Home Latest News WACHEZAJI WA KIGENI KUWAPA CHANGAMOTO WAZAWA

WACHEZAJI WA KIGENI KUWAPA CHANGAMOTO WAZAWA

4746
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


SOKA ni sayansi inayoeleweka na wadau wengi wa mchezo huo wana msemo wao usemao mpira una njia zake.

Mara zote dhambi ya ubaguzi huwa haimuachi mtu akiwa salama lakini pia ukitaka mafanikio basi usiogope changamoto.

Kauli hizi zinaweza kuwa na maana kubwa katika mpira wa Tanzania hasa unapozingatia uamuzi wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Hivi sasa kumekuwepo na mjaadala mkubwa kuhusiana na uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi kufikia 10 ambao kimsingi timu inaweza kuwatumia itakavyoona inafaa.

Katika mijadala hiyo tayari kumekuwepo na hofu ya kuamini kwamba kuongezeka kwa idadi hiyo kutawafanya wachezaji wazawa wakose nafasi ya kucheza katika timu zao.

Wakaenda mbali zaidi kwa kuamini kuwepo kwa wachezaji wengi wa kigeni katika Ligi Kuu kutasababisha kuwepo na timu ya soka ya taifa iliyo dhaifu.

Hebu kwanza tujiulize maswali haya, lini timu ya taifa ilikuwa bora, lini vipaji  vya wachezaji vilikua na kupanda, na lini pia soka la Tanzania lilipanda. Majibu ya maswali hayo bila shaka yanaacha wazi jibu kuwa hakuna.

Hoja zote hizo ukizichunguza kwa makini utagundua wazi hazina mashiko kwani wachezaji wote kwa pamoja bila ya kujali mzawa au mgeni watatakiwa kuwa na kiwango kizuri ili waweze kupata nafasi ya kucheza ndani ya vikosi vyao.

Hakuna kocha atakayekuwa tayari kumpanga mchezaji hata kama wa kigeni lakini hana kiwango kizuri. Kitu kikubwa hapa ni uwezo wa mchezaji mwenyewe kujitambua na kujituma ili kujihakikishia namba katika timu zao.

Toka utaratibu wa kuruhusu wachezaji wa kigeni utumike bado uzoefu unaonyesha wazi wapo wachezaji wa kigeni waliokuwa wakiwekwa benchi licha ya kwamba wametoka katika nchi zilizopiga hatua kubwa kisoka barani Afrika na hata nje ya bara hilo.

Ukifuatilia historia utagundua wazi wapo wachezaji wazawa waliokuwa nje ya kikosi cha kwanza lakini baada ya kupambana waliweza kuwapindua wageni na kuwafanya wakae benchi.

Mara kadhaa Laudit Mavugo raia wa Burundi aliyekuwa akiitumikia Simba misimu miwili iliyopita alisota benchi na nafasi yake kuchukuliwa na wazawa.

Hivi nani angeweza kuamini mchezaji kama Gelson Santana ‘Jaja’ raia kutoka Brazil nchi ambayo inaaminika ulimwenguni wamepiga hatua kubwa angeweza kusota benchi katika kikosi cha Yanga mwaka 2014 na nafasi yake kuchukuliwa na wazawa halikadhalika na Andrey Cotinho pia kutoka Brazil.

Majimaji iliwahi kumsajili mchezaji kutoka Nigeria, Darlington Enyinna lakini licha ya kuwa mchezaji wa kigeni pekee ndani ya timu hiyo bado hakuwa na uhakika wa namba ndani ya kikosi hicho.

Wachezaji wa mifano kama hiyo wapo wengi sana na hiyo bado haihalalishi mchezaji wa kigeni anayesajiliwa ni lazima acheze hata kama hayuko katika kiwango kizuri kwa wakati husika.

Lakini wakati baadhi ya wadau wakipinga hilo lakini hebu tuangalie nini faida ya kuwepo na wachezaji wengi wa kigeni katika ardhi ya Tanzania .

Ukweli ulio wazi ni kwamba kuwepo kwa wachezaji wengi wa kigeni kutaongeza sana ushindani miongoni mwa wachezaji hao hali ambayo itaifanya ligi yetu kuwa bora.

Kufanikiwa kuwa na ligi bora kutaifanya iangaliwe na watu wengi kutoka nje ya nchi hali ambayo itaifanya kuwa na wafuatiliaji wengi lakini kubwa ikiwa kufungua fursa kwa wachezaji wa ndani kutoka achilia mbali sababu ya kibiashara na kiuchumi.

Mseto wa wachezaji hao utazifanya hata timu za Tanzania zitakazowakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kuwa na matokeo mazuri kwa kupata mafanikio makubwa hivyo kuweka rekodi na kumbukumbu nzuri hasa barani Afrika.

Kwa mfano itokee timu ya Tanzania ifanikiwe kuziadhibu timu zinazoaminika ndizo bora barani Afrika kama vile Raja Casablanca (Moroco), TP Mazembe (DRC), Etoile du Sahel (Tunisia), Zamalek au Al Ahly (Misri),ni wazi kutaamsha hali ya kufuatiliwa na mawakala na hata viongozi wa timu kutoka mabara ya Ulaya, Amerika, Asia na kwingineko.

Kitendo cha Ligi kupanda ubora na kuifanya kuangaliwa zaidi huko nje kutakaribisha mawakala wengi kutiririka nchini kuja kuangalia vipaji na hatimaye wachezaji wengi kupata fursa ya kwenda kucheza nje ya nchi.

Hiyo ni fursa pekee kwa wachezaji wa Tanzania kupata nafasi ya kucheza katika ligi mbalimbali ambao nao baada ya kukabiliana na changamoto za huko wataweza kurudi nyumbani na kutoa mchango mkubwa katika soka.

Faida kubwa itapatikana kwa timu ya taifa kwani wazawa watakuwa wamejifunza kitu kutoka kwa wenzao lakini pia ubora wa ligi nao utawafanya wachezaji wa hapa kuwa katika kiwango kizuri hali ambayo pia itazaa Taifa Stars bora.

Hakuna taifa lolote ulimwenguni lililofanikiwa kisoka kwa kutegemea wachezaji wa ndani.

Mabingwa wapya wa Kombe la dunia msimu huu, timu ya taifa ya Ufaransa inaweza kuwa mfano mzuri katika hili kwani asilimia kubwa ya kikosi hicho kina wachezaji wanaocheza ligi mbalimbali barani ulaya.

Hebu kiangalie kikosi cha kwanza cha timu hiyo Hugo Irolis,  Olivier Giroud, Paul Pogba, N’golo Kante (England), Benjamin Pavard (Ujerumani), Samuel Umtiti, Raphael Varane, Antoine Grizman, Lucas Hernandez (Hispania), Blaise Matuid, (Italia) huku Mbappe pekee akitokea Ligi ya nchini humo.

Kitu kikubwa kinachotakiwa ni kuwa na kanuni itakayozibana klabu kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao watakuwa na kitu kitakachowafanya wazawa wajifunze kutoka kwao.

Vilevile muhimu sasa kwa wazawa kuchukulia mtizamo chanya ujio wa wachezaji hao kwani faida kubwa itakuja moja kwa moja kwao. Watakapokuja wageni ni wazi wazawa watakuwa na kitu cha kujifunza kutoka kwao sambamba na wao pia.

Lakini wakati baadhi ya wadau wamekuwa na hofu na wageni kwa wachezaji wetu kiasi cha kufikiria kuwabania nafasi hebu tujiulize nchi zingine wao wanafanya nini.

Ukiangalia Ligi ya Hispania imejaa wachezaji wengi wa kigeni hali kadhalika Ufaransa, Englang na nchi zingine.

Katika Afrika Mashariki Uganda imekuwa ikiongoza katika ukanda huo ukiangalia kwa makini kikosi cha timu yao ya taifa utagundua kina orodha ya wachezaji wengi wanaocheza ligi za nje. Ubora wa kikosi chao unatokana na wachezaji wengi kutoka kwenda nje na kujifunza vitu tofauti.

Katika mantiki hiyo unawezaje kuwabania wachezaji wa kigeni kuja kwa wingi kucheza katika ligi yako lakini wewe ukatamani wa kwako waende kwa wingi nje ili baadaye ufaidike.

Mara kwa mara kumekuwepo na ushauri kwa wachezaji wa kitanzania kuguswa na uthubutu wa kutoka kwenda kucheza ligi za nje. Wengi wanaamini hilo zaidi wakitarajia kuja kupata mafanikio katika timu ya taifa.