Home Latest News Wadau, Serikali walivyoongeza jitihada kuboresha lishe kwa wajamzito, watoto

Wadau, Serikali walivyoongeza jitihada kuboresha lishe kwa wajamzito, watoto

1095
0
SHARE

Na DAMIAN MASYENENE-SHINYANGA

AGOSTI Mosi mwaka huu kati uzinduzi wa maadhimisho ya Nane Nane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alieleza kuwa watoto takribani milioni 3 nchini wana udumavu unaotokana na lishe duni, ambapo mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mwingi wa chakula imebainika kuwa ndiyo yenye idadi kubwa ya watoto walio na udumavu huo.

Jambo hilo lilimshangaza Waziri Hasunga ambaye alitoa maelekezo kwa mikoa hiyo kufanya jitihada za makusudi kuondoa tatizo hilo, pia kuitekeleza kwa vitendo miongozo miwili ya lishe iliyozinduliwa juu ya uboreshaji wa lishe nchini na kuelekeza wananchi kuelimishwa namna ya kuboresha lishe zao ili taifa liwe na watu walio na lishe bora.

Hasunga aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe yenye udumavu wa asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9, Iringa asilimia 47.1, Songwe 43.3, Kigoma 42.3 na mkoa ulioongoza kwa uzalishaji wa chakula mwaka jana na mwaka huu, Ruvuma ukiwa na asilimia 42.2.

Katika kipindi cha mwaka 2018 takwimu zilionyesha kuwa kiwango cha vifo vya uzazi ni 556 kati ya vizazi hai 100,000, kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni 43 kati ya watoto hai 1,000 na kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano ni 67 kati ya watoto hai 1000.

Kwa mujibu wa Shirika la World Vision Tanzania kupitia mradi wake wa Uboreshaji Huduma za Lishe katika Kuimarisha Afya ya Uzazi kwa Mama na Mtoto (ENRICH) katika mikoa ya Singida na Shinyanga, Machi mwaka 2018, lilieleza kuwa hapa nchini, lishe duni huchangia zaidi ya theluthi moja ya vifo vyote vya watoto wa umri kati ya miezi 0 hadi miezi 5.9 na utapiamlo huongeza hatari ya mtoto kufa kutokana na magonjwa mengi, mara nyingi zaidi ugonjwa wa surua, kuhara na nimonia.

Ambapo, Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2015-16, ulionyesha kuwa Mkoa wa Shinyanga kiwango cha udumavu kwa watoto ni asilimia 28, asilimia 3.3 kwa watu wazima, kiwango cha uzito pungufu 12.3 na kiwango cha upungufu wa damu 71, huku mkoa huo ukijiwekea lengo la kupunguza hali hiyo ya udumavu na kufikia asilimia 27 ifikapo mwaka 2025.

Inaelezwa kuwa mtoto ambaye hapati virutubisho na chakula cha kutosha hawezi kukua vizuri, hali hii inaweza kuanzia katika tumbo la mama mwenye utapiamlo. Katika kuimarisha matumizi ya vyakula vyenye wingi wa virutubisho, vikundi lishe vinaundwa, serikali na wadau mbalimbali wanajitokeza kutoa elimu ya lishe kwa mama wajawazito na waliojifungua ili kukabiliana na tatizo hili.

Katika kufanikisha hilo Wilaya ya Shinyanga, Shirika lisilo la Kiserikali la Agape la mjini Shinyanga limeamua kufikisha elimu hiyo ya lishe maeneo ya pembezoni kwa kushirikiana na maofisa wa serikali ili kupunguza tatizo la udumavu dhidi ya watoto, pamoja na kuimarisha kinga zao za mwili ili wakabiliane na magonjwa mbalimbali vikiwamo virusi vya Corona.

Mkurugenzi wa Shirika la Agape, John Myola, alieleza kuwa wameamua kutoa elimu hiyo kwa akina mama wa Kata ya Didia Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, namna ya kuzingatia lishe bora kwa watoto wao ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwamo udumavu na kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Walitoa elimu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kata ya Didia na kukutanisha wanawake 40 kutoka kwenye vijiji vitano vya kata hiyo, kila kijiji kikiwa na akina mama wanne wenye watoto walio na umri chini ya miaka sita, ili wawe mabalozi kwa wenzao, ambapo pia walifundishwa namna ya kulima viazi lishe pamoja na matumizi yake.

Kwa mujibu wa Myola, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wao wa uboreshaji wa lishe bora kwa watoto ili kuwapatia kinga imara ya mwili, ambayo itawafanya kujikinga na magonjwa mbalimbali yatokanayo na upungufu wa kinga mwilini.

“Elimu ambayo tumeitoa kwa akina mama hawa 40 kutoka kwa Ofisa Kilimo, Lishe na wadau wa Lishe, itakwenda kuwa mbegu kwa wenzao ambapo kila mmoja anatakiwa aunde kikundi cha wanawake 10, ili wawe na mashamba darasa ya viazi Lishe, kitendo ambacho kitasaidia kuondoa tatizo la udumavu kwa watoto,”alieleza.

Kwa mujibu wa Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Said Mankiligo, watoto ambao hawanyonyeshwi maziwa ya mama yao ipasavyo, wametajwa kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa mbalimbali, ikiwamo udumavu na upungufu wa akili, kutokana na kukosa kinga bora ya mwili.

Akitoa elimu kwa akina mama zaidi ya 40 wa Kata ya Didia wilayani humo, Mankiligo, alisema kuwa hali ya lishe bora kwa watoto katika halmashauri hiyo si nzuri, ambapo udumavu upo kwa asilimia 33 na hiyo inatokana na wazazi kutozingatia masharti ya unyonyeshaji, ambapo huwafikishi hata mwaka mmoja wanawaachisha watoto kunyonya na kubeba ujauzito mwingine.

“Akina mama wakizingatia elimu ya lishe na kufuata masharti ya unyonyeshaji wa watoto basi naamini tatizo la watoto kuwa na udumavu kwenye halmashauri yetu litakuwa limepungua sana na kufikia malengo kuwa ifikapo mwaka (2025) tuwe tumepunguza hadi asilimia 27 na tutaweza kuvuka kabisa hili lengo pamoja na watoto wetu kuwa na akili nyingi na kufaulu tu masomo yao,”alisema.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Deusi Mhoja akizungumza kwa niaba ya Mkurungezi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba, alipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa kupambana na tatizo huku akiyashukuru mashirika binafsi yanayoiunga mkono serikali katika jambo hilo.

Pia aliwataka akina mama wanaonufaika na mafunzo hayo kuunda vikundi vya ujasiriamali ili wapate mkopo kutoka halmashauri ambao utawawezesha kulima mashamba makubwa ya viazi lishe na kuwaingizia kipato na kukuza uchumi wa familia zao.

Mmoja wa wanawake waliohudhuria mafunzo hayo, Asha Hamisi aliliambia RAI kuwa kumekuwa na changamoto ya udumavu na utapiamlo katika maeneo ya vijijini kutokana na akina mama wengi kutozingatia suala la unyonyeshaji salama kwa watoto wao pamoja na lishe bora.

Ambapo wengi wamekuwa wakiishi kwa mazoea kwa kufuata mila za wazazi wao, huku pia wakishukuru elimu hiyo ambayo itawasaidia kuimarisha afya za watoto wao.