Home Habari Vita ya urais Z’bar yakolea chini kwa chini

Vita ya urais Z’bar yakolea chini kwa chini

1929
0
SHARE

*Baadhi ya mawaziri wa Dk. Shein waanza mikakati

*Dk. Bashiru atua na siri nzito ‘atest’ mitambo 2020

Na MWANDISHI WETU

-ZANZIBAR

VITA ya urais Visiwani Zanzibar imepamba moto ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) pamoja na wa Serikali ya Muungano wakitajwa kuwapo kwenye mikakati mizito.

Hatua hiyo inatokana na Rais Dk. Shein, kuelekea kumaliza kipindi cha miaka 10 ya uongozi ambapo sasa kumeibuka makundi ya chinichini ya kila mmoja akitaka kurithi nfasi hiyo ya kuiongoza Zanzibar.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kiliambia Rai kuwa kwa sasa yameibuka makundi ya wana mtandao ambao wamekuwa wakiendesha mikakati yao kwa siri kwa kuhofia kupoteza nafasi zao kutokana na amri ya Chama iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, akuagiza kufunguliwa kwa majalada ili kufutilia nyendo za kila mmoja.

“Kwa sasa wapo baadhi ya viongozi tena miongoni mwao wakiwamo mawaziri wa Serikali ya Dk. Shein wamekuwa wakitajwa kutaka kuwania urais. Hata hivyo hoja ya uunguja na imepamba moto wakidai ni zamu yao kwani Rais Shein ametoka Pemba.

“Pamoja na hilo kwa sasa wapo ambao wamekuwa wakifanya vikao kwenye hoteli kubwa zilizopo mashambani huko Nungwi wadai ndipo kwenye siri, na si hilo tu wapo wengine wengine ambao kila ikifika mwisho wa wiki wanavuka maji na kwenda upande wa Bara (Dar es Salaam) kuendesha vikao vyao vya kutaka urais.

“Tunajua kwa safari hii namba ya wagombea waliopo wanaweza kufika hadi 20 au zaidi lakini sisi tunataka chama kibaki salama kwani  wote tunajua yaliyotokea huko nyuma (akimaanisha chaguzi zilizopita),” alisema mmoja wa wahafidhina ndani ya CCM Zanzibar

WAOTAJWA

Kwa mujibu wa taarifa ambazo bado hazijadhibitishwa ingawa majina yao wamekuwa wakitajwa mitaani Visiwani Zanzibar kuwa huenda wakajitosa kwenye kinyang’anyiro cha kumrithi Dk. Sheini mwaka 2020 kupitia CCM wapo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo  Machi 3, mwaka huu baada ya kudaiwa kile kilichoelezwa kukaidi agizo la chama la kutoanza kampeni kabla ya wakati.

Hali hiyo ilimfanya Dk. Shein kumtoa kwenye Baraza la Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, ambaye alikuwa akitajwa kwenye mikakati ya chinichini huku akidaiwa kutaka kuvaa viatu vya Dk. Shein mwaka 2020.

Mbali na hao pia anatajwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo Agosti 26, 2019, Makamu wa Samia alitangaza kutogombea urais Zanzibar.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Alisema taarifa zinazoenezwa na watu ambao hakuwataja majina kuwa anataka kuwania nafasi hiyo zipuuzwe, akisisitiza kuwa wadhifa alionao kwa sasa ni zaidi ya urais wa Zanzibar.

Samia alitoa kauli hiyo katika hafla ya siku ya Kizimkazi inayofanyika Mkoa wa Kusini Unguja kila mwaka.

“Kuna maneno kwamba Samia anakuja kugombea urais Zanzibar,  nataka kuwaambia kuwa si kweli na sina nia hiyo. Ukiangalia ngazi za uongozi ndani ya Tanzania mimi ni namba mbili, sina kinachonishawishi nije kugombea huku (Zanzibar) niwe namba tatu.

“Nimeona niseme huku kwetu (Zanzibar) nilipotoka kwa sababu maneno yamekuwa mengi. Chuki nyingi, ufisadi majungu ila kwa Samia mie simo,” alisema Samia ambaye Rais John Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Aliwataka wananchi kutosikiliza taarifa alizodai  zinalenga kumtofautisha na wengine.

ONYO LA DK. BASHIRU

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, aliwatahadharisha baadhi ya wanachama wao walioanza kusaka nafasi ya urais wa Zanzibar kuwa watachukuliwa hatua za nidhamu.

Alitoa kauli wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja akiwa kwenye ziara ya kujitambulisha.

Aliwaonya kuacha mbio hizo kwa kuwa muda wa kufanya hivyo haujafika, huku akiwananga wengine kuwa hata udiwani hawauwezi.

Katibu Mkuu huyo wa CCM ambaye kwa sasa yupo Visiwani Zanzibar kwa ziara ya siku 10, alisema kuwa wanahamishia nguvu za chama Visiwani Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza wiki hii baada ya kuwasili visiwani hapa, Dk. Bashiru Ally, alisema kuwa ni lazima mikakati na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu visiwani hapa yaanze kwa wana CCM kuandaa mikakati ya ushindi.

“Awali ya yote nawashukuru kwa kazi nzuri na kubwa ambayo mmeendelea kuifanya katika kuhakikisha kuwa chama chenu kinaendelea kuwa imara, hivyo nami niseme tu kwamba wembe ni uleule.

“Hivyo nina raha kusema kwamba tumewapiga mapema wapinzani wetu kwenye uchaguzi wa juzi kule Bara na sasa nguvu zote tunazielekeza Zanzibar kwani kazi yetu ni ileile,” alisema Dk. Bashiru.

Akizungumzia lengo la ziara yake Visiwani Zanzibar, alisema ni kukiimarisha chama hicho na kuongeza kuwa ataitumia kushauriana na wanachama kuangalia namna bora zaidi ya kujiimarisha.

“Tunashukuru kwamba kwa sasa tuna raha kule bara kwani tumewapiga mapema na sasa kituo kinachofuata ni Serikali ya Zanzibar kwani nina uhakika kwamba tutahamishia ushindi huo huku ili tuwapige mapema.

KAULI YA DK. SHEIN

Mei mwaka jana katika kile kinachotajwa kuwa huenda kama mkakati wa kutaka kuleta vurugu ndani ya chama hicho tawala, ilimfanya Rais Dk. Shein, kutoka hadharani na kuonya  makada hao walioanza kampeni kabla ya muda.

Dk. Shein aliwataka watambue kwamba yeye bado ni Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa sheria.

Onyo hilo alilitoa kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu, Wilaya ya Kati Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk. Shein alisema makada hao wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya ujenzi wa chama.

Alisema makada hao badala ya kufanya shughuli za ujenzi wa chama zitakazofanikisha kuibakiza CCM madarakani badala yake wanapanga safu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Dk. Shein alisema nafasi ya urais haipatikani kwa kampeni wala makundi yasiyokuwa halali ila hupatikana kwa utaratibu maalumu na kwa mujibu kanuni na Katiba ya CCM.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliwatahadharisha viongozi hao kwa kuwataka kuacha tabia hizo kwa sababu inaweza kuleta migogoro na mgawanyiko usiokuwa wa lazima ndani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema watu hao wanaosaka urais kwa sasa wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia mpaka 2020, watachukuliwa hatua kali za nidhamu ikiwamo majina yao kufikishwa katika vikao vya Usalama na Maadili vya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa kutokana na mienendo yao isyokuwa na manufaa.

Kamati hiyo ya Maadili na Usalama huongozwa na Mwenyekiti wa CCM ingawa kwa ngazi ya uchunguzi Makamu Mwenyekiti husimamia shughuli zote ikiwamo kufungua majalada ya wanaotajwa kila mkoa na wilaya ili kupata taarifa za wahusika.

Aliwatadharisha viongozi, watendaji na wanachama wa CCM kwa kuwataka kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kukisaidia chama kushinda na siyo kuhangaika kumrithi yeye kwenye urais.

“Naheshimu Katiba ya nchi, muda wangu ukifika naondoka madarakani kwa vile huo ndiyo utaratibu wa chama chetu na kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Lakini sifurahishwi hata kidogo kuona baadhi yenu mnaanza kuhangaika na urais badala ya kufanya kazi za kuitafutia ushindi CCM mwaka 2020,” alisema na kuonya Dk. Shein.

Aliwataka mabalozi na viongozi wengine wa ngazi za mashina kukataa kuingizwa katika mitandao hiyo ya kampeni.

KUIMARIKA KWA CCM

Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika na kung’ara miongoni vyama vya ukombozi vilivyoleta uhuru katika nchi zao.

Ingawa haikuwepo wakati wa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 wala mapinduzi ya Zanzibar 1964, CCM inahesabika kama chama cha ukombozi kwa sababu kilizaliwa na vyama viwili vyenye sifa hiyo, TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar chini ya waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.

Wakati CCM ikizidi kuimarika, vyama vingi vilivyoanzishwa katika miaka ya 1950 na 60 vilishatimuliwa madarakani, vikiwemo United National Independence Party (UNIP), Malawi Congress Party (MCP) na Kenya African National Union, (KANU).

UNIP ya Kenneth Kaunda ilikuwa ya kwanza kuangushwa mwaka 1991 baada ya miaka 27 madarakani, ikafuatiwa na MCP ya Kamuzu Banda mwaka 1994 (miaka 29 madarakani) na kisha mwaka 2002 ikawa zamu ya KANU (miaka 39 madarakani).

Baadhi ya vyama vya ukombozi kama Parmehutu cha Rwanda, Mouvement National Congolais (MNC) cha Kongo- Kinshasa vilishafutwa miaka mingi.

Mwisho