Home Habari ‘Wajerumani’ wachelewesha mradi

‘Wajerumani’ wachelewesha mradi

1067
0
SHARE

SIMONNA GABRIEL MUSHI

KUCHELEWA kwa mradi wa mabasi yaendayo kasi kunadaiwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Kijerumani ya Strabag.

Kampuni ya Strabag ndio imepewa kazi ya kutengeneza barabara zitakazotumika kwa mabasi hayo, pamoja na vituo vya abiria.

Tayari awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hizo yenye urefu wa kilometa 20.9 za njia maalumu kutoka Kimara hadi Kivukoni, barabara ya Msimbazi, Fire hadi Kariakoo- Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi njia panda eneo la Morocco ziko katika hatua za mwisho mwisho.

Kiujumla mradi huo ulitakiwa kuanza kazi Oktoba mwaka huu, lakini imeshindikana kutokana na kuwapo kwa madai kuwa kampuni iliyopewa kazi ya kuendesha mradi huo ya UDA-RT, imekwama.

Kuchelewa kwa mradi huo kulimfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka kupatiwa majibu ya sababu ya kuchelewa kwa mradi huo ambao unatajwa kuwa moja ya suluhu za foleni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na RAI mwishoni mwa wiki, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Mtendaji wa UDA-RT, Robert Kisena, alisema kamwe wao hawaucheleweshi mradi huo badala yake kampuni ya ujenzi ya Strabag ndiyo inayochelewesha.

Aidha, Kisena alikanusha taarifa za uongo kuwa kampuni yao imepewa dhamana na serikali katika uwekezaji kwenye mradi huo.

Mbali na hilo, pia alikana madai ya kampuni yao kutolipa kodi stahiki katika kipindi ambacho iliagiza mabasi 140 kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam.

SABABU ZA KUCHELEWA

Akifafanua zaidi kuhusu kuchelewa kwa mradi huo, Kisena alisema mradi huo unahusu mambo makubwa mawili.

Mosi ni ujenzi wa miundombinu na pili ni  upatikanaji wa mabasi stahiki yatakayofaa kutumika katika njia zilizotengenezwa.

“Haya ni mabasi maalumu ambayo huagizwa kwa utaratibu maalumu. na UDA-RT tunaangukia kwenye upatikana wa mabasi haya, kwenye upande wa miundombinu huko ni serikali ndio wanashughulikia.

“Sisi kwa upande wetu tumeleta mabasi hata kabla ya mwezi wa 10, tulileta mabasi 140 mwezi wa tisa na kama mnavyojua hii ni awamu ya kwanza kwa sababu mradi mzima utahitaji mabasi 350, lakini tumeingiza hayo kwanza ili kutathmini mahitaji ya wingi wa watu pindi mradi utakapoanza.

“Kwa hiyo miundombinu ndiyo iliyotuangusha ila baada ya kikao cha waziri mkuu, sasa kila mtu naona ameanza kuchangamka kwa sababu mabasi yapo tayari tunasubiri hao Strabarg wakamilishe ujenzi wa miundombinu,” alisema.

Alisema miundombinu hiyo ikishakamilika na kukabidhiwa kwa UDA- RT kutafungwa mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa ukusanyaji nauli, mifumo ya utoaji taarifa na maeneo maalumu ya wazee na walemavu (ITS).

“Naamini tutakabididhiwa mapema, wakishatukabidhi tunatakiwa kuwa na siku 14 za kufunga mitambo yetu ndipo kazi ianze. Mashine za tiketi zipo, mabasi yapo. Kwa upande wetu sisi tumekamilisha,” alisema.

HOJA YA KODI

Pamoja na mambo mengine, Kisena alisema baada ya kuagiza mabasi hayo 140, kampuni yao ililipa kiasi cha Sh bilioni 8.5 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Si kweli kwamba tumekwepa kulipa kodi, lakini pia si kweli kwamba serikali imetudhamini ili kupata mkopo wa kuwekeza kwenye mradi huu.

“Ila naomba ieleweki kuwa, kuna msamaha wa kodi wa asilimia 15 kwa kila muagizaji wa mabasi bila kujali ni ya kwenda mikoani ama ya mradi wa kwenda haraka, wote wanamsamaha huo, Bunge lilipitisha  sheria hiyo ndio maana tumelipa kodi ya Sh bilioni 8.5,” alisema.

“Uwekezaji kwenye huu mradi umegharimu Sh. bilioni 220, kati yake asilimia 70 tumekopa benki na asilimia 30 zilizobaki ni fedha zetu wabia wa kampuni hii ambao ni UDA, Serikali na Darcoboa ambacho ni chama cha wamiliki wa Daladala Dar es Salaam.

“Fedha hizi pamoja na mambo mengine baadhi zimetumika kuagiza mabasi hayo, kufunga mfumo wa utozaji nauli, fidia kwa wamiliki wa daladala na mafunzo maalumu kwa watu watakaosimamia huu mradi kwa sababu wamepelekwa Uturuki na Ubeljiji kujifunza namna nchi hizo zinavyosimamia mradi mkubwa kama huu.

“Si kweli kwamba tumedhaminiwa na Serikali, isipokuwa serikali ina hisa ndani ya mradi huu na hadi kufikia sasa mradi umekamilika kwa asilimia 60,” alisema.

SOKO LA HISA

Aidha, alisema baada ya mradi huo kuanza, kampuni yao itajiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kufanya kazi kwa uwazi na ufanisi.

Alisema hatua hiyo pia itatoa fursa kwa Mtanzania yeyote kununua hisa na kuwa sehemu ya wamiliki wa mradi huo.

“Tunaifanya kazi hii kwa kushirikiana na ushirikiano wa kisheria kila mtu anajua anachokifanya, tumetengeneza kampuni kisheria. Lakini kubwa zaidi ni kwamba tumetimiza masharti ya mkataba wetu,  hakuna mgongano wowote.

“Tutagawana faida kulingana na hisa, hivyo tukishaipeleka kule DSE, kabla hata hujanunua hisa utajua kampuni inavyoendeshwa. Kinachoendelea kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni kudhania tu, sisi tuko vizuri na tutahakikisha kampuni inakuwa na bodi na uongozi imara,”aliongeza.

FIDIA

Kisena alisema wamiliki wa Daladala ambao wanawakilishwa na vyama vyao ambavyo ni Darcoboa na Uwadali, wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh. bilioni 10.

“Hadi sasa tumewalipa fidia wamiliki 136 ambao wanamiliki daladala 363, kwa sababu kiujumla wamiliki wapo 1000 ambapo wanamiliki daladala 2,000 zinazotoa huduma za usafiri katika jiji la Dar es Salaam, kila leseni au Daladala moja italipwa fidia ya Sh milioni 4, kati ya hizo Sh. milioni tatu ni za mmiliki na Sh. milioni moja mhusika atalazimika kununua hisa katika kampuni hii ya UDA-RT kwa sababu wamiliki wa Daladala wapo wengi lakini hawana mtaji wa kutosha kuingia ubia kwenye kampuni hiyo.

“UDA ilikuwa ikimiliki hisa asilimia 99 na mimi nilikuwa namiliki asilimia moja ili kutimiza masharti ya kampuni ya aina hii, ikumbukwe kuwa awali UDA ilikuwa inaundwa na jiji pamoja na Serikali, Lakini baada ya jiji kutuuzia hisa zake, Serikali imeendelea kubaki na umiliki wa asilimia 23 ya hisa zake ambazo hadi sasa hazijaguswa, hivyo UDA ina hisa asilimia 77 na serikali asilimia 23.