Home Makala Wabunge wa upinzani, CCM hawaaminiki

Wabunge wa upinzani, CCM hawaaminiki

1630
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

‘CONFIANZA’ ni neno kutoka Latini Amerika. Neno hili hutumiwa sana na raia wa Colombia wakimaanisha imani yao kwa serikali iliyopo madarakani.

Kwa lugha ya kimombo neno Confianza ni ‘confidence or trust in the government ability to fulfill its duties and increase general sense’.  Raia wa Colombia wanachofanya ni kuiamini serikali au katika harakati zake za kuleta misingi ya maendeleo yao na kukuza uchumi wa wa nchi yao. Kitendo hicho cha kuiamini serikali yao huita ‘confianza’.

Hiki ni kitu ambacho lazima kifanyike na njia sahihi na ‘confianza’ ni kujitambua na kutambua kisha kuthibitisha mwenyewe serikali inasikia na inasikiliza pamoja na kuwa na watendaji wenye uwezo na wasio na mawaa. Kwamba serikali inafahamu na inakosea, kwani wanaounda serikali ni watu ambao wanatoka katika jamii yetu.

Kwahiyo ukilichanganua neno ‘confianza’ kulingana na jamii yetu ambayo inazalisha viongozi wa serikali, kwamba mahusiano baina ya mtu na mtu yanafanikisha kazi nzuri inayojenga jamii bora. Mahusiano baina ya wananchi na serikali yao, maana huwezi kuwatenga watu na serikali kwani serikali ni watu na watu hao ndiyo serikali.

Mahusiano ya watu na serikali ni sawa na mahusiano ya watu ndani ya jamii yao. ‘Confianza’ linatawala maisha ya watu Latini Amerika tangu siasa, uchumi, tamaduni na jamii kwa ujumla. Kwahiyo tukichukua mfano wa ulinzi shirikishi kwa jeshi la Polisi nchini mwetu na wananchi unapaswa kuzingatia ‘confianza’ baina yao kama sehemu ya serikali na wananchi.

Hii ni imani kubwa juu ya utendaji kazi wa taasisi ama asasi yoyote ya serikali yenye makusudio ya kuhudumia wananchi ndani ya nchi yao. Kwa mfano nchini Dominica husema ‘tengo confianza’ kwa imani juu ya mtu au mtumishi wa umma inatokana na mahusiano yao ya kikazi na kijamii.

Kwamba kila jambo hufanywa kwa uaminifu na taratibu ambazo zinamfanya mwingine aamini utendaji wake, aamini uwepo wake na usalama wake. Lakini kama mtu anakuwa tofauti na kutoiamini serikali yake, raia hao husema ‘abuso de confianza’ yaani kutoaminiana ama kukosa imani na serikali ama mtu Fulani wakiwemo wabunge .

Katika milipuko ya kisiasa kumekuwa na mambo mengi yenye kuonyesha ‘confianza’ au ‘abuso de confianza’. Matendo yote haya yanatokana na mitazamo ndani ya jamii zetu. Wakati mwingine matendo yanapozidi kete ukweli ni uharibifu.

Hata kama tunaamini serikali inatakiwa kukubaliana na matakwa yetu, ni lazima tufahamu kuwa serikali hiyo ni watu, inasikia, inasikiliza, inaona, inawaona,inawapenda, inapendwa, inaheshimu, inaheshimu na kadhalika.

Aidha, huwezi kuwa na chama cha siasa imara ambacho wabunge wake wanaaminika kuhongwa, kulaghaiwa na upande wa utawala. Kauli na matendo yao hayaendani na mrengo wa chama chao.

Vivyo hivyo huwezi kuwa na serikali sikivu kama imeundwa na watendaji (mawaziri) ambao wananuka rushwa. Wananuka kashfa. Wanahusishwa na ujangili. Wanatajwa tajwa kudhulumu vimada na vijikashfa vingi ambavyo vinawaoendelea heshima.

Lipo jambo jingine linalowaondolea mawaziri sifa ya kuaminiwa endapo wanakuwa wafujaji wa mali za umma au mwenendo wao katika madaraka unatia shaka.

Ni mashaka hayo ndiyo yananifanya nijadili nanyi leo, inaelekea na sasa dhahiri wabunge wa upinzani na wale wa CCM hawaaminiki na serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, kumekuwapo na wimbi kubwa la wabunge wa upinzani kuhami CCM, ambapio hadi sasa wabunge zaidi ya nane wamehama vyama vyao na kuelekea CCM.

Licha ya kwamba hoja kubwa inayotolewa na wabunge hao ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na wengine kukosoa mienendo ya chama chao, suala la kuaminiwa bado limebaki kuwa kitendawili.

Hata wabunge waliobaki sasa upinzani bado hawaaminiki kwa sababu ipo idadi kubwa ya wabunge wanaodaiwa kuwa watahamia CCM siku za usoni, hali hii inazidi kuwafanya wananchi kutowaamini wabunge na hata kukata tama ya kupanga foleni na kuunguzwa jua kwa lengo la kwenda kumpigia kura mbunge asiyeamini.

Pia ikumbukwe kuwa kutoaminika huku kwa wabunge hakujatokea tu upinzani kwani Rais Magufuli kwa siku 31 alizokaa madarakani hakuwa baraza la mawaziri. Hakuna sheria yoyote iliyombana kuhusu uteuzi wa baraza hilo. Hata hivyo uteuzi wa baraza la mawaziri uliotangazwa Desemba 10 mwaka 2015 ulinonyesha hali halisi kuna ‘abuso de confianza’ ndani ya serikali na chama cha mapinduzi(CCM).

Kwamba uteuzi wa baraza la mawaziri umeonesha kutoaminiana ndani ya chama na serikali. Uteuzi huo umebeba ishara za wazi kuwa walioteuliwa wamepitia chekeche kubwa mno na wakaonekana wana nafuu zaidi kuliko wengine.

Aidha, uteuzi wa baraza la mawaziri ulitudhihirishia kuwa bado lipo tatizo kubwa na wabunge waadilifu bila kujali vyama wanavyotoka. CCM ndicho kinachopaswa kuunda serikali. Bahati mbaya au nzuri uteuzi wa mawaziri umekuwa na ishara tofauti na ilivyokuwa inafikiriwa.

Ukweli huo unadhihirishwa na teuzi za wabunge kutoka nje ya chama kwa maana ya kuwa watalaam kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri.

Ingawa walioteuliwa kutoka vyuo vikuu na sehemu nyingine nchini ni makada wa CCM, lakini hakuwagombea ubunge majimbo. Maana yake kwa hali ilivyo sasa Wabunge wa CCM hawaaminiki na usafi wao umetoweka. Ni lini wataweza kuurejesha usafi huo ndiyo changamoto inawakabili.

Ni lazima wafike mahali wajiulize kwanini Rais aliamua kuwageukia wataalamu wasiokuwa wabunge licha ya kuwepo wataalamu walio wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano?

Taswira iliyojengeka katika jamii kwa sasa inamwona Ras Magufuli kama mtu pekee anayeaminiwa na wananchi kuliko chama chake. Lakini hatuwezi kumtenganisha Magufuli na chama chake kilichomfikisha hapo baada ya kupigiwa kura na wananchi.

Rai yangu ni kwamba usafi ndani ya CCM na vyama vya upinzani kwa ujumla umetoweka. Ni dhahiri wanasiasa walioshinda ubunge jimboni huko CCM, CUF, Chadema hawaaminiki.

Ni wakati wa kuirudia Rasimu ya Warioba kuhusu kutenganisha uwaziri na ubunge.  Pia kutenganisha mamlaka ya chama juu ya mbunge ili mbunge anapohamia chama kingine kusiwepo na ulazima wa kuingia tena kwenye sanduku la kura ili kumchagua mbunge mwingine, hii itaondoa manung’uniko ya gharama za chaguzi za marudio.