Home Makala Uzazi salama ni haki ya kila mwanamke

Uzazi salama ni haki ya kila mwanamke

1781
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MOJA ya mambo yanayogusa moja kwa moja maisha ya kiumbe hai ni uzazi. Kila kiumbe kilicho na uhai kimezaliwa na mwanamke.

Hata hivyo ipo tofauti ya uzazi kwa viumbe hai, wapo wanaozaliana kwa kutaga mayai na wengine kwa njia ya kawaida.

Viumbe jamii ya ndege na mijusi hawa huzaliana kwa kutaga mayai, tofauti na ilivyo kwa viumbe wengine kama wanyama na binadamu.

Viumbe vyote hivi huhitaji uzazi salama. Hata hivyo makala haya yataangazia zaidi uzazi salama wa binadamu mara baada ya kutunga mimba.

Ingawa idadi kubwa ya wanawake huingia katika majira yake ya hedhi, ukweli ni kwamba si kila mwanamke anaouwezo wa kushika mimba.

Wakati wa hedhi mwili wa mwanamke huangua yai linalotoka sehemu ya kiungo cha uzazi kinachoitwa ovari. Yai hili huteremka polepole kupitia mirija ya ovari likisafiri kwa muda wa siku nane hadi 12 kuelekea nyumba ya uzazi.

Wakati mwanaume anapotoa manii (wakati wa kukutana kimwili), huwa yamebeba mamilioni ya mbegu za kiume, ila moja tu inapokutana na yai la mwanamke, inatosha kutunga mimba.

Baada ya tendo hilo manii zilizokutana na yai na kutungisha mimba zinakwenda kwenye nyumba ya uzazi, ambapo zitapata virutubisho vya kuikuza mimba hiyo.

Muungano wa yai na mbegu ya mwanamme, ambao sasa ni mimba, hukua, hatua hii ya ukuaji wa mimba hadi kuzaliwa kwa mtoto ndio msingi mkuu wa makala haya.

Katika kipindi hiki cha kulea mimba dhana ya uzazi salama inapaswa kupewa kipaumbele kwa mama na mtoto aliyeko tumboni kupatiwa malezi bora, katika kipindi chote cha miezi tisa ya ukuzaji wa mtoto tumboni.

Kwa miaka mingi sasa suala la uzazi salama nchini limekuwa na changamoto kubwa kutokana na suala hilo nyeti kutopewa umuhimu na heshima stahiki kuanzia ngazi ya kaya hadi serikalini.

Kwa ngazi ya kaya, jamii zimekuwa zikishindwa kutoa huduma stahiki kama vile lishe bora na malazi salama kwa mama mjamzito.

Ukija kwenye ngazi ya serikali, huduma ya uzazi kwenye zahanati na hospitali ni duni. Mara nyingi mama mjamzito hana uhakika wa kujifungua salama.

Kutokana na ukweli huo serikali ya awamu ya tano chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imedhamiria kulipunguza kama si kuliondoa kabisa janga hilo.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu amelianisha hilo mwishoni mwa wiki iliyopita aliweka wazi kuwa, serikali imeanza mchakato wa kuboresha vituo 100 vya afya.

Kwa kujua kuwa uzazi salama ni haki ya kila Mwanamke, Ummy aliweka wazi kuwa amedhamiria kulifanikisha hilo ili kuhakikisha suala la uzazi linakuwa salama kwa kila mama mjamzito.

Katika Mkutano wa tatu wa Wafadhili wa Kimataifa wa Afya ya Mama na Mtoto (Global Financing Facility (GFF), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Ummy alisema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo

Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Bodi ya Kimataifa ya Vinara wa Uzazi wa Mpango (Family Planning Reference Group 2020 – FP2020).

“Wizara ya Afya tunajivunia kutengeneza na kukamilisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Kuimarisha Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana (The National Roadmap Strategic Plan to Improve Reproductive, Maternal, Newborn and Adolescent Health in Tanzania – one plane II), ambao ndio Nyenzo ya Kutafuta Uwekezaji wa Rasilimali Fedha katika kutekeleza shughuli mbalimbali kwenye eneo hili.

“GFF ni mojawapo ya wafadhili waliowekeza katika Mpango huu. Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huu wakati wa hafla ya kuwakaribisha wajumbe wa GFF na wawekezaji katika Afya Duniani nilitangaza rasmi kuwa Serikali, Benki ya Dunia /GFF tutaboresha Vituo vya Afya 100 ili kuviwezesha kutoa huduma muhimu za uzazi na za dharura katika  Halmashauri mbalimbali nchini,”.

Kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha mama mjamzito anakuwa na uhakika wa kujifungua bila tatizo, Ummy alisema katika kila kituo cha Afya watajenga Maabara ya kuhifadhi damu, Wodi ya Wazazi na Nyumba moja ya Mtumishi.

Ili kufanikisha hilo vimewekwa vigezo sahihi vya kupata vituo vya afya vitakavyoboreshwa.

DHAMIRA YA WAZIRI

Akilizungumzia hilo kwa msisitizo Waziri Ummy alisema amedhamiria kuanza utekelezaji huo haraka.

“Nimedhamiria tuanze utekelezaji wa Mpango huu haraka iwezekanavyo, kukamilika kwa mpango huu itakuwa ni mchango mkubwa sana wa Serikali ya Awamu ya tano  inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli katika kuboresha huduma za Afya hasa afya ya mama, uzazi na mtoto.

“Hadi sasa, katika vituo vya Afya 489 vya umma ni takribani vituo 113 tu ndio vinatoa huduma muhimu za uzazi na za dharura zinazokidhi viwango. (Basic Emergence Obstetric & Newborn Care (BEMONC) and Comprehensive Emergence Obstetric and Newborn Care -CEMONC).

“Nikiwa na dhamana ya kuongoza Wizara ya Afya lakini pia Mwanamke na Mama, huu utakuwa ni mchango wetu mkubwa katika kuboresha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto hasa kwa wanawake wenzangu waliopo katika maeneo magumu kufikika.

“Kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Afya na Wanawake wa Tanzania tunawashukuru sana Benki ya Dunia /GFF pamoja na Bill and Melinda Gates Foundation, Canada, DFID, JICA, Norway na USAID kwa kufanikisha hili.

“Kwa Pamoja Tunaweza Kupunguza Vifo vya Wanawake Wajawazito nchini.Tushirikiane.”alihitimisha Ummy.

Bila shaka Watanzania bila kujali walipo, wanapaswa kutia shime katika kuufanikisha mpango huu ambao sit u utaleta tija kwa wanawake wajawazito, lakini pia utaufanya uzazi kuwa salama kwa wanawake wote nchini.