Home Habari Vijana wanatambua nafasi yao Uchaguzi Serikali za Mitaa?

Vijana wanatambua nafasi yao Uchaguzi Serikali za Mitaa?

671
0
SHARE

HASSAN DAUDI

NI mwezi mmoja na siku kadhaa zilizobaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Unatarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu. Yapo mengi yaliyozungumziwa mara tu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilipotangaza siku hiyo ya uchaguzi.

Hata hivyo, hapa sitagusia kasoro zilizotajwa na upande wa upinzani dhidi ya kanuni zilizopo, hasa ile ya kipindi kifupi cha kampeni (siku saba), badala yake nimechagua kujikita katika ushiriki wa vijana katika uchaguzi huo.

Unaweza kujiuliza, kwanini vijana na si makundi mengine ya watu? Kwanini si wazee au walemavu? Binafsi nimesukumwa kulizungumzia kundi hilo kutokana na sababu kuu mbili, nikiamini hayo mengine yamekuwa yakizungumziwa kwa kiasi kikubwa.

Mosi, ni takwimu zilizopo. Ni asilimia 3.1 pekee ya raia wa Tanzania milioni 58 wenye umri zaidi ya miaka 64, kwamba zaidi ya asilimia 44.8 ya raia wa nchi hii wana umri chini ya miaka 15, wakati asilimia 52 ni wale wanaoanzia hapo 15 hadi miaka 64.

Kwa mantiki hiyo basi, itoshe kusema haihitaji elimu ya kiwango cha juu kung’amua kuwa Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine, inawategemea zaidi vijana katika shughuli zake za maendeleo.

Je, ikiwa sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania ni vijana, unawezaje kuliweka kando kundi hilo katika mchakato muhimu kama huo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Hakika nastahili kuwazungumzia.

Pili, kama yalivyo makundi mengine, wakiwamo wanawake na wazee, kundi hilo pia ni wadau wakubwa wa kila hatua chanya ya jamii inayowazunguka. Katika hilo, nitakupa mfano wa kile kinachoendelea mitaani, ambacho huenda hujawahi kukutana nacho.

Maeneo mengi, nikitolea mfano jijini Dar es Salaam, kumekuwa na vijana waliojitolea kuimarisha ulinzi (sungusungu) katika mitaa yao, wakiifanya kazi hiyo nyakati za usiku, jambo ambalo kwa kiasi cha kuridhisha kimepunguza matukio ya uhalifu.

Kuonesha ni kwa kiasi gani wanaifanya kazi hiyo kwa nia njema kwa jamii yao, wamekuwa wakijipatia ujira mdogo tu unaotokana na fedha wanazokusanya kutoka kwa wakazi wa eneo lao.

Huo ni mfano ndogo tu wa isivyowezekana kwa namna yoyote ile kuwatenganisha vijana na hatua za maendeleo katika jamii yao walikozaliwa na kukulia.

Lakini sasa, changamoto kubwa ambayo binafsi nimekuwa nikiishuhudia na hata nikitarajia kuiona pia mwaka huu, ni uelewa mdogo wa sehemu kubwa ya vijana juu ya nafasi yao katika ulingo wa siasa, nikilenga zaidi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Utafiti mdogo unaweza kubaini kuwa vijana wa aina hiyo wamewaganyika katika makundi mawili. Kwanza, wapo wale ambao kwa licha ya kuwa na elimu, kutotambua umuhimu wao katika jamii kumewafanya wawe vibaraka wa vyama vya siasa, wakifahamu fika kuwa wenzao wanashinda vijiweni kwa kukosa ajira.

Hao ni wale wanaotumia ushawishi wao ndani ya jamii unaotokana na viwango vikubwa vya elimu walizonazo kuwapigia debe wagombea wasio na sifa, ambao aghalabu hutumia fedha au zawadi zingine kujikusanyia mtaji wa kura za wananchi.

Vijana wa aina hiyo walishawahi kuzungumziwa na mwandishi mahiri wa vitabu nchini, Said Mohamed, katika tamthiliya maarufu ya ‘Kivuli Kinaishi’. Nilibahatika kuisoma tamthiliya hiyo nikiwa kidato cha tano. Naweza kuwafananisha vijana wa aina hiyo na wale waliokuwa viongozi wa Giningi iliyokuwa ikiongozwa na Bibi Kilembwe.

Kile kinachoakisi uhusiano usio na afya kwa jamii kati ya vijana wasomi na wanasiasa, kule Giningi rangi nyeupe ingebadilishwa jina na kuitwa nyeusi endapo tu hilo lingekuwa na manufaa kwa Bibi Kilembwe na wenzake.

Aidha, nikitoka huko, katika msemo maarufu wa Mwalimu J.K Nyerere naye aligusia hilo la vijana wa kundi nililolitaja, aliposema: “Wale waliobahatika kupata elimu, wanatakiwa kulipa jasho walilovuja wenzao (wasio na elimu).

“Ni kama mtu aliyepewa chakula chote cha kijiji chenye njaa ili apate nguvu ya kwenda eneo la mbali kuleta neema. Kinyume chake, mtu huyo anafanikiwa na anashindwa kurudi. Huyo ni msaliti tu…“

Si dhambi kwao kushika nafasi za uongozi, ni jambo zuri na lenye afya kwa ustawi wa jamii lakini alichosisitiza Mwalimu hapo ni kwamba vijana wasomi, ambao wengi wao wamesomeshwa kwa mikopo itokanayo na kodi za wananchi, wakiwamo wazazi wa wenzao wasiosoma.

Msisitizo ni kwamba hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutumia maarifa yao kwa maendeleo ya jamii na si kujinufaisha wao na kikundi fulani cha watu wanaowatumikia katika ulingo wa siasa.

Ukiacha hao, kundi la pili la vijana ni lile lililoamua kupuuzia kila kitu kinachohusu uchaguzi, likiamini ni jambo la kikundi fulani cha watu. Wao watapokea zawadi na fedha za mgombea lakini usitarajie kuwakuta wamepanga foleni kusubiri kuingia chumba cha kupiga kura.

Ikiwa watafika katika baadhi ya mikutano ya kampeni, basi si kwa lengo la kusikiliza na kuchambua sera za wagombea ili kuona umuhimu wake kwa jamii yao, bali walikwenda kupiga ngoma, kucheza na kuimba kwa kuwa walipewa kiasi fulani cha fedha na chama husika.

Hatari iliyopo kwa jamii ni kwamba hata kama kundi hilo litakwenda kupiga kura kutokana na msukumo wa marafiki, kuna uwezekano mkubwa wa kumchagua mgombea asiyefaa kutokana na ukweli kwamba hawakujishughulisha na kampeni, hivyo hawana uelewa mpana wa sera za vyama mbalimbali.

Kama ambavyo imekuwa kwa wenzao wa nchi zingine barani Afrika, mara nyingi kundi hili litakwambia halina mpango na masuala ya uchaguzi kwa sababu halioni mabadiliko yoyote katika maisha yao licha ya kwamba viongozi wamekuwa wakipishana madarakani.

Kwamba kiongozi anayemaliza muhula wake wa kwanza, akitaka nafasi ya kurejea madarakani, hatofautiani kiutendaji na tuliyemwondoa miaka mitano iliyopita kwa kuwa uhaba cha maji na umbali mrefu kuifuata hospitali vimebaki kuwa changamoto licha ya kwamba ni miaka 10 sasa imepita.

Vijana wa aina hiyo wanaona wamesalitiwa na viongozi waliowapeleka madarakani kwa kuwa hakuna mradi wowote ulioanza jimboni licha ya kwamba aliahidi kutengeneza nafasi za kazi wakati wa kampeni zake. Ni katika hilo, mwandishi wa vitabu, Rachel Jackson, aliwahi kuionya jamii juu ya namna inavyoshindwa kuwaandaa vijana, aliposema: “Si kwamba vijana ndiyo wanaoushindwa mfumo, bali ni mfumo ndiyo unaoshindwa kwenda na vijana.”