Home Makala Kimataifa WAKOREA ‘WAMUAMULIA’ RAIS PARK

WAKOREA ‘WAMUAMULIA’ RAIS PARK

1038
0
SHARE

SEOUL, KOREA KUSINI


Ni wazi kuwa Rais wa Korea Kusini Park Geun-Hye yupo kikaangoni akisubiri miujiza. Rais huyo kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini mwake, ni kwamba anaondolewa madarakani na Bunge la nchi hiyo au wananchi.

Wananchi wamejiapiza kuendlea na maandamano ya kila mwishoni mwa wiki yanayolenga kushinikiza Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais huyo, huku pia, maandamano hayo yaliongezeka idadi ya washiriki. Sasa hivi washiriki wanatoka nje ya Mji mkuu wan chi hiyo Seoul, wanakuja kuungana na wenzao kupaza sauti ya kumtaka Park kuachia ngazi.

Wakati hali ikiwa hivyo, upande mwingine wa shilingi unaonesha kuporomoka kwa uchumi wa nchi hiyo. Hali hii nayo inakuwa ni kiashiria kingine kinachohamasisha waandamanaji kuongezeka.

Maandamano ya mwisho wa wiki iliyopita, yalishuhudia uvunjaji wa rekodi ya waliohudhuria. Inaelezwa idadi ilikuwa ni kubwa sana na mara ya mwisho jiji la Seoul kuona waandamanaji wengi hivyo ni miaka ya 1980. Kulikuwa na zaidi ya waandamanaji milioni  1.3. Waandamanaji hao waliwasha mishumaa, huku wakiimba nyimbo na kucheza. Yete hayo waliyafanya katika baridi kali na mvua, huku kelele zao zikipazwa bila kuchoka wakitamka bayana kuwa Rais Park Geun-Hye akamatwe na kuwekwa mahabusu.

Kelele hizo za waandamanaji zilikuwa zinasikika kabisa na Rais Park, ambaye jingo la ofisi yake lipo kilometa 1.5 kutoka walipokuwa waandamanaji hao. Idadi ya waandamanaji wa kipindi hiki ilikuwa kubwa kuliko ile ambayo imekuwa ikijitokeza katika maandamano haya ya kila wiki yaliyoanza mwezi uliopita.

Kama kuonesha mshikamano, waandamanaji hao waliwasha mishumaa yao, ikiwa ni ishara kuwa hawako tayari kuona rais huyo anaendelea kuwepo madarakani wakati tuhuma dhidi yake zikiwa bayana. Ilibidi idadi ya polisi kuongezeka ili kukabiliana na waandamanaji hao na idadi yao ilikuwa 260,000.

“Sidhani kama Rais Park ataachia nafasi yake kwa ridhaa, tunatakiwa kuongeza sauti zetu ili kuwapa nguvu bunge kuendelea na hoja yao ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye,” Lee Seung-Cheol, (23) alimwambia mwakilishi wa shirika la habari la AFP.

Maandamano hayo makubwa ya amani ambayo pia yanahudhuriwa na watoto na hata wazazi wao, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata viongozi wa dini ya Budha, yanaelezwa kuwa ni makubwa kabisa kuwahi kufanywa nchini humo tangu miaka ya 1980.

Rais Park alitoa taarifa ya kuomba radhi  kwa wananchi wake kufuatia tuhuma ya rushwa inayomhusu mshirika wake wa karibu na wa siku nyingi Choi Soon-Sil, ambaye amekamatwa kwa makosa ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka, lakini rais huyo amekuwa akipinga kabisa kitendo cha shinikizo linalotoka kwa wananchi wanaomtaka kujiulzulu kwa kuwa inaelezwa kuwa naye anahusika moja kwa moja katika tuhuma hizo.

Mtuhumiwa huyo kipenzi cha karibu na Rais Park, Choi pia anatuhumiwa kwa kuingilia masuala kadhaa ya serikali licha ya kutokuwa na nafasi ya mamlaka katika serikali hiyo.

Choi (60) anaelezwa kuwa alitumia ukaribu wake na Rais Park kutafuta michango kutoka katika makampuni mbalimbali ili kufanikisha mfuko wa shirika lake la misaaada, kisha akazitumia fedha alizokusanya kwa matumizi binafsi.

Kufuatia hali hiyo, Rais Park alikaririrwa akisema kuwa yuko radhi kutokea mbele ya kamati huru ya uchunguzi na pia kwamba, yupo pia huru kufanya hivyo kwa Kamati itakayoundwa na Bunge ili kumchunguza kwa kuwa anaamini hana jambo lolote baya ambalo anahusika nalo.

Hata hivyo, kiwango chake cha kukubalika kimeshuka sana na hali hii haikuwahi kumpata rais yeyote wa nchi hiyo aliyekuwa madarakani. Hadi sasa washauri wa juu wa rais pamoja na wakubwa wa makampuni makubwa nchini humo, wanatajwa kuhusika katika kashfa hii nzito.

Makao makuu ya makampuni ya SK, Lotte na Samsung yalivamiwa na waendesha mashtaka wa serikali pamoja na maafisa kutoka wizara ya fedha na mifuko ya hifadhi. Uvamizi huu ulikuwa ni muendelezo wa uchunguzi dhidi ya maafisa kutoka katika makampuni hayo, namna walisvyoshiriki katika kashfa hii.

Kura ya kutokuwa na imani na Rais Park inapigwa wiki hii katika bunge la nchi hiyo. Kura hiyo inaweza kumuendea vibaya rais huyo kutoka na kwamba wabunge wa chama chake pamoja na wale wa upinzani wanaendelea kuungana katika kutaka kumuondoa madarakani.

Kura ya maoni iliyofanywa wiki iliyopita inaonesha kuwa kati ya rais 10, raia 9 wa nchi hiyo wanataka Rais huyo ajiuzulu, aondolewe na pia achukuliwe hatua zaidi. “Nimekuja katika maandamano haya kwa kuwa nataka kuwaonyesha watoto wangu kuwa ni wananchi ndio wanaomiliki serikali ya nchi hii na sio wale walio madarakani,” Shim Kyu-Il, (47) aliliambia shirika la  AFP.

Waandamanaji hao hawakujali hali ya baridi kali iliyokuwepo katika jiji la Seoul, bali walivalia mavazi ya baridi huku wakibeba miamvuli na kuendelea na maandamano yao bila kujali hali hiyo.

Viongozi wa dini ya Budha wakiwa wamevaa mavazi yao ya kanisani, walionekana nao kutoa kauli za kutaka rais huyo wa nchi hiyo pamoja na mshirika wake  Choi, wengine ni  kiongozi mkuu wa kampuni la Samsung, Lee Jae-Yong wote wapelekwe gerezani.

Kulikuwa na magari makubwa yaliyobeba vipasa sauti na vilitumika vema kufikisha ujumbe wa kumata Rais Park kuachia ngazi. Yang Duk-Joon, (53) anasema kuwa baadhi ya wanavijiji walikuja mjini humo kwa mabasi kushiriki maandamano wakitokea, majimbo ya Kusini maeneo ya mji wa Muan.

“Tuko hapa kumuondoa Park ambaye ameharibu nchi yetu,” alisema Yang, na kuongeza kuwa bei ya mchele imeshuka kwa asilimia 40 mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana.

Kama Bunge la nchi hiyo litapitisha kura ya kutokuwa na imani na rais huyo, basi atatakiwa kuachia ngazi na nafasi yake itapaswa kukaliwa na Waziri Mkuu. Lakini kura hiyo ili ianze kufanya kazi hata kama itakuwa imepata kura za kutosha kutoka katika Bunge, itatakiwa kuidhinishwa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.

“Japokuwa Mahakama hiyo imejaa majaji wa mrengo wa kushoto, hawatakuwa na uwezo wa kukataa maamuzi ya watu wanaotaka Park aondolewe madarakani,” anasema Kang Won-Taek, Profesa wa Masuala ya Siasa nchini humo.

Mwisho.