Home Habari kuu Vyama vianze kudhibiti utengenezaji wapiga kura

Vyama vianze kudhibiti utengenezaji wapiga kura

472
0
SHARE

Leonard Mang’oha

WAKATI tukielekea kuanza mwaka mpya 2020, mwaka ambao Tanzania inarejea katika sanduku kuwapata viongozi wa Serikali na wawakilishi wa wananchi watakaoshika hatamu kwa miama mingine mitano hadi hapo 2015, tayari joto la uchaguzi limeanza kupanda.

Joto hilo limeanza kupanda kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kwa upande wa Zanzibar tayari mamlaka zinazohusika ka nichaguzi zimeanza kukutana na vyama vya siasa kuvielekeza taratibu zinazopaswa kuzingatiwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo wenye maana kubwa kwa Tiafa.

Gumzo jingine kwa upande wa Zanzibar ni katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho baadhi ya watu wanatajwa kuhaha kumrithi Rais Dk. Mohamed Shein anayemaliza muda wake wa miaka 10 kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utaratibu wa chama chake.

Kwa upande wa Bara bado joto halionekani kuwa juu hasa katika nafasi ya Rais kutokana na Rais aliyepo madarakani, Dk. John Magufuli, kuwa katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi hivyo si rahisi kwa wana-CCM kuonesha wazi kuitaka nafasi ya mwenyekiti wao ikiwa bado utaratibu wa chama unamruhusu kugombea tena.

Ni vigumu kwa maana kwamba utaratibu wa chama ni kwamba ikiwa kiongozi anayeongoza dola bado anazo sifa za kushika nafasi hiyo hakuna sababu ya kumwondoa badala yake kumwezesha kuendelea katika nafasi hiyo.

Lakini pamoja na utaratibu huo tayri kumekuwapo minong’ono huku nyuma ikiwahusisha baadhi ya wana-CCM kutaka kuchuana na Dk. Magufuli ndani ya chama hicho ili wapate nafasi ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kwa kuwa hayo ni ya CCM tuwaachie wao watajua namna ya kumalizana maana wamekuwapo miaka mingi na wanafahamu jinsi ya kuvivuka viunzi hata pale vinapotokea kuwa vigumu na hatimaye mambo kuendelea, hili linaweza kudhihirisha na yale yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hadi kufikia hatua ya wanachama wake waandamizi kukihama chama.

Katika vyama vya upinzani nako jatopia limeanza kuwa juu japo huko joto lake mara nyingi huwa la kawaida labda kwa sababu nia yao ya kwanza huwa ni kukiwezesha chama kushika hatamu kuliko mtu kushinda urais kwa sababu hawajawahi kupata nafasi ya kuongoza.

Nasema kwao ni chama kwanza kwa kutazama historia katika chaguzi kadhaa zilizopita ambapo hakukuonekana kuwapo na mchuano mkali miongoni mwa wanachama kutaka kugombea urais na hili linadhihirisha na hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kilipoamua kumsimamisha, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, licha ya kuwa mwanasiasa huyo kuhamia huko siku chache baada ya kuenguliwa na CCM kuwania nafasi hiyo.

Joto linaloonekana kuwano ni katika kuwapata viongozi wa kuviongoza vyama vyao kuvuka 2020, ambapo vyama vya upinzani vinaweza kuwa katika hali ngumu zaidi kutokana na hali ambayo imekuwa ikijitokeza katika chaguzi mbalimbali za marudio na hata ule wa Serikali za Mitaa ambao vyama vyote vikuu vya upinzani viliususia kwa madai ya kutoendeshwa katika hali ya usawa.

Vilevile baadhi ya vyama vineshuhudia wafuasi na viongozi wake wakivihama na kujiunga na CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Dk. Magufuli na na hata pale vyama vivyo viliporejea katika uchaguzi huo aidha vilishindwa kwa kura ama wagombea wake walienguliwa kwa madai ya kukosa sifa.

Ndani ya chadema tumeshuhudia joto kali lililojitokeza katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho ulimalizika jana na kupata viongozi wake wapya watakao kiongoza chama hicho hadi mwaka 2024, ambapo tumeshuhudia Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrik Sumaye, akijiengua akilalamikia kuhujumiwa.

Vyama vingine hali joto halionekani kuwa juu pengine kutokana na ushiwishi wa wastani wa vyama vyenyewe, kwa sababu vyama vingi havina wabunge hivyo kupunguza mvutano miongoni mwao.

Tukirejea ndani ya CCM huku mambo huwa moto karibu kila uchaguzi hata kama uchaguzi wenyewe ni wa marudio ni lazima moto uwake. Tayari tetesi zimekuwa zikiwahusisha baadhi ya wanachama wake wakiwamo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaoonesha nia ya kugombea ubunge katika majibo mbalimbali.

Hata hivyo wengi wao wameekuwa wakifanya hivyo kwa usiri mkubwa wakihofia kuonekana kwa sababu kwa utaratibu wa chama na maelekezo ya viongozi wakuu wa chama ni kosa kwa mwanachama kuanza kujinadi kuwania nafasi yoyote  kabla ya muda.

Lakini wako baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitajwa kutaka kugombea, mmoja wao akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Paul Makonda, ambaye alianza kuhusishwa kutaka kutupa karata yake katika Jimbo la Kawe kumwondoa Halima Mdee wa Chadema, kisha akatajwa Ubongo na sasa anahusishwa na Jimbo la Ukonga linaloongozwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara.

Wakati joto hilo likiendelea kupanda tayari baadhi ya wanachama wanatajwa kuanza kuweka mipango ya kutafuta wapiga kura kupitia viongozi wa chama na wetu wengine wenye ushawishi katika chama kwa ngazi tofauti tofauti.

Jambo hili linatajwa pia kufanyika kupitia wenyeviti wa mikoa na hata wilaya. Na katika kuonya hili Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Hamphrey Polepole, akiwa mkoani Arusha hivi karibuni aliahidi kuwa atahakikisha anawashughulikia viongozi wote wasiokuwa na nidhamu ambao wamekuwa wakiwatengeneza watu ili waweze kuwachagua kwani kufanya hivyo ni utomvu wa nidhamu.

Kauli ya Polepole ameitoa katika mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha kuziba nafasi ya, Loata Sanare, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro.

Polepole anasema atahakikisha anashughulika na kiongozi yeyote anayewatengeneza watu ili waweze kumchagua kwa namna yoyote ile iwe ni kwa kutoa rushwa au lah na hataki mzaha kabisa katika hilo huku akiwataka wana-CCM kupiga kura katika uchaguzi huo wa mwenyekiti kwa haki na kamwe wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote.

Kauli hii ni vema ikasimamiwa kikamilifu kuhakikisha inakomesha utengenezaji wa wapiga kura badala yake watu wachaguliwe kwa nguvu ya ushawishi na uwajibikaji wa mtu. Kitendo cha kutengezeza watu wa kukupigia kura ni dhahiri kinaambatana na vitendo viovu vya rushwa ambayo hata Mwenyekiti wa CCM, Dk. Magufuli mwenyewe amekuwa akivieleza katika hatuoba mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa.

Ni dhahiri ili kuwatengeneza watu ili wakupigie kura ni lazima utawashawishi kwa fedha na ahadi mbalimbali ambazo mwisho wake husababisha kuwa na bora viongozi na si viongozi bora wenye kusimamia haki na ukweli katika jamii.

Matokeo ya vitendo hivyo ni kuongeza mianya ya rushwa na ufisadi katika jamii ambamo ambayo Dk. Magufuli amekuwa kinara wa kuyakemea hadharani kiasi cha kujipatia umaarufu kupitia uamuzi wake wa kutumbua majipu pale anapobaini kuna ufisadi umetendeka.