Home Afrika Mashariki Vijana wabebeshwa ushindi wa Ukawa

Vijana wabebeshwa ushindi wa Ukawa

1345
0
SHARE

USHINDANI wa kisiasa uliojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, pamoja na mambo mengine, unatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hamasa ya mabadiliko waliyonayo vijana. RAI limebaini. Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ndiye anayetajwa kuwavutia vijana wengi zaidi kutokana na hoja kwamba yeye ndiye wakala sahihi wa mabadiliko.

Lowassa alipachikwa nafasi hiyo ya wakala wa mabadiliko tangu akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hadi alipoamua kujiengua ndani ya chama hicho na kutimkia Chadema baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mbio za urais.

Waziri Mkuu huyo anatajwa kuwa sehemu ya hamasa kwa vijana kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura tangu akiwa CCM na kasi iliongezeka zaidi baada ya kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema kinachoshirikiana na chama cha Wananchi- CUF, NCCR-Mageuzi na NLD chini ya kivuli cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni zinabainisha kuwa zaidi ya vijana milioni tano walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR). Wakati NEC ikibainisha idadi hiyo ya vijana, juzi Taasisi ya utafiti ya Twaweza imeeleza kuwa vijana wengi wanamuunga mkono Lowassa ambaye amebebeshwa bendera za vyama vinavyounda Ukawa kwenye mbio za urais. Tafiti mbalimbali za kisomi zilizokuwa zikitolewa kabla ya Lowassa kuhamia Ukawa zilionyesha anakubalika zaidi kwa vijana. Katika utafiti uliofanywa na taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET), ulionyesha kuwa Lowassa ameongoza kwa asilimia 27, huku Dk. Magufuli akishika nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia 6.6.

Katika utafiti huo ambao ulitumia mfumo wa sampuli nasibu (random sampling), vijana wengi zaidi walitoa maoni yao. Wahojiwa 334 sawa na asilimia 26.7 walikuwa kati ya umri wa miaka 36 – 45 na wengine 201 kati ya miaka 18 – 25 wakiwa ni asilimia 16.1. Wahojiwa wachache yaani zaidi miaka 66 walikuwa ni 70 sawa na asilimia 5.6. Wanawake katika wahojiwa walikuwa 626 sawa na asilimia 501, huku wanaume wakiwa ni 624 sawa na asilimia 49.9. Asilimia 30 ya wahojiwa wote walitoka mijini, huku asilimia 70 wakitoka maeneo ya vijijini. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameielezea hali hiyo kuwa ya kipekee kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwani pamoja na wengi wao kumkubali Lowassa, lakini pia wapo wanaompigia chapuo mgombea urais CCM, Dk. John Magufuli. Wengi wanaamini ushindi wa Lowassa na Ukawa yake uko mikononi mwa vijana kwa sababu wao ndio wanaonekana zaidi kutaka mabadiliko. Hatua hiyo inatajwa kuongeza chachu, hamasa na ugumu wa uchaguzi wa mwaka huu kama vijana watajitokeza kupiga kura kama walivyofanya wakati wa kujiandikisha.

Hamasa ya vijana kutaka mabadiliko imetafsiriwa kuwa kichocheo cha Lowassa katika kufanikisha safari yake ya matumaini aliyoianza miaka kadhaa iliyopita na kwamba pamoja na kuungwa mkono na vijana wa Ukawa, lakini pia nyuma yake yapo makundi kadhaa ya vijana waliosalia ndani ya CCM. Uwapo wa wanaCCM wanaomuunga mkono Lowassa umeshtukiwa na Dk. Magufuli ambaye amekiri wazi kuwapo kwa makundi yanayomuunga mkono yeye mchana huku usiku wakihamishia nguvu zao Ukawa.

Hali hiyo inayotajwa kuongozwa zaidi na vijana inadaiwa kutishia kwa kiasi kikubwa ushindi wa Dk. Magufuli ambaye kwa kiasi kikubwa anatajwa kuwa ni mgombea wa CCM aliyeamua kujibeba mwenyewe bila kutumia turufu ya chama chake kama ilivyo kwa Lowassa ambaye jina lake ni mtaji mkubwa kwa wapiga kura. Ripoti ya juzi ya Twaweza mbali ya kumpa ushindi mkubwa Dk. Magufuli, lakini imebainisha wazi kuwa katika kipengele cha kiongozi anayeaminika kuleta mabadiliko Lowassa ndiye namba moja kwa asilimia 12 huku akifuatiwa kwa asilimia saba na Dk. Magufuli.

Matokeo hayo madogo yanayosomeka kwenye kipengele cha mabadiliko ambacho ndio msingi wa hamasa ya vijana katika uchaguzi wa mwaka huu yanatajwa kutosha kumbeba Lowassa. Aidha, ushiriki mkubwa wa vijana katika kuwania uongozi wa kisiasa nao umetajwa kuwa jambo linaloweza kumbeba Lowassa, hasa ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano wa idadi kubwa ya watu kujitokeza kupiga kura tofauti na ilivyokuwa kwenye chaguzi zilizopita. Kwa mujibu wa tafiti zilizotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, zaidi ya watu milioni 24.2 nchi nzima wanatarajiwa kupiga kura.

Mhadhiri wa kitivo cha siasa kutoka Chuo Kikuu cha St. Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu aliliambia RAI kuwa ni kweli vuguvugu na hamasa ya vijana litaleta mabadiliko makubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Mabadiliko ya awali ni kujitokeza kwao kujiandikisha, tuliwaona kwenye foleni wamejiandikisha kwa wingi, kwenye kupiga kura wanasema wana vichinjio, kila kijana amejitayarisha, ni wazi kuwa watajitokeza kwa wingi kupiga kura na kwa kweli hakuna kijana › Wahojiwa 334 sawa na asilimia 26.7 walikuwa kati ya umri wa miaka 36 – 45 na wengine 201 kati ya miaka 18 – 25 wakiwa ni asilimia 16.1. Wahojiwa wachache yaani zaidi miaka 66 walikuwa ni 70 sawa na asilimia 5.6. aliyejiandikisha ili kuipigia kura CCM ndio maana hata wameamua kubadilisha lugha na kusema wanataka mabadiliko jambo ambalo si ajenda ya chama hicho tawala kwani wao ndio waliikataa Katiba mpya ambayo ndiyo nguzo kuu ya mabadiliko. Sasa ni mabadiliko gani wanayataka CCM nje ya Katiba hiyo? Kwa upande wake Dk. Benson Bana alisema upo uwezekano wa vijana kubeba ushindi wa Ukawa, lakini nao huwa wanapima, “Kwa mfano vijana wapya wapiga kura zaidi ya milioni tano, wamejiandikisha kupiga kura, Lakini tusisahau kuwa vijana hao wamegawanyika, hivyo huwezi kujenga hisia kuwa vijana wote wanalalia huku. “Na uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti kwa sababu masuala yamejikita kwa watu binafsi, Dk. Magufuli ameamua kuitosa CCM na kusimama mwenyewe kwa sababu ni mchapakazi, nako kule kwa wapinzani Lowassa ameitosa Ukawa kwa sababu amewekeza vizuri kwenye urais, hivyo tunamuona Lowassa ana muonekano mzuri kwa wapiga kura wake.

“Hivi vyama vyote vimewekwa kando, ingawa si jambo zuri, kwani uchaguzi ni namba na kura, CCM na Ukawa hawana mvuto tena kwa watu wengi ndio maana tunaona kuwa mgombea binafsi anaweza kubeba karata hiyo,”alisema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama cha ACT Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo alisema ni kweli vijana ndio nguzo ya ushindi ya Ukawa na ndio maana tafiti nyingi zinaonesha kuwa vijana wengi wanamuunga mkono Lowassa tofauti na ilivyo kwa Dk. Magufuli ambaye anaungwa mkono na watu ambao hawajasoma pamoja na wale waliopo vijijini.