Home kitaifa ‘Viongozi kichocheo cha ujangili’

‘Viongozi kichocheo cha ujangili’

877
0
SHARE
Naibu Mkurugenzi wa Kuzuia Ujangili nchini, Robert Mande.

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MKWAMO wa mkakati wa kutokomeza kabisa matukio ya ujangili kwenye hifadhi mbalimbali nchini unadaiwa kuchangiwa pakubwa na ushiriki wa baadhi ya viongozi.

Pamoja na kuwapo kwa mafanikio makubwa ya kupambana na ujangili nchini yaliyochangiwa na ushirikishwaji wa jamii inayozunguka hifadhi, imeelezwa kuwa wapo baadhi ya viongozi wamekuwa mstari wa mbele kufadhili mitandao ya ujangili.

Naibu Mkurugenzi wa Kuzuia Ujangili nchini, Robert Mande, ndiye aliyeibua madai hayo wakati wa mazungumzo yake na Waandishi wa Habari za Mazingira wa Tanzania na Thailand walioko kwenye programu ya kuandika habari za kupinga ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Waandishi hao wako katika programu maalumu iliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la RTI lionalotekeleza mradi wa USAID-Protect. 

Mande alisema pamoja na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kupambana kwa nguvu na ujangili, lakini wapo baadhi ya viongozi wanashiriki kikamilifu kwenye uhalifu huo.

Mande ameweka wazi kuwa kwa sasa kuna kizingiti kikubwa kilicho mbele yao ambacho ni aina mpya ya rushwa inayowagusa baadhi ya viongozi umma na wafanyabiashara wakubwa.

Mande amesema Ujangili umekuwa ni tatizo kubwa sana nchini hasa kati ya miaka ya 2010 hadi 2014 kiasi kwamba zaidi ya asilimia 60 ya tembo waliokuwepo walitoweka jambo ambalo liliilazimu serikali kuanzisha mpango maalumu wa kitaifa wa kupambana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu. 

Mwaka 2013 Serikali ilianzisha Operesheni Tokomeza kutokana na ukubwa wa tatizo, ambapo iliunganisha vyombo vyote vya usalama ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Tatizo hili lilikuwa kubwa kutokana na kuwa na uhitaji mkubwa wa soko huko Asia ambapo kilo moja ya jino la tembo iliuzwa kwa dola 500 hadi 2000, hivyo ni biashara ambayo iliwaleta pamoja watu wenye uchu wa pesa na kutajirika na pia inaunganisha makosa ya rushwa, utakatishaji wa fedha, uwindaji haramu na mengineyo. 

“Na hivi karibuni katika kuchambua tumegundua kuwa kuna tatizo jingine kubwa la ushiriki wa wataalamu waliopo serikalini au waliopo kwenye mashirika ya umma na ya binafsi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia rasilimali, na ndio unaosababisha ujangili kuendelea na kuwa mgumu kupambana nao.

“Mande amesisitiza kuwa, wamegundua hilo ni tatizo kubwa Kitaalamu na ni aina mpya ya rushwa ambayo inahusisha watendaji serikalini, ambayo wanaiita ‘White Collar Crime’

Alisema ni rahisi kwa mtu mwenye nafasi kushawishiwa kushiriki kwenye uhalifu bila kujulikana kutokana na nafasi yake ya utendaji ndani ya Serikali.

“Kupambana na mhalifu ambaye humjui na ana nafasi kwenye udhibiti wa sheria ni ngumu sana, kutokana na hali hiyo tumewashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika kikosi chetu kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili, Utalii na Mazingira ili kuweza kupambana na ujangili wa wanyama pori kikamilifu,” alisisitiza Mande

UJANGILI UMESHUKA

Miaka sita iliyopita hali ya ujangili ilikuwa inatisha, halikuwa jambo la ajabu kwa kila siku kusikia taarifa za kuuliwa kwa tembo.

Hata hivyo kwa sasa hali ni tofauti, tangu mwaka 2016 mambo yamebadilika, ujangili umepungua kwa kiasi kikubwa.

Mande alilizungumzia hilo kwa kumwaga pongezi nyingi kwa Rais Magufuli ambaye anaonekana kusimamia kwa karibu rasilimali za nchi.

“Ninachopenda kuwaeleza hapa ni kwamba kuanzia mwaka 2016 hadi sasa ujangili wa tembo umeshuka sana, haya ni matunda ya ushirikiano baina ya vyombo vyote vya Serikali na sekta binafsi,” alisema.

Alisema ujangili ulikuwa tishio kwenye miaka ya 2000 hadi 2014, ambapo asilimia 60 ya tembo walitoweka na ndipo Serikali ilianzisha mpango wa kitaifa wa kupambana na ujangili.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Freddy Manongi alisema  kuna mafanikio katika kupambana na ujangili kwani katika kipindi cha miaka minne ujangili umepungua kwa kiasi kikubwa sana nchini Tanzania, huku akitilia mkazo kupungua zaidi kwa ujangili huo katika Hifadhi ya Ngorongoro.

“Kipindi cha nyuma ilikuwa ni kitu cha kawaida kuona mizoga ya tembo, mimi mwenyewe sijaona mzoga wa tembo uliouawa kwa ujangili katika hifadhi kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli. Na kama utaukuta mzoga basi utakuwa umekufa kwa sababu nyingine kama vile magonjwa na lazima utaukuta na meno yake,” alisisitiza Kamishna Manongi.

“Vilevile, changamoto kubwa sasa ni idadi ya watu kuongezeka na kufikia 95,000 ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro hali ambayo inasababisha ongezeko la shughuli za binadamu ndani ya hifadhi lakini pia idadi ya mifugo inaongezeka sana. Na muingiliano kati ya binadamu na wanyama unasababisha magonjwa kama vile minyoo na kimeta.

“Kwahiyo suala la binadamu kupata magonjwa yanayotokana na wanyama pori sio zuri na hatukubaliani nalo na sio lengo letu la Uhifadhi wala la maendeleo  . 

Pia ongezeko hilo sio zuri sana kwa hifadhi kwani kuna ongezeko la  idadi ya watu wanaoumizwa na wanyama wanaouwawa na wanyamapori. 

Na ukiangalia wenyeji ndani ya hifadhi wanategemea mifugo hiyo kwa maisha yao, hivyo kama watauwawa basi hali yao itaendelea kuwa duni. Kwahiyo ule muingiliano sasa hivi unatuletea shida kweli kwani tunajiuliza huu mfumo utaendelea mpaka lini, hali itakuwa vipi kwakuwa sasa ardhi inakuwa ndogo kukidhi mahitaji, tumeanza mikakati yakufanya mabadiliko ili wanyamapori waendelee na watu wawe na maisha mazuri,” alisema Dk. Manongi

Alisema kama Mamlaka wamekuwa wakipata fedha nyingi kutokana na wanyama pori, lakini bado maisha ya watu yameendelea kuwa duni hali inayowafanya wadau wa uhifadhi kuumiza vichwa kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya tatizo hilo.

“Tunapata fedha nyingi sana kutokana na uhifadhi, ni zaidi ya shilingi bilioni 120 kwa mwaka na tumekuwa tukitoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya jamii, lakini bado hatuoni maendeleo na watu bado wanazidi kuwa masikini, na eneo linazidi kuharibika kutokana na ongezeko la makazi ya kudumu, ongezeko la maisha ya binadamu. Hivyo ni vyema kutatua huu mtego wa maendeleo na uhifadhi kwa kuangalia mfumo mzuri ambao utaboresha maisha ya binadamu  na uhifadhi wanyamapori na mali kale zilizopo.”

Kwa upande wake Meneja mradi wa taasisi ya PAMS, Max Jenes amesema  wameiona haja ya kuwashirikisha vijana kikamilifu kwakuwa wanaelewa kwauharaka zaidi na ambao ndio taifa la kesho, lakini kama namna yakuwatambua kuwa wao pia wana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii zao na haswa katika mausala ya uhifadhi.

“Kwa upande wetu tumejikita katika kuwaelimisha vijana haswa wa sekondari, tunawafundisha masomo maalumu ya uhifadhi huku tukiwapatia vitabu vya hadithi lakini pia tunafanya michezo inayoambatana na mashindano maalum pamoja na kufanya shughuli za nje kama vile kupanda miti,” alisema Max

KAMPENI YA OKOA TEMBO

Mratibu wa kampeni ya Okoa Tembo Tanzania inayofadhiliwa na mradi wa USAID PROTECT, Shubert Mwarabu, amesisitiza kuwa katika mapambano haya ya ujangili ni vyema vijana wakawa na moyo wakujitolea kwani suala zima la uhifadhi wa wanyamapori linawahusu watu wote na ni suala ambalo kila mmoja ana wajibu katika hilo.

“Tunafurahi kusema kwamba kampeni yetu ambayo tunatumia muziki ili kuwajuza watu kinachoendelea  imepata mwitiko mkubwa na kuleta matokea chanya katika suala zima la kupambana naa ujangili,”.

HITIMISHO

Serikali kupitia Wizara yake inaendelea kuimarisha vivutio vya utalii hapa nchini kwa kupanua jiografia ya maeneo ya utalii sambamba na kuongeza vivutio ili kuongeza idadi ya watalii na mapato. Kazi hii muhimu, ambayo kufanikiwa au kutofanikiwa kwake hakuathiri tu Bara la Afrika bali ulimwengu mzima kwa ujumla inahitaji wadau wote wa uhifadhi waendelee kufanya kazi pamoja kwani ndiyo njia sahihi yakupambana na ujangili.