Home Afrika Mashariki WAFANYABIASHARA RUKWA WATAMANI SOKO LA EAC

WAFANYABIASHARA RUKWA WATAMANI SOKO LA EAC

973
0
SHARE

NA JIMMY CHARLES

NCHI sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), tayari zimo ndani ya umoja wa forodha kwa miaka zaidi ya 10 sasa.

Umoja huo unatajwa kuchangia tija kubwa kwenye uchumi wa nchi washirika. Biashara kati ya nchi na nchi na watu na watu imeongezekana kwa kiwango kikubwa hata hivyo bado zipo changamoto kadhaa zinazoikabili jumuiya hiyo, hasa soko la pamoja.

Changamoto hizo zinagusa nchi na hata mtu mmoja mmoja, Joel Amon, mratibu wa asasi ya kutunza mazingira ya Kaeso yenye makazi yake Sumbawanga mkoani Rukwa, anasema kuwa pamoja na jamii kubwa ya vijana na wanawake wa mkoani Rukwa kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini ukweli unasalia kuwa zipo changamoto nyingi hasa zile za soko la pamoja.

Alisema mpaka kufikia sasa hajaona faida ya soko la pamoja linalozihusisha nchi wanachama wa EAC.

“Mimi naijua jumuiya hii, lakini naona bado zipo changamoto kadhaa, nimekuwa nikifanya kazi na vijana na wanawake wengi, ukweli ni kwamba bado hawajaifahamu jumuiya hii, lakini pia kuna changamoto ya soko, bado sijaiona faida ya moja kwa moja ya uwapo wa soko la pamoja,” alisema.

Amon, anasema Rukwa iko mbali na nchi wanachama wa EAC, lakini kwa karibu inaunganishwa na Mkoa wa Kigoma ambao unapakana na nchi za Rwanda na Burundi.

Anasema hakuna umbali kutoka Rukwa kwenda Kigoma hatua hiyo inahalalisha haja ya wakazi wa Rukwa kuitumia fursa ya kibiashara na nchi hizo jirani.

Mwalimu Anastazia Mkaja, anasema kuwa wakazi wa Rukwa wanahitaji elimu ya kutosha ya namna ya kulitumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Wengi hatujui umuhimu wa haya mambo, ninachokiamini ni kuwa wapo watu wachache wanafaidika na vitu hivi, lakini sisi inatuwia vigumu.

“Ukweli ni kwamba mkoa wetu hauungani na nchi wanachama wa EAC moja kwa moja, lakini Mkoa wa Kigoma ambao tuko jirani nao unatuunganisha na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, hivyo tunapaswa kuzitumia fursa hizi,” alisema.

Mkuu wa mkoa huo, Zelothe Steven, anasema zipo fursa nyingi ndani ya EAC kwa wakazi wa mkoa wake na kwamba ni jukumu lao kuhakikisha wanazitumia ili kujiletea maendeleo wao, familia zao na Taifa kwa ujumla.

“EAC ni kitu kikubwa chenye fursa mbalimbali si kwa watu wa Rukwa tu, bali kwa Watanzania kwa ujumla, ni jukumu letu kuhakikisha tunazitumia fursa hizo kikamilifu,”alisema.

EAC imefanikiwa kuziweka pamoja nchi sita za Afrika Mashariki hali inayotoa mwanya wa kwa wananchi wa nchi hizo kufaidika katika masuala mbalimbali yakiwamo ya soko la pamoja.

VIPINGAMIZI KUELEKEA SHIRIKISHO

Kwa ujumla, mataifa wanachama wa EAC kwa kiasi kikubwa wanaona neema ya Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini utafiti usio rasmi unaonyesha kuwa Watanzania wengi wana mtazamo hasi dhidi ya shirikisho hilo la pamoja.

Tanzania imekuwa na historia ya amani tangu ilipopata Uhuru ikilinganishwa na fujo na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoshuhudiwa katika mataifa ya Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda na hata Sudan Kusini.

Hata hivyo, kwa wakati huu zipo jitihada za EAC kujaribu kudumisha utulivu na mafanikio katikati ya migogoro inayoendelea katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Pembe ya Afrika na Sudan Kusini.

Pia ni Tanzania pekee yenye ardhi kubwa kuliko mataifa yote wanachama, hii inatoa hofu kwa Watanzania wakiamini kuwa kuridhia uwapo wa shirikisho ni kuruhusu kuchukuliwa kwa ardhi yao.

Uhaba wa ardhi ni suala nyeti katika eneo la Afrika Mashariki, hasa nchini Kenya, ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe upande wa Mlima Elgon mwaka 2007 yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 150 huku wengine zaidi ya 60,000 wakiachwa bila makazi.

HATI YA KUSAFIRIA

Hati ya kusafiria ya Afrika Mashariki ilizinduliwa rasmi Aprili 1, 1999 lengo likiwa ni kurahisisha usafiri na kuvuka mipaka ya nchi husika.

Ni halali kwa kusafiri ndani ya eneo la Afrika Mashariki (Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Tanzania) bila kuwa na kizuizi.

Hati ya kusafiria inapatikana katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji katika miji ya Nairobi, Kampala na Dar es Salaam. Ni raia tu wa Afrika Mashariki wanaoweza kuomba hati hiyo.

VIZA MOJA KWA WATALII

Lilikuwa tarajio la wengi kuwa kabla ya mwaka 2006, kungekuwa na viza moja kwa watalii wote wanaozuru Afrika Mashariki, iwapo mpango huo ungeidhinishwa na mamlaka ya sekta husika chini ya Jumuiya hii. Kama  ingekubalika basi Viza hii ingetumika kote katika ardhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Chini ya pendekezo hili Viza yoyote mpya ya Afrika Mashariki ingeweza kupokelewa kutoka ubalozi wowote katika eneo la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, hadi sasa hili halijafanikiwa na limekuwa moja ya changamoto kubwa.