Home Makala Wakenya waache kuwazodoa viongozi wa Watanzania

Wakenya waache kuwazodoa viongozi wa Watanzania

1038
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) ya Kwanza, ilivunjika kwa sababu za kisiasa zaidi kuliko sababu za kiuchumi au kijamii. Nakumbuka sana safari za East African Railways (EAR) kwa sababu tulikuwa tunapanda mabasi yake Tukuyu-Mbeya-Iringa-Dodoma.

Pale Dodoma wanafunzi wa Kigoma Tabora-Mwanza walipanda treni na Dar walipanda treni inayotoka bara. Mwalimu Julius Nyerere hawakuiva na Jenerali Idd Amin wa Uganda, Jomokenyata wa Kenya alikuwa hasomeki–alikuwa anaugua ugonjwa unaoitwa ‘senility’ yaani ugonjwa wa kizee—hupoteza kumbukumbu, hulala lalala hata akiwa anamazungumzo na wageni, hupenda kupumzika kwa muda mrefu na anakuwa hawezi kazi ngumu ya kufikiri. Huyo ndiye aliyekuwa Rais wa Kenya.

Hali hiyo ya rais wa nchi kuwapo kama sanamu baadhi ya mawaziri wa Kenya ambao walikuwa hawaipendi Jumuia, walianza kukodolea macho biashara za EAC , shirika la ndege (East African Airways), Shirika la Bandari, Shirika la Reli nakadhalika.

Walitumia udhaifu wa Rais Kenyatta na kuanzisha vita vya maneno na Tanzania. Charles Njonjo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya na aliutumia ukaribu wake na Kenyatta kutoa kauli tata dhidi ya Tanzania na EAC.

Sehemu kubwa za mali ya Jumuia zilikuwa Nairobi na ilipoanguka, Wakenya wakashangilia wakisema Watanzania wamefilisika ni watu wenye njaa sababu ya Ujamaa wa Nyerere.

Sasa amezuka mtu anayeitwa Richard Mriti wa huko Kenya amevaa viatu vya Njonjo na kuanza kutukana. Sitayarudia maneno yake, ila niseme tu kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliamua kufunga mpaka wetu na Kenya.

Kilichotokea baada ya hapo wanakijua Wakenya—ilibidi waombe radhi kwa sababu viwanda wanavyojivunia—kwanza vingi ni vya wageni, halafu walisahau kwamba soko lao kubwa ni Tanzania.

Richard Mriti na wenye husda na Tanzania kama yeye, hawajui kwamba kampuni za Kenya zimewekeza kwa wingi Tanzania.  Hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, miradi kutoka Kenya ilikuwa na kiasi cha $1.68milioni.

Kenya inanunua bidhaa kidogo sana kutoka Tanzania kiasi cha Kshs 15.58 bilioni, wakati inauza bidhaa zake kwetu kiasi cha Kshs 41.05 (2011).

Tanzania ni nchi kubwa kieneo—365,756 kilometa mraba na watu milioni 45.25 (2013). Kenya ina ukubwa wa kilometa mraba 224,445 na watu milioni 44.35. Tanzania inaongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa uchumi mpana na ni nchi ya 12 katika Afrika.

Richard Mriti na wenye mawazo finyu kama yeye—waache kuichokoza Tanzania. Rais John Magufuli sio rais wa Kenya, ni Rais wa Tanzania—mwacheni. Mbona sisi hatukumsema vibaya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alipoburuzwa The Hague akikabiliwa na shitaka la mauaji ya kimbari.

Kenya kila mara inaiota Tanzania na kutaka kuitenga huku wakijua fika kwamba wanaihitaji Tanzania zaidi kuliko Tanzania inavyoihitaji Kenya.

Ukowapi Umoja wa Waliotayari (Coalition of the Willing)—umoja wa kupikwa na uliotungwa na Kenya? Hata kama Kenya ingefanikwa kuitenga Tanzania—isingepoteza kitu kwa kuwa ni mwanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inaziunganisha nchi 14—Angola, Lesotho, Botswana, Malawi, Congo(DR), Swaziland, Afrika Kusini, Msumbiji, Seyschelles, Mauritius na Tanzania.  Hili ni soko kubwa sana na lina fursa nyingi kuliko Jumuia ya Afrika Mashariki.

Kenya  fundo limewakwa kooni baada ya Tanzania kuwanyang’anya mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Mombasa. Bomba hilo litapita Tanzania kwenda Bandari ya Tanga.

Rais Yoweri Museveni alikaririwa akisema, Uganda iliamua kupitisha bomba Tanzania kuwakwepa Wajaluo wa Kenya: “Raila akishindwa na Uhuru, ‘Waruo’ watabomoa pipeline yetu kama vile waling’oa reli.”

Mnaona! Kenya wanahistoria mbaya. Museveni alishawashutukia—mwaka wa 2008, wakazi wa mtaa wa watu wa hali ya chini wa Kibera, waling’oa takriban kilometa mbili za reli inayokwenda Uganda na kuathiri shughuli za usafiri kati ya nchi hiyo.

Reli hiyo inapitisha pia bidhaa za Rwanda, Burundi na mashariki mwa Congo. Ndoto ya Kenya reli mpya ya Standard Gauge—imepotea baada ya Tanzania kwa msaada wa China—itaanza kujenga reli kama hiyo kutoka Dar es Saam hadi Kigoma na Mwanza. Reli hiyo itahudumia pia nchi za Rwanda, Burundi na congo (DR).

Rais Magufuli kutohudhuria mkutano wa hivi majuzi kwenu Nairobi, hakuna uhusiano na ubovu wa miundombinu wala kufungiwa vyombo vya habari.

Watanzania wameacha kupanda mabasi kwenda Bukoba kupitia Namanga na Nairobi, Kampala na Mtukula—kwa sababu barabara kutoka Bandari ya Mtwaara, Kusini mwa Tanzania, imetandikwa lami hadi Rusumo mpakani na Rwanda na barabara inachepuka hadi Bukoba.

Wakenya wamezoea kutangaza vitu vizuri vya Tanzania kwamba viko Kenya—hata daraja la juzi juzi la Kigamboni, waliweka picha yake mtandaoni kuwahadaa watalii wa kigeni kwamba liko Kenya.

Ni watu wenye kuamka usingizini na kuropoka kwamba uchumi wa Tanzania unaendeshwa kwa msaada wa wafadhili kutoka Magharibi. Kenya wamejisahau kwamba wamefika hapo walipo, kwa sababu wakati Tanzania ikiwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa Wafrika wao walikuwa washirika wa Makaburu na misaada na mikopo toka Magharibi.

Wanarudia habari ya sera zilizoshindwa, kama walivyoukebehi Ujamaa, wanaonesha chuki ya wazi kwa Tanzania—kwa kuanza uchokozi wa maneno—kama kwamba ndio ujenzi wa Umoja. Ulimi mkali kwa jirani ni ishara kwamba unayo mengi mabaya moyoni mwako.

Wapo Wakenya wengi tu wanaoishi miongoni mwetu na hawabaguliwi. Wanaoishi kiujanja ujanja bila kufuata taratibu—ndio waliofurushwa. Kenya waache uchonganishi kwa kuandika maneno yasiyofaa kama alivyofanya Richard Mriti. Msimchokoze chatu aliyelala.