Home Makala Vigogo CCM waitafakari vyema kauli ya JPM

Vigogo CCM waitafakari vyema kauli ya JPM

1385
0
SHARE

Nashon Kennedy

MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Dk. John Magufuli kwa mara nyingine ametangaza vita ndani ya chama hicho kikongwe, kwa watu hasa wanachama wenye dhamira chanya ya kutumia fedha kwenye uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa hataki CCM ombaomba. 

Kiongozi huyo wa nchi alikwenda mbali zaidi huku akionya kuwa utakapofika wakati wa uchaguzi, viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa wasiende na majina ya wagombea wanaowataka mifukoni mwao. 

Alisema na hapa ninamnukuu; “ndiyo maana wakati mwingine huwa nakuwa mkali. Huwa nawaadhibu kwa niaba yenu (wana-CCM) kwa niaba ya ilani kwa sababu nafahamu chama kinataka mambo yafanyike, kinataka matokeo,”.

Lakini kubwa kwenye mkutano wake huo na viongozi hao wa chama hicho tawala, Rais Magufuli alisema wapo wanachama wengine ambao chama kiliwapoteza kutokana na kuwanyima haki zao, ambapo alifafanua kuwa wengi wa wanachama hao wanataka kugombea nafasi za uongozi lakini wanavurugwa na baadhi ya vigogo wa CCM na kuamua kukihama chama hicho tawala.

Hii ni kauli nzito aliyoitoa Mwenyekiti huyo wa CCM hasa wakati huu ambao taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, ukizingatia CCM ni miongoni mwa vyama vikongwe Kusini mwa Jangwa la Sahara vilivyoendesha harakati za ukombozi kwa baadhi ya nchi za Bara la Afrika. 

Ni dhahiri Rais Magufuli ameonyesha kuwa ndani ya chama hicho kikongwe cha siasa bado hali ya kisiasa si ya kuridhisha na kwamba kwa kauli yake hiyo, CCM inabidi ijitafakari na irejee katika misingi ya kuaminiana, kuheshimiana, kujenga hoja madhubuti zenye mwelekeo wa kuleta umoja, mshikamano wa kweli ambao katika maamuzi ya aina yoyopte yatakayotolewa katika vikao vya chama hicho yasiyo ni yale ya kutiliwa shaka na kuwafanya baadhi ya wanachama wake kununua muda wote na kama alivyobainisha Rais Magufuli kuamua kukihama chama hicho. 

Katika biashara ya siasa duniani kote, ukiona chama cha siasa kinajivuna hadharani kwa kuwapoteza baadhi ya wanachama wake, hicho chama kwa lugha nyingine hakijui biashara ya siasa.

Wakati mwingine Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imekuwa ikijivuna kuyafunga baadhi ya maduka ya wafanyabiashara, hoja sio kufunga maduka bali hoja ni kutafuta suluhu ya matatizo waliyonayo ili waendelee kufanya biashara ili Serikali iweze kukusanya kodi yake, vivyo hivyo kwa CCM.   

Juhudi za Rais Magufuli za kupambana na rushwa hazikuanza leo, alianza wakati akiwa Naibu Waziri na Waziri kamili wakati wa awamu ya tatu na ya nne ya uongozi wa marais wastaafu wa awamu hizo, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. 

Moja ya mambo aliyokerwa nayo kwa wakati huo, ni pamoja na watu waliovunja sheria kwa kujenga kwa makusudi ndani ya hifadhi ya barabara na wale waliokuwa wakijihusisha na uvuvi haramu, ambapo baadhi ya vigogo nao kwa wakati huo walikuwa ni wahusika wakubwa wa biashara ya uvuvi haramu ambapo hutumia makokoro ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria katika kuvua samaki. 

Tuliziona juhudi za Rais Magufuli za kupambana na yote hayo kwa juhudi na maarifa licha ya kukumbana na changamoto za hapa na pale za kiutendaji, ambazo wakati mwingine ziliweza kumkwaza kwenye utendaji wake. 

Suala la rushwa ni tete kwani hata vitabu vya dini vinaonyesha ni jinsi gani rushwa iliweza kumshawishi mmoja wa wanafunzi na kipenzi chake Yuda Isikariote ambaye alimwuuza Bwana wake (Yesu Kristo) kwa rushwa ya vipande 30 vya fedha! 

Athari za rushwa hata kwa mataifa makubwa duniani bado ni changamoto, lakini pia rushwa kwa nchi yenye watu masikini kama Tanzania madhara yake ni makubwa zaidi. 

Madhara ya rushwa hasa wakati huu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ni kuondoa uhuru wa mpiga kura, wagombea wenye vipaji na wenye uwezo wa kuongoza hushindwa kugombea kwenye uchaguzi kwa kukosa fedha na hii huharibu dhana nzima ya uwakilishi kwa kuwa watakaokuwa wamechaguliwa hawana ridhaa kamili ya wapiga kura wao.

Rushwa pia ina madhara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kiasi cha kuifanya jamii ya watu wanaoishi pamoja kuwa na kiu ya kusubiri kupewa na kufanya maamuzi ya mkato kwa kumpa haki mtu ambaye hastahili na kumchagua ambaye hastahili kwa ushawishi wa rushwa. 

Matukio yote ya rushwa huonekana kwenye chaguzi mbalimbali za chama na serikali ambazo zimekuwa zikiendeshwa kuanzia ngazi za vitongoji, mitaa, vijiji, Kata, wilaya, mkoa hadi Taifa. 

Uchaguzi ni hatua muhimu ya wananchi kuonyesha ukomavu wao wa kidemokrasia na kupitia taasisi zao za vyama, wanalo jukumu la kushiriki kikamilifu kwenye mchakato huo kwa kuwachagua viongozi bora na si bora viongozi kwa ajili ya ustawi wa maisha yao. 

Wanatakiwa kufanya maamuzi yao bila vitisho wala kushurutishwa kwa rushwa au namna yoyote ile maana uchaguzi ni jambo linalohusu maisha ya watu na ustawi wao. 

Mwananchi akimchagua diwani au mbunge makini au kiongozi wa nchi makini maana yake ni kuwa atakutana na fedha zake za kodi kwenye barabara, huduma bora ya afya na ujenzi wa miundombinu imara itakayomwezesha kusafirisha mazao yake kwenda kwenye soko na huduma zingine muhimu.

Mwananchi anapokubali kupokea hongo ya fedha, rushwa, t-shirt na kofia za vyama vya siasa, maana yake anauza uhai wake wa watoto wake na wajukuu wake kwa kipindi ambacho uongozi uliochaguliwa utakoma kuwepo madarakani. 

Kwa miongo kadhaa sasa, chaguzi nyingi zinazofanyika ndani ya CCM zimekuwa zikigubikwa na rushwa ambayo imekuwa ikifanyika kisayansi zaidi na tumeona juzi Rais Magufuli akilalamikia uwepo wa rushwa hiyo. 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii, zipo rushwa ambazo hutolewa kama mikopo ya kwenda kwenye Saccos na zingine hutolewa kama zawadi au misaada ya ujenzi wa majengo ya taasisi za umma na baadhi ya wagombea ambao sio waaminifu. 

Kwa kifupi rushwa ndani ya CCM ina sura za kutisha, hubadilika mithili ya rangi ya kinyonga na watoaji wa rushwa hiyo ni watu wenye mbinu nyingi kulingana na mazingira ya mahali, nyakati na sehemu na kwa nani anayetarajiwa kukabidhiwa rushwa hiyo. 

Na ndio maana ilifika mahali rushwa ndani ya uchaguzi wa chama ilipata baraka kutoka kwa vigogo huku ikipewa majina laini likiwemo jina la takrima, ambalo kwa miaka kadhaa tulishuhudia mijadala mikali ya ndani ya chama hata bungeni ya kutoa baraka kwa jina hilo. 

Katika uchaguzi Mkuu wa chama uliopita, nilikuwa miongoni mwa wagombea wa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia Wilaya ya Ilemela.

Kwenye kinyang’anyiro hicho sikuweza kubahatika kuchaguliwa katika nafasi hiyo na badala yake Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela, ulimchagua Israel Mtambarike kuwa MNEC wa Wilaya ya Ilemela na viongozi wengine wa chama mkoa na wilaya zingine walichaguliwa. 

Safari yangu haikuishia hapo, katika uchaguzi mkuu uliopita, pia niligombea nafasi ya udiwani kupitia CCM katika Kata ya Kisaka Wilaya ya Serengeti, ambapo nilishiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama, ingawa vilevile kura hazikutosha na hivyo niliishia kwenye kura za maoni. 

Kuna mambo kadhaa ambayo niliyagundua ambayo hasa yamekuwa yakiendeshwa na chama katika kuwapata wagombea wake, huku yakiwa na changamoto kubwa ya tatizo la rushwa.

Kiuhalisia rushwa ndani ya CCM ni mbegu iliyoota kuanzia kwa wana CCM wenyewe, viongozi na hata marafiki na wapenzi wa CCM. 

Ni kitu cha kawaida sana pale wana CCM wanapomjua mtu anayetaka kutia nia ya kugombea ikiwa hata kwa tetesi, wao humwendea na kumwambia anawaachaje.

Ushawishi wa rushwa ndani ya CCM huanza kujengwa kisaikolojia kwa wagombea kabla hata ya kuitishwa kwa vikao muhimu vya chama. 

Ningeshauri kwa wanachama wanaoonekana kuwa na ushawishi mkubwa wa rushwa ndani ya chama na wao wadhibitiwe kwa kufutiwa uanachama wao.

Uchambuzi na kigezo muhimu kwa mgombea ndani ya CCM si sifa za uongozi na uwezo wa kuongoza, bali ni uwezo wa fedha alionao hata kama aliwahi kukosa sifa za yeye kuwa mgombea. 

Kwa bahati mbaya sana kinachotazamwa na viongozi wa chama katika ngazi za kata na wilaya hata mkoa kwa nafasi za udiwani na ubunge ni uwezo wa kifedha alionao mgombea na hii imesababisha vyama na nchi kuwakosa viongozi bora wenye sifa zisizotiliwa mashaka! 

Kwa utafiti wangu mdogo, mgombea wa nafasi ya ubunge au udiwani lazima awe ama mfanyabiashara au mwenye ukwasi wa fedha ndiye anayepewa nafasi na baraka ya kuchaguliwa kuwa diwani ama mbunge. 

Na tathimini ndogo niliyoifanya kwa mtu ambaye anawania nafasi ya udiwani hadi apate ushindi wa kiti hicho lazima atumie kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakizidi Sh milioni 250-300 na kwa nafasi ya ubunge si chini ya Sh milioni 300 hadi Sh milioni 400 kwa wakati ule. 

Swali la kujiuliza hapa kwa mwanachama mwenye sifa ya uongozi kwa nafasi zote mbili na akawa hana uwezo wa kifedha ni kukosa nafasi hizo. Kwa lugha nyingine ni kuwa kwa miaka kadhaa nchi imewapoteza viongozi wengi wenye sifa kwa kukosa fedha kwa ajili ya kushindwa kutoa rushwa au kununua uongozi. 

Hapo utashuhudia ofisi nyingi za chama ngazi ya wilaya na kata zinageuzwa kuwa ofisi za wagombea wenye fedha. Wao ndio wanaofadhili fedha za kuendesha vikao, kutafuta miziki na kufadhili burudani kwa ajili ya kampeni ili mradi azma yao ya kutaka kuongoza inafikiwa. 

Kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka 2015 wa ngazi ya udiwani, ambapo binafsi nilikuwa mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM ambapo baadhi ya viongozi wa chama hukosa sauti ya kusimamia maadili na kanuni ndani ya chama na hivyo kuruhusu wagombea wenye fedha kufadhili baadhi ya mambo muhimu. 

Aidha suala la maadili ya uongozi halipewi uzito unaostahili. Suala hili hujitokeza mara nyingi wakati wa kura za maoni na hivyo kusababisha mchakato huo katika ngazi ya kata kuwa na mzigo mkubwa wa gharama kutoka kwa wagombea. 

Mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ni wa gharama kubwa kuliko hata uchaguzi mkuu wenyewe wa kuelekea kwenye uchaguzi wa kapu kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa. 

Mathalani katika uchaguzi huo wa udiwani, ambapo tulikuwa wagombea saba kila mgombea alichangia gharama ya Sh 112,500 kama gharama ya uchaguzi ikiwemo ya Sh 10,000 ya kuchukulia fomu.

Hakuna sababu yoyote ya jimbo moja liwe la ubunge au udiwani kuwa na wagombea wengi zaidi ya 10/12 wa CCM.

Katika uchaguzi huo katika hatua ya awali hakuna vigezo mahususi vya kuwapata wagombea makini na wachache wenye sifa wasiojihusisha na rushwa, ingawa CCM imekuwa ikitumia hoja kuwa ni ushiriki mpana wa kuwapata wagombea wake na kila mtu kutimiza haki yake ya kidemokrasia. 

Mfano kadi za wagombea wa chama haitazamwi kikamilifu na hili ndilo eneo muhimu la kuanza kudhibiti viongozi bora, mfano baadhi ya wanachama wanaoenda kugombea hulipia ada zao kwa mara moja katika kipindi cha miaka mitano. 

Ili JPM aweze kufanikisha vita hii ya rushwa ndani ya CCM, ni sharti akijengee uwezo wa kutosha chama kiuchumi kuanzia ngazi ya kata na wilaya ambako huko ndiko kuna uchaguzi na uongozi muhimu wa chama, hatua ambayo ameianza vizuri.

Ni matumaini yangu kuwa viongozi wa chama watamsaidia Rais Magufuli katika jambo hili kubwa ili baadaye nchi iweze kuwapata viongozi watakatifu na sio wataka vitu.

Chama kiwe na miradi na vitega uchumi vya kutosha ili kuwezesha viongozi wake kutokuwa na ushawishi wa kuomba rushwa hata kwa mambo ya utendaji yaliyo ndani ya uwezo wao, hili nalo ni tatizo kubwa ndani ya CCM, mathani viongozi wa kata wa vijiji hawana hata usafiri wa kutekeleza majukumu yao ya kichama na wa kata pia. 

Mfano katika kupitisha majina ya wagombea nafasi za ubunge kuna udhaifu mkubwa ambao huonyeshwa na makatibu wa CCM wa wilaya, ambao ndio watendaji wakuu wa shughuli za kila siku za chama.

Baadhi ya viongozi na watendaji walio ndani ya CCM, hufikia hatua ya kuwalamba miguu wagombea nafasi za ubunge walio na fedha kwa kuishia kupendekeza majina yao kwenye vikao vya maamuzi kwa kuwashawishi wajumbe. 

Kwa upande wa kata, kwa wanachama wanaowania nafasi za udiwani, makatibu wa CCM wa kata nao kutokana na kuwa hoi kiuchumi na kukosa vitega uchumi ndani ya chama, tegemezi lao katika utekelezaji wa majukumu hata yale ya kawaida ya chama hutegemea wagombea wanaojitokeza kuwania nafasi ya udiwani.

Hakuna sababu ya mwanachama wa CCM kutumia gharama zake kwenye mchakato wa kuomba uongozi mwisho wa siku, hataweza kutekeleza majukumu yake kwa kufuata kanuni, taratibu za chama zilizopo maana yeye atakuwa ameununua uongozi na hali kama hii ndiyo inayoendelea kukigharimu CCM. 

Ni vyema mfumo wa kuwapata wagombea ndani ya CCM ukabadilishwa, watume majina yao mapema (wajisajili mapema) chama kipate muda mpana wa kuwachunguza mienendo na tabia zao, ikiwa ni kwa kiwango gani wanakubalika kwa jamii kabla ya kutumia ushawishi wa rushwa ili waweze kuchaguliwa.

Chama kipige marufuku watu wanaotumia umaarufu wao wa fedha na utajiri katika kuwania nafasi za uongozi. Mara nyingi baadhi ya wafanyabiashara waliochaguliwa kuwa ama wabunge au madiwani, baadhi yao wamepata kutumia nafasi hizo kwa kupitisha na kufanya mambo yao, lakini baadhi yao hawana dhamira ya dhati ya uongozi bali ni kutaka kupata “identity” tu ya ubunge au uongozi ili waweze kufanya mambo yao.   

Kwa awamu hii ya tano, mwenyekiti wa CCM ni vyema akaendelea na mpango wake aliouanzisha ndani ya chama wa kutenganisha siasa na uongozi, ili watu wenye dhamira ya dhati ya kufanya siasa kama zilivyo taaluma zingine wafanye siasa na wanaofanya biashara waifanye kwa uhalali ili serikali iweze kukusanya kodi. 

Ifanyike tathimini ya kina kila unapofika wakati wa uchaguzi kwa kila mgombea ili kujiridhisha kama ana dhamira ya dhati ya uongozi kwa nafasi anayoomba. 

Yote haya yakifanyika kwa dhati kwa kutanguliza uzalendo tutakuwa tumemsaidia Rais Magufuli katika vita dhidi ya rushwa ndani ya CCM na pia kuendelea kuijenga CCM mpya ambayo wanachama wake watakuwa hawaimbi tena wimbo wa rushwa kwa kikolezo cha unaniachaje! Mungu ibariki Tanzania.