wamiliki wa kampuni ya Canaco kwa kukiuka masharti ya mkataba ikiwemo kugawa mgodi kwa TGF pasipo kufuata taratibu za kimkataba.

Alisema Serikali haitamvumilia mwekezaji yoyote ambaye atavunja sheria.