Home Habari VIFAA VYAONGEZWA KUPAMBANA NA UKIMWI MBEYA, RUVUMA

VIFAA VYAONGEZWA KUPAMBANA NA UKIMWI MBEYA, RUVUMA

1745
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kuhakikisha vita dhidi ya Ukimwi na maambukizi mapya ya ugonjwa huo yanafanikiwa, Serikali imeongeza vitendea kazi zaidi kwa mikio ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa miaka mingi sasa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha janga hilo linatoweka kabisa na nguvu kubwa imekuwa ikiwekwa katika kuwakinga Watanzania.

Ili kufanikisha hilo mwishoni mwa wiki iliyopita Serikali imetoa magari matano ya kisasa, vifaa mbalimbali vya ofisi pamoja na kompyuta kwenye mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Songwe.

Lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha  uratibu wa UKIMWI nchini hasa kwenye mikoa hiyo unafanyika kwa weledi na kwa wakati sahihi.

Dhgamira kuu ya Serikali ni kuona uratibu wa ugonjwa huo unaanza kufanyika ngazi ya chini kwa maana ya kwenye mitaa, vijiji, Kata, Halmashauri, mikoa hadi Taifa.

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania  ( TACAIDS) Dk. Leonard Maboko alisema kuwa lengo la Serikali ni kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na hii itawezekana  kama uratibu utaimarishwa kuanzia kwenye jamii kwa maana ya kaya.

Dk. Maboko aliongeza kuwa anaamini kuwa baada ya serikali kutoa vitendea kazi hivyo, ambavyo ni silaha kwa watendaji, ni wazi kasi ya kupambana na tatizo hilo itaongezeka.

“Naamini waratibu wa Kudhibiti UKIMWI wa TACAIDS katika Mikoa watakuwa hawana kipingamizi kwenye utendaji wa kazi, watawafikia  wananchi, wataandaa na kuwasilisha taarifa kwa wakati.”

Aidha aliwataka waratibu wa mikoa iliyopewa vifaa hivyo pamoja na waratibu wa mikoa yote kuhakikisha wanavitumia kwa usahihi na kuvitunza vifaa hivyo ili vilete tija iliyokusudiwa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera , Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu,  Jenista Mhagama alisema kuwa hali ya maambukizi ya VVU  nchini inatoa mwongozo wa kuwapo kwa mbinu mbadala za kukabiliana na maambukizi mapya.

Alisema katika kushughulikia hilo, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana  na Serikali ya Marekani kupitia  Idara yake ya Ulinzi (DOD)ilianzisha Mkakati wa Kikanda wenye kulenga mazingira na vichocheo vinavyofanana katika Mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma ili kukabiliana na maambukizi mapya kwa kuunganisha nguvu na rasilimali.

“Hadi sasa kila mkoa tayari umetengeneza mpango mkakati wa Kudhibiti UKIMWI kulingana na vihatarishi vilivyotajwa kwenye utafiti wa viasharia vya VVU na UKIMWI vya mwaka 2016/2017.”

Mhagama aliagiza viongozi wote kushiriki katika kutekeleza mwitikio wa UKIMWI kwa kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika mpango mkakati ulioainishwa na mkoa husika katika maeneo ya kinga  ,matunzo na matibabu ili kupunguza athari zitokanazo na UKIMWI.

Alimshukuru Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson kwa kufanikisha upatikanaji wavifaa hivyo yakiwamo magari ambayo anaamini yatasaidia kuimarisha uratibu na kuwafikia walengwa hasa katika ngazi za Vijiji, Mtaa na Kata.

Kwa upande wake Balozi wa Patterson  alisema kuwa lengo la ushirikiano wa Marekeni na Tanzania kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi ni kuwawezesha  watanzania kufanya kazi ya kujenga nchi imara ,yenye afya na ustawi zaidi.

“Nami ninafurahi kuendeleza mtizamo huu,  kuhakikisha kwamba jamii ya Watanzania waliojitoa na kuwa na dhamira ya dhati,wanapata nyenzo zinazohitajika katika kujenga maisha bora ya baadae.”

Aliongeza kuwa Serikali ya Marekani inajivunia kuunga mkono jitihada nyingi za ushirikiano kwenye masuala ya Afya ikishirikiana na Watanzania ili kuimarisha uwezo wa kushughulikia malaria, Afya ya mama na mtoto, uzazi wa mpango, Kifua kikuu, Lishe, VVU na UKIMWI.

Magari sita yaliyonunuliwa yatasaidia kuboresha uratibu na uwajibikaji kwenye programu za UKIMWI za mikoa kuboresha usimamizi  na uangalizi  katika mikoa na Makao Makuu ya TACAIDS, lengo likiwa ni  kuboresha afya katika mikoa iliyofikiwa.

Magari hayo sita yamegawanywa kwenye mikoa mitano, huku gari moja likisalia makao makuu ili iwarahisishie kazi waratibu na wasimamizi wa mipango endelevu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme  alishukuru kwa mikoa ya Nyanda za juu kusini kupatiwa msaada huo kwa kuwa mikoa hiyo ndio yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU na UKIMWI.

“Vifaa hivi vitasaidia kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika kupambana na maambukizi ya VVU. Kwa kufanya hivyo jamii wataelewa kuwa wanao wajibu mkubwa wa kufanya ili kukabiliana na maambukizi ya VVU badala ya kutegemea serikali na wadau wa maendeleo pekee.”

Mndeme aliongeza kuwa mradi huu umekusudia kushirikisha viongozi wakuuwa siasa kama wakuu wa Mikoa na Wilaya katika kusimamia Mwitikio wa UKIMWI ili kuongeza uwajibikaji.