Home Habari Vyama vya upinzani Afrika Mashariki ‘vimebanwa kila kona’

Vyama vya upinzani Afrika Mashariki ‘vimebanwa kila kona’

374
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA

MIEZI mitano iliyopita nilikuwa najadiliana kirafiki na Mtangazaji wa BBC Swahili Dira ya Dunia, Zuhura Yunus hususani kwa upande wa vyama upinzani. Kimsingi swali lilisema, je hali ya kisiasa Afrika mashariki inaonyesha kuwa viongozi wake hawapendi kushirikiana pamoja na kuendesha siasa zenyewe na wanasiasa kutoka vyama vya upinzani?

Hata hivyo Zuhura Yunus alifafanua kuwa ipo tofauti ya siasa za Tanzania na Kenya, lakini nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan kusini zikaonekana kushabihiana baadhi ya mambo, wapinzani wanaishia korokoroni kila mawio na machweo.

Hivi karibuni kulikuwa na mjadala kama huo kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikiuliza wasomaji wake, “Je ni wakati wa kukubali kuwa baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki yameshindwa kustahimili siasa ya vyama vingi? Haya ni maoni yangu kuhusiana na mjadala tajwa.

Swali hilo ni muhimu katika muktadha uliopo. Ni swali linalogusa siasa za pande zote tatu; wanasiasa kutoka vyama tawala wanajikuta wakiwa kwenye mtanziko juu ya uhalisi wa vyama vya upinzani na hali zao kwa ujumla.

Pili; ni swali ambalo linawagusa wanasiasa wa upinzani kuona namna gani wanakabiliana na viongozi waliopo madarakani ili kuendesha siasa za kila siku. Tatu; mapokeo ya wananchi kutoka vitendo vya wanasiasa kutoka pande mbili za kwanza. Ninazigawa nchi zote katika hali yake ya kisiasa ili kupata picha kamili.

Nchini Tanzania shughuli za kisiasa zinaweza kudaiwa zinaendeshwa kama kawaida, lakini mazingira ya ‘kawaida’ yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Kwanza, tumeshuhudia wimbi la vyama vya upinzani kupoteza wabunge 12 tangu mwaka 2015.

Wabunge 11 wameshajivua uanachama wa vyama vya upinzani na kujiunga na chama tawala cha CCM ambako pia waliteuliwa kugombea nafasi hizo na kushinda, wakati Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amevuliwa ubunge kwa madai ya kukosa sifa. Katika hoja ya wabunge 11 kuhamia CCM, tunaweza kusema ni uhuru wa kisiasa, lakini kuna walakini juu ya vitendo vizima.

Nassari  alipoteza sifa ya kuwa mbunge baada ya taarifa ya Spika wa Bunge kubainisha kuwa amekiuka Ibara ya 71(c), ambayo inafafanua kuwa mtu yeyote atapoteza ubunge kama atashindwa kudhuhuria vikao vya mikutano ya Bunge vitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika.

Kanuni ya 146(1) na 2 ya kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha Nassari hakuhudhuria mkutano wa 14 uliofanyika Januari 29 hadi Februari 9 mwaka huu. Ni makosa ya Mbunge mwenyewe, lakini Kiti cha Spika kilipaswa kulinusuru taifa hili kuingia kwenye gharama kubwa za uchaguzi.

Kwa nchi masikini kama Tanzania ikiwa inatumia fedha nyingi kwenye chaguzi ndogo ambazo zinaepukika maana yake kinachoangaliwa zaidi ni masilahi ya kisiasa ya vyama kuliko wananchi wanaohitaji huduma za afya,elimu, miundombinu na kadhalika. 

Shughuli za kisiasa kwa vyama vya upinzani imeelekezwa kuwa ni marafuku kwa wabunge kufanya siasa za kitaifa badala ya majimbo yao. Inaelekezwa kuwa wabunge wafanye mikutano kwenye majimbo yao.

Huko majimboni wana changamoto ya kukubaliwa au kukataliwa vibali vya mikutano na kuambiwa sababu lukuki. Si hilo pekee, vibali vinaweza kutolewa lakini mbunge akazuiwa kufanya mikutano ndani ya jimbo lake.

Mathalani Peter Msigwa wa jimbo la Iringa Mjini, Esther Matiko, Peter Lijualikali ni baadhi ya wabunge waliozuiwa kufanya mikutano kwa sababu mbalimbali licha ya kuwa na vibaya. Wakati mikutano ya siasa za kitaifa ikifanywa ‘haramu’ tumeshuhudia viongozi waandamizi wa CCM wakifanya mikutano katika mikoa mbalimbali nchini kwa kile kilichoitwa ‘kukagua shughuli za chama’.

Tunafahamu kuwa vyama upinzani vinasumbuliwa hata kwenye mikutano ya ndani. Kikao cha Sekretarieti ya chama cha ACT-Wazalendo kilizuiwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi kwa sababu ya ‘kuhofia’ wafuasi wa chama cha Wananchi-CUF ambao walidhaniwa kuwa watafanya fujo. ACT-Wazalendo kimepokea wanasiasa wapya hivi karibuni akiwemo galacha wa siasa za upinzani nchini Maalim Seif Sharrif Hamad.

Tafsiri tunayopata katika tukio hilo ni kwamba badala ya Jeshi letu pendwa la Polisi kuwalinda viongozi wa ACT-Wazalendo waliopanga kufanya mkutano, wao wanataka mkutano uvunjwe. Hili ni jambo linalosababisha mashaka makubwa juu ya mwenendo mzima wa shughuli za kisiasa na mustakabali wa vyama vya upinzani.

Wanasiasa wa upinzani kufungwa jela au kuswekwa rumande imekuwa ‘fasheni’ ambayo ndiyo kielelezo cha demokrasia kwa sasa. Si busara kutaja wanasiasa wote walioswekwa rumande, lakini inatosha kukiri kuwa masuala hayo yapo, na yanawagusa wapinzani.

Inawezekana tukavipatia changamoto vyama vya upinzani nchini Tanzania, kwamba kwanini havitumii fursa ya kufanya siasa kwenye majimbo yao ya uwakilishi badala ya kung’ang’ania za kitaifa? Jawabu linalojionyesha wazi juu ya wale waliofanya mikutano majimbo na mazingira waliyokutana nayo yamewaachia ukiwa.

Nchini Kenya, nguli wa siasa  Raila Odinga ameungana na serikali ya rais Uhuru Kenyatta kwa kile kilichoitwa ‘Handshake’ ya kuleta mshikamano,umoja na amani kwa masilahi ya Wakenya. Katika mazingira hayo haiwezekani kutokea wanasiasa wa upinzani wakaanza amsha amsha dhidi ya Odinga.

Ni vigumu kutokea upinzani mkali dhidi ya Raila Odinga, akina Moses Wetangula (Ford), Musalia Mudavadi (ANC) na Kalonzo Musyoka (Wiper)  hawatazamiwi kufanya hilo, hali ambayo inashusha ari ya siasa za vyama vingi. Kwa sababu Odinga alikuwa Kiongozi wa kambi hiyo, ambapo ameweka masilahi binafsi pembeni na kulinda taifa. Kwahiyo hapa ni siasa za fursa, kwamba chama cha Jubilee kimetumia fursa ya kuwa madarakani kutoa madaraka kwa mwanasiasa wa upinzani hivyo kumaliza kabisa ari,nguvu na kasi ya wafuasi wa upinzani, na kubaki kusubiri tukio jingine (uchaguzi) badala ya siasa za wakati wote.

Kinachoweza kutokea nchini Kenya sasa ni kuibuka upinzani mpya kati ya pande mbili za rais Uhuru Kenyatta na William Ruto kuhusu uchaguzi wa mwaka 2022 kwa sababu Odinga yupo katikati yao, hali ambayo inazua minong’ono ni wapi Uhuru Kenyatta atasimama kwenye uchaguzi ujao, je atamuunga mkono Ruto au Odinga (iwapo ataamua kugombea)?

Nchini Uganda, Mbunge Robert Ssentamu (Bob Wine), ambaye ni mpinzani mkubwa wa rais Yoweri Museveni alishia kupigwa virungu,akaumizwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini dhidi ya nchi yake, kisha akalazimika kwenda kufuata matibabu nchini Marekani.

Nchini Rwanda na Burundi wanasiasa wa upinzani kufungwa jela imekuwa kama ‘sehemu zao’ za kulala. Wapinzani wa viongozi wote wawili hawana amani. Nchini Burundi licha ya vikwazo vya hapa na pale, kiongozi wa upinzani, Agathon Rwasa amefanikiwa kusajili chama chake CNL mwezi februari mwaka huu. Lakini wimbi la wafuasi wa mwanasiasa huyo wanaendelea kukamatwa, wakati wafuasi wa CNDD-FDD wakiwa huru kwa lolote.

Nchini Rwanda, Diane Rwigara alifunguliwa mashtaka ambayo baadaye yalitupiliwa mbali na mahakama. Diane alipaswa kuwa miongoni mwa wagombea urais katika uchaguzi uliopita, lakini hali haikuwa hivyo, alishtakiwa kwa uhaini,kudanganya majina ya wadhamini wake kwenye mbio za urais, pamoja na ukwepaji kodi. Lakini yote hayo yalimfika baada ya kuingia mokwa moja kwenye siasa za upinzani. Mwanasiasa Victoire Ingabire aliachiliwa huru baada ya kufungwa jela huku sababu za hatua hiyo zinajulikana.

Mazingira ya siasa kwa sasa na aina ya watawala waliopo Afrika mashariki yametengenezwa ombwe la kisiasa la kuonekana kana kwamba ni uadui dhidi ya maendeleo, ukosefu wa uzalendo,ukosefu wa adabu na utii, na kuvifanya vyama vingi vya siasa kama vile ni makundi ya watu wasiostahili kuwepo katika nchi zao. Hii si sawa.