Home Michezo Wafadhili watie mkono timu za Taifa

Wafadhili watie mkono timu za Taifa

712
0
SHARE

serengetiboysNA MWANDISHI WETU

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeanza kuwa na dalili njema baada ya kufanya vizuri katika baadhi ya mechi zake.

Serengeti Boys ilicheza mechi yake ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Misri Aprili mwaka huu na kushinda kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza kabla ya kurudiana na kushinda tena kwa mabao 3-2.

Lakini hivi sasa iko nchini India ikishiriki michuano maalumu ya kirafiki na katika mechi ya kwanza ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Marekani kabla ya kuishinda India kwa mabao 3-1.

Duniani kote ustawi wa soka lake ukiwemo mhimili wa timu ya taifa ni msingi imara unaotokana na soka la vijana.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kutambua umuhimu huo limekuwa likifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ina programu ya kukuza soka la vijana.

Katika jitihada hizo tayari ina mpango maalumu wa kutengeneza wachezaji wengi watakaofanikisha kupatikana kwa timu za taifa za vijana na hata ile ya wakubwa kutokana na msingi imara iliowekeza katika ile ya Serengeti Boys wakiwemo watoto wanaolelewa katika kituo cha vijana cha Alliance cha jijini Mwanza.

Katika kituo cha Alliance watoto wanaolelewa hapo ni wale wenye kati ya miaka 10 hadi 13. Ina maana kwamba watoto hao ndio watakaounda timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 wakati Tanzania ikiwa mwenyeji wa fainali za vijana za Afrika kwa wachezaji wenye umri huo.

Kikosi cha sasa cha Serengeti Boys licha ya hivi sasa kutakiwa kushiriki michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afcon za mwakani pia kitatoa wachezaji wanaoweza kufanya maajabu katika kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022.

Kuna kila sababu ya wadau sasa kuzigeukia timu hizi za vijana zinazosimamiwa na Kim Poulsen, badala ya kusubiri kutoa mchango wao zitakapovuka na kuwa kwenye timu kubwa ya taifa ‘Taifa Stars’.

Kwa mfano uwekezaji hasa ule wa kiufadhili ukifanyika sasa ni wazi utasaidia si tu kuleta morali kwa wachezaji bali hata kusaidia kukuza vipaji na uwezo wao hasa ikizingatiwa kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuipatia uzoefu wa kutosha.

TFF kama taasisi inayosimamia mchezo huo hapa nchini imethubutu na kuonesha njia ambayo kwa muda mrefu waliotangulia walishindwa.

Tuamini kuwa sasa wanapaswa kupewa ushirikiano na wadau kama kweli taifa litakuwa na ajenda moja ya kweli ya kutaka kuweka nia ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, Qatar za mwaka 2022 kwavile zile za Russia za mwaka 2018 kimsingi tushakosa nafasi.

Serengeti Boys ya sasa ambayo wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 ina maana mpaka kufikia mwaka 2022 watakuwa na umri chini ya miaka 23 hivyo kuwa kikosi sahihi kabisa kushiriki michuano hiyo iwapo tu kitakuwa na uzoefu pamoja na sapoti kubwa kutoka kwa wadau.

Zao la Serengeti Boys baada ya miaka saba ambapo wachezaji wake sasa watakuwa wameshavuka umri na kuwa chini ya miaka 23 wakiwa chini ya matunzo sahihi huku wakiongezwa baadhi ya wachezaji wakongwe wanaocheza soka la kulipwa kama kina Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Faridi Mussa na wengine watakaokuwa wakicheza nje kwa wakati huo.

Wakati nchi kama Ufaransa ikimtegemea kinda wake, Anthon Martial, kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu yake ya taifa ikumbukwe hiyo haikutokea kwa bahati mbaya matunda yake yanatokana na jitihada zilizofanywa hapo awali.

Nchi kama Ivory Coast inaweza kuwa mfano mzuri kwa Tanzania ya sasa kutokana na uwekezaji wa academy ya Asec Mimossa ambayo ilitoa matunda ambayo wachezaji wa nchi hiyo wakitamba katika ligi mbalimbali duniani.

Baada ya kushindwa kutwaa Kombe la Afcon mwaka 1994 nchini Afrika Kusini waliamua kuwekeza katika academy ya Asec Mimosa ambapo iliwachukua miaka kadhaa kuona matunda yake.

Wachezaji kama Solomon Kalou, Kolo Toure, Didier Zakora, Emmanuel Eboue, Gervinho, Emmanuel Kone na Yaya Toure ni baadhi tu ya wachezaji wengi walioibuliwa katika mpango huo kupitia academy ya Asec Mimosa iliyokuwa chini ya Mfaransa, Jean-Marc Guillou.

Serikali ikiamua kuunga mkono jitihada hizi za TFF ni wazi itasaidia kujitokeza kwa wafadhili wengi kuwekeza kwa timu hizi ili matunda yapatikane hapo baadaye.

Ni jambo jema wadau wa soka Tanzania kama vile kampuni za kibiashara kujitokeza kuanzia sasa ili kuwekeza kwa vijana hawa ili matunda ya kweli yapatikane katika wakati mwafaka.

Kuna kila sababu ya Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 huko Qatar iwapo tu Watanzania wataamua sasa na kuwekeza kwa timu hizo kuanzia sasa.