Home Afrika Mashariki Vazi la Taifa limeishia wapi?

Vazi la Taifa limeishia wapi?

2249
0
SHARE

TANGU mwaka 2004 kumekuwa na harakati za Tanzania kutaka kuwa na vazi lake la taifa, lakini juhudi hizo zinaonekana kushindikana, huku sababu za msingi zikishindwa kuwekwa wazi na wahusika. Suala la vazi la taifa ni muhimu sana kwa lengo la kujenga utaifa na kutambulika kwa haraka kwa raia wa Tanzania, hasa anapokuwa nje ya nchi na pia kutangaza utamaduni wa Mtanzania.

Tanzania inapokosa vazi la taifa pia inakosa utambulisho wa taifa na raia wake, kwani kunakuwa na uvaaji holela usiokuwa na tija kama taifa au kushindwa kuitambulisha nchi kimataifa kupitia mavazi. Desemba 15 mwaka 2011, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, wakati huo ikiwa chini ya Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilifanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Kubuni Vazi la Taifa.

Kuteuliwa kwa Kamati hiyo kuliamsha imani miongoni mwa Watanzania sasa kupata utambulisho wa vazi lake. Kamati hiyo iliyokuwa na watu wanane, Mwenyekiti alikuwa ni Joseph Kusaga, Katibu Angela Ngowi, ambaye ni miongoni mwa wanamitindo mahiri nchini, huku wajumbe wa kamati wakiwa ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye alitangaza kujiondoa Desemba 22, 2011.

Licha ya kamati kuzinduliwa rasmi na Waziri Nchimbi, tayari kuanza kazi yake ya mchakato wa kubuni vazi la taifa, lakini mpaka sasa haijulikani nini kimetokea hadi kutopatikana kwa vazi hilo lililotarajiwa kupatikana ndani ya siku 75 tu. Kazi ya kamati hiyo haikuwa kuanza mchakato mpya wa Vazi la Taifa, bali ilipaswa kumalizia mchakato ulioanza mwaka 2004. Aprili mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri, Waziri Nchimbi akahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Fenella Mukangara, ambaye kimsingi alipaswa kufuatilia suala hilo. Septemba 10, 2012, Kamati ya Vazi la Taifa chini ya Kusaga ilikabidhi ripoti kwa Waziri Mukangara kupitia kwa Katibu wa Kamati hiyo, Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo. Wakati wa makabidhiano hayo, Angela alisema katika mchakato wa kupata vazi hilo, walipokea zaidi ya michoro 200 kutoka kwa wasanii 88 wa hapa nchini na kupitisha michoro sita iliyokuwa imekidhi vigezo na kuikabidhi kwa wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya kutoa uamuzi wao. Baada ya kupokea ripoti hiyo Dk. Fenella akaiagiza menejimenti ya wizara yake chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu, ichague vitambaa vitatu kati ya vitano vilivyopendekezwa na kamati na kupelekwa ngazi ya sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, kamati ya ufundi ya makatibu wakuu na hatimaye Baraza la Mawaziri. Leo hii ni miaka mitatu tangu ripoti hiyo itue kwa waziri husika, lakini hakuna kinachozungumzwa tena kuhusiana na vazi hilo, hivyo kuwaacha midomo wazi Watanzania wakiwa hawajui hatima ya vazi hilo. Kitendo cha ukimya huo kimesababisha Watanzania kuendelea na kasi ya kushabikia mavazi ya tamaduni za nje (hasa za nchi za Ulaya na Afrika Magharibi), si kwenye mavazi tu, bali hata katika sanaa nyingine kama vile filamu na muziki kwa kasumba tu kwamba hizo ndizo bora na hazina mpinzani.

Endapo ahadi ya serikali ingetimia, leo hii Watanzania wangekuwa ‘wakijimwaya’ na vazi hilo ambalo kwa namna yoyote ile ni fahari na heshima kwa kila Mtanzania. RAI ilifanikiwa kuzungumza na mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Millen Magese kuhusu mtazamo juu ya suala hilo, ambapo bila kusita alionesha wasiwasi wake na hatua hiyo ya serikali kulikalia kimya suala hilo ilhali lilikuwa linakaribia mwisho. Wabunifu wa mavazi wako wengi na tayari wameshapendekeza michoro, hivyo kitendo cha kulikalia kimya suala hilo siyo tu linarudisha nyuma jitihada hizo, bali pia linawavunja moyo wahusika waliohangaika nalo toka hatua za awali. Flaviana Matata naye ni mmoja wa wanamitindo wa kimataifa anayekerwa na hali hiyo, ambapo kwa mtazamo wake ni aibu kwa Tanzania mpaka sasa kutokuwa na vazi lake la taifa na badala yake wananchi wale ndio kuwa wavaaji wakubwa wa mavazi ya wengine, hasa wanapotoka nje ya nchi.