Home Latest News WAHUNI NA HATARI YA KUVURUGA MKUTANO MKUU ANC

WAHUNI NA HATARI YA KUVURUGA MKUTANO MKUU ANC

881
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Chama tawala cha Afrika ya Kusini – African National Congress (ANC) kinapambana kuzima mgawanyiko wa ndani ya chama hicho ambao unatishia kuvuruga maandalizi ya Mkutano Mkuu wake wa 54 baadaye mwezi huu huku makundi hayo yakipambana vikali kuhusu nani atakayemrithi Jacob Zuma kama kiongozi mkuu wa chama hicho.

Jumatatu iliyopita Halmashauri Kuu ya chama hicho (ANC-NEC) iliamua kuthibitisha uongozi wa jimbo la Eastern Cape baada ya hali ya sintofahamu iliyojitokeza katika mkutano wa chama wa eneo hilo.

Uthibitisho huo kutoka chombo cha juu cha chama hicho kilionekana kumpandisha chati Naibu Rais wa chama hucho, Cyril Ramaphosa kwa sababu utawala wa jimbo hilo unamuunga mkono katika harakati zake za kumrithi Jacob Zuma atakapoachia hatamu za uongozi baadaye mwezi huu.

Chama hicho pia kitachagua timu ya viongozi wa kitaifa kuchunguza malalamiko ya ghasia zilizouharibu mkutano wa chama wa jimbo la Eastern Cape.

Malalamiko hayo yalitolewa na wafuasi wa mpinzani wa Ramaphosa, Nkosazana Dlamini-Zuma, mke wa zamani wa Rais Zuma na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa AU. Sintofahamu iliyoibuka ilisababisha mkwamo wa mkutano huo kwa kipindi cha siku tatu, na hivyo kutoa ishara ya hali kama hiyo ya misuguano mikali ya makundi kuweza kuchelewsha vikao vya mkutano mkuu unaotrajiwa kufanyika Desemba 16 – 20 mwaka huu.

Wadadisi wa mambo ya siasa nchini humo wanasema hali hii, ambayo imeonekana pia katika maeneo mengine, inatia wasiwasi iwapo chama hicho kinaweza kuendesha uchaguzi wa kuaminika.

Na kuuahirisha mkutano mkuu kutamaanananisha kswamba Zuma atabakia kuwa kiongozi mkuu wa ANC wakati ambapo utawala wake umekuwa ukikumbwa na kashfa kadha, zikiwemo za ufisadi na kuwaongezea hofu wawekezaji wanaoomba kupata ukweli kuhusu hali ya siasa katika nchi pekee Barani Afrika yenye uchumi wa kisasa.

Hali hii inaweza kusababisha kupungua kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyi – rand na wasiwasi wa kushuka kwa viwango vyake vya kupata mikopo.

Lakini hata hivyo Katibu Mkuu wa chama hicho Gwede Mantashe na Mweka Hazina wake Mkuu Zweli Mkhize walisema mapema wiki hii kwamba Mkutano Mkuu wa chama utafanyika kama ilivyopangwa.

Aidha, chama hicho katika kile kilichoonekana kuwa hali isiyo ya kawaida wiki iliyopita ilitoa taarifa rasmi iliyo kanusha ripoti zilizozagaa kwamba Halmashauri Kuu ya chama hicho ilikuwa ikijadili kimng’oa Mantashe kutoka wadhifa wake wa Ukatibu Mkuu wa chama.

Misuguano ya makundi mawili – lile la Ramaphosa na la Dlamini-Zuma imeonekana kuwa mikali katika majimbo ya Eastern Cape na KwaZulu-Natal. Tofauti pia zimeripotiwa katika matawi mbali mbali ambako chaguzi zao zilitakiwa kukamilishwa wiki hii.

Atakayekuwa kiongozi ajaye wa chama hicho kikongwe Barani Afrika ndiyo atakeyekuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Rais mwaka 2019. Wachunguzi wa mambo wanasema makundi ndani ya chama hicho yanatishia kukinyang’anya chama hicho uwingi (majority) katika Bunge, uwingi ambao kimekuwa nao tangu Nelson Mandela alipokiongoza na kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ulioshirikisha watu wa asili ya mataifa yote mwaka 1994.

Hali ya kutoridhishwa na uongozi wa Jacob Zuma ulionekana katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana ambapo kura za chama hicho zilifikia kiwango cha chini kabisa katika historia yake – asilimia 54 na kupoteza udhibiti wa mji mkuu wa nchi hiyo – Pretoria na mji mkuu wa kibiashara – Johannesburg.

Kwa upande wake Ramaphosa amekuwa akizungumzia vita dhidi ya ufisadi katika kampeni zake na kumtuhumu Zuma kuhusu suala hilo, ingawa si kwa namna ya waziwazi.

Zuma amekuwa akikabiliwa na tuhuma kubwa kubwa ikiwamo ile kwamba aliwaruhusu wanafamilia wa Gupta kuchota mabilioni ya fedha kutoka makampuni ya serikali. Hata hivyo Zuma na familia hiyo wamekuwa wakizikana tuhuma hizo.

Wachunguzi wa mambo wanasema baadhi ya maswahiba wa Zuma waliohusishwa na kashfa hiyo kubwa bila shaka wana hofu kwamba iwapo kundi lao litapoteza katika uchaguzi wa chama baadaye mwezi huu wanaweza wakajikuta wanakabiliwa na mashitaka mahakamani.

Hadi sasa waendesha mashitaka na wapelelezi wa kipolisi wamekuwa na kasi ndogo mno kuchunguza uhusika wa Zuma na maswahiba zake katika kashfa hiyo.

Siku zote ripoti za Mkaguzi Mkuu wa serikali na zile za kitengo cha kupambana na ufisadi huonyesha matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini ni ni nadra sana kwa maafisa na watendaji wakuu wa serikali kuwajibishwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema kuna masilahi makubwa sana ya kupoteza, na kwa sababu ya jinai hizi, kuna uwezekano mkubwa wale wanaondolewa kutoka nyadhifa zao kujikuta wakikabiliwa na mkondo wa kisheria. Wanasema watu wa aina hii wako tayari hata kuhakikisha mkutano unavurugika kabisa.

Kwa upande wake, mgombea Cyril Ramaphosa anasema Mkutano Mkuu huu ni ‘nafasi ya dhahabu’ kwa chama hicho kujivua gamba na kurudi katika enzi zake.

Akizungumza wiki iliyopita katika hafla moja ya chama hicho mjini Pretoria, Ramaphosa ambaye ni Naibu Rais wa ANC anayemaliza muda wake alisema mkutano huu ni muhimu sana katika historia ya miaka 105 ya chama hicho cha ukombozi.

Alisema: “Wengi watasafiri kutika nchi za mbali kwa sababu huu ni mkutano wa kufa na kupona kwa chama chetu, na ni mkutano ambao utakijenga tena chamam na tuko tayari kukifanya kuwa na nguvu zaidi na kuhakikisha kinaibuka kutoka mkutano huu kikiwa na nguvu mpya.”

Aidha, Ramaphosa aligusia kile atakachokifanya iwapo atachaguliwa. Alisema changamoto kubwa inayoikabili nchi ni ukosefu wa ajira, kutokuwapo usawa katika jamii na umasikini kwa ujumla.

Alisema mamilioni ya wananchi hawana kazi na wengine wanaondolewa kazini kila siku na kwamba suluhisho ni kuwa na uchumi mzuri na madhubuti.

Aliwataka wananchi, hasa wa asili ya Afrika ambao ndiyo wengi kuwa na ushiriki mkubwa katika uchumi wa nchi.

Alisema: “Ni miaka 23 sasa tangu tujikomboe,  na hii ni miaka mingi sana. Wananchi wanataka kuwa mameneja, wanataka kuwa wamiliki wa uchumi wao. Wamechoshwa na hali ilivyo ya kutengwa ma kuwekwa pembeni.”

Ramaphosa alikuwa anazungumzia hali ya kiuchumi ilivyo sasa ambapo Wazungu bado wanadhibiti sekta karibu zote za kiuchumi. Aidha aligusia suala nyeti – lile la ardhi kwa kusema kwamba atahakikisha ardhi iliyoporwa na Wazungu inarudishwa mikononi mwa wananchi.