Home Afrika Mashariki WAKENYA WAMEAMUA

WAKENYA WAMEAMUA

1160
0
SHARE

 

download

NAIROBI, KENYA

UCHAGUZI Mkuu wa Kenya umefanyika juzi huku amani ikitamalaki kwenye maeneo mengi ya nchi hiyo, kinyume na ilivyotarajiwa.

Hatua hiyo inafuta na kuondoa dhana na dhamira ya kuwapo kwa machafuko na mapigano kwenye uchaguzi huo kama ilivyokuwa mwaka 2007.

Pamoja na uchaguzi huo kuwa na ushindani mkali wa mbio za Urais kati ya wanasiasa wawili Raila Odinga anaewania nafasi hiyo kwa mara ya nne sasa na Uhuru Kenyatta anayetetea kiti chake, wachambuzi wa mambo wanaweka wazi kuwa amani ilitawala.

Ushindani wa Raila na Kenyatta, si tu uliwagusa Wakenya wenyewe, bali pia Watanzania.

Watanzania wengi hasa wa mijini walijikuta wakigawanyika makundi mawili kundi moja likimuunga mkono Odinga ambaye anatajwa kuungwa mkono na Rais Dk. John Magufuli pamoja na Uhuru ambaye anaungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Kuhusishwa kwa wanasiasa hao wawili wa Tanzania kunatajwa kuwaweka njia panda Watanzania na pengine Tanzania yenyewe kwa ujumla.

Wanaobeba hoja hiyo wanaamini kuwa endapo Uhuru atatetea kiti chake upo uwezekano mkubwa wa kuteteresha uhusiano wa marais hao na kwamba jambo pekee ambalo linaweza kunusuru uhusiano wa marais wa nchi hizi mbili ni Raila kukalia kiti cha urais nchini Kenya.

Hata hivyo, uamuzi wa ni nani anapaswa kuliongoza Taifa hilo la Kenya uko mikononi mwa Wakenya wenyewe, ambao tayari wameshaamua baada ya kupiga kura juzi.

NI UCHAGUZI GHALI

Inaelezwa kwamba uchaguzi huo wa Kenya uliofanyika juzi ni miongoni mwa chaguzi ghali zaidi Barani Afrika.

Gharama za uchaguzi huo zinatarajiwa kufikia Dola za Kimarekani bilioni moja na hivyo kuufanya kuwa uchaguzi ghali zaidi katika kile kinachoitwa uwiano wa gharama kwa kila mpiga kura – (cost-per-voter basis).

Matumizi ya fedha kwa upande wa serikali na taasisi binafsi zote ziko juu kuliko wakati wowote katika historia za chaguzi katika nchi hiyo.

Wakati wananchi wa Kenya wakisubiri matokeo rasmi ya mwisho kuhusu uchaguzi huo wachambuzi wa mambo wanasema hali ya hofu kubwa iliyosambaa nchini kuelekea uchaguzi huo ilitokana na si kingine bali historia ya ghasia za uchaguzi hasa ule wa 2007 ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya wananchi 1,200.

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema maumivu haya wakati wa chaguzi hayatokani na suala la ukabila, husuani baina ya Waluo na Wakikuyu, suala ambalo limekuwa likitangazwa sana ili kuaminisha ulimwengu, bali ni mapambano kati nguvu ya demokrasia na wezi wa kura ili kujipatia ushindi isivyo halali.

Wadadisi hao wanaenda mbali zaidi na kusema ni mapambano kati ya walichonacho na wasichonacho. Ni mapambano ya wasichonacho kujaribu kuwaondoa wakandamizaji wao. Wanasema Kenya ni nchi ambayo ghasia za 2007 zilikuwa zinatabiriwa kutokea, na zilitokea kwa haraka zaidi bila ya matarajio.

 

Hata hivyo, nchi za Magharibi zimekuwa zinataja kwamba ikilinganishwa na jirani zake Tanzania, Uganda, Somalia na Ethiopia, Kenya kwa miaka mingi ilikuwa ni nchi tulivu na iliyopiga maendeleo makubwa kiuchumi.

 

Walikuwa wanaongeza kwa kusema muonekano wa Kenya katika uso wa dunia ulikuwa unatamaniwa na nchi nyingi Barani Afrika, kwani ni nchi pekee katika Ulimwengu wa Tatu (Third World) ambayo ni mwenyeji wa taasisi na mashirika kadha ya Umoja wa Mataifa, na pia kuwa kitovu cha mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibanadamu yanayohudumia nchi za ukanda huo.

 

Hivyo kutokana na mtazamo wa nchi za Magharibi katika sifa hizi, kuibuka ghafla kwa ghasia baada ya uchaguzi wa 2007 uliwastua sana.

 

Na ndiyo imekuwa sababu kubwa ya kuwapo hofu safari hii, ikiongezewa na malalamiko kutoka vyama vya upinzani kuhusu uchaguzi uliopita wa 2013 ambao walidai kulikuwapo wizi wa kura.

 

Hadi siku mbili kabla ya uchaguzi, kura nyingi za maoni zilimuonyesha mgombea urais wa chama cha Jubilee, rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta akiongoza kwa asilimia nyembamba dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga wa kutoka vyama vya muungano wa NASA.

Kuna watu wamekuwa na hofu nyingine kwamba pamoja na sheria na kanuni za uchaguzi zilizorekebishwa sana – nyingi kwa msukumo kutoka upinzani, bado hii haina garantii ya kutoibuka kwa ghasia wakati na baada ya uchaguzi.

Pengine hii ina mizizi ya ki-historia ambayo inakwenda nyuma zaidi ya miaka 50. Jomo Kenyatta na Odinga walikuwa maswahiba wakuu katika siasa ambao baadaye, katika miaka ya 60 walijenga uadui mkubwa. Sasa hivi watoto wao wanaliendeleza bifu lile.