Home Makala Wabunge wapunguze mihemko

Wabunge wapunguze mihemko

1115
0
SHARE

Na Tobias Nsungwe

UNAWEZA ukasema kila fani ina upungufu wake siku hizi. Kasoro nyingine hazikutarajiwa kutokea katika kizazi hiki.

Sehemu nyingi mambo hayafanyiki kulingana na taratibu zilizowekwa. Tunajenga nchi inayopenda njia za mkato hata katika mambo ya msingi. Jamii inakuwa njia panda hasa inapoona hata viongozi wakifanya mambo ya hovyo.

Wakati Injili inaletwa haikutarajiwa kuona makasisi wakiwadhulumu waumini wao. Kamwe haikutarajiwa watumishi ‘kuuza’ huduma ya Bwana Yesu. Siku hizi baadhi ya wanaojiita wachungaji huwatoza waumini wao fedha kwanza ndipo wawaombee au kuwatoa mapepo.

Nimesikia juzi mchungaji mmoja akiwahimiza waumini wake kutoa sadaka huku akisema ni aibu kwa mkazi wa Dar es Salaam kukosa hata Shilingi 100,000 ya kutoa sadaka kwenye kanisa lake.

Kuna wachungaji wametuhumiwa kuiba, kuna wainjilisti wametuhumiwa kuzini na hata kubaka. Wako pia watu wanaojiita wachungaji ambao wametuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na hata uasherati.

Watu kama hawa kamwe si watumishi wa Mungu. Ni matapeli kama matapeli wengine wanaotumia dini kujipatia maisha ya kifahari na umaarufu katika jamii. Wachungaji hawa feki wanafanya kosa kubwa la kujinasibisha na kazi ambayo si yao. Juhudi za Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe za kuhakiki upya taasisi za dini lazima liungwe mkono ili wachungaji matapeli waweze kuumbuliwa. Hatuwezi kuendelea kuwa na wachungaji ambao huwapa waumini wao sharti la kusali wakiwa uchi.

Wachungaji hawa feki na wavivu wamekimbia kazi halali kama kilimo, uvuvi, useremala au ujenzi na kuja mjini kuwapumbaza watu wa aya za Biblia huku wakijua fika kuwa kwa kufanya hivyo wanachafua majina ya viongozi wetu wa dini tunaowaheshimu sana. Sioni mantini kwa mtu kujiita askofu wakati usoni na moyoni mwake amejaa ulaghai na elimu duni.

Wapo pia maimamu na masheik wanaoipotosha jamii kwa matendo yao. Ni jukumu la viongozi halali wa dini ya Kiislamu na waumini kuwaumbua wale wanaotumia Korani tukufu kupotosha watu huku wakihusishwa pia na matendo maovu katika jamii. Sheria zinawekwa kwa ajili ya kudhibiti maovu katika jamii. Hata hivyo wakati mfumo wa sheria unaanza hapa nchini hasa baada ya kuja wakoloni wa Kiingereza mwaka 1920 haukuwategemea baadhi ya watu wafanye mambo ya hoyo kutokana na hadhi zao katika jamii.

Wakati wa ukoloni rushwa halikuwa tatizo kubwa sana. Hilo lilianza kuwa tatizo kubwa kuanzia miaka ya mwanzo ya Uhuru. Ndio maana ikaanzishwa Sheria ya kudhibiti rushwa. Kabla ya hapo haikutemewa kwamba mtumishi wa Serikali angethubutu kutoa au kupokea rushwa. Watumishi wa Serikali walionekana kama ni watu ‘wenye hadhi fulani’ katika jamii.

Hivi sasa tunaambiwa asilimia 68 ya Watanzania hutoa rushwa kutokana na uhafifu wa huduma kwa wananchi au kama njia mojawapo ya kupata huduma kwa haraka zaidi ingawa wanatambua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.  Kwa mujibu wa duru za mahakama na Bunge nchini si rushwa ya mali tu inayofanywa bali pia kuna rushwa ya mapenzi ambayo mara nyingi hudaiwa na watu wenye madaraka si hapa kwenye idara kadhaa.

Hata yalipokuwa yanaanzishwa magazeti haikutarajiwa kwamba wahariri wake wangepokea rushwa kwani zilipokuwa zinaundwa kanuni za uendeshaji wa vyombo vya habari mameneja wa vyombo hivyo walidhaniwa kuwa watu wenye hadhi fulani. Hivi sasa kuna mjadala mkubwa kuhusu hadhi za watu waliokabidhiwa majukumu mazito katika idara mbalimbali.

Bunge litaanza vikao vyake mwezi ujao huku bado Watanzania wakitafakari yaliyojiri katika vikao vya bunge la bajeti liliisha mwezi Julai. Vikao vilivyopita vilitawaliwa na misukosuko mingi huku wabunge wa upinzani wakimtuhumu Naibu Spika, Dk Tulia Mwansasu kutowatendea haki.

Wabunge na viongozi wa Chadema wamedai mara kadhaa kwamba Ofisi ya rais na Chama cha Mapinduzi (CCM) wanamtumia Dk Tulia kuwabana wabunge wa upinzani bungeni. Wanadai mara nyingi kwamba Naibu Spika anawapendelea wabunge wa chama tawala. Hivi juzi Dk Tulia amejibu mapigo kwa kusema kwamba ukiwa umekaa kwenye kiti cha Spika malalamiko kwamba unapendelea hayakosekani kuoka pande zote.  Kwa ujumla hisia za wapinzani kwamba Dk Tulia ni ‘mtu wa Ikulu’ zinachagizwa na ukweli kwamba kiongozi huyo kijana ni mbunge wa kuteuliwa na rais. Hakuchaguliwa na wananchi na safari yake ya kuukwaa u-Naibu Spika ilionekana kuwa na shinikizo la wakubwa wa CCM. Nasema hizo ni hisia tu.

Wengi mtakumbuka kwamba wabunge wa upinzani walikuwa wakitoka bungeni kila Dk Tulia anapokalia kiti ili kutuma ujumbe wa kutokuwa na imani naye. Jambo lile lililaaniwa pia na Rais John Magufuli. Hivi sasa juhudi zinahitajika kuwaweka sawa wabunge wa upinzani na Dk Tulia ili kadhia hiyo isijirudie.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema hivi karibuni kwamba kusingekuwako misuguano kama wabunge wangefuta kanuni. Amesema tatizo lililopo sasa ni kwamba karibu asilimia 70 ya wabunge ni wapya na hivyo hawajui au hawataki kufuata kanuni kwa vile wamejawa na mihemko zaidi kuliko busara.

Ofisi ya Bunge imepanga kuwapiga msasa ili wabunge wote wazielewe kanuni na kuzifuata au zile zilizopitwa na wakati zifanyiwe marekebisho. Anasema Ndugai kwamba wakati kanuni za Bunge zikitungwa ziliwatarajia wabunge kuwa ‘watu wenye hadhi na staha fulani’

Elimu ya darasani pekee haitoshi. Wabunge wajifunze kuongea kwa staha na adabu hasa wanapowazungumzia viongozi wa kitaifa kama vile Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Abeid Amani Karume, Mzee Rashidi Kawawa au Mzee Ali Hassani Mwinyi. Ni wajibu wa kila mbunge kumheshimu rais hata kama hatokani na chama chake.

Wabunge wafundishwe jinsi ya kuwasilisha hisia zao kwa viongozi wa dini. Hatutarajii mbunge wetu akashifu viongozi wa dini eti kwa sababu tu amesemea bugeni. Wabunge pia wajifunze pia lugha ya kuwasemea watu wanaotokana na makundi maalumu kama jamii kama vile walemavu, watoto, wazee, wanawake au watoto.

Wabunge wengi ni vijana. Hivyo basi wajifunze kuwasiliana na watu waliowazidi umri. Ubunge usiwape kiburi kiasi cha kujibizana na wazee ndani na nje ya Bunge.  Tumeshuhudia baadhi ya vijana wakiwatukana wazee bungeni. Hayo si maadili ya Watanzania. Wabunge pia wafundishwe kujua mipaka yao. Kazi ya mbunge ni kushirikiana na wenzake kutunga sheria, kuishauri na kuiwajibisha Serikali. Si kazi ya mbunge kutimua watumishi wa umma.

Kanuni hazikutarajia kuona watu wakorofi wakiingia bungeni. Wakati kanuni zinatungwa hazikutabiri kwamba iko siku wabunge watatoa matusi bungeni wala haikutarajiwa wapigakura kuwapeleka watu wababaishaji bungeni. Bunge lilipoanza kazi zake nchini mwaka 1956 haikutarajiwa kuona wabunge wakitoka nje wakati rais au waziri mkuu akihutubia Bunge.

Wakati akina Pius Msekwa na Anna Makinda wakitunga kanuni hawakutarajia kuona wananchi watachagua wabunge wasio na staha kiasi cha kubishana na mamlaka za mhimili huo wa pili wa dola kila mara. Mzee Samuel Sitta alipokuwa akiongoza vikao vya kupitisha kanuni za Bunge haikutarajiwa kuona kuwa kutatokea wabunge wanaoendesha mambo yao kwa hisia.

Kauli na mambo wanayoyafanya baadhi ya wabunge ndani ya Bunge vinawaondolea hadhi ya kuitwa ‘waheshimiwa’.  Msisimko wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulifanya baadhi ya wapigakura kuwachagua watu wasiofaa kuwa wabunge. Dhambi ya kuchagua watu kwa mihemko itawatafuna wapigara kura kwenye baadhi ya majimbo kwa miaka mine na nusu.