Home Makala Kimataifa VETA SI VYETI NI MAARIFA

VETA SI VYETI NI MAARIFA

4007
0
SHARE

Hongera nyingi VETA. Tangu kuasisiwa kwake VETA imekwua ikifanya kazi kubwa na yenye manufaa katika kuwapatia vijana maarifa na stadi zinazowawezesha kujiajiri na kuajiriwa. Katika kipindi chote hiki mitaala ya mafunzo ndani ya VETA imeelekezwa katika ufundi stadi, udereva na utoaji wa huduma mbalimbali. Turidhike na hapa tulipo au tunahitaji kusonga mbele zaidi?

Mwelekeo wa uchumi wa nchi yetu sasa umebadilika. Tumeamua kuijenga Tanzania mpya kwa kuelekeza jitihada zetu kwenye Tanzania ya viwanda. Hapana shaka kuwa msingi wa ujenzi wetu ni viwanda vidogo vidogo na vya kati. Hata mbuyu ulianza kama mchicha. Na hapana shaka pia kuwa viwanda vya aina hii vinahitaji uzalishaji zaidi wa mazao ghafi ya kuchakatwa na zana zake.

Kwa mnasaba huu VETA inayo majukumu mapya mawili. Mosi, kutengeneza mtaala wa mafunzo yanayohitajika na kundi kubwa la Watanzania katika kuongeza maarifa ya uzalishaji wenye tija. Tunatambua sote kuwa karibu asilimia themanini ya Watanzania ni wakulima, wafugaji na wavuvi. VETA ni chombo muhimu chenye maarifa, uwezo na nguvu ya kulikomboa kundi hili kubwa.

Pili, VETA haina budi kujumuisha katika mitaala yake stadi za kuunda zana ndogondogo zitakazochochea uzalishaji, uongezaji thamani ya bidhaa ghafi na utunzaji wa mazingira. Nakusudia zana kama vile za kuchakata mbegu za mafuta, umwagiliaji, palizi na huduma za mashambani, zana zitakazowasaidia wafugaji wa wanyama, nyuki na samaki, na huduma nyinginezo.

Serikali zetu katika awamu zote zimejitahidi kusambaza vyuo vya VETA nchi nzima. Hali hii inatoa wasaa kwa VETA kwanza kuyafahamu mazingira ya kujiografia na ya kiuchumi kwa kila wilaya; na pili, wasaa wa ushirikiano na wataalamu wa Halmashauri za Wilaya katika kuendesha tafiti zitakazoiwezesha VETA kupata njia na namna bora ya kushiriki safari ya Tanzania ya viwanda.

Nastahabu kurudia kukiri na tena kwa msisitizo kuwa VETA inafanya kazi kubwa na yenye manufaa. Bali tunapaswa kujiuliza iwapo hapa tulipo sasa panatosheleza? Hapana! Dunia inabadilika na mahitaji ya mwanadamu si suala mnato na mgando bali ni mnyumbuliko na mabadiliko. Kukumbatia hilo kwa hilo kila uchao ni kutenda kazi kwa mazoea kusiko na tija, na ni ajizi na uvivu wa kufikiri.

Hivyo ni kweli kwamba ni lazima tuagize vimashine vya kupukuchua mahindi kutoka China, India au Vietnam! Siku hizi tunaingiza hapa nchini vimashine vya kukamua mbegu za mafuta, majembe yanayotumia mota, vinyangarika vya kuwindia ndege kwenye mashamba ya mpunga na vinginevyo vingi tena kwa gharama ya pesa za kigeni zinazotokana na wakulima kuota vibiyongo kwa sababu ya jembe la mkono.

Wataalamu wetu ndani ya VETA mnayo maswali mengi na muhimu ya kujiuliza ili tupate jawabu la kututoa hapa tuliponasa na kutuwezesha kupiga hatua mbele. Hamna budi kuumiza kichwa ili kulitambua tatizo na kisha mjenge dhamira ya makusudi na mjisheheneze ujasiri wa kuzikabili changamoto za kuifikia dhamira yenu. Jambo hili zito ni jepesi ikiwa mtajenga nidhamu ya kujituma.

Kwa mtu mbumbumbu kama mimi naweza kudhani na kuamini kwamba wataalamu wetu wa VETA hawawezi kuyatenda tunayoyataraji kutoka kwao kwa sababu hawana uwezo kama walionao wenzao huko China, India au Vietnam. Lakini atatokea msomi anikosoe kuwa huko ni kuwadharau wataalamu wetu kwani taaluma za wataalamu wetu ni funguo tosha za kuyafikia maarifa. Ni ukweli mtupu.

Basi kwa kuwa nimeelimishwa hilo naweza nikaibukia kwingineko kwamba kwa sababu yanayofanywa na VETA ni mengi sana kwa hivyo yanatosha. Anaweza kutokea msomi mwingine akaniambia suala hapa sio unayafanya mangapi bali unafanya nini na kwa lengo gani. Suala muhimu ni kitendo kusadifu lengo. Toba!

Hii ndio shida ya kulumbana na msomi. Akizimwaga hoja zake inakuwa shughuli pevu kuzipindua. Naam! Ameniambia suala sio unafanya mengi kiasi gani bali unafanya nini na kwa lengo gani. Hapa ananirejesha katika mishughuliko ya kutwa nzima inayofanywa na wajukuu wangu na magharibi ikiingia hulala fofofo kwa uchovu. Kumbe matendo yenye tija lazima yawe na malengo.

Basi na mimi nimeshawishika kukubaliana na matendo yenye kushabihi malengo. Nashauri mitaala ya VETA ya sasa ilenge shughuli za Watanzania kulingana na jiografia ya maeneo ya nchi yetu na mahitaji ya kiuchumi. Mwelekeo uzalishaji. Aidha, utapunguza vijiwe uzembe, uzururaji na kasi ya vijana kukimbilia mijini.

Kutoka ndani ya pachipachi za moyo wangu ninaamini kwamba tunayo yahamu na kuyataraji kutoka VETA yanawezekana. Imani yangu hii siijengi tu kwa utashi bali kwa sababu zinazoingia akilini na zenye mashiko. Ndani ya VETA tunao wataalamu waliosheheni taaluma mbalimbali na kwa pamoja suluhisho litapatikana. Kijinga na kijinga huwasha moto.

Kinachohitajika VETA ni mabadiliko ya mtazamo, dhamira ya kuitafsiri ndoto ya Tanzania mpya na kujikita kitakita katika tafiti. Wakulima, wafugaji na wavuvi ni uwanja wa medani ya vita ambavyo VETA inatakiwa kupigana na kushinda. Ramani ya uwanja wa vita lazima iwe na usahihi na uhalisia wa ardhi husika. Kinachokosewa na kurekebishwa ni ramani sio uwanja wa mapambano.

Wataalamu ndani ya Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji wanapaswa kuionyesha VETA maeneo ya maadui, nguvu na udhaifu wao katika vita hii. Kwa hakika tafiti katika suala hili ni vita vya lazima. Serikali haina budi kuishika mkono VETA. Serikali iisaidie VETA iwe na kijiji cha utafiti ili kuwa na matokeo.

Hayupo mwanadamu aliyezaliwa na jembe mkononi ili awe mkulima, au bakora mkononi ili awe mfugaji, na au ndoana mkononi ili awe mvuvi. Ni mazingira ya kijiografia ndio yanayotengeneza tamaduni za kiuchumi kwa jamii mbalimbali. VETA kupitia tafiti itafungua milango zaidi ya uzalishaji na kukuza uchumi.