Home Latest News WABUNGE REJESHENI MATUMAINI KWA WATANZANIA

WABUNGE REJESHENI MATUMAINI KWA WATANZANIA

801
0
SHARE

NA LAMU KILIMBA,

NDUGU wabunge wetu wa upinzani, Chama tawala (CCM) pamoja na wale wateule kwa unyenyekevu mkubwa nawasalimu, poleni sana kwa kazi nzito za kulijenga taifa letu. Nyinyi ni sauti zetu bungeni, mpo huko kwa niaba yetu, Watanzania wenzangu naomba mpokee ujumbe huu muhimu ulio ndani ya mioyo ya Watanzania wengi, tafadhali acheni uvyama japo kwa muda mkapiganie haya kwa niaba yetu hasa katika bunge la bajeti, tunatambua mapenzi makubwa mliyonayo kwa vyama vya siasa tafadhali unganeni kwa muda tu japo mpaze sauti katika haya.

Wabunge bila kujali itikadi, kapazeni sauti zenu mrejeshe matumaini ya watumishi waliopotea katika mioyo yao, watumishi wanatabasamu usoni huku mioyo yao ikiwa yenye hasira, chuki na kukata tamaa dhidi ya Serikali, maslahi yao sasa wanasubiri mpaka hapo Serikali itakapofanya kwa hisani si haki yao tena kitumishi, maslahi na haki za watumishi vimeporwa na uhakiki wa watumishi hewa mwaka sasa hakuna nyongeza ya mishahara, hakuna uhamisho, hakuna mikopo, makato ya kodi si rafiki tena, wakati watumishi wakilalamika mishahara kiduchu Serikali inataka wafanye mazoezi wakati maisha yao ni mazoezi tosha, nyumba za watumishi, ofisi za watumishi, vifaa vya kazi ni zaidi ya mazoezi bado wanatakwa wafanye mazoezi mengine. Tafadhali wabunge wetu kwa niaba yetu msipitishe bajeti mpya mpaka mishahara ya watumishi iongezwe, kodi ipunguzwe kutoka 11% mpaka 9% kama alivyotoa ahadi Mh wetu kwenye May Mosi 2016, chonde chonde tunajua mapenzi mliyonayo kwa vyama, lakini fanyeni maamuzi magumu kwa niaba yetu maana mna nguvu kikatiba.

Tafadhali acheni uvyama mpinge tabia ya viongozi kuvunja sheria makusudi, haijalishi dhamira iwe njema au mbaya hakuna mwenye kibali cha kuvunja sheria zetu tulizojiwekea wenyewe, hivyo tunaomba mtusaidie kukomesha tabia ya viongozi wanaovunja sheria kwa kisingizio cha kurejesha uadilifu hatuwezi kufanya makosa kuondoa makosa wala si utaratibu wetu kama taifa, vyombo vya usafiri vinatolewa matairi eti kukomesha madereva wasio wastaarabu, ona watu wanatajwa hadharani eti kisa tuhuma tena na viongozi wasio na mamlaka kikatiba, tazama watumishi wanavyofanywa na wakubwa kwa kisingizio cha kurejesha uadilifu wa watumishi. Kwa niaba yetu msipitishe bajeti mpya mpaka Serikali itoe kauli kukemea tabia hii ya kufanya makosa ya kisheria kushughulikia wavunje sheria, tunaomba mtusaidie mrejeshe utaratibu wa kuheshimu sheria katika kutatua mambo mbali mbali ya kitaifa, kila Mtanzania awe chini ya sheria.

Wabunge wetu tunaomba msipitishe bajeti mpya mpaka tupate majibu juu ya kodi zilizoibuka ghafla kwenye benki zetu na makampuni ya simu, Watanzania wanapata maumivu makubwa gharama kubwa za kutuma fedha, kutoa fedha tofauti na matumaini waliyopewa kwenye uchaguzi mkuu 2015, kinyume na maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, katika bajeti iliyopita Watanzania wanakatwa makato m pesa, tigopesa, airtel money, hallopesa na kwenye benki nchini, tafadhali msikubali kupitisha bajeti mpaka mrejeshe matumaini yetu juu ya gharama hizi kandamizi. Ninyi mna nguvu kikatiba tafadhali acheni uvyama mtusaidie wapiga kura wenu.

Acheni itikadi za vyama mkahoji hatima ya fedha kutoweka kwenye mzunguko, wananchi wapo hoi taabani biashara haziendi wala si wapiga madili kama tunavyojifurahisha hali ni mbaya kweli kweli tena wanyonge ndiyo wamenyongwa haswaa, wapiga kura wenu wamepoteza matumaini kiasi cha kumkumbuka mkuu mstaafu wakati ndiyo kwanza safari inaanza. Tafadhali tumieni nguvu yenu kikatiba kuitaka serikali pesa zirejeshwe kwenye mifuko ya hifadhi za jamii, benki za biashara na taasisi za kifedha kama ilivyokuwa awali, tafadhali kwa sauti zisizo na itikadi msipitishe bajeti mpaka tupate majibu ya huu uchumi uliokua kwenye takwimu huku mtaani hali ikiwa mbaya.

Acheni itikadi na mapenzi kwa vyama mkasema ukweli kuhusu viashiria vya njaa tafadhali, kwa mamlaka mliyonayo kikatiba ombeni Serikali itoe majibu ya kisayansi namna ya kukabiliana na ukame, wakulima hawajui hatima yao maana kilimo chao cha kusubiri rehema ya mvua si rafiki msimu huu, wabunge acheni kupenda vyama kuliko wapiga kura wenu wanaokunywa uji asubuhi mpaka usiku kutibu njaa, unganeni kwa pamoja kuitaka Serikali itoe majibu namna ya kujihami na viashiria vya njaa kwa sauti zenu tunaomba tupate majibu kuhusu bei vya vyakula kuwa ghali. Kwa niaba ya wapiga kura wengine naomba msipitishe bajeti mpya mpaka tupate bei rafiki ya unga, maharage, mchele, ngano na vyakula vingine muhimu kwa maisha ya Watanzania ambapo sasa kuvipata ni anasa kutokana na bei kuwa kubwa.

Wekeni pembeni mahaba kwa vyama mrejeshe mgawanyo wa madaraka ndani ya taifa letu, Mwl Nyerere alituachia utaratibu na msingi ya kuheshimu mipaka ya kufanya kazi, RC afanye majukumu yake, DC afanye majukumu yake, polisi hivyo hivyo, Waziri pia awe na mipaka, wataalamu wafanye mambo yao ya kitaalamu na wanasiasa wafanye siasa zao pasipo kuvuruga mambo ya kitaalamu, Tanzania tuna katiba, sheria, kanuni, utaratibu na misingi mizuri ya kufanya kazi, tafadhali tunaomba mpiganie suala hili muhimu msikubali mamlaka kuingiliana hata bunge haliwezi kubaki salama endapo mgawanyo wa madaraka hautazingatiwa. Wabunge wetu kumbukeni mgawanyo wa madaraka ndilo zao la utawala wa kuzingatia katiba na sheria, ndiyo misingi ya haki za wananchi, ndiyo jibu la kudumu umoja wetu tuliachiwa na baba yetu wa taifa. Tunaomba mkapaze sauti zilizoungana kizalendo kurejesha heshima kwa mipaka ya madaraka mkilipuuza hili usoni tutashuhudia mdogo akimpiga mkubwa hadharani, lazima mahakama iwe huru, bunge liwe huru kila mamlaka ifanye shughuli zake kwa kuzingatia mipaka tuliyojiwekea.

Tafadhali wekeni vyama kando msipitishe bajeti mpya mpaka tupate majibu ya ahadi za Serikali kwetu na utekelezaji wa bajeti zilizopita, sisi wapiga kura wenu tunahitaji kujua bajeti iliyopita imetekelezwa kwa asilimia ngapi? Na kwanini iwe utekelezaji hafifu? Kila wizara itoe majibu yasiyo ya kisiasa kwanini bajeti zilizopita hazitekelezwi kikamilifu? Kwanini Serikali ilete bajeti mpya? Tafadhali tunaomba tujue kwanini tunapitisha bajeti mpya wakati tuna viporo? Tunawasihi msipitishe bajeti mpya bila majibu ya kisayansi kuhusu viwanda tulivyoahidiwa karibu kila wilaya, msikubali saundi za waziri wa viwanda, msipitishe bajeti bila majibu kuhusu milioni 50 kila kijiji, msikubali kupitisha bajeti bila majibu sahihi kuhusu ajira kwa vijana waliosoma kwa kodi zetu, tafadhari msipitishe bajeti bila majibu ya miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege na miradi mingine iliyo simama ghafla huku wapiga kura tukiwa njiapanda tukijiuliza tatizo bila majibu. Tafadhali tunaomba angalau kwa bunge la bajeti mpaze sauti za kizalendo kurejesha utekelezaji wa ahadi za Watanzania, rejesheni matumaini ya ajira, matumaini ya viwanda, matumaini ya kilimo cha kisasa fanyeni hivyo kwa faida ya wapiga kura vyama acheni kando kwa muda.

Mwisho, kwa unyenyekevu mkubwa nawatakia utekelezaji mwema wa maombi haya muhimu kwenu, wapiga kura na taifa kwa ujumla wake, natambua mnapenda sana vyama vyenu pengine mnaogopa kuitwa wasaliti, mamluki, wanafiki na majina mengine ya kukatisha tama, wala msiogope tuko nyuma yenu.

Kumbukeni mpo bungeni kwa niaba yetu wala si vyama, vyama ni magari tu lakini nauli ni sisi wapiga kura, mna nguvu kikatiba wala hamtashindwa kikubwa msimame pamoja kama wabunge Watanzania wenye kuifikiria Tanzania zaidi kuliko vyama.

UMOJA NI USHINDI, PAMOJA MTAREJESHA MATUMAINI YETU SISI WAPIGA KURA WENU. 

lamuelizayo@gmail.com
+255766033331