Home Latest News WAACHENI MAPADRI WAOE, ENZI ZA KONSTANTIN ZIMEPITA

WAACHENI MAPADRI WAOE, ENZI ZA KONSTANTIN ZIMEPITA

1105
0
SHARE

Na Joseph Mihangwa

HABARI kwamba Kanisa Katoliki linakusudia kubadili msimamo wake wa kihafidhina kuruhusu waumini wake waliooa kuwa mapadri, ni kaa la moto kwa wahafidhina wa dini za mapokeo,     wakitafsiri hatua hiyo kuwa ya usaliti wa “Neno” (Injili) na ishara ya “mwisho wa dunia” ya Kitheolojia.

Tangu kuasisiwa kwa kanisa karne ya kwanza (Baada ya kuzaliwa Kristo – BK) na baadaye kubatizwa kuitwa “Kanisa Katoliki la Roma”     (Roman Catholic Shurch) karne ya nne (BK), Kanisa hili limepitia migogoro kadha wa kadha yenye kulibomoa na baadhi yenye kuliimarisha pia.     Kwa mfano, karne ya 16, Padri Martin Luther (1483 – 1534), alipojiengua kutoka kanisa hilo akipinga “ufisadi”, ubabe na upotoshaji wa Injili na kuanzisha Kanisa la Kilutheri, kanisa hilo liliyumba vibaya barani Ulaya.

Pia kujiengua kwa Uingereza kutoka Kanisa hilo na dhidi ya Papa kipindi hicho hicho, “uasi” ulioanzishwa na Mfalme Henry wa VIII wa Uingereza kwa kuanzisha Kanisa la Ki-Anglikana baada ya kukataliwa na Papa kutaliki mke wake, Catherine, nako kulitikisa Kanisa hilo la Roma likazidi kusinyaa.

Akitangaza hivi karibuni, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amesema suala la Mapadri kuruhusiwa kuoa linajadiliwa na litapigiwa kura na Baraza la Maaskofu barani Amerika ya Kusini lilikoanzia ili kupata uamuzi wa mwisho, na kwamba mpango huo unatarajiwa pia kuenezwa sehemu nyingi duniani, ikiwamo Afrika. Amesema, hatua hiyo inatokana na upungufu wa mapadri na kuongezeka kwa “Wapagani” pamoja na Ukatoliki kuzidiwa kete na makanisa ya Kiprotestanti yaliyotokea kupokea waumini wengi.

Yote hayo na yanayoendelea kulisibu kanisa hilo kongwe   duniani ni kutokana na kushindwa kwake kusoma alama za nyakati, wala kukubali usemi wa wahenga kwamba: “Wakati Ukuta” na kuendelea kufungwa nira kwa minyororo ya tamaduni za kale za Kiyahudi na Kirumi.

Na hapa napenda kumnukuu “Mwenyeheri”, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akisema: “Katika historia, watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana katika uhuru wao kama binadamu.  Kanisa lisiposhiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonyaji, basi kanisa haliwezi kuwa na uhusiano na maisha ya binadamu na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu” (J. K. Nyerere: Binadamu na Maendeleo).

Mwalimu anasema kwa msisitizo juu ya hiki kimekuja kuitwa “Theolojia ya Ukombozi”, kwamba, “kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi na mapinduzi ambayo lazima lichukue sehemu kubwa ya wajibu wa kuyaongoza mapinduzi hayo.”

Ni kwanini Kanisa Katoliki limeamua kuvunja sheria hii kuu ya kidini ya tangu enzi za kale, ya kukataza wachungaji kuoa? Papa Francis anajibu: “Hapa ni suala la Kanuni Kuu; Nidhamu kuliko Sheria zozote, ndiyo inayopaswa kuongoza.”

Ikumbukwe pia kuwa Kanisa Katoliki tayari lilikwisharuhusu mapadri wa Kianglikana wenye kuoa, walioamua kuhama Kanisa Anglikana na kujiunga na Kanisa hilo kutumika kama mapadri.

Sheria za Kanisa anazozungumzia Papa Francis ni za tangu enzi za Mitume   na kutoka himaya ya Kirumi ya kale hadi zama za Shirikisho la nchi za Kikristo za Ulaya (Christendom) lililozaa ukoloni mkongwe kwa nchi zetu na Ukristo wa Kimagharibi ukiwa sehemu ya mchakato wa ukoloni huo.

Ni kwanini mageuzi makubwa kwa Kanisa Katoliki mara nyingi yameanzia nchi za Marekani ya Kilatini (Latin America) ni swali la Kitheolojia na kisiasa linalopaswa kujibiwa kwa vigezo vya harakati za ukombozi katika dunia ya leo.

Ni katika nchi hizo, dhana ya “Theolojia ya Ukombozi” ilitagwa, kutotolewa na kulelewa na kanisa hilo. Ni theolojia inayotaka ukombozi wa mwanadamu uanzie hapa duniani ili aongoze maisha yasiyo ya dhiki kwa kusababishwa na mifumo hasi au na binadamu mwenzake, wakati mtu huyu akijiandaa kwa maisha ya milele ulimwenguni.

Wakati theolojia hii ikiendelea kupata upinzani kutoka kwa wahafidhina wa Kikatoliki kwamba ina mrengo wa fikra za Ki-Karl Marx, Waliberali wa Kikatoliki kama Kardinali Karl Rchnner wanaona ndio msingi mkuu wa Kikristo, kwamba theolojia lazima ijielekeze kwenye haki badala ya ubabe na ubeberu dhidi ya maisha na utamaduni wa wengine kwa njia huru ya utamadunisho.

Aylward Shorter, katika kitabu chake “Theology of Enculturation” (uk. 62) anatafsiri neno “utamadunisho” kuwa ni “uinjilishaji wa watu ndani ya tamaduni zao kwa njia ya upatanisho na Mungu.”

Naye Askofu Desiderius Rwoma (wa Dayosisi ya Singida) anakiri kwa mtizamo chanya katika kitabu chake, “Inculturation: The challenge of our Time”, kwamba “kuna ufa kati ya imani na utamaduni unaotakiwa kuzibwa bila kupuuza kwamba kila ujumbe wa kidini hukabiliana na binadamu katika utu na historia yake na kwa mazingira yake, ambapo si sahihi kumlazimisha kitheolojia kuachana na asili (utamaduni) yake.

Askofu Rwoma anaonya akisema: “Tusikubali kuwa au kuitwa majemedari walioshindwa katika majimbo ya Kanisa la Kiafrika; tunataka majibu yapatikane kwa mahitaji na matakwa chanya ya nyakati zetu” (uk. 6).

Mwafrika alikuwa mcha Mungu kwa haki yake kwa njia na kwa misingi ya utamaduni wake kabla ya kuletewa dini na theolojia ya mapokeo – Ukristo na Uislamu. Edward Archerman anakiri hilo katika kitabu chake “Cry, Beloved Africa” (Funguka Afrika) kwamba: “Sisi wazungu tumebadili theolojia asilia ya Kiafrika na kuweka yetu, yenye asili na mazingira tofauti na Afrika bila kibali cha Mungu.”

Majadiliano kati ya Theolojia ya Ukombozi na Kanisa Katoliki la Roma ambalo kwa sehemu kubwa, theolojia yake inaendelea kushabihiana na enzi za kale,  hayaepukiki hivi kwamba kanisa halipaswi kufumbia macho mambo ya kijamii na kisiasa; na kwamba, “Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi,” Mwalimu Nyerere  alsema.

Tutamke mapema hapa kwamba, mfumo   wa Ukristo ulioasisiwa kufuatia kifo cha Kristo kwa kulifinyanga finyanga neno (Injili) lake, ni wa Kirumi wa “dogma” (amri/sheria ya Kaizari isiyohojika]) na “sakramenti” kwa maana ya kiapo cha askari cha utii kwa Kaizari, Amiri Jeshi. Ni kusema kwamba, dogma na sakramenti, maneno yanayohusu mamlaka ya Kaizari, yaligeuzwa kuwa Katiba ya imani katika kuzamisha theolojia na tamaduni za wapelekewa “Injili” waliopewa jina “Wapagani.”

Kupanuka kwa Ukristo kuwa dini ya kimataifa kuanzia karne ya tatu kulitokana na nguvu ya Kijeshi ya Rumi ya kale chini ya Mfalme Constantini wa kwanza, aliyepania kuteka dunia ya wakati huo. Kuridhiwa kwa Ukristo kuwa sehemu ya Katiba ya utawala wa Roma (theocracy) kulifanya imani hiyo kuwa dini ya utamaduni wa Rumi.

Kuanguka kwa himaya ya Rumi kulifuatiwa na kujiunda upya kwa vikundi vya nchi zilizokuwa tiifu kwa Rumi kwa misingi ya dini iliyoanzishwa na kujiita “Ushirika wa nchi za Kikristo” (Christendom) ambao ndani ya kuta zake utamaduni wetu (mpya) wa “kisasa” ulitotolewa enzi hizo zilizoitwa “Zama za Giza” (Dark Ages) na kazi ya umoja huo ikawa ya kupeleka “mwanga” kwa “Wapagani” wa dunia.

Kwa mchanganyiko wa ukoloni na ghera (zeal)     ya kimisionari, himaya ya nchi za Kikristo, kama sehemu ya utamaduni wa Kimagharibi, ilipanuka sehemu kubwa ya dunia kati ya karne ya 16 na karne ya 19kamahimaya ya Rumi iliyohuishwa kwa kiu ya kuteka nchi mpya na kuzifanya makoloni yake.

Ukristo “Mpya” uliototolewa ndani ya “Christendom” na kupandikizwa kwetu si sawa na ule wa enzi za Kristo, bali ni mchanganyiko wa imani za Kikristo, mila (za Kipagani) na jadi za kale za wazungu hao waliojikweza kwa ubeberu na kuona heri Ukristo uenezwe kwa mila, jadi na mazingira yao, badala ya kuheshimu pia mila na jadi zetu na kwa mazingira yetu.

Tuangalie chimbuko la theolojia ya sasa inayolitia Kanisa Katoliki matatani zama hizi kwa kukubali kuendelea kuishi zama za Mfalme Constantine wa Kwanza, aliyebinafsisha Kanisa na kufariki bila kubatizwa.

Kaizari Konstantini alichukua wadhifa huo kwa njia ya uhaini kufuatia kifo cha baba yake, Kaizari Konstantin Chlorus, Julai 25, 306 katika mji wa Eboraco (sasa York) nchini Uingereza.  Alitangazwa Kaizari na jeshi, kinyume na utaratibu uliowekwa na Kaizari Dickletiano.

Dickletiano alikuwa ameigawa himaya pana ya Roma katika kanda nne, zikiongozwa na Makaizari wanne chini ya Kaizari Kiongozi kurahisisha utawala,  lakini kufuatia kifo cha baba yake, Konstantini alikaidi utaratibu huo na akajinyakulia Kanda ya Kaskazini iliyoundwa na Britania na Gallia (Uingereza na Ufaransa) kwa nguvu na vita.  Akaweka makao yake (Ikulu) katika mji wa Trier.

Ndoto ya Konstantini tangu mwanzo, ilikuwa kwa yeye kubakia mtawala pekee wa himaya yote ya Roma. Hivyo, Kaizari huyu mpenda vita, mkatili na mwenye uchu wa madaraka alianzisha vita kali kuwamaliza Makaizari wengine, akianzia na Kaizari Maxentio wa Kanda ya Magharibi (Italia na Afrika, na Makao Makuu yake Roma) mwaka 312; wakafuatia Makaizari Maximino, Daria na Luciano, shemeji yake Konstantini.

Baada ya kuwaua kwa kuwakata vichwa kisha kuvitundika juu ya mlingoti na kuvizungusha katika Kanda zao kwa fedheha, Konstantini sasa alitaifisha Kanisa Katoliki na kulifanya la dini ya himaya yake kwa tamko la Milano la mwaka   313, ili Kanisa liendane na matakwa yake. Kutaka akubalike kwa viongozi wa kanisa hilo, alitoa rushwa ya majumba ya fahari, mali, vyeo na heshima ya kiutawala wa kidunia. Viongozi wakuu wastaafu wa Kanisa, Eusebio na Laktantio, walikaribishwa Ikulu kama washauri, walimu na waandishi wa Kaizari.

Na pale viongozi wa kanisa walipoonja utamu wa rushwa ya Kaizari wakalewa kwa vinono, waliiasi imani ya kweli, na hivyo mwaka 314 maaskofu wakaitisha mtaguso mdogo (Sinodi) katika mji wa Arelato (Arles) nchini Ufaransa, wakaazimia kuanzia hapo Wakristo wote kuwa Askari wa Kaizari, wenye wajibu wa kulinda na kupigania himaya ya Kaizari, kinyume na mwanzo ambapo hawakuruhusiwa kazi za kijeshi, kubeba silaha au kuua, wala kushuhudia adhabu ya kifo, maana ilisemwa “mpende nduguyo na adui pia”.

Maaskofu wakafanywa Makasisi wa Jeshi kubariki Jeshi la Kibeberu na kuandamana na majeshi kwenye uwanja wa vita na hawakuruhusiwa kuoa. Wakinzani wa Kaizari walioona mauaji kuwa yalipingana na upendo, waligoma au kuwagomesha wengine kwenda vitani.  Hao waliteswa kwa kusulubishwa msalabani.

Kuanzia hapo, mauaji ya halaiki vitani yakahalalishwa na kushangiliwa kama ushindi na “mapenzi ya Mungu; msalaba, kifaa kilichokuwa adhabu ya aibu kwa Wakristo ukageuzwa bango, bendera na ishara ya ushindi wa “Wakristo” vitani kutimiza ndoto ya Kaizari Konstantini-“in hoc signo vinces”.

Msalaba zaidi ukawa ishara ya utukufu wa enzi (duniani), ukavaliwa na viongozi wa kanisa, kwa maana wao ndio walioongoza majeshi vitani. Tangu hapo, mafundisho ya dini yakafuata mkondo wa imani za Kirumi.  Dogma, amri ya Kaizari ikabatizwa kuwa “Kanuni ya imani”; “Sacramentum” (Sakramenti) yaani, kiapo cha Askari cha utii kwa Kaizari kikabatizwa kuwa “njia ya wokovu”. Wakati huo huo, Mtakatifu Augustino (wa Hippo) akashawishika kuunda dhana ya “Vita Halali”, (The Just War Theory), kuhalalisha vita na kuifanya kuwa shughuli kuu ya nchi za himaya ya Kikristo (Christendom) hadi leo.

Tabaka za “Mabwana na Watwana” zikapewa jina la “Wakleri” na “Walei”; Wakleri kwa maana ya watawala, Mabwana wa kanisa ambayo ni tafsiri potofu ya neno la Kiyunani “Kleros”, tofauti na matakwa ya maandiko (Mt. 25:34); “Walei” kwa maana ya watwana watiifu, ambalo ni tafsiri mbovu ya neno la Kiyunani “laos” na kinyume cha maandiko (Mt. 13:1-9, 18:2-23, 36 – 43).

Ukinzani wa roho na mwili, ulioundwa na falsafa ya Wayunani kuhalalisha ukandamizaji wa halaiki ya watumwa ukarejeshwa na kuingizwa katika kanuni ya imani kutetea utumwa.  Kwa sababu hiyo Kanisa likajitumbukiza katika wimbi la mauaji vitani na kushabikia ukoloni na ubeberu wa kiroho, unyonyaji wa halaiki kutokana na uchoyo wa mali, vyeo na utukufu wa kidunia ambao ndiyo asili kuu ya maovu.

Kwa jinsi hii, Askofu wa Roma ambaye sasa alipewa jina “Papa”, yaani “Baba”,akayarithi madaraka ya Kaisari pamoja na mbwembwe zake, akawa mtawala, Kiongozi wa majeshi (Yesu hakuwa na jeshi) na bwana wa watwana`waliomlimia mashamba yake kama Kabaila mkuu wa Italia nzima.  Akajiimarisha kimadaraka na kiuongozi Kikanisa   kama mrithi wa kiti cha Petro; akaimarisha utawala msonge wa ki-imla katika Kanisa na utamaduni mkongwe wa ubaguzi na unyanyasaji wa halaiki na viapo kama tabia ya ukoloni ya kuwatawala watu, kuwanyanyasa na kuwaogofya, wasitambue haki, heshima na hadhi yao katika jamii, madhila na majonzi yaliyozaa leo upinzani chini ya dhana ya “Theolojia ya Ukombozi”.

Kwa Kanisa Katoliki kubinafsishwa na Kaizari Konstantini na kuingizwa katika mfumo wa Kifalme, Viongozi wa Kanisa waliimeza ndoano ya ufahari, wakarubuniwa na tamaa ya mali, vyeo na madaraka. Wakakopa lugha ya falsafa ya utawala wa mamwinyi kama kielelezo cha lugha ya dini, yaani “theolojia”, na kupotosha ukweli wa imani.

Kwa hiyo, historia ya ulimwengu wa Magharibi na Ukristo ni historia ya vita visivyokoma, unyonyaji na uporaji wa mabara na upekechaji wa silaha usio na kifani kwa ajili ya kuendelea kupora.     Ndiyo tabia inayounda mifumo ya tawala za kikatili za ukoloni wa ukabaila, ukoloniwa ubepari, ukoloni wa utandawazi (utandawizi) kwa unafiki wa kuleta maendeleo, kujenga “demokrasia” na “utawala bora” kwa misingi ya utamaduni wa Kimagharibi, kana kwamba Afrika haikuwa au haina misingi ya dhana hizo.

Ndiyo tabia inayounda utamaduni wa ulimwengu wa Magharibi, uliofaulu kuiteka dini (imani) ya kweli na kuifinyangafinyanga kwa mfano wake, na hivyo kuzuia mchakato wa mapinduzi ya kujenga ulimwengu bora wa heshima na furaha kwa kila mtu.

Je, haikusemwa, Mungu ni wa Mataifa? Maana yupo Mungu mmoja tu, atakayewaokoa wenye dini, atakayewaponya pia wasio na dini kwa imani ile ile ya mema (Mdo. 17:25; Mt. 15:30)

“Ujamaa” ambao ndio msingi mkuu wa utamaduni (dini) wa Mwafrika maana yake ni upendo kwa kutambua haki, heshima, uhuru na usawa wa binadamu, kujali udugu kati yao na kujenga mshikamano wa amani.

Yeyote anayesema “Nampenda Mungu (kwa ibada za kidini) na huku anamchukia binadamu mwenzake (ubaguzi wa kiuchumi, kiutamaduni) ni mwongo, maana mtu asiyempenda mwenzake anayemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hajamwona (1Yoh.4:20).  Mtu huyo ni Kaizari wa zama zetu, awe Mkristo, Mwislamu, Mhindu au “Mpagani.

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972