Home Habari WAKURUGENZI KUTOSIMAMIA UCHAGUZI

WAKURUGENZI KUTOSIMAMIA UCHAGUZI

315
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

Sasa tunaweza kusema bila shaka yoyote, na hili tumekuwa tukilisema siku zote – kwamba tangu ujio wa demokrasia ya vyama vingi hapa nchini zaidi ya robo karne iliyopita hakujatokea chaguzi zilizo huru na haki. 

Sababu kuu ya mapungufu haya katika suala zima na muhimu kuhusu demokrasia ya kweli ni kwamba mmoja wa washindani katika chaguzi hizo ndiye anayesimamia chaguzi kupitia uwakala. 

Wiki iliyopita Mahakama Kuu ilitoa hukumu muhimu sana na ya kihistoria kuhusu demokrasia ya ushindani, katika suala lilipelekwa mahakamani hapo na mwanaharakati mmoja – kwa kuvitangaza kuwa batili vifungu vya sheria ya uchaguzi vinavyowapa majukumu wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa kusimamia chaguzi katika maeneo yao na kutangaza washindi – hususan katika ngazi ya Wabunge na Madiwani.

Mahakama ilisema watendaji hawa ni wateule wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala (CCM) na wengi wao ni wanachama wa chama hicho. Baada ya hukumu hiyo wakili wa kujitegemea Bi Fatma Karume aliyemwakilisha mlalamikaji alisema upande wao ulipeleka ushahidi kuhusu wakurugenzi 74 nchi nzima ambao walithibitika kuwa ni wanachama wa CCM na wengine kuonekana katika mikutano yake.

Na hakika tumeona kwa mfano katika uchaguzi uliopita na hata zile chaguzi ndogo za Wabunge jinsi baadhi ya “wasimamizi” hao wa uchaguzi walivyokuwa wakituhumiwa kwa madai ya kutangaza mshindi ambaye siye aliyeshinda na madai mengine ya upendeleo kama vile kuwanyima haki mawakala wa vyama – ‘kuwakwepa’ wagombea wa upinzani wanaporudisha fomu za ugombea na mikwara mingine kadha dhidi yao. 

Yumkini kwa wanasiasa na wanaharakati wanaotetea haki hukumu hiyo ni kizingiti kimoja muhimu kilichovukwa, hata hivyo haitarajiwi iwapo utawala wa chama hicho utaliridhia kirahisi rahisi tu – kwani inakuwa kama vile mtu anaondolewa nofu la nyama kutoka mdomoni. Na tayari tumesikia Mwanasheria wake Mkuu akisema serikali imetoa kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Zaidi ya hapo tayari Mbunge mmoja wa CCM amesikika (baada ya hukumu) akisema bayana kwamba wapinzani wasifurahie sana hili kwa sababu utawala wa chama chake unaweza kuleta kitu mbadala cha kuteua watu wengine wa kusimamia uchaguzi ambao wanaweza kuwaumiza zaidi wapinzani katika chaguzi kulko hawa wakurugenzi wanaowalalamikia. Maneno ya ajabu kweli kweli.

Kauli kama hizi, na nyingine ambazo tutazisikia au kufikiriwa na utawala katika kukabiliana na hukumu hii ya mahakama inaonyesha wazi jinsi utawala huo unavyoishi na demokrasia ya vyama vingi kwa shingo upande. 

Kwa muda hivi kumekuwapo wito kwamba bora nchi ikaurejea mfumo wa demokrasia ya chama kimoja ili kuondokana na unafiki – pamoja na kuepuka farakano zinazoweza kutokea – kama tumekuwa tukiona katika baadhi ya nchi Barani humu – na mfano mzuri ni jirani yetu tu – Kenya kwa uchaguzi wao wa mwaka 2007.

Chaguzi katika mfumo wa demokrasia ya kweli zinahitaji vitu viwili vikuu: “uhuru” na “haki” – bila hivyo ni kama kujidai tu uchaguzi umefanyika basi. Tuchukulie “haki” kwa mfano ambacho ndiyo kitu kikuu katika vitu hivyo viwili. ‘Haki’ ina misingi yake katika ‘sheria asili” (natural law) na

haihitaji mazingira yoyote ya kiutawala – kwani si kitu cha kutoa kama fadhila.

Utoaji haki, katika mifumo ya kimahakama kwa mfano – una msingi wake mkuu unaosema “Siyo tu kwamba haki itendeke, bali pia ionekane inatendeka” (Justice must not only be done, but must also be seen to be done) – msingi uliotokana na hukumu moja katika mahakama kuu nchini Uingereza katika miaka ya 1920. Jaji mmoja Gordon Hewart alitoa msingi huo katika rufaa moja aliyeitolea hukumu baada ya kuona mahakama ya chini haikuonekana ikitenda katika mchakato wa kesi.

Sasa umapomuweka kada wa chama tawala kusimamia uchaguzi na kumtangaza mshindi kamwe huwezi kusema bila shaka yoyote kwamba haki itatendeka, kwani haionekani kwamba inaweza kutendeka kutokana na sifa za 

huyo mtoa haki.

Aidha suala hili pia linahusu Tume ya Uchaguzi (NEC) yenyewe ambayo ndiyo “huwaajiri” wakurugenzi hao wa wilaya na manispaa. Mtoa haki huyo yaani Mwenyekiti wa NEC, Mkururugenzi wake na Makamishna huchaguliwa na Rais wa nchi, ambaye hapa kwetu pia ni mwenyekiti wa chama cha siasa kinachotawala, na mara kadha imetokea kuwa huyo huyo ndiye huwa mgombea urais kupitia chama hicho. Ni vigumu sana Tume hiyo kumtangaza mshindi mgombea wa upinzani.

Mazingira ya namna hii yanatia shaka katika utoaji maamuzi ya haki pamoja msisitizo wake (Tume) kwamba siku zote imekuwa ikitoa haki bila upendeleo wowote.

Ingawa ni ukweli kwamba uendeshaji wa uchaguzi na kutangaza matokeo siyo sawa sawa na uendeshaji wa kesi na kutoa hukumu mahakamani, lakini ni stahiki (relevance) kuhusu haki inayopaswa kutolewa na mamlaka zinayosimamia uchaguzi. Naamini ipo sababu kwa nini Katiba iliona kwamba Mwenyekiti wa NEC lazima awe na sifa za jaji wa Mahakama Kuu na sababu moja ni hii ya msingi mkuu wa kutoa haki. 

Katika miongo ya karibuni dunia imekuwa ikishuhudia katika nchi mbali mbali chaguzi zinavyozidi kuwa za ushindani mkubwa baina ya vyama katika kuwania mamlaka ya nchi. Sasa hivi uvurugaji wa demokrasia kidijitali hasa katika kupindua matokeo ya uchaguzi umetokea kuwa shughuli kubwa duniani, shughuli ambayo hufanywa na makampuni makubwa kwa malipo ya mamilioni. 

Na ni upande wa utawala ulio madarakani (siyo ule wa upinzani) ndiyo wana uwezo na nyenzo za kuajiri makampuni haya, na tumesoma yanayodaiwa kufanyika na kampuni ya Uingereza ya Cambridge Analytica kuhusu uchaguzi wa Kenya na hata ule wa Marekani wa mwaka 2016.

Hata hivyo napenda kupinga vikali mawazo ya baadhi ya watu kwamba tume huru ya uchaguzi haiwezi kupatikana duniani. Hilo si kweli na watu wenye mtazamo huo bila shaka wana ajenda zao za siri – hususan katika kutafuta sababu ya kuendelea kukumbatia hali iliyopo (status quo) katika kuendesha uchaguzi.

Tume huru za uchaguzi zipo – mfano Afrika ya Kusini, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Israel, Japan na kadhalika. Uingereza kwa mfano nimefuatilia chaguzi zao tangu miaka ya 70 lakini sijasikia malalamiko kutoka upinzani kuhusu upendele wa wazi wa tume au taasisi yao inayosimamia uchaguzi. 

Miezi miwili iliyopita, Ethiopia chini ya Waziri wake Mkuu anayetiahidi kujenga demokrasia na kuondoa farakano za kisiasa zilizokuwapo kwa muda mrefu alimteua kiongozi wa zamani wa chama kikuu cha upinzani Birtukan Mideksa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Katika orodha hiyo sikuitaja Marekani kimakusudi kwani mifumo yao ya uchaguzi ni mgumu (complicated) kidogo kwani kila jimbo lina tume yake ambayo ndiyo huwa wakala wa uchaguzi wa rais. Katika uchaguzi wa 2000 kati ya wagombea urais George Bush na Al Gore kulizuka sintofahamu kubwa katika uhesabuji wa kura katika jimbo la Florida ambako mdogo wa Bush, Jeb Bush ndiyo alikuwa Gavana wa jimbo hilo. 

Al Gore alilamika kuibiwa kura ili kumwezesha Bush kushinda jimbo hilo ambalo matokeo yake ndiyo yalikuwa yakingojewa ili kumtangaza mshindi kitaifa. Hata hivyo sintofahamu hiyo ilitinga Mahakam ya Juu ya nchi hiyo (Supreme Court) ambayo ilitoa uamuzi wa kura za majaji 5-4 kumpa ushindi Bush. 

Wengi walisema uamuzi huo wa mahakama zaidi ulilenga kulimaliza suala hilo lililokuwa linachukua muda mrefu na hivyo kuitia doa Marekani mbele ya jumuiya ya kimataifa.