Home Habari Vifaa ‘feki’ umemejua maumivu kwa Watanzania

Vifaa ‘feki’ umemejua maumivu kwa Watanzania

1444
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

LICHA ya Watanzania kuonesha nia ya kutumia nishati itokanayo na mfumo wa umemejua, upatikanaji wa vifaa bora na sahihi kwa matumizi ya uzalishaji wa nishati hiyo jadidifu unazidi kusuasua.

Kusuasua huko kunatokana na wimbi la vifaa feki vya mfumo wa umemejua ambavyo vimeendelea kushamiri katika soko la Tanzania na kuathiri watumiaji wa nishati ya umemejua ambayo sasa matumizi yake imefikia wastani wa asilimia mbili ikilinganishwa na nishati nyingine Tanzania bara.

Ukweli huo unadhibitishwa na ripoti iliyotolewa Machi mwaka jana na taasisi ya utafiti ya Ipsos ambayo ilibainisha kuwa asilimia 72 ya vifaa vya umemejua vinavyouzwa kwa bei ‘chee’ havina ubora unaotakiwa.

Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘Solar off grid Market Research in Tanzania 2018,’ imebainisha kuwa kumekuwapo na ongezeko kubwa la wauzaji wa vifaa hivyo ambavyo huingizwa nchini kwa njia za panya na kusababisha mamlaka husika likiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au Tume ya Ushinda (FCC) kushindwa kuhakiki ubora wa vifaa hivyo.

Vifaa feki vilivyobainika

Ofisa Ukaguzi na Upimaji wa Ubora wa Vifaa vya Umemejua kutoka TBS, Anicetus Ndunguru, amelieleza RAI kuwa kuanzia mwaka 2015 hadi Disemba 2018 jumla ya betri na solar 3,972 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 298.9 zilikamatwa na kuharibiwa hapa nchini, wakati betri na solar 2,547 zilirudishwa zilikotoka. Pia aliongeza taa 1400 za solar zenye thamani ya Sh milioni 10 ziliharibiwa

Athari za uwapo wa vifaa feki

Ingawa watu milioni 10 duniani sasa wanapata nishati kwa njia ya mfumo wa umemejua, Taasisi ya Kuendeleza Nishati Asilia na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania (TaTEDO inasema kuwapo kwa tatizo la vifaa feki vya umemejua vinavyoingizwa nchini ni mojawapo ya chanzo kikubwa kinachorudisha nyuma jitihada za Serikali.

Mmoja wa watumiaji wa umemejua kutoka Chanika, Kelvin Sanga, anasema uwapo wa vifaa feki vya umemejua ni janga ambalo Serikali na taasisi zake inatakiwa kulidhibiti ili wananchi wasipate hasara.

“Kwa sababu vifaa hivi tunanunua kwa bei ghali, lakini unapokuja kutumia siku moja mbili, vinaharibika ni hasara kwetu watumiaji. Lakini pia inatukatisha tama hata kutumia umemejua,” anasema.

Aidha, Meneja Mauzo kutoka Kampuni ya Chloride Solar, Ahmed Abdalla, anasema baadhi ya bidhaa kutoka China zimetamalaki katika soko la vifaa vya umemejua nchini, na kwamba bidhaa hizo baadhi ni feki jambo linachangia kudumaza matumizi ya nishati hiyo nchini.

“Lakini kuna changamoto ya ujio wa wachina kwa sababu ni wajanja sana, wameleta vifaa ‘fake’ jambo ambalo linavuruga soko la solar nchini. Kwa hiyo mtu anaingia gharama kufunga solar alafu baada ya siku mbili tatu havifanyi kazi,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa TAREA, Prosper Magali ambaye anasema ni kweli kumekuwapo na ongezeko la vifaa feki vya umemejua jambo ambalo linakwamisha juhudi za kuhamasisha watanzania kutumia nishati hiyo.

Anasema licha ya TBS kudhibiti ubora wa bidhaa kuanzia katika nchi vinapoagizwa bado kumekuwapo na njia sizizo rasmi ambazo zinachangia uingizwaji wa vifaa feki nchini.

“Hata katika bandari zote TBS wameweka wakaguzi lakini tunaona vifaa feki bado vinaingia ni jambo linalotukwaza sana,” alisema.

Jitihada zinazofanyika

Aidha, alisema TAREA imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakaguzi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na udhibiti wa vifaa hivyo, ikiwamo TRA, TBS na taasisi nyingine za Serikali ili kutambua ubora wa bidhaa hizo za umemejua kabla ya kumfikia mtumiaji.

“Kwa upande wa watumiaji huwa tunawaelimisha kwa kupitia vyombo vya habari, makongamano na maonesho kama vile siku ya nishati jadidifu ambayo huadhimishwa kila mwaka na hufanyika mikoa mbalimbali hasa ile yenye matumizi makubwa ya umemejua,” alisema.

TBS

Ofisa Ukaguzi na Upimaji wa Ubora wa Vifaa vya Umemejua kutoka TBS, Anicetus Ndunguru anasema shirika hilo hukagua ubora wa vifaa vya umemejua kwa namna mbalimbali ikiwamo kutumia kuna mfumo wa udhibiti wa ubora kutoka kwenye nchi zinazokoagizwa kabla ya kusafirishwa kuletwa nchini.

“Tunao mawakala hususani nchi za Asia na Ulaya ambao hukagua bidhaa hizo kama zina ubora na mwekezaji husika hupewa cheti cha ubora. Akija huku sisi tunadhibitisha kwa kupitia hizo nyaraka.

“Ila bidhaa nyingi zinazalishwa nje ya nchi, ikitokea nyingine zimepita kuja nchini bila kukaguliwa, tuna maabara maalumu ya kupima vifaa vya sola, ni maabara iliyokamilika kabisa.

“Kwenye bidhaa za sola, kuna taa, betri, panel, inverter, chaja controller na vifaa vingine, vyote hivi maabara yetu ambayo ilianza tangu mwaka 2017 inapima ubora wake,” anasema.

Aidha, anaongeza kuwa iwapo mzigo wa vifaa hivyo ukihakikiwa na kubainika kuwa vifaa havina ubora unaotakikana, huharibwa nchini au kusafirishwa kurudishwa kwenye nchi ulikotokea kwa gharama za mwagizaji.

“Na wale walioingiza kwa njia zisizorasmi huwa tunafanya ukaguzi kwenye maduka na wasambazaji mbalimbali na hata kununua ili kupima ubora wake.

“Kwa ujumla udhibiti wa bidhaa za sola unaimarika, na wafanyabiashara hukimbia kutokana na hasara kwa maana mtu akiharibiwa mara moja hataki kukutana na kadhia hiyo tena,” anasema.

Hali ya upatikanaji wa umeme

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme, katika nchi za Afrika Mashariki(EAC), Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na umeme, kwamba watu milioni 36 sawa na asilimia 71 ya idadi ya watu nchini hawajafikiwa na umeme, Burundi ni watu milioni 10 sawa na asilimia 93 ya idadi ya watu nchini humo.

Aidha, kwa nchi za EAC, Kenya inaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya watu waliofikiwa na umeme, kwa mujibu wa ripoti hiyo miaka miwili iliyopita watu waliokuwa na umeme Kenya ni asilimia 56, Tanzania asilimia 32.8, Rwanda asilimia 29.37, Uganda asilimia 26.7 na Burundi asilimia 7.5.

Kwa mantiki hiyo, kuendelea kuharibiwa kwa soko la vifaa vya umemejua ni mojawapo ya chanzo kinachoendelea kuzorotesha upatikanaji wa umeme nchini hasa vijijini. Kiujumla asilimia 87 ya watu duniani wasiofikiwa na umeme wanaishi maeneo ya vijijini.

Ripoti hiyo ya benki ya dunia inaonesha watu bilioni moja duniani au asilimia 13 ya watu duniani wanaishi bila umeme. Kwa nchi za Jangwa la Sahara, Afrika ya Kati na kusini mwa Asia ndiko kunkoongoza kwa kutokuwa na umeme.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni moja ya nchi zilizoonesha jitihada za kuwaunganishia wananchi wake umeme, nyingine ni Bangladesh, Ethiopia, Kenya ikifuatiwa na Tanzania ambazo zote zinaongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kwa asilimia 3 kila mwaka kuanzia mwaka 2010 hadi 2016.

Lakini katika kipindi kama hicho, India ndio nchi iliyoongoza duniani kwafikishia umeme watu wake kwani zaidi ya watu milioni 30 kwa mwaka waliunganishiwa umeme.