Home Makala Vigogo wanaohama na kurudi CCM hujizika kisiasa

Vigogo wanaohama na kurudi CCM hujizika kisiasa

1188
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

Wiki mbili zilizopita Chama Cha Wananchi (CUF) kiliwasimamisha uanachama wanachama wake kadhaa wakiwemo Wabunge watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hatua hiyo ilitokana na mgogoro uliozuka wakati wa mkutano Mkuu wa chama hicho ulioitishwa kuchagua viongozi wakuu wa chama hicho na pia kuziba pengo la aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu nafasi hiyo Agosti mwaka jana.

Hadi sasa hatima yao kamili haijajulikana kwani wanatakiwa kuitwa kwenye vikao vya juu vya chama kujieleza kabla ya hatua kamili kuchukuliwa dhidi yao.

Mara nyingi suala la wanachama wa vyama vya siasa kufukuzwa kutoka vyama vyao (au kusimamishwa uanachama) na pia kuvihama vyama vyao limekuwa ni mtihani mkubwa kwa pande zote mbili – chama na mwanachama husika. Na hasa kama wanachama hao ni Wabunge.

Na kwa suala la kufukuzwa chamani kwa sababu yoyote ile, hasa kwa wanachama wa upinzani, wanapoamua kurudi CCM, basi ndiyo huwa mwisho wao kisiasa. Nitaeleza hapo mbele.

Aidha, utawala uliopo madarakani huangalia sana masilahi yake hata kama mwanachama husika anayefukuzwa siyo wa chama tawala – yaani CCM.
Kwa mfano harakati za uongozi wa Chadema mwaka 2014 za kumfukuza uanachama Zitto Kabwe, aliyekuwa Mbunge wa chama hicho wa Kigoma Kaskazini uliangaliwa sana na utawala wa CCM, kwani yeye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali (PAC) nafasi ambayo aliipata kwa nguvu za Wabunge wa CCM.

Wachunguzi wa mambo walisema Zitto alikuwa anakubalika CCM kwa sharti ya yeye kuwa upinzani. Siku zote yeye amekuwa akikana dai hilo. Hatimaye alifukuzwa na kukimbilia mahakamani ambako alipata zuio la muda hadi kipindi cha Bunge kilipomalizika alijiunga na chama kipya cha ACT na kufanikiwa kutetea Ubunge wake kupitia chama hicho.

Na wadadisi wa mambo waliendelea kusema kutokana jinsi kamati yake ya PAC ilivyolisimamia sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow Bungeni mwishoni mwa mwaka ule, utawala wa CCM na Chadema pia ulimwangalia kwa jicho jingine, siyo lile la awali.

Lakini kulikuwapo hili pia: Katika miezi ya mwisho mwisho ya Bunge la Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa mwaka 2005, Wabunge wawili wa Viti Maalum wa Chama cha Wananchi (CUF) – wakati huo ndiyo chama kikuu cha upinzani nchini walifukuzwa na chama chao kwa makosa ya kwenda kinyume na maagizo ya chama Bungeni.

Spika wa Bunge, wakati huo Pius Msekwa alikataa kutambua ufukuzwaji wa Wabunge hao kwa madai kwamba utaratibu haukufuatwa. Hivyo waliendelea kuwa Wabunge hadi Bunge lilipomalizika muda wake.

Kwa hivyo hata lile sakata la ‘kufukuzwa’ chamani kwa Zitto Kabwe halikuwa mfano hai uliokamilika– yaani tangu ujio wa vyama vingi karibu robo karne iliyopita, hakuna Mbunge (wa Jimbo) wa chama chochote cha upinzani aliyefukuzwa na kufukuzwa kwake kulikamilika.

Aliyekuwa Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed aliendelea kuwa Mbunge kutokana na zuio la Mahakama, pamoja na kufukuzwa kwake kutoka chama chake.

Hali kadhalika ilivyokuwa kwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila wa NCCR-Mageuzi, ingawa huyu baadaye alisamehewa na chama chake.

Kwa upande wa CCM hakuna Mbunge aliyefukuzwa kutoka chamani tangu ujio wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Mwaka 2014 Mwakilishi wa CCM wa jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar, Mansour Yusuf Himid, ambaye pia alikuwa Waziri wa Serikali ya Zanzibar alifukuzwa chamani kwa kwenda kinyume cha sera na maagizo ya chama, lakini hakukuwa na vuta nikuvute yoyote wala kwenda mahakamani kutafuta zuio, na baadaye alijiunga chama cha upinzani CUF.

Katika historia ni Wabunge wawili tu wa chama tawala (wa TANU, yaani kabla ya CCM) waliofukuzwa, mwaka 1968, wakiwemo Wilfrem Mwakitwange na Modest Chogga.

Na tukija kwa upande wa kuhama vyama, pia hili lina mazito yake, hasa kwa wale wanaotoka upinzani na kuhamia chama tawala – CCM. Hawa tunaweza kusema ‘wanarudi’ kwa sababu, kwa wale ambao ni vigogo, ndiko walikokuwa huko nyuma – enzi za mfumo wa demokrasia wa chama kimoja.

Lakini mara nyingi hawa hurubuniwa tu, kwani baada ya muda hutoswa na kupotea kutoka nyanja za siasa. Salim Msabaha, Mbunge wa CUF wa Mji Mkongwe, Zanzibar katika miaka ya 90 alidai alitekwa na watu wasiojulikana – kumbe ilikuja kudhihirika kwamba alirubuniwa na CCM.

Kutokana na hatua yake hiyo, alikuwa moja kwa moja kajifukizisha kutoka CUF. Baada ya kupewa nyadhifa mbalimbali katika CCM haikupita miaka mingi akawa hasikiki kabisa kisiasa.

Mfano mwingine ni aliyewahi kuwa mwanachama mashuhuri wa CUF, Richard Tambwe Hizza aliyehamia CCM kwa mbwembwe nyingi, lakini sasa hivi hayuko kabisa katika medani za siasa, ingawa katika kampeni za uchaguzi wa mwaka jana alionekana katika majukwaa ya UKAWA.

Aidha, aliyewahi kuwa Mbunge machachari wa Ubungo (baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi), Dk. Masumbuko Lamwai wa NCCR-Mageuzi. Naye tangu arejee CCM hajasikika kabisa kisiasa – ingawa ilielezwa aliachana na siasa na kurudia taaluma yake ya uanasheria.

Mara nyingine kuhama chama hufanywa kuwa tukio kubwa kwa lengo la propaganda tu kwa lengo la kukikweza chama. Kwa mfano – siku za mwisho mwisho za kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, aliyewahi kuwa Mbunge wa CUF wa jimbo la Chake Chake, na Kiongozi wa kwanza wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Fatma Magimbi alitangaza kukihama chama chake na kurudi CCM.

Hilo lilifanyika katika mkutano mkubwa wa hadhara wa kampeni uliohutubiwa, pamoja na vigogo wengine wa CCM, pia na mgombea wa urais wa CCM Jakaya Kikwete maeneo ya Kawe, Dar es Salaam. Akiwa jukwaani alimkabidhi mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kadi ya CUF na kupewa ya CCM.

Lazima nikiri kwamba tangu siku hiyo, sijalisikia jina la mama huyu likitajwa popote pale, katika vyombo vya habari au kwingineko. Kuna baadhi ya watu walisema kuwa mama huyu kutokana na hatua yake hiyo huenda alitarajiwa kupewa wadhifa hususan ule wa Ubunge wa kuteuliwa.

Kikubwa CCM wanachotaka ni propaganda – lile  tukio la kutangazwa kuhama kwa mwanachama wa upinzani, hasa kama ni kigogo katika chama hicho. Baada ya hapo dili inakuwa imemalizika. Lakini tumeona tofauti katika utawala huu wa Rais John Magufuli.

Wakati wa Mkutano Mkuu wa chama chake maalum wa kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti baadhi ya vigogo waliohama kutoka chama hicho na kujiunga Chadema kabla ya kampeni za uchaguzi wa mwaka jana walitangaza kurejea chamani. Hata hivyo Magufuli alionekana kuwakejeli kwa kuwafananisha kama ng’ombe waliokatika mikia waliorudi kundini.

Na si hapo tu – mwezi uliopita Magufuli huyo huyo alizuia tukio moja lenye kiashiria za kipropaganda katika mkutano wa hadhara alioufanya jijini Mwanza.

Viongozi kadha wa chama chake walikuwa wametayarisha orodha na kadi za wanachama wa upinzani (na wale waliokuwa wamekihama chama hicho na kujiunga na upinzani) ili wamkabidhi jukwaani pamoja na kadi zao na kutangaza wamerudi chamani na hapo hapo kupewa nafasi ya kuongea jukwaani kuwaponda wapinzani.

Ilionekana Magufuli alilitambua hili mapema na hivyo kuzuia tukio hilo lisifanyike kwa kusema wakafanyie huko kwenye matawi ya chama. Alinikumbusha ya kigogo mwingine wa CCM, Juma Mwapachu ambaye wakati wa kampeni mwaka jana aliamua kujiondoa chamani na kurudisha kadi ya chama tawini kwake na mwaka huu, baada ya kubadili mawazo alikwenda tena tawini hapo hapo kuichukua kadi yake.

Lakini hali huwa tofauti kabisa iwapo anayefukuzwa anaamua kwenda chama kingine cha upinzani, siyo chama tawala. Kwa mfano David Kafulila aliwahi kuwa Chadema, akafukuzwa kule lakini akaamua kuingia NCCR-Mageuzi, na baadaye kuwa Mbunge. Hali kadhalika Wilfred Lwakatare aliyekuwa mwanachama na Mbunge wa CUF alihama kutoka CUf na kujiunga Chadema na hatimaye kuwa Mbunge tena.