Home Habari Vita vya ndani vinaimaliza CCM Mbeya

Vita vya ndani vinaimaliza CCM Mbeya

1877
0
SHARE

PENDO FUNDISHA-MBEYA

“Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu” usemi huu umekuwa ukitumiwa na watu hasa wazazi na walezi wa familia pale watoto wanapoonywa  baada ya kufanya au kutenda mambo yanayokiuka maadili au misingi ya familia.

Kauli hiyo hutolewa hasa pale mtoto anaonekana kushindwa kutii au kufuata maagizo yanayotolewa na wazazi mara kwa mara hali inayopelekea wazazi au walezi kuchoshwa na vitendo hivyo na hapa uamua kutumia usemi huo.

Wakimaanisha kwamba mtu asiye kubali kupokea ushauri au kusikiliza anachoambiwa basi malipo ya ukaidi huo, huja kumkuta na kwa asilimia kubwa huwa ni mabaya na ya kujutia.

Usemi huu, huenda ukakikuta Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya (CCM) baada ya kuonekana kushindwa kupokea,kusikiliza na kutii ushauri unaotolewa na wanachama, wadau na hata viongozi ngazi ya juu pale wanapokiona chama hicho kikipoteza mwelekeo wa kisiasa.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Pombe Magufuri ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa ni miongoni mwa baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu ambao wameaanza kushtushwa na mwenendo mbaya wa chama hicho na kutoa tahadhari mapema kabla mambo hayajaharibika.

“Ninawaeleza ukweli hapa hapa hadharani, mwenye kusikia na asikie, kupigana vita kwa wanaCCM wenyewe kwa wenyewe hakutawafikisha mahali popote zaidi kunawabobomoa ni vema mkabadilika,”hii ni kauli aliyoitoa Rais wakati akiwahutubia wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mikutano vya Rwanda Nzovywe vya Jijini Mbeya.

Amesema, siasa za kukomoana na zile zinazotaka wote wakose zinazoendekezwa na CCM Mkoa wa Mbeya, zitaendelea kuwagharimu kama hawatakubali kubadilika.

Amesema, wanaccm Mkoa wa Mbeya wamekuwa wakipigana vita wao kwa wao na huo ndio ugonjwa mkubwa unachokigharimu chama hicho na kupeleka kupoteza jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo hivyo kuwataka kujenga umoja.

Kupitia nafasi hiyo, Mwenyekiti huyo CCM Taifa, alimtaka Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Jocob Mwakasole kuhakikisha anajenga umoja wa wanachama wake na huo ndio ujumbe anaomuachia.

Wakati wa kumtafuta Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, miaka miwili iliyopita mmoja wa  mgombea nafasi hiyo, Said Salmini, baada ya kushindwa na kushika nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Jocob Mwakasyole awaweka bayana wanaccm  mkoa wa Mbeya kwamba hawapendwi kukosolewa wala kuelezwa ukweli na hilo ndio tatizo kubwa.

 Mgombea huyo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Usalama Mkoa wa Mbeya, (RSO), kwenye uchaguzi huo alipata kura 366 huku mshindani wake Jacob Mwakasole  akipata kura 568 na sababu kubwa iliyosababisha mgombea huyo kushindwa kushika nafasi hiyo licha ya jina lake kuonekana kuzungumzwa na wajumbe wengi ni majibu ya ukweli aliyokuwa akiyajibu pindi alipoulizwa na baadhi ya wajumbe.

Aidha, moja ya swali la msingi ambalo lilidaiwa kumkosesha kura kwa wajumbe wengi ni lile alilotakiwa kuelezea msaada alioutoa ndani ya chama wakati wa mchakato wa kumpata mgombea nafasi ya ubunge Jimbo la Mbeya Mjini mwaka 2015 pindi akiwa Mkuu wa Usalma Mkoa wa Mbeya.

“Umetueleza kwamba ulikuwa Mkuu wa Usalama Mkoa wa Mbeya, hebu tuambie ulikisaidiaje chama wakati wa mchakato wa kumpta mgombea  nafasi ya ubunge atakayepeperusha bendera ya chama na kushindana na Mbunge Joseph Mbilinyi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2015?”swali lililoulizwa na mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.

Akijibu swali hilo, mgombea Said Salmini aliwataka wanaccm kutambua kuwa kipindi akiwa kwenye nafasi ile alikuwa ni mtendaji wa serikali na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya ni kukishauri chama jambo ambalo alilitekeleza kwa asilimia 100.

“Naomba niwaelewesha kazi yangu ilikuwa ni kukishauri chama jambo ambalo nilifanya, hakuna asiyefahamu kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2015 hali ilikuwa ngumu na mimi nilitumia nafasi kubwa kukishauri chama lakini kilipuuza ushauri wangu na mwisho kikavuna kilichokipanda, hivyo nahitaji hii nafasi ili nirekebisha mapungufu na madhaifu aliyoyaona,”alisema Salmin.

Inaelezwa kuwa jibu hilo lilionekana kuwa mkuki kwa baadhi ya wanaccm kwani walielezwa ukweli hivyo kuamua kupiga kura za hasira kwa madai kwamba mgombea huyo ameonyesha dharau.

“Sawa swali ameulizwa lakini hakutakiwa kujibu hivyo angetafuta njia nyingine hivyo ameonyesha dharau kubwa sana, mimi binafsi sidhani kama kura yangu ataipata,”alisema Jeilusi Mwasamfupe Mjumbe wa mkutano huo.

Akizungumza baada ya uchaguzi mgombea huyo, aliwataka wanaccm kujitahidi kumsoma Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli anachokitaka ni CCM MPYA itakayokwenda na mabadiliko ya kweli kwani wakati wa siasa za ukabila, udini na makundi umepita.

“Hili kulikomboa Jimbo la Mbeya Mjini ni lazima wanaccm tujikane wenyewe, tuachane na makundi, ukabila, unafiki na udini, ikumbukwe chama ni taasisi inayowatumikia wananchi wote hivyo kama tutachagua viongozi kwa vigezo hivyo haramu, hatutamtendea haki Mwenyekiti wetu Taifa,”alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Rodrick Mbogolo akiwa ziarani Mkoani Mbeya, aliwaeleza wanaccm kwamba ni uwendawazimu wa chama  kusema ‘CCM MPYA’ wakati wanachama bado wamevaa au kuendelea kukumbatia koti la zamani.   

Mbogolo, anasema wakati umefika kwa wanaccm kupokea habari njema ya mabadiliko makubwa yanayotarajia kufanyika ndani ya chama hicho na kubwa zaidi ni kuhakikisha chama hicho kinazaliwa upya  kwani mambo ya kale yamepita  sasa yanakua mapya.

Anasema, mwanaccm hawezi kusema  ccm mpya wakati ameendelea kuvaa koti la zamani kwani ccm mpya inatarajia kwenda na wanachama wanaoheshimu umoja, upendo na mshikamano.

Anasema, ndani ya ccm hasa Mkoa wa Mbeya, chama kinakazi ya kutekeleza ahadi walizitoa kwa wananchi kupitia ilani ya CCM, ya kuwafikishia wananchi maendeleo lakini chama kimepoteza muda sana kwa kuvutana wenyewe kwa wenyewe.

“tunayo kazi ya kuleta maendeleo ya watanzania na wanambeya lakini wanacc mbeya mmepoteza muda na mmewaumiza watanzania wa Mbeya, kwa kuwacheleweshea muda vya kutosha hivyo mnahitaji kufanya mabadiliko lakini yatawezekana kama mtaanza kuzibadili nafsi zenu,”

“kwa hili nitapenda kuzungumzia  mambo matatu ya kwanza ni mabadiliko na mageuzi  ya mtu binafsi, chama cha siasa kinaundwa na watu na wanachama walioamua kuishi pamoja kushirikiana wanaamini kwa pamoja na itikadi moja,”anasema.

Anasema, endapo watakuwa  wababe kwa kauli mbaya na ubaguzi kwa wananchama wake na watanzania basi kitapotea na kishindwe kufika pale kilipokusudia na  dhambi hiyo haitakuja kufutika midomoni mwa watanzania.

“wapo viongozi wanaowabagua wanachama wenzao kwa kuwafitinisha, kuwatenga , kuwazalirisha na hali hiyo inatokana na kwamba ndani ya nafsi zao  kumejaa chuki, unafiki, masengenyo hivyo kuwafanya baadhi ya wanachama kukosa raha ndani ya chama chao,”anasema.

Anasema , wanachama hao wamefungwa na wababe, hali iliyopelekea baadhi yetu kukichukia chama kutokana na makandamizo yanayotoka kwa viongozi, wapo waliohamia upande wa pili kutokana na manyanyaso haya, chama kinahitaji mabadiliko, mbeya tunapoteza, kwa sababu ya fitina.

Anasema, watu wamegawanyika na kujaa kwenye makundi na kazi yao kubwa wanayoifanya ni kushughulikiana, ukiangalia wengi wao hata vikao vya kujenga chama hawashiriki laki vikao nivya kushughulikiana utawakuta wapo kila siku.

“tumechoka kupoteza jimbo la mbeya mjini, tunataka wananchi wa mbeya wapumue lakini kama sisi tutafanya mabadiliko kwani madhumuni ya chama cha siasa chochote, na hata madhumuni ya ccm sehemu ni kushiriki uchaguzi kwa lengo la kushinda na kuunda dola sasa tunawezaje kuunda dola kama sisi tumekalia fitina,”

“ tunawezaje kushinda uchaguzi kama sisi tumejaa ukandamizaji, tunawezaje kushinda uchaguzi kama kauli zetu kwa wananchi ni mbaya,  hili haliwezekani na hata ukisoma sehemu ya kwanza ibara ya nne ya katiba yetu  inasema chama kinaamini kwamba, binadamu wote ni sawa, na kila mtu anastahili heshima, ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, mbona hatuthaminiani wala kuheshimiana, mbona tumebaki tukishughulikiana sana, mbona tumebaki tukipakana matope, wakati imani za mwanachama zinaamini katika usawa wa binadamu, nipo hapa nataka wanachama wa ccm tufanye mabadiliko ndani ya nafsi zetu,”anasema.

Katibu wa Nec Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, akiwa kwenye ziara Mkoani Mbeya na kuzungumza na wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, aliwahasa wanaccm kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi ili kujiimarisha na kumudu mfumo wa Dunia.

Alisema, CCM mpya na Tanzania mpya zinaenda na kasi ya mabadiliko hivyo lazima na chama kibuni mbinu kwa ajili ya kujiimarisha  na kuweza kumudu mfumo wa dunia unavyokwenda na ndio sababu ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vipengele vya kwenye katiba.

Licha ya yote haya kuzungumzwa na viongozi ngazi ya juu ya CCM na serikali lakini hivi karibuni CCM Mkoa na Serikali ya Mkoa wa Mbeya, vimeingia kwenye mvutano wa kimaslahi wakati wa utatuzi wa changamoto ya maeneo ya matumizi ya biashara yaliyotengwa na halmashauri kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo (WAMACHINGA) wa Jijini hapa.

Wakati serikali ya Mkoa ikiwaondoa wafanyabiashara hao kwenye maeneo hatarishi na yaliyopigwa marufuku, ikiwemo miundombinu ya barabara, uongozi wa CCM Mkoa wa Mbeya, umewataka wafanyabiashara hao kurejea kwenye maeneo hayo na kutoa onyo kwa serikali kutoendelea kuwabughuzi wapiga kura wao.

Akizungumzia sababu za kuwarejesha na kuwaruhusu wafanyabiashara hao kuendelea na shughui zao za kibiashara kwenye maeneo yaliyopigwa marufuku na serikali, Mwenezi wa Siasa na Itikadi CCM Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, alisema chama kinatekeleza wajibu wa kuwalinda wananchi hasa pale wanapoona hawatendewi haki na serikali wanayoisimamia.

 “Chama kwa utaratibu tuliwasiliana na serikali, tuliwaandikia barua na ilitujibu lakini licha ya majibu hayo, kikao cha kamati kuu ya halmashauri Mkoa kiliketi na kutoka na maazimio kwamba machinga wale warejee kwenye maeneo yao ya awali hadi pale serikali itakapowatafutia eneo litakalo fanana na biashara zao na hilo ndilo agizo lililotolewa na chama,”alisema.

Alisema, siku zote serikali inatakiwa kutii maelekezo au ushauri unaotolewa na chama na hapa kunatatizo la uelewa kwani chama si mara moja kimekuwa kinailekeza serikali mambo ya kufanya na yanafanyika na yanapoonekana kufanyika, serikali ndio hubeba sifa hizo.

Alisema, uamuzi wa kuwarejesha wafanyabiashara hao ni halali na unatakiwa kutekelezwa na serikali kwani asilimia kubwa watendaji wamekuwa wakiangalia matatizo badala ya haki za watu.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, akizungumzia tamko na agizo hilo la chama dhidi ya serikali, alisema serikali inafuata taratibu, kanuni na sheria za usalama barabarani, usafi wa mazingira, mipango miji na afya ya mlaji hivyo maeneo ya awali waliyokuwa wakiendeshea biashara wamachinga hayakuwa rafiki na hasa ukizingatia jiographia ya Mkoa wa Mbeya.

Alisema, serikali ipo kwenye mkakati wa kuboresha maeneo hayo hasa ukiangalia idadi ya watu kuwa kubwa, matumizi ya vyombo vya moto ukilinganisha na miaka ya nyuma na kwamba sheria zinaeleza kwamba kutokujua sheria isiwe sababu ya mtu kuvunja sheria hivyo wafanyabiashara wameelekezwa maeneo muhimu na sahihi kwa biashara zao hasa wale wanaopanga barabarabani.

“Machinga anayetembeza biashara zake, serikali haina shida naye, tuliowaondoa ni wale waliopanga vitu au bidhaa zao kandokando ya barabara na wamepelekwa maeneo sahihi, na naomba kusisitiza kwamba wale watakao kaidi agizo hili hatua za kisheria zitachukuliwa,”alisema.