Home Latest News VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI: UDHAIFU WA SASA UNATOKANA NA HISTORIA YAKE

VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI: UDHAIFU WA SASA UNATOKANA NA HISTORIA YAKE

1392
0
SHARE
Wafanyakazi wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) wakiandamana katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka jana jijini Dar s Salaam.
NA HILAL K. SUED

Mara ya mwisho nchi yetu ilishuhudia mgomo ambao uliitikiwa kwa karibu asilimia 100 ya wafanyakazi ilikuwa ni miaka 57 iliyopita (1960) wakati bado hatujapata uhuru wetu na wakati bado nchi ikiitwa Tanganyika.

Mgomo huo ulioitishwa na chama cha wafanyakazi wa Shirika la Reli la Afrika ya Mashariki upande wa Tanzania, TRAU ulikuja baada ya serikali ya ukoloni kukataa nyongeza za mishahara na masilahi mengine kwa wafanya kazi.

Kwa wale wanaokumbuka TRAU ilikuwa inaongozwa na Katibu wake Mkuu machachari, Christopher Kasanga Tumbo (sasa marehemu) na ulilazimisha serikali ya ukoloni ya Waingereza kuita Wazungu na Makalasinga kutoka Kenya na Uganda kuja kuendesha treni zetu, kuwa mastesheni masta, na hata watoza tiketi ndani ya treni (ma-TTE).

Baada ya hapo hakujatokea mgomo mwingine wowote wa maana ulioitishwa na kuitikwa kwa asilimia kubwa ya wafanyakazi kama huo. Migomo ilioitishwa na ilioitikiwa na idadi chache ya wagomaji ilitokea mwanzoni mwa miaka ya 90, baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi. Hii ni pamoja na ule wa wafanyakazi wa serikali na mashirika ya umma wa mwanzoni mwa mwaka 1993 na ule wa walimu wote nchini mwishoni mwa 1994.

Katika hii miwili, angalau ule wa walimu ndiyo uliitikisa kidogo serikali kwani ulibahatika kuwa na kiongozi shupavu, Peter Mashanga. Lakini yote hii miwili haikufanikisha malengo ya wagomaji kwani serikali iliweza kutumia kila mbinu, zikiwemo za vitisho au za kurubuni baadhi ya viongozi na wafanyakazi pia.

Hali hii ya kuwepo udhaifu mkubwa kwa wafanyakazi nchini kutokuwa na uwezo wa kupigania haki zao unatokana na siasa ya ujamaa ambayo nchi iliikumbatia kuanzia katikati ya miaka ya 60 na ambayo ilikuwa haivumilii migomo ya aina yoyote, hali ambayo iliendelea kwa muda wa karibu ya miaka 30 ifliyofuata.

Mgomo huo wa 1960 wa wafanyakazi wa Shirika la Reli ulitokea baada ya nchi kujipatia Serikali ya Madaraka, au tuseme ‘uhuru nusu’ — kabla ya uhuru kamili uliokuja mwishoni mwa 1961. Kwa hivyo baada ya uhuru kamili hao wafanyakazi waliogoma waliomba walipwe sehemu ya mishahara waliyokatwa kwa idadi ya zile siku walizogoma.

Serikali huru ya Tanzania ilikataa katakata kuwalipa eti tu kwa sababu wafanyaklazi hao waligoma wakati bado nchi ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni, kwa hivyo wahusika halisi wa suala hilo ni serikali ya kikoloni iliyokuwapo.

[Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema hata kwa serikali ya sasa ya Tanzania, suala la kutokuwa na uthabiti kwa malipo ya mafao ya wafanyakazi wa upande wa Tanzania wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977 ina sheria-hukumu yake kihistoria (historical precedent).]

Na pamoja na ukweli kwamba vyama vya wafanyakazi vilikuwa ni mojawapo ya vikundi/taasisi muhimu zilizochangia vuguvugu katika harakati za kuuondoa ukoloni, lakini baada tu ya wakoloni kuondoka serikali ikaanza kuviminya kwa maelezo kwamba hakuna sababu ya kuigomea serikali iliyo huru, kwani serikali hiyo si tayari imesha wakomboa wananchi wote?

Februari 25, 1964, serikali iliviunganisha vyama vyote vya wafanyakazi nchini, wakati huo vikiwa chini ya mwavuli wa Mwungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanganyika (Tanganyika Federation of Labour – TFL) chini ya mwenyekiti wake Rashidi Kawawa na kuunda chama kipya kilichoitwa National Union of Tanzania Workers (NUTA).

Kulikuwapo mwenyekiti wake na katibu mkuu ambaye ndiyo alikuwa mtendaji mkuu wa chama hicho na ambaye alikuwa anateuliwa na Rais wa Jamhuri. Baadaye ikawa kwamba waziri wa kazi ndiye pia alikuwa katibu mkuu wa NUTA. Kwa ujumla kuanzia hapo kitanzi cha serikali kwa wafanyakazi nchini kikawa kimekamilika.

Kazi kubwa ya NUTA, pamoja na vyama vingine vilivyofuata, ambavyo vilikuwa ni kile kile tu lakini kwa majina tofauti – yaani JUWATA na OTTU (OTTU ilipitishwa kwa ya sheria ya Bunge mwushoni mwa miaka ya 80) ilikuwa ni kuhakikisha wafanyakazi hawagomi. Hilo ndilo lilikuwa jukumu kubwa la Katibu Mkuu wa vyama hivyo, ambaye kama nilivyosema, ndiye pia alikuwa waziri wa kazi.

Kwa hivyo wafanyakazi wa Tanzania wakawa wamelemazwa kabisa katika kudai haki zao, hata zile za msingi kabisa. Na hali hii ya kusikitisha, ambayo mtu anaweza kuiita sumu mbaya, ilienea katika nyanja nyingine katika jamii nzima. Jamii ikawa ya hovyo hovyo kabisa kimawazo katika kudai haki zao, na waliamua kuumia au kuungulika kimya kimya.

Hali hii pia iliirahisishia kazi serikali, kwani pindi tu inapotindikiwa mapato katika bajeti yake, basi huamua kupandisha kodi katika bidhaa muhimu, au kuanzisha kodi nyingine huku wafanyakazi, na wananchi kwa ujumla walikaa kimya bila kufanya chochote. Nchi nyingine, upandishaji wa bei wa bidhaa muhimu huamsha maandamano na ghasia kubwa mitaani pamoja na magari kuchomwa moto.

Bila shaka serikali iliuona udhaifu huu na ikaanza kuutumia kikamilifu – kwa kupandisha bei ya bidhaa (wakati huo bei za bidhaa muhimu zikiwa zinadhibitiwa na Tume ya Bei) kila kukicha bila kujali adha iliyokuwa inawapata wananchi.

Aidha ilikuwa mtindo katika sherehe za kila mwaka za sikukuu ya wafanyakazi ya Mei Mosi kwa Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi kumwalika Rais wa Jamhuri kuhutubia umma. Katika mkutano wenyewe na hasa baada ya gwaride la wafanyakazi wa taasisi na vitengo mbalimbali, kwanza husimama Katibu Mkuu (Waziri wa Kazi) na kuanza kutoa malalamiko kwa niaba ya wafanyakazi kuhusu uduchu wa kima cha chini cha mishahara ukilinganisha na upandaji wa bei ya bidhaa muhimu n.k.

Na baadaye Rais husimama na katika hotuba yake huwasifia wafanyakazi nchini katika jitahada zao, kukumbushia historia ya wafanyakazi katika harakati za ukombozi kutoka kwa wakoloni, na pia kuwaelezea ufinyu wa bajeti ya serikali n.k.

Aidha mara chache hutumia fursa hiyo kutangaza pia nyongeza za mishahara ambayo huanza Julai mwaka huo yaani kuanza kwa mwaka mpya wa fedha. Watu wote hupiga makofi na kushangilia na mkutano kumalizika.

Sidhani kama Watanzania wengi walikuwa wanatambua kwamba nyongeza hiyo – ambayo ilikuwa ni kama punje chache tu za njugu (peanuts) ilikuwa inatokana na huruma ya serikali yenyewe na si harakati za wafanyakazi wenyewe kupitia kwa “Katibu Mkuu” wao ambaye pia alikuwa Waziri wa serikali.

Ile migomo niliyotaja ya mwaka 1993 na 1994 ilikuja baada ya hali kidogo kubadilika wakati ambapo Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi hakuwa tena waziri wa kazi. Mgomo wa 1993 uliitishwa na Katibu Mkuu Bruno Mpangala, lakini wengi waliouitikia waliamua kurejea kazini kwa hofu ya kufukuzwa kazi, kwani hawakuzoea kabisa kugoma.

Pengine hali halisi ya udhaifu wa vyama vya wafanyakazi katika kutetea masilahi ya wanachama wao ilielezwa na Christopher Kasanga Tumbo katika miaka ya 90 baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzishwa wakati akiongoza moja ya vyama vya siasa vilivyoanzishwa – UMD.

Katika mahojiano na gazeti moja mapema mwaka 1993, aliwadhihaki viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa kusema: “Kugomesha wafanyakazi si lelemama. Watagomeshaje hawa wakati wao (viongozi) wakiwa katika ofisi zilizo magorofani wakipulizwa na viyoyozi? Hawawezi hata kuteremka chini na kujichanganya na wanachama wao (wafanyakazi).”

Aliongeza: “Mimi wakati nahamasisha mgomo ule wa mwaka 1960, nilikuwa nikitembelea kila stesheni ya reli na kulala kwenye mabaraza ya stesheni hizo kuwaeleza wafanyakazi haki zao na kuwakumbusha tarehe ile ikifika waweke vitendea kazi chini. Nilikuwa nalala nao chini kwenye sakafu.”

Kwa hivyo tatizo kubwa sasa hivi katika vyama vya wafanyakazi ni kutokuwapo kwa uongozi thabiti katika vyama hivyo, viongozi wanaowajali wanachama wao na masilahi yao. Mara nyingi tumekuwa tunasikia kuwa hawa badala yake huamua kushirikiana na waajiri katika kukandamiza haki za wanachama, hali inayoashiria kuwapo na hisia za rushwa.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi hata wamesikika wakiwatahadharisha wanachama wao kutogoma, kitu ambacho kinaathiri harakati nzima za kudai haki. Matokea yake ni kwamba wafanyakazi wengi nchini wanajikuta wanaminywa haki zao na waajiri wao na kuendelea kuumia kimya kimya.

Mara kadha wafanyakazi wa kiwanda fulani huamua kutoingia kazini, au kuwafungia milango waajiri wao milango, hadi kwanza kieleweke. Wafanyakazi hawa wenye ghadhabu huonyeshwa katika TV wakitoa maelezo ya kusikitisha jinsi wanavyotendewa na waajiri wao, na utadhani hawana viongozi wao wa vyama vya wafanyakazi kuwatetea.

Hata hivyo nitakuwa sitendi haki iwapo nitasema hakuna kabisa viongozi thabiti wa kutetea masilahi ya wafanyakazi, kwani wapo ingawa ni wachache, isipokuwa tu serikali huwa na uwezo wa kutumia mbinu mbali mbali kunyamazisha harakati zao. Miaka mitatu iliyopita tuliona jinsi ule mgomo wa madaktari ulivyosambaratika.

Kuandaa mgomo ni kazi yenye changamoto nyingi na kitu cha kwanza – baada ya mazungumzo kati ya pande mbili kuvunjika) ni kwa mamlaka (serikali) kuutangaza siyo halali na kuwa tayari kwenda mahakamani kupata hukumu ya kuharamisha mgomo, ikibidi hata kulazimisha mahakama kukaa usiku ili tu kupata hiyo hukumu iwapo mgomo ulipangwa kuanza siku inayofuata. Hii ilishatokea kuhusu mgomo uliopangwa na walimu miaka kadha iliyopita.

Sasa na itokee mgomo umeruhusiwa, jee viongozi waamewatayarishaje wanachama wake katika mgomo ambao unaweza kuwa wa muda mrefu – hasa katika kuwapatia malipo ya kujikimu (strike pay) wakati wa mgomo, kwani katika kipindi hicho wafanyakazi hawatakuwa na kipato kingine?

Malipo haya ni lazima yatoke katika michango yao ya kila mwezi wanayokatwa katika mishahara, ikitegemewa kwamba fedha hizo ziliwekezwa vizuri na vyama vya wafanyakazi, na siyo kupondwa tu na viongozi wake.

Na viongozi wakiweza kutayarisha mambo yote haya ya msingi, pamoja na jinsi ya kukabili vitisho vya serikali dhidi yao vikiwemo kukamatwa, kupelekwa mahakamani n.k.  basi huenda wakaweza kufanikiwa. Vinginevyo ni bora wanyamaze kimya. Kugomesha wafanyakazi si “lelemama,” alisema marehemu Kasanga Tumbo.