Home Habari kuu ‘viongozi wengi waoga’

‘viongozi wengi waoga’

1583
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Mwenendo wa baadhi ya viongozi hasa Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakurugenzi kutishia, kuadhibu na wakati mwingine kuwaweka ndani baadhi ya wananchi, wanasiasa na hata watendaji wa Serikali, inatajwa kusababishwa na woga. RAI linaripoti.

Katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kuripotiwa kwa matukio ya wateule hao wa Rais, kutoa adhabu kwa viongozi wenzao hadharani.

Hatua hiyo inayoonekana kumea siku hadi siku imeonekana kuikera Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hali iliyomsukuma Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Zainab Chaula kukemea hali hiyo.

Katika mazungumzo yake na Wakuu wa wilaya na wakurugenzi 66 walioteuliwa Agosti mwaka huu, Dk. Chaula alisema anakerwa na vitendo vya viongozi wa wilaya kuwaweka ndani watumishi wanaowaongoza .

Aliwataka viongozi hao wa wilaya kufuata kanuni, taratibu na miongozo ya utendaji, kwani wizara yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka maeneo mbalimbali nchini yanayohusu uhusiano usioridhisha kati yao na wanao waongoza.

Katika kudhihirisha kuwa kinachofanywa na wateule hao si kitu kizuri, Dk. Chaula aliwataka viongozi hao kuheshimu taaluma za watumishi wanaowaongoza kwa sababu wapo katika nafasi zao kisheria.

“Tumekuwa tukisikia mkuu wa wilaya kamkamata yule mara kamuingiza yule ndani, hapana, tusifanye hivyo. Mnapaswa kutambua kuwa mpo kwa mamlaka, masuala ya kuingizana ndani, hapana.” Alisema.

Aidha, Agosti mwaka huu pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola aliwaonya wakuu wa mikoa na wilaya kutotumia vibaya sheria kuwaweka ndani wananchi akisema dhamira ya Serikali si kuwanyanyasa wananchi wake.

Kauli ya Lugola imekuja ilikuja siku chache baada ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo kukemea tabia hiyo akiwataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.

Mbali na Tamisemi kukerwa na hatua hiyo, lakini pia baadhi ya wasomi wameonekana kuungana na hatua hiyo, huku wakisema kuwa mwenendo huo wa viongozi wa wilaya na mikoa unasababishwa na woga na hofu ya kutumbuliwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utetezi wa Mtandao wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema hofu iliyojengwa miongoni mwa viongozi wa serikali ndio sababu ya kutumia madaraka yao vibaya.

“Kutokana na hali ya sasa ilivyo viongozi wengi wamekuwa waoga wanafanya kazi kwa hofu hivyo wanataka kuonesha kuwa wapo kazini.

“Pia sasa masuala ya utawala wa sheria hayazingatiwi sana. Hayapewa kipaumbele na wala hakuna anayeweza kuwakemea, mfano yule polisi aliyempiga mwandishi pale uwanja wa Taifa,  IGP Sirro hakukemea badala yake aliunga mkono kwa kumtetea askari… ingawa Tamisemi wamejitokeza kukemea ila inatakiwa kuwa suala endelevu katika kukemea tabia hiyo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala alisema hali inayotokea sasa ni kwamba awamu iliyopo imeamua kutenganisha uchumi na utawala bora.

Alisema licha ya Mwalimu Julius Nyerere kusisitiza umuhimu wa maendeleo kwa wananchi kuwa yaendane na utawala bora, awamu hii ya tano hali imekuwa tofauti.

“Tunaona imekuwa ni utawala wa kibabe, watumishi wanatumbuliwa ovyo na  viongozi wa chini nao wanafanya kama wakubwa wao kwa kuwasweka rumande kwa makosa hata ya kushindwa kutaja vema jina la Mkuu wa Wilaya.

“Ni mambo ambayo hatukuwahi kuyashuhudia katika serikali zote zilizopita licha ya kwamba sheria ilikuwapo, ila sasa kumekosekana hekima na busara na mwisho wa siku ubabe ndio umekithiri,” alisema.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema kukosekana kwa semina elekezi zilizokuwa zikitolewa kwa viongozi hao ni moja ya sababu ya madudu yanayofanyika sasa.

“Nafikiri awamu hii kwa njia rahisi wanataka kubadilisha mambo yalivyokuwa nchini, wanataka kuonesha utofauti zaidi, kama watu wanatumbuliwa ovyo na mwisho njia wanazotumia ni kudhalilisha watu.

“Licha ya kwamba sheriaya kuwaweka watu mahabusu saa 48 ilikuwapo lakini sivyo wanavyoitumia, kuna vigezo, kuna wengine mfano mkuu wa mkoa wa Iringa nilimsikia anasema ‘mweke kwa masaa yangu’. Kinachoonekana ni kwamba kiongozi wa juu anaposema nao wanafuata, bila kujua tafsiri sahihi ya madaraka yao, pia wanaongoza kwa uoga sana kwani hawajui wanamfurahisha vipi mkubwa,” alisema.

MATUKIO

Kuna orodha ndefu ya matukio ya viongozi wa wilaya na mikoa kuwatisha, kuwaadhibu na kuwakweka ndani watu wa kada mbalimbali, kwa uchache tumeorodhesha matukio ya aina hiyo tisa yaliyotokea ndani ya mwaka huu.

BUNDA

Oktoba 2, mwaka huu. Mapema mwezi huu Mtendaji wa kata ya Kitengule wilaya ya Bunda, Deus Bwire aliamrishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Lidya Bupilipili kupiga magoti mbele ya viongozi wenzake kwenye kikao.

Mtendaji huyo alikumbwa na kadhia hiyo baada ya kuwatetea watendaji wenzake ambao walichelewa kupata taarifa ya kikao hivyo kushindwa kuhudhuria kikao cha mkuu huyo wa Wilaya.

IIRINGA

Septemba 27, mwaka huu. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alimsimamisha kazi na kumtupa rumande kwa saa 48 Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Sitta.

Sita alipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwaambia Chama Cha Viziwi kuwa Manispaa hiyo haiwezi kuwasaidia kwa sasa kwa sababu fedha nyingi zimetumika kwenye ziara za mkuu wa mkoa.

HAI

Agosti 16, mwaka huu.  Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya aliamuru kukamatwa kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Tudeley Estates Ltd, Jensen Natal na Mwanasheria wa kampuni hiyo, Edward Mroso kwa tuhuma za kukwepa kodi ya serikali kiasi cha zaidi ya Sh800 milioni.

ILALA

Agosti 14, mwaka huu.  Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alimsweka rumande kwa saa 48 Diwani wa Kata ya Kitunda, Nice Gisunte baada ya kusahihisha maelezo ya mkuu huyo wa wilaya mbaye alikuwa katika ziara kwenye kata hiyo.

Mjema alifika katika kata hiyo kuzindua kisima cha maji na kutoa salama kwa wananchi kuwa kisima hicho ni matokeo ya utendaji kazi  mzuri wa CCM.

Hata hivyo, Gisunte aliposimama alitoa salaam za Chadema kisha akawaeleza wananchi kuwa kisima hicho kimeanza kufanya kazi baada uchaguzi wa 2015 chini ya uongozi wa diwani (wa kata hiyo) na Meya (Manispaa ya Ilala) ambao wote ni wa Chadema.

KINONDONI

Julai 27, mwaka huu. Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alimuagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo kumkamata na kumuweka ndani kwa saa 48 mmiliki wa kampuni ya Total West Solution kwa kukaidi agizo la  kuwalipa stahiki zao wafanyakazi wa kampuni yake kwa awamu tatu.

KONGWA

Juni 22, mwaka huu. Mhandisi wa Idara ya ujenzi wilayani Kongwa Donatian Mieda aliwekwa mahabusu kwa saa 48 kwa amri ya Mkuu wa wilaya hiyo, Deo Ndejembi kwa madai ya kuisababishia serikali hasara.

SAME

Juni 1, mwaka huu. Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Sinyamule aliagiza Diwani wa Kata ya Bombo awekwe ndani chini ya ulinzi mkali kwa saa nane kutokana na kushindwa kusimamia ujenzi wa bweni la shule ya Sekondari Bombo na kumtaka apewa siku mbili za  kuleta maelezo kwa nini asichukuliwe hatua.

SONGWE

Februari 2, mwaka huu. Mbunge wa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe, Frank Mwakajoka alikamatwa na polisi kisha kuwekwa mahabasu kwa saa 48 kwa kile kinachodaiwa kuwa ni amri ya Mkuu wa wilaya hiyo, Jumaa Irando.

MBULU

Januari 1, mwaka huu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga alimuagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo kumkamata Eliud Petro (50) akituhumiwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais.