Home Uchambuzi VIONGOZI LINDI MSALABA HUU NI WENU

VIONGOZI LINDI MSALABA HUU NI WENU

1883
0
SHARE

NA JIMMY CHARLES, LINDI

HAKUNA binadamu yeyote mwenye akili timamu asiyependa maendeleo yake na ya jamii iliyomzunguka kwa ujumla.

Kila binadamu timamu anapenda maendeleo, anapenda kuishi maisha bora yenye kumfanya aifurahie dunia.

Hilo ndilo hitaji la wanavijiji wa vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti vilivyopo wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Jamii hii inalalamikia uwapo wa mwekezaji asiye na tija, mwekezaji aliyeshikilia eneo lao kubwa kwa miaka mingi, huku kukiwa hakuna chochote kinachofanyika kwenye maeneo hayo.

Malalamiko yao ni kwa kampuni ya BioShape iliyokuwa na dhamira ya kuzalisha nishati kwa kutumia mimea ya mibono, ambayo ilitajwa kuwa nishati salama kwa mazingira.

 Ujio wa kampuni ya BioShape mwaka 2006, ulikuwa wenye heri na furaha tele kama nilivyopata kusema katika makala zangu zilizotangulia, kila mkazi wa vijiji hivyo hasa Mavuji alifurahia.

Kwa namna walivyotua nchini wakiwa na ahadi kedekede isingekuwa rahisi kwa  mwananchi hao kukusikiliza neno lolote baya linaloihusu kampuni hiyo hiyo ya kigeni kutoka Uholanzi.

Kampuni hiyo ilitua nchini kwa lengo la kuzalisha mafuta kwa kutumia mbegu za mibono. Uzalishaji huo ulitajwa kuwa salama kwa mazingira.

Kiasi cha dola milioni 9.6 kilidaiwa kutumika katika mradi huo wa nishati ya mimea ambao kwa sasa umeacha maumivu na masononeko kwa wananchi wa Kilwa.

Mwaka 2006, kampuni hiyo ilikodi zaidi ya hekta 40,000 za eneo la pwani lenye misitu katika wilaya ya kusini ya Kilwa kwa ajili mibono (Jatropha), ambayo mbegu zake hutumika kutengenezea mafuta ambayo yanaweza kuendesha mitambo mbalimbali yakiwemo magari.

Ukodishaji huo wa ardhi ya vijiji hivyo unatajwa kutawaliwa na harufu mbaya ya rushwa iliyosababisha wajuzi wa mambo kuwarubuni wanakijiji ili kutoa ardhi yao bila vikwazo.

Nao walitoa kwa kuaminishwa kuwa tiha ingekuwa sehemu ya maisha yao, jambo la kusikitisha ni kwamba tija ile iliishi kwa muda mfupi mifukoni mwao na baadae kutoweka na kuwaachia maumivu na masononeko ambayo yamewatawala hata sasa.

Kwa wiki nne mfululizo nimekuwa nikiandika makala zenye kuzungumzia kadhia wanayokumbana nayo wanavijiji hao.

Makala zangu zilizanza kwa kumwomba Rais Dk. John Magufuli asikie kilio cha wananchi wake hao kwa kumwomba aone haja ya kufuta umiliki wa ardhi hiyo kwa mwekezaji ili eneo lirejeshwe kwa wanakijiji ama lielekezwe kwa mwekezaji mwingine.

Nasisitiza kumwomba Rais Magufuli asikilize kilio cha wananchi wake hao ili angalau waondokane na dhana potofu iliyojengeka vichwani mwao kuwa Serikali haiwajali.

Wananchi wa vijiji hivyo wameachwa na sononeko,wanasononeka, kinachowasononesha ni baadhi ya viongozi wao kuwakengeusha kwenye mchakato mzima wa ujio wa BioShape na hadi kuondoka kwao pamoja na ukimwa uliotawala.

Kutokana na kilio cha wananchi hao, nalazimika kuamini kuwa msalaba huu wa kuhakikisha haki ya wananchi wa vijiji hivyo inapatikana uko mabegani mwa viongozi wa Lindi kwa ujumla wake kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya mpaka mkoa.

Jambo la kutioa moyo ni kauli ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Zablon Bugingo. Kiongozi huyu hana muda mrefu kwenye wilaya hiyo, lakini anaonekana kusononeshwa na suala hilo.

Bugingo, anasikitishwa na mchakato mzima wa suala hilo, lakini anashindwa kufikia maamuzi ya papo kwa hapo kwa sababu suala hilo ni la kisheria na mwenye dhamana ya kufuta au kumilikisha ardhi ni Rais.

Kwa ustaarabu na unyenyekevu mkubwa uliotawaliwa na upendo kwa watu anaowaongoza Bugingo anasema pamoja na ugeni wake kwenye Halmashauri hiyo, lakini anachokijua yeye ni kwamba Halmashauri iliridhia ujio na umiliki wa ardhi kwa  BioShape.

Hata hivyo anasema kwakuwa suala hilo kwa sasa halina mwelekeo mzuri, Halmashauri wanaiona haja ya kulirejesha eneo hilo ili aidha lirejeshwe kwa wananchi na kupangia matumizi bora au lielekezwe kwa mwekezaji mwingine mwenye tija.

“Tayari Waziri wa Ardhi ameshatuelekeza cha kufanya ili kulirejesha eneo hilo kwa wananchi  na tayari utaratibu umeshaanza,” alisema.

Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Godfrey Jaffary, aliiambia timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira waliokuwa chini ya mwamvuli wa JET kuwa, uwezekano wa eneo hilo kurudi kwa wananchi upo.

“Nikiri wazi kuwa kwa sasa wananchi wa vijiji hivyo vinne ambavyo ardhi yao iko chini ya mwekezaji, hawawezi kuitumia ardhi hiyo kwa sababu ni mali halali ya mwekezaji.

“Lakini uwezekano wa kurejeshewa ardhi yao upo, lakini mwenye uamuzi wa mwisho ni Rais. Tayari mwekezaji anaonekana kushindwa kutekeleza baadhi ya makubaliano hivyo ni suala la Rais kuamua tu.”

Akizungumzia hatua ya BioShape kutaka kulimilikisha eneo hilo kwa kampuni ya Somanga Property, Jaffary alisema suala hilo liliwafikia na hawakubaliani nalo.

“Tumesikia kuwa ardhi yote aliyokabidhiwa BioShape inataka kukabidhiwa kwa kampuni nyingine, sisi hatukubaliani na suala hilo kwa sababu utaratibu wa kisheria haujafuatwa.

“Ikumbukwe kuwa mwekezaji wa kwanza ameshaonesha dalili za kukiuka mkataba, sasa anawezaje kummilikisha mwekezaji mwingine kinyuma na utaratibu, hilo haliwezekani.”

Jitihada za kuwapata viongozi na watendaji wa mkoa wa Lindi bado zinaendelea ili kuhakikisha suala hilo linafikia tamati na tija inapatikana kwa pande zote husika.