Home Latest News Vita ya wafalme watatu wagombeao taji moja

Vita ya wafalme watatu wagombeao taji moja

1212
0
SHARE

MWANDISHI WETU NA MITANDAO,

ILIKUWA ni katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, mwaka 2011. Fainali iliyosubiriwa kwa hamu na wadau wengi wa soka. Walitaka kuuona ufundi wa Barcelona. Walitaka kuuona ubabe wa Manchester United.

Kwenye dimba la Wembley, mashabiki 87,695 walikusanyika ndani ya Uwanja huo mkubwa zaidi England, kushuhudia mtanange huo wa kihistoria.

Kocha wa United kwa wakati huo, Sir Alex Ferguson alikaa kwenye benchi lake, mwenye kutetemeka kwa presha ya kuiona timu yake ikicharazwa na soka lisilo la huruma. Hakuwa na nafasi ya kubadili chochote, alimilikiwa kuanzia ndani ya uwanja hadi kwenye benchi lake la ufundi.

Mpaka filimbi ya mwisho inapulizwa kuashiria mchezo umemalizika, Barcelona iliyotukuka ya kocha Pep Guardiola iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 na kukamilisha usiku utakaokumbukwa na mashabiki wa jiji la Manchester.

Kumbukumbu zinawekwa kwa maana yake, hii iliwekwa kwa ajili ya kuwakumbusha mashabiki wa United kuwa siku yao ya kufurahi ipo karibuni kufika. Na imefika.

Mwaka huu, 2016, mashabiki wa United duniani kote wana sababu ya kuwa na tabasamu na kufurahi. Wanammiliki kocha waliyeota kumuona kwenye benchi la Old Trafford, Jose Mourinho.

Na tayari katika mchezo wa kwanza wa kirafiki chini ya Mourinho, wameonja raha ya ushindi. Ushindi wa maana chini ya kocha wa maana.

Tuhamie London kidogo, kuna matumaini makubwa kuwa simba aliyelala, Chelsea ataunguruma tena chini ya Muitaliano Antonio Conte ambaye katika michuano ya Euro alizima ndoto za Wahispania na alikaribia kuwaliza Wajerumani kutokana na mifumo yake dhabiti.

Tukirudi tena ndani ya jiji la Manchester, katika klabu ya City, wao wamemchukua Guardiola.

Sasa tutaiona Ligi Kuu ya England ya ukweli. Karibuni England, waheshimiwa Guardiola na Conte. Karibu tena, mheshimiwa Mourinho.

Mmepata nafasi ya kutuonesha ni kwanini mashabiki wenu wanawaamini kuwa mtafanya makubwa msimu huu.

Kwanini wamediriki kuwaita wafalme watatu watakaogombania taji moja.

Usiku wa fainali ya Wembley miaka mitano iliyopita haukutuonesha tu ni jinsi gani Barcelona ilivyokuwa na ufundi wa kucheza soka la ‘tiki-taka’, bali ni timu iliyokuwa ikicheza soka lenye vitu vingine zaidi ya hilo.

Siku hiyo, tulishuhudia namna walivyokuwa wakikaba. Ni tofauti na timu nyingine yoyote. Walikaba kuanzia eneo la United. Hawakuwapa nafasi ya kumiliki mpira. Ilionekana ni kama Barca ilizidisha wachezaji uwanjani na nguvu yao ilikuwa ni yenye kushangaza.

Ni ngumu kuifanya Barcelona icheze soka lake bila Lionel Messi, Xavi au Andres Iniesta.

Lakini unaweza ukawafanya wacheze soka la kudhalilisha na kupiga pasi murua bila ya wachezaji hao, ndio mfumo wa Guardiola. Ndicho alichokuwa akikifanya akiwa Bayern Munich. Na ataendelea nacho ndani ya Man City.

Mbele ya mabeki atawatumia ipasavyo viungo wake Ilkay Gundogan sambamba na Fernandinho. Nolito atatumika kama winga wa kulia, kushoto atatumika Kevin De Bruyne na David Silva nyuma ya Sergio Aguero.

Upande wa Mourinho, yeye atakuwa na jukumu moja tu, kutafuta mfumo sahihi wa Manchester United.

Alipotua Chelsea kwa mara ya kwanza alitumia mfumo wa 4-3-3, alipokuwa Inter aliupenda mno mfumo wa 4-4-2, alipotua Real Madrid na Chelsea kwa mara ya pili alibeba mataji kwa mfumo ambao huenda akautumia ndani ya United, mfumo wa 4-2-3-1.

Ujio mpya, Henrikh Mkhitaryan atacheza upande wa kulia, sambamba na nahodha Wayne Rooney katikati na Anthony Martial kushoto. Kwahiyo Zlatan Ibrahimovic au Marcus Rashford mmojawapo atasimama kama mshambuliaji wa kati.

Kama wakipata kiungo wa kati atakayesimama na Morgan Schneiderlin au Michael Carrick mbele ya mabeki, kikosi cha United kitakuwa ni moto wa kuotea mbali kwani Mourinho anajulikana kwa soka lake la kukaba kwa nguvu, mashambulizi ya kushtukiza.

Conte yeye bila shaka ataendelea kuuamini mfumo wake wa kutumia mabeki watatu nyuma kama alivyokuwa akifanya akiwa Juventus na timu ya taifa ya Italia ambako alipenda mno kuwa na ukuta imara wenye Leonardo Bonucci katikati, Giorgio Chiellini na Andrea Barzagli pembeni yake huku nyuma yao akisimama langoni Gianluigi Buffon.

Atapewa kiasi kizuri cha pesa za usajili, na uwepo wa mkongwe John Terry sambamba na Gary Cahill na Branislav Ivanovic, na mwezi Septemba atamtumia pia kinda mwenye nguvu na kasi katika eneo la ulinzi, Kurt Zouma.

Kikosi cha Conte kitakuwa na winga wao mwenye kipaji, Eden Hazard, kiungo Cesc Fabregas ambao kwa pamoja watakuwa wakiendesha mashambulizi ya Chelsea kutoka kila pande. Pembeni kulia wakiwa na Cesar Azpilicueta, Willian ambao watakuwa wakishambulia kutokea pembeni kwa kasi.

Aidha uwezo wa kufunga alionao Diego Costa, mashuti makali ya Mbelgiji, Michy Batshuayi ukiongeza na tabia ya kocha wao ya kuwafundisha wachezaji wake namna ya kupambana na kutokata tamaa, Cheslea itakuwa ni ya tofauti na ile ya miaka 10 iliyopita.

Makocha wote hao watatu wana matarajio makubwa msimu huu. Hakuna atakayetaka kumaliza nafasi ya pili. Utakuwa ni msimu mgumu kuwahi kutokea miongoni mwao.